Ufufuo: Nyaraka za Petro #20
Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa: https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii ya Kiswahili Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for this Kiswahili Translation has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

1.3  Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;
1.4  ili tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.
1.5  Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani ili/[hata] mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.
1Petro 1:3-5 SUV

Utangulizi: “Tumaini lenye uzima” ambamo tunazaliwa upya ni ufufuo. Mungu amepanda mbegu ya kweli ndani yetu (Matt. 13; Mrk. 4; Lk. 8), na hivyo tumezaliwa mara ya pili, si kwa mwili, bali kwa maji ya Neno la Mungu na huduma ya Roho Mtakatifu ya ujumbe huo kwetu sisi (Yoh. 3:5; 3:8; 4:10). Kwa imani yetu katika Bwana Yesu Kristo, tunao huu uzima mpya wa milele ndani yetu kwa sasa na tunaishi kwa matarajio (au tumaini) kwamba Bwana wetu atakapokuja tena, uzima huu wa milele ulio ndani yetu utasitawi na kuwa mwili mpya ambao ndani yake tutaishi tukiwa Naye milele. Tumaini hili letu ni tumaini “lenye uzima”, kwa sababu linatizama mbele kwenye uzima wa milele tukiwa katika mwili wa milele, “mwili wa ufufuo”.

Ufufuo: Fundisho la ufufuo lilikuwa na mvuto wa kipekee kwa wasomaji wa karne ya kwanza wa ule waraka wa Petro. Kama tulivyoona katika masomo yaliyotangulia, Wakristo wale walikuwa masikini na walionewa/walinyanyaswa. Katika maumivu na mateso yao (ambayo ni mada muhimu na pana/kubwa sana katika nyaraka za Petro), kulikuwa na umuhimu sana wa kuelekeza tumaini lao katika wakati ambamo hawatalazimika tena kuvumilia matatizo na magumu ya maisha haya. Yaweza kuwa sahihi kabisa kusema kuwa haiwezekani kupevuka kiroho bila kupitia kiasi fulani cha mateso na magumu. Ili kukua kiroho, ni lazima tubadilishe namna yetu ya kufikiri, iwe kama ile ya Mungu, vipaumbele vyetu viwe ni vile vipaumbele vya Mungu, na mtazamo wetu uwe ni ule mtazamo wa Mungu. Mungu anatumia mateso yetu kubadilisha mtazamo wetu katika dunia na kubadilisha mtazamo wetu juu ya matukio ya maisha yetu. Anatumia mateso ya dunia hii kutusaidia sisi ili tujifunze kumwegemea Yeye. Fundisho la kanuni ya Biblia ya ufufuo wa miili yetu ya hapa duniani ambayo itabadilishwa na kuwa miili ya kustaajabu ya milele ni moja kati ya vipaumbele ambavyo “fikra zetu mpya” zinapaswa kuelekea. Kwa macho ya tumaini, tunaweza kuiona ile siku ambapo mwili wetu mpya utakuwa kitu halisi.

Wakati mtume Paulo alipohutubia watu wa Athene katika mlima wa Areopago akitetea imani yake katika “Mungu wao asiyejulikana”, Wa-athene wale (walikuwa ni watu wenye vyeo na madaraka) walimsikiliza kwa upole mpaka pale Paulo alipowaambia kuhusu ufufuo wa Bwana Yesu Kristo (Matendo 17:22-34). Aliposema tu “ufufuo kutoka katika wafu” baadhi ya wasikilizaji wake waliacha kumsikiliza, baadhi walimdharau waziwazi, na wachache sana waliguswa katika mioyo yao, na hao ndio waliopata msukumo/shauku ya kujua zaidi katika mioyo yao. Leo hii, kama ilivyokuwa miaka 2,000 iliyopita, dhana ya kufufuka kutoka katika wafu bado inatenganisha watu, wako wanaoamini na wako wasioamini, ambao wako tayari kuishi maisha yao mbali na Mungu.

