Mitihani ya maisha ya Mkristo na ushuhuda wa Biblia

Ndugu yangu katika Kristo, mateso ni sehemu ya maisha ya Mkristo. Kwa upande mmoja Mungu anaruhusu ujaribiwe na kuteswa na Shetani pamoja na majeshi yake ya kibinadamu na malaika waasi ili:

1. Wewe mwenyewe uweze kujidhihirishia nguvu ya imani yako na kutiwa moyo pale unaposhinda;
2. Uweze kushuhudia kwa Wakristo wenzako nguvu ya imani yako;
3. Ushuhuda huu huonekana mbele za malaika pia, ambao wakati wote wana shauku ya kujua nini kinaendelea katika mpango wa Mungu hapa duniani;
4. Wewe kama Mkristo uweze kukua kiroho; uweze kuitumia fursa hii kuongezeka katika nguvu za kiroho na kuzidi kumtumainia Bwana kwamba atakuokoa;
5. Uweze kumpa fursa Mungu wetu ya kukuonyesha neema Zake zilizo kuu;
6. Na haya yote hukuongezea hazina ya thawabu yako huko mbinguni pindi unapofaulu mitihani yako hii.

Majaribu, magumu, mateso utakayopitia yanalingana na kiwango chako cha kukua kiroho ambacho utakuwa umefikia kwa wakati huo. Mungu wetu ni mwenye huruma sana, na kamwe hataruhusu upitie magumu ambayo huna ubavu nayo kwa wakati huo, ingawa wewe mwenyewe unaweza kuona kama vile mzigo uliopewa ni mzito sana! Kwa kiasi kikubwa, Mungu anakupa mkono wa pongezi pale anaporuhusu upitie magumu kwani anakuwa ameona umekua kiroho kwa kiasi gani katika mwendo wako na Kristo.

Waebrania 12:1-2:
12.1  Basi na sisi pia [kama waumini wanaotajwa katika sura ya 11], kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii [watu na malaika], na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi [maeneo ya tabia zetu ambamo tuna udhaifu mkubwa zaidi]; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,
12.2  tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye [ameshinda na] ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.

Kwa upande mwingine, Mungu anajua uwezo na nguvu zako zote; anakuelewa wewe hata ndani ya moyo wako. Anazijua nguvu zako; hawezi kuruhusu wewe ukabiliwe na mzigo ambao utakuzidi nguvu – uwe wa majaribu au mitihani.

1Corinthians 10:13:
10.13  Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida [katika maisha] ya wanadamu; ila [zaidi ya hapo] Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo [kustahamili]; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea [namna ya kutatua tatizo], ili mweze kustahimili [shinikizo].

In English:
No trial has come upon you which is out of the normal experience of mankind. Furthermore, God is faithful, and He will not allow you to be tested beyond your ability to endure it, but will provide with the testing a resolution to it, so that you may be able to bear up under it.
1st Corinthians 10:13
Mifano ya mateso, majaribu, mitihani, nk, kutoka katika Biblia:

Daudi:

Daudi alipakwa mafuta ili awe mfalme wa Israeli wakati mfalme Sauli akiwa bado anakalia kiti cha ufalme wa Israeli (1Sam. 15:28; 16:13). Jambo hili lilimletea mitihani mikubwa Daudi; lakini ni wazi Mungu alikuwa na makusudi yake ambayo yalikuja kudhihirika hapo baadaye katika maisha ya hawa wafalme wawili. Kwani licha ya kwamba Daudi alimfanyia kila jema aliloliomba kwake (1Sam 16:21-23), Sauli alimchukia Daudi na alitafuta kila njia ya kumwua (1Sam. 18:10-11; 19:9-17). Hata hivyo, katika hali ya hatari iliyofuata mchakato huu, Mungu alionyesha matendo yake makuu katika kumlinda mfalme Daudi na kumwokoa katika mitihani yake yote, kwa sababu Daudi alimwamini na kumtegemea Yeye (1Sam. 17:45-51). Kupitia mitihani ya Daudi, Mungu alidhihirisha uweza Wake mkuu katika kuwaokoa wale wanaomwamini na kumtumainia. Zaburi nyingi ambazo Daudi aliziandika akiwa katika Roho Mtakatifu zinadhihirisha jinsi Mungu mwenyewe alivyomwokoa Daudi kutoka katika shida, dhiki, hatari, mateso, n.k. ya aina nyingi.

