Kuzaa Matunda – Utumishi – na Thawabu za Milele: Nyaraka za Petro #18
Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa: https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsisri Hii ya Kiswahili Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for This Kiswahili Translation has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

Utangulizi: Tumekuwa tukidhihirisha kwamba malengo ya maisha ya Mkristo ni kukua kiroho na kuwasaidia/kuwahudumia wengine ili wafanye vivyo hivyo. Mpaka hapa katika masomo yetu tumezungumzia tatu kati ya awamu nne za Mpango wa Mungu ambazo zinahusiana na sehemu ya kwanza kati ya mbili za malengo ya maisha ya Mkristo, ambayo ni kupevuka kiroho kwa kila mtu anayeokolewa. Awamu hizi tatu ni: 1) kusikiliza (kama muumini, kuchukua hatua chanya za kupata habari za Mungu); 2) kuamini (kukubali na kupokea kweli za Biblia ndani ya mioyo yetu kwa imani, hivyo kufanya kweli hizi kuwa sehemu ya fikra zetu); 3) kuzi-ishi (kuzitumia kweli hizi katika maisha yetu; kuelekeza mawazo yetu katika misingi ya kweli, haswa katika nyakati za shinikizo na majaribu; kufanya juhudi za kuishi kulingana na kweli; kutumia maadili ya imani, tumaini na upendo katika maisha yetu). Hatua hizi tatu za mwanzo (ambazo huendelea maisha yetu yote, bila kukoma) zinatupatia matayarisho ya kututia nguvu ambazo ni muhimu kwetu katika kuanza awamu ya nne katika Mpango wa Mungu kwa maisha yetu: kusaidia/kutumikia/kuhudumia. Kuwasaidia Wakristo wengine (na kuwafanyia uinjilisti wasioamini ili wawe Wakristo) ndio utimizo wa lengo lakuwepo hapa duniani na ndio msingi wa thawabu zetu za huko mbinguni. Huu ni wajibu wetu pia. Kwani mara tunapoanza kupevuka kutokana na kusaidiwa na wengine, ni wajibu wetu pia kunyoosha mkono wa upendo na kuwasaidia wenzetu wengine wafikie lengo hilo hilo.

Kusaidia: Watu wengi wanaposikia neno “mtumishi”, mara moja wanafikiria Mchungaji pale kanisani kwao, na kwa kweli wachungaji ni “watumishi” katika maana ya Kibiblia, lakini neno hili “mtumishi” linahusisha msaada na huduma zote ambazo waumini wanatoa kwa waumini wengine katika kanisa la Kristo (na kwa wasioamini pia). Neno la Kiyunani diakonos (διάκονος) maana yake halisi ni mtumishi, na pale Kristo anapowaambia wanafunzi wake (walipogombania ukubwa) kwamba yeyote kati yao anayetaka kuwa mkuu wa wenzake ni lazima awe mtumishi wa wote (Matt. 20:26-27), tunapata uhalali wa kutafsiri neno hili kama “mtumishi”. Tatizo ni kwamba neno la Kiingereza “minister” lina vidokezo vya mamlaka, nafasi/wadhifa, fahari na aina fulani ya upekee, vidokezo ambavyo havimo kabisa katika neno la Kiyunani diakonos/mtumishi. Kiuhalisia, kila mmoja katika Mwili wa Kristo ni mtumishi kwa wote, na hakuna sehemu moja inayokaa peke yake, kama vile macho, masikio, miguu, mikono yetu haiwezi kufanya kazi peke yake bila kutegemeana na viungo vingine vya mwili (1Wakor. 12:12-26). Mungu ameunda Kanisa la Kristo katika namna ya kwamba kila mmoja wetu ana kazi ya kufanya. Kila Mkristo ana utumishi muhimu, wa kipekee (yaani huduma) kwa faida ya wengine katika “Mwili” wa Kristo. Baadhi ya huduma zinaweza kuonekana kama vile zina mvuto zaidi, na zingine kuonekana kuwa ni za kawaida; nyingine huwa zinaonekana zaidi na kadamnasi, na nyingine kuwa kama hazionekani kabisa kwa watu; nyingine zina thawabu nyingi za kidunia (hapa duniani), na nyingine huonekana kuwa ni mzigo na shida kubwa kwa wale wanaojiwajibisha nazo. Kitu kimoja tu ni cha uhakika: Mungu ametupatia sisi sote jukumu fulani la kutimiza katika utumishi wetu katika Kanisa la Bwana Yesu. Cha muhimu ni kujiuliza: “Je, tunafanya kazi yetu au la?”

Kuzaa Matunda (Utumishi):

Mimi ni mzabibu halisi na Baba yangu ni mkulima. Kila tawi langu lisilozaa Yeye alikata, na kila tawi linalozaa Yeye hulipogoa (prunes) ili liweze kuzaa zaidi. Yoh. 15:1-2 SUV.

Kwa wale miongoni mwetu walio tayari kumfuata (kuzaa matunda kama matawi katika mfano hapo juu), Mungu anaelekeza na kuendesha maisha yetu kwa kusudi la kutuwezesha kuzaa matunda kwa kiwango cha juu. Zaidi ya hapo, ni kwa ajili hii tumeumbwa upya katika Bwana Yesu Kristo (Waefe. 2:10). Ni muhimu sana kukumbuka, hata hivyo, kwamba japokuwa sisi “matawi” ndio wakala, Mungu ndiye chanzo pekee cha kazi njema tunayokamilisha katika maisha haya. Mbali na Bwana wetu Yesu Kristo hatuwezi “kuzaa matunda”, lakini pale tunapofuata, tunapotii, tunapokaa ndani Yake, tunawezeshwa na Mungu kufanya ile huduma ambayo Yeye ametuchagulia (Yoh. 15:5).

Haiwezekani kutenganisha kuzaa matunda kwa mafanikio, na kukua kiroho, kwani vitu hivi viwili vimeunganishwa katika Wakolosai 1:10. Kudumaa kiroho kunapunguza uwezo wetu wa kulisaidia Kanisa na kuwasaidia wengine katika kukua kiroho. Hii haina maana kwamba hatuwezi kuzaa matunda mpaka tufikie kiwango fulani cha kupevuka, bali hata kwa akili za kawaida utaona kuwa tutaweza kuwasaidia wengine ikiwa sisi wenyewe tunaendelea kukua pia. Mwandishi wa barua kwa Waebrania aliwakosoa wasomaji wake katika jambo hili: japokuwa walikuwa Wakristo kwa muda mrefu, bado walihitaji msaada kutoka kwa wengine badala ya wao wenyewe kuwa tayari wanawasaidia wengine (Waebr. 5:12).