Imani katika ufufuo ni sehemu ya lazima katika imani yetu ya Kikristo, kwa sababu mhimili wa imani hii uko katika kujiamini kwetu katika wokovu kutoka katika mauti kwa ufufuo kwa kufuata mfano wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kama Paulo anavyosema, kama hakuna ufufuo, basi Kristo hakufufuliwa. Na kama Kristo hakufufuliwa, basi mafundisho yote ya maandiko ni ya uwongo na imani yetu ni batili na tupu. Zaidi ya hayo, Paulo, pamoja na mitume na mashahidi wote wa ufufuo wa Bwana wetu wataonekana kuwa ni mashuhuda wa uwongo dhidi ya Mungu, ikiwa Kristo hakufufuliwa. Kama ni kweli hakuna ufufuo kutoka mauti, basi Kristo hakufufuka, na hivyo imani yetu haina maana yoyote, kwani bado tutakuwa tunahesabiwa dhambi zetu. Wote waliokufa kabla yetu watakuwa wameangamia. Kama kweli tunaishi hapa kwa ajili ya maisha haya tu, kama hakuna uwezekano wa maisha/uzima baada ya kifo, kama tumaini letu la uzima wa milele ni la uwongo na litakufa pamoja nasi, basi sisi Wakristo ni watu wa kusikitikiwa zaidi ya wote katika maisha haya (1Wakor. 15:12-19). Tukiliweka jambo hili kwa dhahiri, ufufuo ni njia pekee tunayoweza kuitumia katika kushinda kifo, hivyo ufufuo ambao msingi wake ni imani kwake Yeye ambaye alishinda kifo ndilo lengo kuu la tumaini letu la Kikristo. Kwani tumaini letu linakaa juu ya ahadi kwamba Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanaye wa pekee, ili kwamba wale wote walio tayari kumfuata Mwanaye huyo wapate fursa ya kuwa washindi dhidi ya mauti kupitia ufufuo, kuzaliwa upya na hata uzima wa milele (Yoh. 3:16; 1Wakor. 15:54-57).

Fikra adilifu ya tumaini inaelekea moja kwa moja kwenye kesho yenye baraka ambayo imeahidiwa kwa kila anayeamini. Haijalishi [ma]jukumu na mizigo tunayobeba ni mizito na inachosha kiasi gani, tunaweza kuelekeza macho yetu kwa kujiamini kuelekea kwenye “tumaini lenye baraka” na la furaha na faraja/tulizo litakaloambatana na “ufunuo uliotukuka” wa Bwana Yesu Kristo (Tito 2:13). Sehemu ya tumaini hili ni matazamio ya ushindi dhidi ya uovu, na maajabu ya Ufalme wa Mbinguni ambao Bwana wetu atauasisi pale atakaporudi; lakini sehemu nyingine kubwa ya tumaini inayotajwa na Tito ni matazamio ya kuupokea mwili uliotukuka, usioharibika, na tukiwa na mwili huo, tutaishi na Bwana wetu milele. Ni kwa sababu hii tunayachukulia mambo yote ya kidunia kuwa yana thamani ndogo sana yakilinganishwa na kupata ufufuo (2Pet. 1:8-11), kwamba tunafanya bidii ya kuboresha/kutimilisha mwendo wetu wa maadili ya Kikristo ili tuingie katika Ufalme bila kujikwaa (2Pet. 1:8-11), na kwamba tunaweka fikra zetu katika mambo ya mbinguni, tukitazamia mabadiliko ya miili yetu duni ya sasa na kwenda kwenye uhalisia wa uraia wetu halisi ambao ni wa Mbinguni na si wa duniani (Wafi. 3:15-21).

Hulka/Asili ya Ufufuo:

1. Ufufuo ni sehemu muhimu ya hadhi yetu ya baadaye: Bila ya ufufuo, uzima wa milele hautowezekana, kwani “mwili na damu haviwezi kuurithi uzima wa milele” (1Wakor. 15:50). Tunaishi maisha yetu hapa duniani tukiwa na miili hii ya nyama, lakini uraia wetu halisi ni wa mbinguni (Wafi. 3:20-21), na tunajiamini kwamba kama tulivyo sasa na umbile hili la kidunia (kama ilivyokuwa kwa Bwana wetu), siku moja tutakuwa na umbile la mbinguni kama la Bwana wetu Yesu Kristo Mfufuka (1Wakor. 15:49).

2. Ufufuo unapaswa kutofautishwa na matokeo ya kurejeshewa pumzi na fahamu [tu] (resuscitation): Ni muhimu kuelewa kwamba neno ufufuo linamaanisha hali ya kudumu, ya milele, na siyo kurudi kwa muda kwa huu mwili wetu tulio nao sasa. Pale Kristo alipomfufua Lazaro kutoka mauti, alirudi kwa muda tu, na Martha alisema kweli kabisa alipozungumza kwamba “ufufuo” wa mwisho wa kaka yake unapaswa kuingojea “siku ya mwisho”. Lakini Mungu Baba aliuthibitisha utumishi wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa namna kadhaa, mojawapo ikiwa ni kufufua wafu (Matt. 11:5; Lk. 7:22), na watu wote walioamshwa kutoka mauti na Bwana wetu bado wanaingojea miili yao ya ufufuo (Lk. 7:11-17; 8:40-42), [kwani kwa uhakika watu hawa wote walikufa baadaye hapa duniani kwa sababu nyingine za kiasili]. Papo hapo, tunaweza kuona kuzinduliwa kwa Lazaro kukitimiza moja kati ya malengo yake katika Injili ya Yohana, kwani tunasoma kwamba kuenea kwa habari za mwujiza ule kulikuwa ndiyo chanzo cha makundi makubwa ya watu kumlaki Bwana wetu siku ile ya Jumapili ya Matawi (Yoh. 12:17-18). Mwujiza uliofanana na huo ni ule ufufuo [wa muda] wa waumini waliokufa mara kabla ya kusulibiwa Bwana wetu; kwa kuwarejeshea uhai kwa muda tu, Mungu alithibitisha mbele za watu wote mafao ya kazi ya Mwana wake msalabani kwa ajili yetu sote (Matt. 27:52-53).