Daudi alikimbilia kwa Wafilisti na wengineo katika juhudi za kuokoa maisha yake; pia alijificha nyikani na katika mapango ya jangwani na porini; lakini katika hili Mungu alifanikisha kumpatia Daudi jeshi la mashujaa (1Sam. 22:1-5) ambalo alikuja kutawala nalo pale alipochukua rasmi ufalme (mara baada ya kifo cha Sauli). Katika shida za Daudi ndipo Mungu akamtayarishia nyenzo zilizomwezesha kutawala kwa ufanisi mara baada ya kifo cha Sauli [hapo baadaye].

Mfano mwingine wa jinsi Mungu anavyowaokoa wale wanaomwamini unapatikana katika 1Samueli sura ya 30 na sehemu ya sura ya 31. Katika kumkimbia mfalme Sauli na kuokoa maisha yake, Daudi alilazimika kujiunga na Wafilisti katika vita mbalimbali walizopigana. Daudi aliihifadhi familia yake pamoja na familia za askari wake katika mji wa Siklagi. Wakati Daudi na askari wakiwa vitani mahala pengine, Waamaleki wakashambulia mji ule wa Siklagi na wakachukua mateka wake zao, watoto wao na mali zao. Watu wa Daudi walichukulia hili kuwa ni kosa la Daudi, na walitaka kumwua kwa kumpiga mawe, “lakini Daudi alijitia nguvu katika Bwana, Mungu wake” (1Sam. 30:6). Mungu alilifanyia kazi tumaini hili kuu Daudi alilolionyesha Kwake, na kuwaongoza hata kuwaokoa familia zao na mali zao na kupata mali nyingine za ziada katika ushindi mkubwa walioupata dhidi ya Waamaleki wale. Imani na tumaini la Daudi kwa Mungu wake lilimletea ushindi mkuu katika mitihani yake.

Yosefu:

Masimulizi ya Yosefu ni marefu sana katika kitabu cha Mwanzo; lakini naomba usome tu sura za Mwanzo 37 na 38, uone jinsi Yosefu alivyoteseka, akiwa mvulana mdogo sana wa miaka 17 tu! Kutupwa shimoni na ndugu zake (ili aliwe na wanyama wa mwituni); fikiria, mtoto huyu alishikwa na hofu, wasiwasi, stress kiasi gani akiwa katika shimo lile ambamo hakuweza kutoka na kujiokoa. Halafu aliuzwa na hao hao ndugu zake na kupelekwa Misri ambako mateso mengine yalikuwa yanamngojea. Kwani aligeukwa na mke wa mwajiri wake ambaye hakumfanyia kosa lolote! Akafungwa jela kwa uwongo na usaliti ule wa mke wa mwajiri wake – alisingiziwa kesi ya ubakaji. Kama Yosefu asingekuwa na imani … Lakini tunaona kwamba Yosefu alikuwa na imani na matumaini makuu kwa Mungu wake. Na kwa imani hii alishinda majaribu na mitihani hii yote.

Hapo tunaona kwamba mpango wa Mungu ni mkuu na ni vigumu kuuelewa wakati wa magumu yetu; lakini Mungu siku zote hututakia mema, na hufanyia kazi matendo yetu (na yale magumu yanayotusibu) ili yaweze kuwa mema kwa ajili yetu:

18 Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu[ni], wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako. 
19 Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu? 
20 Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo. 
21 Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema.
Mwanzo 50:18-21

Ayubu:

Kumbuka pia masimulizi maarufu sana ya Ayubu na mateso aliyoyavumilia kutoka kwa Shetani ambaye aliomba ruksa kwa Mungu ili kumtesa Ayubu, akiamini kwamba Ayubu atatelekeza imani aliyokuwa nayo kwa Mungu wake. Lakini kutoka kwa Ayubu tumeyapata maneno haya maarufu sana hapa duniani:

… Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; Jina la Bwana na lihimidiwe!
Ayubu 1:21b

Imani kuu ilioje tunaishuhudia kutoka katika mfano huu wa kuigwa wa Ayubu!

Kuna wakati tunahisi kama vile dunia nzima iko dhidi yetu. Lakini kumbuka Zaburi ya 23 (imeandikwa na Daudi!!):

ZABURI 23:
1 Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.
2 Katika malisho ya majani mabichi hunilaza [mahitaji ya kimwili], Kando ya maji ya utulivu huniongoza (maji ya ile Kweli; Isa. 55:1; Yoh. 3:5; Ufu. 22:17).
3 Hunihuisha nafsi yangu [i.e. maisha ya kimwili na kiroho]; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
4 Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.
5 Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika.
6 Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.