Waumini wanaoshindwa kuendelea kiroho (katika namna endelevu) kwa kufuata hatua zile mahususi za kusikia, kuamini na kulitumia Neno la Mungu katika maisha yao, wataona uzalishaji wao ukikosa matunda ya kiwango kinachokubalika. Fundisho la mpanzi linatuambia kwamba muumini anayeshindwa kuishinda mitihani ya mashaka ya maisha, kishawishi cha kutafuta utajiri duniani, na kishawishi cha maisha ya anasa, ni sawa na mmea unaosongwa na magugu: masuala ya duniani yanasonga uzalishaji wa matunda, ambalo ndilo lilikuwa kusudi la yeye kupandwa shambani (Matt. 13:22-23; Luka 8:14).

Kama tawi linalokatwa katika Yoh. 15:2 linavyotuonyesha, kukosa kuzaa matunda kabisa ni jambo zito sana. Tunaona mfano mwingine wa fundisho la talanta, ambapo watumishi wanaoleta faida wanasifiwa na kuthawabiwa, wakati mtumishi anayefukia talanta yake (hivyo harudishi faida yoyote) anatupwa nje gizani na Bwana wake (Matt. 25:14-30). Hapa, mtumishi anayefukia talanta yake, na tawi linalokatwa katika Yoh. 15:2, wanawakilisha watu wasioamini. Haiwezekani kwa muumini wa kweli wa Yesu Kristo kutozaa matunda kabisa (Yakobo 2:26)! Japokuwa baadhi yetu tunaonekana kuwa na “talanta” nyingi zaidi ya wengine, sote tunapewa “talanta ya kiroho” [sawasawa] tuitumie kwa ajili ya Mungu katika maisha yetu. Tunapaswa kuchukua tahadhari tusipoteze “faida” katika “talanta” tunayopewa, na hivyo kuacha nafasi yetu mahususi kutotumika. Kama tumekua kiroho, ni lazima tumepata msaada mkubwa kutoka kwa waumini wengi wengine ambao inawezekana hata hatuwajui. Je, hatupaswi basi tuwe na shauku ya kutoa msaada kwa wengine walio safarini kuelekea kwenye upevu wa kiroho kama sisi tulivyosaidiwa?

Kuzaa Matunda Maana Yake Nini?

I. Kuzaa Matunda ni Kutoa [Msaada]

Mmea kama mti ukizaa matunda, matunda hayo ni baraka kwa wale wanaoyavuna na kula. Katika namna hiyo hiyo, “mazao yetu” ya Kikristo hayapo kwa faida yetu bali yapo kwa ajili ya kubariki maisha ya wengine. “Kuzaa matunda” ni, katika kiini chake, kitendo cha kujitoa. Inataka juhudi ya kujitoa mhanga kwa ajili ya mema ya kiroho ya wengine. Ukubwa wa zawadi unayoitoa hauna umuhimu: sarafu mbili za yule mjane zilikuwa na thamani zaidi mbele za macho ya Mungu kuliko pesa nyingi zilizotolewa na matajiri (Mrk 12:42; Lk 21:2). Hata aina ya zawadi haina umuhimu: hata kikombe cha maji baridi kikitolewa kwa Jina la Bwana kitapata thawabu yake – Matt. 10:42; Marko 9:41- (katika nchi za baridi-baridi kama Israeli, haswa msimu wa baridi – winter – watu hunywa maji ya vuguvugu). Na zawadi hiyo siyo lazime iwe ya kitu kinachoonekana kwa macho. Kufundisha, kufariji, kutia moyo, kusaidia kufanya kazi, maneno na matendo ya upendo, yakifanywa katika Jina la Bwana, kwa ajili ya utukufu wa Mungu, hizi ni zawadi zinazotolewa kwa upendo wa Kristo, ambazo zinaendana na vipaji vyetu vya kiroho, zinatukumbusha juu ya ile Zawadi Kuu kutoka kwa Mungu, ya Mwanaye, Bwana wetu Yesu Kristo.

Kuzaa matunda, utumishi, kazi/matendo, huduma ya Kikristo, au vyovyote tutakavyoamua kuita “kutoa Kikristo” kunavuka mipaka ya zawadi za pesa pekee. Wakati anawasifu Wafilipi kwa zawadi walizompa, Paulo aliweka wazi kwamba alifurahia zaidi thawabu iliyoongezwa katika hazina yao mbinguni kwa matunda yao mema na halali ya zawadi ile kwake kuliko pesa alizopokea (Wafi. 4:17; cf. 2Wakor. 8:1-4). Katika dunia ya leo ya kubeza mawazo ya wengine, tuna tabia ya kutoamini kauli kama hii, au kuona kuwa imetiwa chumvi. Lakini katika suala la mtume Paulo, tunaweza kuwa na uhakika kuwa hisia zake hizi ni za kweli, kwani hakuna aliyeishi maisha magumu na yenye shida zaidi yake katika kumtumikia Mungu (2Wakor. 11:16-33). Kwa Paulo, pesa ni aina mojawapo tu ya “mbegu” ya kupanda katika shamba la Bwana (2Wakor. 11:8-9), au aina [mojawapo] ya nyenzo ya kutuwezesha kutumikia. Kutoa pesa, ambako kunataka juhudi (ya kutafuta hiyo pesa), na kujitoa mhanga (katika kumpa mtu), ni sawasawa na tendo lolote la kuzaa matunda Kikristo katika taswira zake hizo mbili: utumishi wowote tunaoufanya kwa ajili ya Mungu ni lazima, ili uwe utumishi wa kweli, tujitoe nafsi na miili yetu ili kusaidia katika wokovu wa wengine. Kristo alitufundisha tuwape wale wanaotuomba (Matt. 5:42). Basi, na tusisahau mahitaji ya pesa ya Kanisa la Kristo, lakini pia tusifikirie kuwa pesa inaweza kuchukua nafasi ya tendo la wema, neno la kutia moyo, sala (maombi) kwa ajili ya mwingine, au kuifundisha kweli iliyo muhimu kwa ajili ya mafundisho ya Kanisa la Kristo.