3. Ufufuo unapaswa kutofautishwa na mabadiliko-bila-kifo (transmutation): Idadi ndogo ya waumini walimaliza uhai wao hapa duniani katika namna isiyo ya kawaida kabisa. Enoki, Musa na Eliya ni mifano ya waumini ambao “walibadilishwa”, yaani miili yao haikufariki. Watu hawa waliingizwa katika milele/mbingu bila ya kufa. Katika mifano ya Musa na Eliya (japo namna ya kubadilika kwao ni tofauti), sababu ya kubadilishwa kwao yaweza kuwa ni ili waweze kurudi na kutoa “huduma au utumishi zaidi” katika wakati wa dhiki kuu (Ufu. 11:1-13). Hata hivyo, licha “kuondoka kwao” kusiko kwa kawaida, Enoki, Musa na Elia bado wanaingojea miili yao ya ufufuo kama ilivyo kwa waumini wengine waliofariki.

4. Ufufuo unapaswa kutofautishwa na hali/miili ya mpito: Katika Ufunuo sura ya saba, mara baada ya kusimikwa kwa wale 144,000, Mtume Yohana anatusimulia kwamba aliona “umati mkubwa wa watu, ambao hakuna yeyote awezaye kuwahesabu, kutoka katika kila taifa, kila jamaa na kila lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele ya Mwana Kondoo, wakiwa wamevaa mavazi meupe na wameshika matawi ya mitende mikononi mwao” (Ufu.7:9-17). Aliposhindwa kumjibu malaika aliyemwuliza baadaye kuwa hao watu ni nani[?], Yohana aliambiwa kwamba “hao ni wale waliotoka katika ile dhiki kuu – great tribulation” (aya ya 14). Hawa ni waumini waliotangulia, waliovaa mavazi meupe, wanatambulika kuwa ni wanadamu, na hata wanaimba wimbo wa utukufu wa Mungu (aya ya 10). Yote haya licha ya ukweli kwamba hawamo tena ndani ya miili yao waliyozaliwa nayo [hapa duniani], wala hawajaingia [bado] “katika miili yao ya ufufuo” (kwani kwa wakati huu ufufuo haujatokea bado kwani ni Bwana Yesu pekee aliyefufuka mpaka sasa kutoka katika mwili wake wa kibinafamu). Hii inatuonyesha kwamba, baada ya kifo cha mwili huu, kuna mwili wa mpito ambao ni bora zaidi ya huu tulio nao [kwani utakuwa na maskani yake mbinguni], lakini si zaidi ya ule wa utukufu ambao utakuwa wetu katika ufufuo. Aya zingine za maandiko zinaunga mkono hoja hii, kwa mfano mazungumzo mafupi kati ya nabii Samweli (aliyekwisha kufa wakati huo) na mfalme Sauli (1Samweli 28:13-19), kutokea kwa Musa na Eliya katika ule mlima alikogeuka sura ([alikogeuka] mwonekano mzima) Bwana wetu (Lk. 9:28-36), na, mfano wenye mvuto sana, lile fundisho-fumbo la Lazaro na tajiri wakiwa Paradiso – Abraham’s Bosom - (Lk. 16:19-31). Katika mfano huu wa mwisho, Bwana wetu Yesu Kristo anatupa maelezo mengi kuhusu mwili huu wa mpito, makazi yake na hali yake, kama ilivyokuwa kabla ya Bwana wetu kupaa mbinguni. Lazaro, yule tajiri na Abrahamu, wote wanatambulika [kama walivyo], na (ukitoa uwepo wao katika milele), hawatofautiani na watu walio hai. Ni wazi, tunachoweza kufahamu kuhusu hali yetu ya mpito [katika milele] mbinguni [baada ya kifo na kabla ya ufufuo], kunatokana na fununu chache tunazoweza kuzipata katika maandiko, lakini, kama mfano wa hapo juu unavyoonyesha, itakuwa ni kosa kubwa kufikiria kwamba utu wetu au hata umbo letu la kibinadamu litabadilika kwa kiasi kikubwa. Tunategemea hali hii ya mpito (na ile ya mwisho ya ufufuo) kuwa nzuri zaidi kwa kiasi ambacho kwa sasa hatuwezi kujua, na kuliko hali ya sasa, bila ya kubadilisha utu wetu kimsingi (mbali na kutokuwako na dhambi, hali ambayo sote tutakubaliana, ni ya kuipokea kwa mikono miwili!).