Na mtume Paulo, ambaye naye alipitia mateso, mitihani na magumu makuu, anatufundisha:

8.28  Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.
Warumi 8:28

Neno la Mungu ni KWELI, na linapaswa kutumainiwa. Siwezi hapa kukusimulia magumu ambayo mimi mwenyewe nimeyapitia katika maisha yangu kama Mkristo. Mara tu baada ya kuamini na kuokolewa, nilianza kupitia magumu mengi sana. Na yalikuwa magumu kweli! Hiyo ni hadithi ya siku nyingine. Nakushauri, nakusihi ndugu yangu katika Kristo, jipe moyo katika Jina la Bwana Yesu Kristo, ambalo kwalo sote tunaokolewa, hapa duniani na hata kufika mbinguni. Imani yetu Kwake ndiyo kamba inayohakikisha usalama wetu wakati wa magumu; kwa hakika tumeelekezwa kuonyesha furaha wakati wa magumu na mitihani yetu!

5.3  Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi;
5.4  na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini [la thawabu ya milele];
5.5  na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi
Warumi 5:3-5

1.3  Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;
1.4  tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.
1.5  Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.
1.6  Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu na mitihani ya namna mbalimbali;
1.7  ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo [haidumu, huisha, hufifia], ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.
1.8  Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa ha[mu]mwoni sasa, mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka, yenye [inayoonyesha] utukufu [mkuu ujao],
1Pet. 1:3-8

Njia kuu ya kupambana na mateso na magumu ya maisha yako ni kukua kiroho, kuongeza nguvu zako za kiroho. Hili linafanyikaje? Kwa kusoma Biblia yako kila siku; kwa kupata mafundisho ya Biblia kutoka kwa Mwalimu wa Biblia mwenye umahiri wa kutosha katika kufundisha Neno la Mungu; kwa kupambana na magumu yako ukitumia misingi ya Neno la Mungu unalojifunza kila siku; kwa sala na maombi; kwa kuwasaidia wengine katika magumu yao kupitia huduma yako ya Kikristo kwa Kanisa la Bwana Yesu.

Kanisa la Bwana Yesu Kristo ni lipi? Ni mkusanyiko wa watu wote ambao wameweka imani yao, tumaini lao la uzima wa milele kwa Bwana wetu Yesu Kristo, kwa kazi Yake aliyoifanya pale msalabani katika kulipia dhambi zetu zote (Yoh. 3:16;
Waefe. 2:8-9).

Nitamaliza fundisho hili fupi kwa maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo ambayo ameyasema kwa lengo la kutupatia sisi wanafunzi Wake, wafuasi Wake, tumaini, tegemeo lisilotingishika hata pale tunapokabiliwa na mazingira au jambo la kutisha namna gani. Maneno haya, Bwana wetu aliyasema kwa wanafunzi Wake katika kipindi kile cha mwishoni kabisa mwa huduma Yake hapa duniani, wakati akijua kwamba kukamatwa kwake ku-karibu. Alijua kwamba atalazimika kuwaacha wanafunzi wake peke yao, wanafunzi ambao walikwishazoea kupata ulinzi Wake katika kila mazingira ya kutisha ambayo yaliwakabili (mf. Mark 4:35-41); alijua pia kwamba Roho Mtakatifu ambaye atakuja, hatakuja mara moja, bali palikuwa bado na zaidi ya mwezi mzima mbele ndipo Msaidizi huyo angekuja, na alijua kwamba bila Yeye wataingia katika mazingira ya kutisha kwelikweli katika kipindi cha kukamatwa, kuteswa, kifo chake, n.k. Hivyo aliwapa maneno haya ili yaweza kuwatia nguvu na kuwapa matumaini; ili wajue kwamba Yeye yuko nao wakati wote, na kwamba ile kazi muhimu ya kumshinda Shetani ilikwishamalizika; kilichobakia ni wao kuwa na imani imara, basi:

Yohana 16:33:
16.33 Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo [mtapitia] dhiki [tribulation]; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu!

Mkristo mwenzangu, nakutakia mema, nakuombea mema. Nitaendelea kukuombea ili uweze kupita na kufaulu mitihani yako migumu unayoipitia kwa sababu ya imani yako; na kwa kweli nina imani kwamba kwa matumaini tuliyo nayo katika Bwana wetu, utaokolewa kutoka katika mateso, shida, magumu, mitihani yako!! Ubarikiwe sana. Amen.

Mimi ndugu yako katika Kristo,

Respicius Luciani Kilambo

https://sayuni.co.tz