Maandiko yanatufundisha kwamba Abeli, japokuwa amekwishakufa, bado anashuhudia kwa ulimwengu kwa imani yake kwa Mungu kupitia ile sadaka aliyoitoa (Waebr. 11:4). Sadaka yake ya damu inawakilisha uhitaji wa mbadala, mwokozi, wa kulipa gharama ya dhambi; kwa kuukubali ukweli huu kwa njia ya sadaka, Abeli hakusaidia mwanadamu mwenzake kwa njia ya kimwili (kama kutoa pesa kwa wanaohitaji), bali alifanikisha lengo muhimu ambalo Mungu alimpangia, lengo ambalo bado linazaa matunda leo, likituonyesha kwamba tangu mwanzo kabisa mwa historia ya wanadamu, waumini wa kweli walielewa uhitaji na ahadi ya mwokozi ambaye baadaye alikuja.

Mfano huu wa Abeli tunauona kwa waumini wengi wa zamani: baadhi ya matendo ya utumishi wao ambayo mpaka leo tunayajua ni matendo yao ya imani yanayotutia moyo mpaka leo. Yakobo anapowakemea waumini wanaodai wanayo imani japo hawaifanyii matendo, mfano wake wa matendo mema ni utayari wa Abrahamu wa kumtii Mungu katika mtihani mgumu sana: kumtoa sadaka mwanaye wa pekee, Isaka (Yakobo 2:21-23). Kitendo hiki cha utii cha Abrahamu hakikuwasaidia wengine kimwili, lakini kinatufundisha sisi leo hii kwa kututia moyo tumwamini Mungu na kumtegemea kama Abrahamu alivyofanya (War. 4:17). Vivyo hivyo kwa waumini wengine wakuu wa zamani. Danieli, Daudi, Stefano, hawakuwa wakuu kwa sababu ya zawadi zao za pesa, bali kwa sababu ya matunda waliyozaa katika kushuhudia uaminifu wa Mungu katika matendo yao ya imani kwake. Katika mifano yote hii mikubwa tunayoiona katika Biblia, hiki ndicho kiini cha zawadi ile: matunda yanayotufurahisha sisi tunaoyatumia ni utegemezi wenye nguvu, unaosisimua, unaomtukuza Mungu na unaotutia moyo na kutupa msukumo katika maisha yetu ya Kikristo, waliouonyesha waumini wale wa kale. Aina hii ya “matunda” kwa hakika inahitaji kiasi kikubwa cha upevu wa kiroho kabla ya “kuiva”.

Sasa tumekamilisha [m]duara, tumerudi pale tulipoanzia. Ili tuwe na mafanikio katika kuzaa matunda ya kiroho, ni lazima tufanikishe kiasi fulani cha kupevuka kiroho kwa kupitia mchakato wa kusikiliza (au kusoma), kuamini na kuyaishi mafundisho, kitu ambacho kimekuwa mwelekeo wa masomo yetu mpaka hapa. Kwani, kama sisi wenyewe hatujafika mahala pa kumwamini kikwelikweli, tunawezaje (kwa ufanisi) kumwonyesha mtu asiyeamini kwamba Mungu ni wa kuaminiwa? Kama hatujafikia kiwango cha kuamini kwamba kuna thawabu ya mbinguni, tutawezaje kumpa faraja mtu aliye na majonzi au kumpa motisha mtu aliyechoka kiroho aendelee na furaha katika Kristo? Kama hatujajifunza kumpenda Mungu zaidi ya vyote hapa duniani, tutawezaje kukabiliana na jambo lolote ambalo linahitaji kujitoa mhanga kwa kiasi kukubwa kwa ajili Yake? Hii ni mifano tu, lakini vyovyote vile utumishi wetu utakavyokuwa, hautakua na mafanikio (hata kama utaanza) mpaka “mtumishi mwenyewe” atakapokuwa na kiasi fulani cha mtaji wa kiroho uliomo rohoni mwake ili aweze kumpa “yule anayemtumikia”.

Kuzaa matunda ni, mwanzo hadi mwisho wake, kutoa, siyo kwa Mungu, bali kwa Wakristo wenzetu, wale ambao tayari ni Wakristo, na wale tunaowapatia Injili ili wawe Wakristo, ikiwa wataamini. Mungu hana uhitaji wa kitu chochote kutoka kwetu (Matendo 17:25), na kwa kweli anaweza, bila shida yoyote ile, kufanya kila tendo la utumishi lililokabidhiwa kwa Kanisa Yeye mwenyewe. Hivyo, tunapaswa kuuchukulia mchakato wa kuzaa matunda, tendo/matendo ya kutoa Kikristo, katika hali yake halisi: ni heshima ya pekee kwetu sisi kuruhusiwa kufanya kazi katika shamba ambalo Mungu anaweza kulilima lote Yeye mwenyewe, na hivyo kujitoa kidogo katika kuiga na kushukuru, ile zawadi kuu kuliko zote, Bwana wetu Yesu Kristo (2Wakor. 9:15; War. 5:15-17).

II. Utumishi (Kuzaa Matunda) Huwezeshwa:

Si kwa nguvu, wala si kwa uwezo, bali ni kwa Roho yangu. Zakariah 4:6 SUV.

Tumekwishaona kwamba kwa sababu sisi ni matawi tu, hatuna uwezo wa kuzaa matunda mbali na Mzabibu ambamo ndani yake sisi tumo. (Yoh. 15:1-2). Sisi sote ni vifaa tu katika mpango wa Mungu isipokuwa tu huduma yetu inategemea utayari wetu wa kushiriki katika majukumu Mungu anayotupangia. Hakuna tendo la kuzaa matunda hata moja linalokubaliwa na Mungu ambalo linafanikishwa kwa nguvu ya mwanadamu. Kabla ya kuumba majira (time), Mungu alitayarisha matendo yote mema aliyotaka sisi tuyatimize katika maisha yetu hapa duniani (Waefe. 2:10), na hakuna hata tendo moja kati ya matendo hayo linaloweza kufanikishwa bila ya msaada wa Roho wake Mtakatifu (1Wakor. 12:3). Kama ilivyokuwa vigumu kujenga upya hekalu baada ya Waisraeli kurejea kutoka utumwani kule Babiloni (muktadha wa Zakaria 4:6 hapo juu), vivyo hivyo kazi nyingi za utumishi tunazoitwa na Bwana tuzifanye zinaweza kuonekana kuwa ni ngumu na zisizowezekana kwetu. Lakini hakuna kisichowezekana kwa Mungu (Mwa. 18:14; Lk 1:37), na kama alivyomhakikishia Zerubabeli kwamba Roho wake Atatia nguvu kazi yao, nasi Wakristo, ambao tuna Roho wake ndani yetu, siyo tu pamoja nasi (Yoh. 14:17), tunapaswa kuwa na moyo thabiti tunapokabiliwa na upinzani katika utumishi wetu, hata kama inaonekana kuwa hali ni ngumu na hakuna uwezekano kwa wakati huo.

Roho Mtakatifu ndiye anayewezesha na kufanikisha utumishi wote na kazi za vipaji vyote vya kiroho (1Wakor. 12:6b; 11b). Sisi kama matawi, Yeye anatenda kazi kupitia kwetu ili kuzaa matunda yote, yale matunda ya maisha safi, bora ya Kikristo (Wagal. 5:22), na matunda ya utumishi wetu kwa watu wengine. Kitu muhimu, cha msingi katika uzalishaji matunda ni ki/vipaji alivyopewa Mkristo huyu. Kila mmoja wetu ana kipaji au vipaji vya kiroho, na, ni Roho Mtakatifu anayeamua kuhusu kipaji gani akupatie, ni Yeye anayetoa, ni Yeye anayekitia nguvu ya utendaji kipaji hicho/vipaji hivyo (1wakor. 12:11). Kama kweli tuna nia ya kutumikia, tunapaswa kuamini kwamba Mungu atatuongoza kuelekea kwenye matumizi ya kweli na bora ya kile kipaji au vipaji alivyotupatia. Ikitokea kwamba tunajikuta tukifanya kazi fulani katika Kanisa, na sisi wenyewe tunaona/tunahisi aina ya utumishi tulio nao katika Kanisa haiendani na kipaji tulicho nacho, basi ni lazima 1) tukumbuke kwamba waumini wote katika mwili wa Kristo (Kanisa) ni muhimu sana (1Wakor. 12:12-26); 2) tukumbuke kutojaribu kukimbia yale majaliwa ya kwanza ya utumishi Mungu aliyotupangia (Yonah 1:1-3:3); na 3) tukumbuke kuwa uchaguzi wa kipaji tulicho nacho ni wa Mungu, na hivyo tuuheshimu uamuzi huo na tuamini kwamba ni bora kabisa kwetu. Mwisho, ni kitu kisichofaa kabisa kudhani (na kufuatilia) shauku ya vipaji vya kiroho ambavyo kwa sasa haviwezeshwi, kama vile kunena kwa lugha, unabii, uponyaji na vingine kama hivyo. Tukiwa ni Wakristo wenye weledi (yaani siyo kwamba hatuna na hatupendi hisia, bali tunasema hisia zinapaswa kuongozwa na weledi – 1Wakor. 14:32-33; 14:40), tunapaswa kuukubali ukweli kwamba vipaji hivi kwa sasa havitolewi na Roho Mtakatifu, kama vile ambavyo kwa sasa hateui Mitume tena, na wala haruhusu mtu yeyote kuandika/kuongeza sura/vitabu vingine vya Biblia.

Uchaguzi na uwezeshaji wa Roho Mtakatifu wa huduma yetu ya Kikristo hauishii kwenye vipaji vyetu tu, bali unahusisha uzalishaji wa matunda katika ujumla wake. Katika 1Wakor. 12:4-7, tunafundishwa kwamba taswira zote za utumishi wetu zinaongozwa na Mungu: ni “Roho yule yule” anayesimamia “vipaji”, “utumishi”, na “utendaji kazi”. Makundi haya matatu yanawakilisha: 1) vipaji halisi vya kiroho (kwa mfano kusaidia, kutia moyo, uinjilisti, n.k.); 2) utumishi mbalimbali (kwa mfano uongozi na mahala popote utakapolazimika kukaa/kuishi hapa duniani katika makanisa mbalimbali); na 3) uzalishaji wa matunda ya “shamba”. Makundi mawili ya mwanzo yanajieleza kwa uwazi ; kwa mfano unaweza kuwa na kipaji cha kiroho cha kusaidia, na ukakitumia kipaji hicho kwa kusaidia katika gharama mbalimbali za kanisa lako la jirani ambalo ndio linatoa fursa ya utumishi wako. Kipengele cha tatu kinachotajwa katika 1Wakorintho 12 ni, hata hivyo, chenye kutupa mwanga zaidi ya vyote: ufanisi halisi wa utumishi wako, msingi wake siyo juhudi zako pekee, bali pia unategemea “rutuba ya shamba” unamofanya kazi. Hivyo “udongo” unaolima unaweza kuwa na rutuba nyingi, kidogo au kiasi cha wastani tu, lakini Mungu aliyajua yote hayo kabla na kwa kweli aliyaweka katika mpango wake kabla ya historia ya viumbe wake wa hapa duniani na mbinguni kuanza. Hii maana yake ni kwamba mwinjilisti, kwa mfano, matunda ya kazi yake hayatatathminiwa kwa idadi ya watu wanaookolewa; bali huduma yake itapimwa ufanisi wake kwa vigezo vingine (yaani juhudi na ubora wa kazi yake ukilinganisha na “rutuba” ya shamba alilopewa, au utayari wa wale aliowahudumia katika kutaka kuokolewa). Kwanza, nabii Yeremia na manabii wengi wengine wa Agano la Kale walifanya juhudi kubwa sana, lakini matunda ya juhudi zao yalikuwa finyu sana. Hivyo tusikatishwe tamaa kwa kuona kuwa utumishi wetu ni kama vile hauna matunda ya kuonekana kwa macho ukilinganisha na utumishi wa wengine ambao kwa machoni unaonekana una mafanikio zaidi, kwani tutavuna kile Mungu alichokipanga katika wakati mwafaka kwake (Wagal. 6:9). Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, jinsi tunavyotimiza utumishi tuliokusudiwa na kupangiwa na Mungu, Yeye atafanikisha malengo yake (cf. Isaya 55:11).

III. Uzalishaji wa Matunda Hutuzwa:

15.58  Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana.
1Wakor.15:58 SUV

Kama waumini wa Kristo, tutaishi milele. Tutafufuliwa katika miili ya utukufu na tutakuwa na Bwana milele yote, na, ni mwishoni wa mjadala mrefu kuhusiana na ufufuo katika 1Wakor. 15 ndipo Paulo anasema hilo hapo juu: kazi yetu si bure katika Kristo, kwa sababu tutakuwa naye tukifurahia matokeo ya kazi hiyo milele.

1. Tathmini, Hukumu na Thawabu:

22.12  Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.
Ufu. 22:12 SUV

Kama ilivyo katika aya nyingi nyingine za maandiko, (mf. Isa. 40:10; 62:11; etc), aya hii inaweka wazi kwamba kila mmoja wetu atasimama ili ahukumiwe kwa jinsi alivyoutumia muda wake hapa duniani, ili tuweze kulipwa kwa “ajili ya yale ambayo ametenda akiwa katika mwili wake, yawe mema au mabaya”. Ukaribu wa kurudi kwake Bwana, na ufahamu kwamba Yeye mwenyewe atatathmini maisha yetu unapaswa kututia motisha ya kuendelea kuvumilia katika kazi ya ufalme Wake. Kama tunaendelea kiroho katika namna ambayo Mungu alikusudia, basi hii na iwe njia ya kututia moyo kama nasi tunavyopata moyo kutokana na msingi wa thawabu kwa muda na huduma yetu hapa duniani, kwani Mungu si bahili, akitupatia kipimo cha thawabu inayojaa hata kumwagika, na anatuahidi faida kuu kwa mtaji wowote tutakaoutumia (Matt. 10:42; 19:29; Lk. 6:38; Waefe. 6:8).

2. Yesu Kristo Ndiye Hakimu:

5.10  Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara [thawabu] ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.
2Wakor. 5:10 SUV

Mungu amemteua Kristo kuwa hakimu wa walio hai na waliokufa (Matendo 10:42). Katika nafasi hii, Bwana wetu atahukumu ulimwengu kwa niaba ya Baba yake (War. 14:10-12; 2Tim. 4:1; 4:8). Kiti cha hukumu (kwa Kiyunani bema – βημα) cha Kristo, ni mahakama ambapo kila muumini/mfuasi Wake atasimama mbele yake na kujibu maswali kuhusu wakati/maisha yake hapa duniani (War. 2:16; cf. Waebr. 13:17; na Pet. 4:5). Kwa kuwa kila mmoja wetu atatoa maelezo yake mwenyewe kwa Bwana kuhusu yote tuliyoyafanya (na ambayo hatukuyafanya kama ilivyokuwa wajibu wetu) (War. 14:12), tunapaswa kutia bidii katika “kumfurahisha Yeye katika mambo yote” - 2Wakor. 5:9), na kulifanya zoezi hilo kuwa la kutuhakikishia thawabu ya milele, badala ya kudhihirisha maisha yaliyofujwa (1Wakor. 3:11-15).

3. Hulka ya Hukumu Hii:

Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu. War. 8:1 SUV

Tathmini ya maisha ya Mkristo ni tofauti kabisa kimsingi na hukumu nyingine zitakazofanyika siku zijazo. Kama waumini wa Bwana Yesu Kristo, hatuko tena chini ya hukumu ya adhabu ya Mungu (Yoh. 3:18); hatutaingia katika hukumu ambayo matokeo yake ni uzima wa milele au kifo (kifo - kama itakavyokuwa kwa wasioamini), kwani sisi tumekwishatoka katika kifo na kuingia katika uzima (Yoh. 5:24; cf. 1Wakor. 11:32). Tathmini yetu itakuwa, badala yake, inahusika na ubora wa utumishi wetu wa Kikristo hapa duniani (1Wakor. 3:10-15).

4. Mchakato wa Hukumu/Tathmini Hii:

4.4  Maana sijui sababu ya kujishitaki nafsi yangu, lakini sihesabiwi haki kwa ajili hiyo; ila anihukumuye mimi ni Bwana.
4.5  Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake [kutoka] kwa Mungu.
1Wakor. 4:4-5

Tathmini ya maisha yetu ya hapa duniani itakayofanywa na Bwana wetu haitafanywa kwa viwango vya hapa duniani. Yeye anajua motisha zote zilizojificha za mioyoni mwetu; anajua, siyo tu yale yote tuliyoyafanya, na ikiwa alitutuma au alituagiza tuyafanye, bali pia ni kwa nini tuliyafanya yale tuliyoyafanya (War. 2:6-10). Hivyo, hata kama ulimwengu hauwezi kuelewa au kuona faida ya yale tunayoyafanya, kazi yetu kwa ajili ya Bwana ina maana na faida kuu (1Wakor. 15:58). Vivyo hivyo, si kila jambo litendwalo hapa duniani ati kwa ajili ya Bwana, litakuwa na thawabu. Katika 1Wakorintho 3:10-17, Paulo anaelezea jinsi/namna Bwana wetu atakavyotathmini kazi zetu za hapa duniani. Kiwango/kipimo kitakachotumika ni rahisi tu: ili kupata thawabu, chochote tunachokifanya kinapaswa kutokana na msingi wa Bwana Yesu Kristo (aya ya 11). Kwa maneno mengine, ili ziwe halali, kazi zote zinapaswa kuadilisha; ni lazima zifundishe watu kumrejea Kristo na kujenga imani, tumaini na upendo kwa wote wanaomwamini Yeye. Yote tuliyoyafanya yanayofikia kiwango hiki yana thamani halisi (ile “dhahabu, fedha na vito” vya aya ya 12); kwa uzalishaji huu halali, tutapata thawabu. Lakini kama, kwa upande mwingine, matumizi yetu ya muda na rasilimali ambazo Mungu ametupatia haviadilishi, havijengi juu ya ule msingi wa Bwana Yesu Kristo, haviongezi nguvu katika imani, tumaini na upendo wa Wakristo wenzetu, basi juhudi zetu zote katika jambo hili ni bure tu. Kazi hizi ni “miti, majani na nyasi”. Katika ile siku ya kutathminiwa kwetu, kila tulilofanya litawekwa wazi na matendo yetu yatadhihirishwa na kutathminiwa “kwa moto” (aya ya 13); kazi zetu halali zitastahimili kipimo cha moto, lakini matendo yale ambayo hayakuendeleza Injili ya Bwana wetu Yesu Kristo na maendeleo ya watakatifu wake yatachomwa moto. Je, haitii moyo kujua kwamba Bwana wetu ndiye atakayeamua thamani ya kazi zetu za Kikristo? Hakimu wetu mwaminifu ataona thamani halisi katika kila tulichofanikisha kwa ajili Yake, lakini pia mengi ya yale yanayoonekana na mwanadamu kwamba ni yenye thamani na ya kusisimua hayatastahimili kipimo cha moto.

Hata waumini watakaopoteza muda wao hapa duniani wataokolewa: kama watavumilia katika imani, japo kazi zao zitachomwa, wao wenyewe wataokolewa (aya ya 15). Hata hivyo, ni muhimu kuona hapa kwamba kuhusiana na hili, Paulo anatuonyesha kundi jingine la tatu, ukiondoa kundi la kwanza la kazi halali, na kundi la pili la kazi ambazo zinapoteza muda tu. Kama matendo ya mtu yeyote yanaenenda kwa makusudi ya kudhuru Kanisa la Mungu, mtu huyu atahukumiwa na kuangamizwa (aya ya 17). Mwisho, tunapaswa kusema kwamba kupata thawabu, mwisho wa yote, kunategemea kuendelea kwetu na imani: kama tutashindwa kuitunza imani yetu mpaka mwisho, thawabu hiyo itaangamia pamoja nasi, kwani thawabu zinaweza kupotea au kuongezeka, kama vile imani inavyoweza kupotea au kuongezeka (1Wakor. 9:24-27; 2Yoh. 1:8; Ufu. 3:11).

5. Wakati wa Hukumu/Tathmini:

Naye atawatuma malaika zake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka upande mmoja wa mbingu mpaka upande mwingine. Mathayo 24:31.

Bwana wetu atakaporudi hapa duniani katika ushindi na utukufu, sisi pia tutakusanywa pamoja kumlaki Yeye (1Wathess. 4:12; 1Wakor. 15:50-58). Wakati wa kurudi Bwana wetu mara ya pili na wa “kukusanyika pamoja naye” (2Wathess. 2:1: cf. Isa. 27:12-13), pia unaanzisha wakati wetu wa kutathminiwa na kuthawabiwa (Matt. 16:27; 19:28; 20:8; Luk. 14:14; Ufu. 11:18). Atakaporudi mara ya pii katika utukufu mkuu na kuuvamia ulimwengu wa Shetani kwa ushindi mkuu (Matt. 24:29-31; Ufu. 19:1-20:6), Bwana Yesu Kristo ataendesha tathmini kamili ya taifa la Israeli (Isa. 1:25-28; 4:2-6; Eze. 20:33-38; Zak. 13; Mal. 3:2-3; War. 11:26). Ni wakati huo pia atawatathmini waumini wote waliofufuliwa (kwa lengo la kuwapatia thawabu zao za milele kutokana na utumishi wao: War. 2:16; 1Wakor. 3:10-17; 2Wakor. 5:10). “Siku” hii ndefu “ya hukumu” itamalizika na tukio la ufufuo wa mwisho kabisa wa waumini wa mileniam (ile miaka 1,000 ya utawala wa Bwana Yesu Kristo), mwishoni mwa ile “siku ya Bwana”, (usemi unaojumuisha kurudi mara ya pili kwa Bwana wetu + mileniam kama TUKIO MOJA KUU: linganisha 2Petro 3:10 na 2Peter 3:8; tizama pia Matendo 2:20; 1Wakor. 3:13; 1Wathes. 5:2; 2Wathess. 2:2), hukumu/tathmini yao, na hukumu ya mwisho ya wasioamini mbele ya Kiti cha Enzi, Kikuu, Cheupe (Ufu. 20:11-15).

6. Uhalali wa Motisha ya Thawabu ya Milele:

11.24  Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;
11.25  akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;
11.26  akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake [kwa ajili ya] Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo [yake ya milele].
Waebrania 11:24-26 SUV

Kama Waebrania 11:26 inavyoonyesha, Musa alifanya uamuzi mgumu wa kuacha utajiri, madaraka na cheo katika tabaka la utawala la Misri, kwa kuwa aliamini kuwa atapata thawabu kuu kutoka kwa Mungu. Hivyo basi, ahadi ya thawabu ya milele ni motisha halali kwa waumini wote (Waebrania 11:39-40). Tunapovumilia mateso na mitihani hapa duniani, tunangojea kwa shauku kutimizwa kwa yote ambayo Mungu ametuahidi, na thawabu ni, kwa hakika, sehemu mojawapo ya tegemeo hilo (2Wakor. 5:1-10). Thawabu za milele zinatupa moyo wa kuimarisha imani yetu, mwelekeo wa tumaini letu, na kuenenda kwa msingi wa upendo wetu. Utumishi wote wa Kikristo unatuletea thawabu na unatusaidia kujenga imani tuliyo nayo katika uzima wetu wa milele (1Tim. 3:13), na wakati huohuo, ule ufahamu wa uhakika kwamba tutatathminiwa kwa utumishi wetu unapaswa kutufanya tuenende kwa bidii katika kuutumia wakati wetu na fursa zetu hapa duniani (1Peter. 1:17). Hivyo, japo ni kweli kwamba sisi ni “watumishi tu tunaotimiza tunachotakiwa kufanya” (Luka 17:10), tusipoteze lengo letu kuu, ile “tuzo” ambayo kwayo tumeitwa katika Bwana Yesu Kristo (Wafi. 3:7-14).

7. Umuhimu na Maana ya Thawabu:

8.18  Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama [yakilinganishwa na] utukufu ule utakaofunuliwa kwetu. Warumi 8:18 SUV.

Baraka na thawabu kwa waumini zinazidi kwa kiasi kikubwa sana magumu yote tunayolazimika kukabiliana nayo hapa duniani, kiasi kwamba Paulo, mtu ambaye katika utumishi wake alikabiliana na mateso ya kila aina, akitumia analojia ya mizani anayaita “mepesi” yanapolinganishwa katika mzani na “uzito wa utukufu” unaotokana na kupitia magumu hayo kwa ufanisi (yaani wokovu, ufufuko na thawabu). Uaminifu wetu katika yanayoonekana kuwa ni “mambo madogo madogo” hapa duniani utavuna thawabu kuu katika ufalme wa mbinguni (Luka 19:17), na upinzani tunaokabiliana nao katika majukumu yetu unasaidia kuimarisha thawabu yetu (Matt. 5:12). Kwa sababu hizi, ni muhimu kwetu kuwa na “mtazamo chanya” kuhusiana na thawabu: tupende kuthawabiwa na Mungu, na siyo wanadamu (Lk 14:14); tuelekeze tumaini letu kwenye thawabu za milele za mbinguni, na siyo kwenye furaha za kupita za kimwili za maisha ya hapa duniani (Matt. 6:20-21); tunapaswa kufanya jukumu la kumfuata Bwana wetu kuwa ni la kwanza kabisa katika maisha yetu, tukijua kuwa mwishoni tutafaidika na hilo (Lk. 18:22).

8. Viwango vya Thawabu:

15.41  Kuna fahari moja ya jua, na fahari nyingine ya mwezi, na fahari nyingine ya nyota; maana iko tofauti ya fahari hata kati ya nyota na nyota. 1Wakor. 15:41 SUV.

Wokovu ni zawadi ya bure [kutokana na hiari Yake] kutoka kwa Mungu, inayotokana na kazi Yake katika Yesu Kristo na haupatikani kwa juhudi yoyote kwa upande wetu, kama Waefeso 2:8-9 inavyodhihirisha (cf. Tito 3:5). Msitari wa 10 wa sura hiyo hiyo pia unadhihirisha kwamba, kama viumbe wapya wa Mungu, tumeumbwa upya katika Kristo “ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa ili tupate kuishi katika hayo”. Mafanikio ya “matendo mema” tunayotakiwa kuyafanya yanahusisha kujiwajibisha na kuufuatilia kwa karibu sana utendaji huo kwa upande wetu, na kiwango cha juhudi na kuzaa matunda halali kinathawabiwa kutokana na kiwango cha juhudi hiyo (Matt. 25:20-23; 1Wakor. 9:24-27). Ni katika tumaini la thawabu hizo kwa juhudi zetu tunaambiwa “tusichoke kutenda mema” (Waga. 6:9-10), kwani Mungu ni mwenye haki katika kutathmini juhudi zetu zote, ziwe kubwa au ndogo, na kutufidia kwa kiwango sambamba na stahiki (Dan. 12:3).

Fundisho la Mataji: Maandiko yanazungumzia, kwa makusudi kabisa, thawabu zetu za milele kiujumla-jumla tu, kwani sasa tunaona tu taswira hafifu ya utukufu unaokuja (1Wakor. 13:12). Moja kati ya maelezo ya wazi kabisa ya thawabu ambazo Wakristo watapata, yanatolewa kwetu katika taswira ya TAJI. Neno la Kiyunani stephanos (στέφανος, chanzo cha jina Stephen), katika uhalisia wake linamaanisha taji la maua, majani au, mara chache, dhahabu, na ni tofauti, kimsingi, na diadema (διάδημα, cf. kwa Kiingereza “diadem”) ambalo linaashiria alama ya ufalme pekee (cf. Ufu. 12:3; 13:1; 19:12). “Taji” linaloitwa stephanos lina historia ndefu sana na ya kusifika katika historia za Uyunani na Rumi, lakini kuna uzi mmoja unaounganisha matumizi yake mengi kabisa: katika mazingira ya kijeshi, riadha, sanaa au siasa, taji la stephanos hutolewa kama thawabu/tuzo kwa huduma ya mafanikio makubwa au mwenendo wa kipekee wa aina fulani katika jukumu fulani. Vivyo hivyo katika Agano Jipya, mataji yanaashiria thawabu wanazopewa waumini kwa mafanikio halali wanayopata katika utumishi wao hapa duniani. Maandiko yanatutajia mataji matatu mahususi, kila moja likiwakilisha kiwango pekee cha mafanikio hapa duniani.

1. Taji la Uadilifu au Uongofu:

Taji la Uadilifu au Uongofu linaendana na uadilifu wa imani na linatuzwa kwa Wakristo wote wanaokua kiroho hadi kufikia upevu katika Bwana Yesu Kristo, na wanaendelea na kiwango hicho kwa uimara mpaka mwisho. Katika 1Wakor. 9:25-27, Paulo analinganisha maisha ya Kikristo na mbio za riadha, na anatuambia kwamba, kama ilivyo katika riadha, si kila mmoja anatuzwa taji la ushindi. Kama ilivyo katika riadha siku hizi, washindi wa mashindano haya katika ulimwengu huo wa kale walipata sifa kubwa sana. Paulo anatukumbusha kwamba thawabu inayowakilishwa na taji la mbinguni ni ya milele, haichakai na kamwe haiwezi kulinganishwa na thawabu za kupita tu za maisha ya hapa duniani (War. 8:18). Ni muhimu kutambua hapa kwamba hata muumini mkuu wa kiwango cha Mtume Paulo hakuyaona mafanikio yake kuwa ni hakikisho kwamba wokovu wake umekwishapatikana, bali alikuwa bado ana jukumu la kuenenda kwa uadilifu mpaka mwisho. Katika aya ya 27 ya 1Wakor. sura ya 9, Paulo anaonyesha nia ya kuwataarifu waumini wengine juu ya jambo hili muhimu, pamoja na shauku ya kuendelea na mchakato wa kupevuka kiroho (kama ilivyo katika aya nyingi nyingine za maandiko, cf. Wafilipi 3:13-14). Kwani ni katika kuendelea na mchakato wa kupevuka kiroho ndipo tunajihakikishia kwamba haturudi nyuma (2Pet. 1:10). Kwa wale wote ambao “wameshinda” katika maisha haya kwa kukua katika Yesu Kristo na kuishi maisha yanayoendana na uongofu tulio nao kwa imani (1Yoh. 5:4; Ufu. 2:7; 2:11; 2:17; 2:26; 3:5; 3:12; 3:21), kwa wote ambao kwa namna hiyo “wamependa ujio wa Bwana”, katika siku ya kurudi kwake, taji la uongofu/uadilifu litakuwa ni thawabu yao na watapewa na Yule “Hakimu wa haki” Bwana Yesu Kristo (2Tim. 4:8).
2. Taji la Uhai:

Taji la uhai linaendana na uadilifu wa tumaini na hutuzwa kwa waumini wote wanaoendelea na mchakato wa kupevuka kiroho katika maisha yao ya duniani chini ya shinikizo kali, wakidhihirisha kupevuka huko katika jinsi imani yao inavyopimwa na kuboreshwa katika mitihani mbalimbali; wakishikilia tumaini [hili] katika utukufu wa milele mpaka mwisho wa maisha yao ya hapa duniani kama ambavyo Mungu amewapangia. Kwa sababu hii, muumini aliyepevuka anayatizama magumu ya maisha kwa furaha, kwani anajua kwamba mitihani ya aina hii inadhihirisha imani yake na inazaa subira imara ya tumaini linalovuka pazia la sasa la machozi na kuuona utukufu wa milee ijayo (War. 5:3-5; Yak. 1:2-5). Pamoja na uthibitisho wa tumaini hili linaloundwa katika tanuri la moto la maisha ya duniani, anapata “sifa, utukufu na heshima katika siku ya ufunuo wa Bwana Yesu Kristo” ikionyeshwa na taji la uhai (1Pet. 1:6-7). Kwa kuimarisha imani yetu na kudhihirisha tumaini letu katika wakati wa magumu, tunauonyesha ulimwengu kwamba tunampenda Bwana Yesu Kristo zaidi ya tunavyoupenda ulimwengu, na tunaahidiwa taji la uhai kama thawabu halisi (Yak. 1:12). Taji la uhai ni motisha ya nguvu kwetu ili tuvumilie magumu na majaribu yoyote ambayo Shetani anatuletea, tukijua kwamba Mungu ni mwaminifu katika kutupatia thawabu kutokana na uaminifu wetu Kwake (Ufu. 2:10).

3. Taji la Utukufu/Adhama/Fahari: Taji la utukufu linaendana na uadilifu wa upendo na linatuzwa kwa waumini wote ambao kwa uaminifu na ubora wanatimiza utumishi waliopewa katika maisha yao, na hivyo kuakisi upendo wa Mungu mpaka mwisho aliotupangia. Ni kwa sababu hii Paulo anaweza kuwaita wale anaowahudumia “mataji”, kwani wanadhihirisha uaminifu wake, upendo wake katika utumishi wake kwao na kwa Bwana na ile thawabu inayoonyeshwa (Wafi. 4:1; 1Wathess. 2:19). Katika 1Pet. 5:1-4, taji la utukufu linaahidiwa na mtume Petro kwa wachungaji [waumini] wote ambao utumishi wao unaendeshwa kwa mafanikio (taji hili halitanyimwa kwa waumini wanaotumikia katika namna nyingine - kando ya uchungaji – bali hapa linaahidiwa kwa wachungaji kwa mfano tu). Kwa milinganisho michache, Petro anatuonyesha mwenendo wa utumishi tunaopaswa kuwa nao: “si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyotaka muwe, si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumikia. Msijifanye mabwana juu ya wale walio chini ya uangalizi wenu, bali kuweni mifano kwa hilo kundi” (aya ya 2-3; cf. 1Wakor. 9:16). Si jambo la kushangaza kwa Petro kutilia mkazo suala hili, kwani kulijali kundi la Kristo, kitu ambacho watumishi wote wanatakiwa kufanya, ndilo jambo ambalo Bwana wetu alilipa kipaumbele katika fikra zake pale alipofanya mazungumzo ya mwisho, yaliyoandikwa, na Petro (Yoh. 21:15-19), na kwa kurudia kwa mkazo akamwambia Petro kwamba upendo wowote halisi Kwake Bwana Yesu unapaswa kuonyeshwa katika utumishi. Kama kweli tunampenda Bwana Yesu Kristo, basi tutautumikia Mwili Wake, Kanisa, kutokana na utumishi tuliopewa, vipaji tulivyopewa, kila mmoja wetu. Utumishi huu ndio unaodhihirisha upendo wetu, na unathawabiwa na taji la utukufu. Kama Bwana Yesu alivyotuambia katika mfano wa mtumishi mwaminifu, utumishi wa namna hii utapata thawabu kuu pale Atakaporudi (Matt. 24:45-51; Lk 12:41-48).

4. Taji la Miiba: Kutokana na mwenendo wa kisasa wa makundi yanayojiita ya Kikristo kuahidi utajiri (usitawi katika mali) katika maisha haya, hoja moja ya mwisho ni muhimu izungumzwe. Ikumbukwe kwamba Bwana wetu, baada ya kuishi maisha ya utumishi mtimilifu, utumishi ambamo mwisho wake akafa kwa ajili yetu sote, alipewa thawabu katika maisha haya na ulimwengu usio na shukrani kwa kuvikwa taji la miiba (Matt. 27:29), hili likifanywa dhidi Yake licha ya kwamba Yeye ndiye Mfalme wake anayestahili (Waebr. 2:9). Kama ambavyo tunapaswa kuungojea wakati aliopanga Mungu kwa Kristo kutwaa utawala wake halali (Ufu. 19:12), hivyo nasi, tukiwa adui wa mtawala wa sasa wa ulimwengu, Ibilisi, tusitazame thawabu za maisha haya (Zab. 17:14; cf. 1Wathess. 3:3-4). Tumaini letu linapaswa kuelekezwa kwenye urithi usioharibika kamwe ulio katika ufalme ujao ambao hautofifia (1Pet. 1:4).

Hitimisho: Kwa wale wote wanaosikiliza Neno la Mungu, wakaamini, wakajitahidi kuishi kutokana na mafundisho ya Neno hilo, kukua kiroho ndiyo matokeo yake, pamoja na maadili ya imani, matumaini na upendo. Matokeo ya upendo wa Kikristo (ambao unatiwa nguvu na imani na matumaini) ni utumishi: yaani kuwasaidia watu wengine wamwamini Kristo, wapevuke katika Yeye kama sisi wenyewe tulivyofanya. Basi na tuendelee kustahamili katika majukumu yoyote ya kiroho ambayo Mungu ametupatia hapa duniani, tukijua kwamba jukumu hili si la bure katika Yesu Kristo Bwana wetu (Waga. 6:9-10). Kwa namna hii, tutakuwa na uhakika kwamba “neema na ustawi wa kiroho” utatolewa kwa ajili yetu (kutokana na sala/ombi la Petro katika 1Pet. 1:4) ili kutusaidia sisi sote katika kazi yetu ya juhudi za upendo wa Kikristo katika kuwasaidia wengine wafanikishe mpango wa Mungu kwa maisha yao.

=0=

Translated from: Production and Eternal Rewards: Peter’s Epistles #18

=0=

Basi, na tuonane katika sehemu #19 ya mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!