5. Ufufuo ni kweli: Maswali kuhusu hulka na uhalisia wa ufufuo hayako siku hizi tu. Licha ya mafundisho ya Agano la Kale (yakishuhudiwa na Danieli 12:2), msisitizo wa wazi wa Bwana wetu juu ya somo hili (cf. Yoh. 5:28-29), na uelewa wa wale waliokuwa makini na mafundisho Yake (Yoh. 11:23-24), wakati wa [mwanzo wa] Agano Jipya ufufuo ulikuwa ni suala la kutilia shaka kati ya wale waliojiona wasomi na wenye ufahamu mkuu juu ya mambo. Wakati akijitetea mbele ya mfalme Agrippa, mtume Paulo alimfanya mfalme (Agrippa) asikie haya/soni kwa kumbana ili akabiliane uso kwa uso na suala la ufufuo. Akitupilia mbali desturi za vizazi na vizazi, Paulo aliweka wazi kwamba kiini na mwelekeo wa kumwabudu Mungu ni matarajio ya ufufuo, ambalo ndilo tumaini halisi lililo msingi wa imani ya Kiyahudi (cf. Matendo 24:14-15):

26.6 Na sasa ninasimama hapa nihukumiwe kwa ajili ya tumaini la ahadi baba zetu waliyopewa na Mungu,
26.7 ambayo kabila zetu kumi na mbili wanataraji kuifikia, wakimwabudu Mungu kwa bidii mchana na usiku. Nami ninashitakiwa na Wayahudi kwa ajili ya tumaini hilo, Ee Mfalme.
26.8 Kwa nini limedhaniwa kwenu kuwa ni neno lisilosadikika, kwamba Mungu awafufua wafu?
Matendo ya Mitume 26:6-8 SUV.

[Ama] kwa hakika, watu wa kizazi kile cha wakati wa Kristo mara nyingi walikuwa wanakanganyikiwa kuhusu ufufuo na hulka ya ufufuo kama ilivyo kwa Wakristo wengi wa leo. Dhehebu mojawapo kubwa la wakati huo, Masadukayo, walikataa uwepo/uhalisia wa ufufuo (Matt. 22:23-33). Hata wanafunzi wake Bwana Yesu walikuwa gizani kwa kiasi kikubwa kuhusiana na suala hili, kama tunavyosoma katika mdahalo wao juu ya “maana ya huu ufufuo kutoka katika wafu” (Mk. 9:10). Maswali kuhusu ufufuo aghalabu huulizwa kuhusiana na wakati wa tukio hilo na/au hulka ya mwili wa ufufuo.

Mwili wa Ufufuo:

Hulka ya mwanzo, hulka ya mpito na hulka mwisho ya mwanadamu siku zote ni ile ile katika maana moja muhimu. Mwanadamu ni kiumbe wa kimwili na kiroho. Tangu Mungu “alipomuumba mtu kutoka katika mavumbi ya ardhi na kumpulizia pumzi ya uhai”, kila “mtu aliye hai” amekuwa na hulka hii yenye taswira mbili (Mwa. 2:7; cf. Mwa. 5:1-3). Katika maisha ya sasa ya hapa duniani, mwili umetoka katika mavumbi ya ardhini, lakini tunatazamia ile siku tutakapofanywa tuwe kama Bwana wetu, tutakapokuwa na mwili [usio na asili ya dhambi] unaooana na hulka yetu ya kiroho badala ya hii hulka ya uharibifu, ya kimwili tuliyo nayo sasa (1Wakor. 15:44-49). Wanadamu tumeumbwa na Mungu ili tuwe na muungano wa mwili na roho, na katika kila awamu ya mpango wa Mungu, hivyo ndivyo tulivyo. Katika awamu hii, mwili wetu ni dhaifu, ulioharibika katika hulka yake, kwa dhambi. Dhambi iliyomo katika miili yetu (War. 7:18-20), inaendelea kuwa na ushawishi ulioenea mwili mzima na wenye uchochezi juu ya nafsi zetu siku zote za maisha yetu haya, lakini roho zetu hazina doa la aina yoyote ya dhambi, na, ikiwa tunaweka imani yetu katika Mwana wa Mungu katika maisha ya awamu hii, tutaishi bila dhambi hapo milele (katika awamu fupi ya mpito na ile ya ufufuo). Hivyo kifo ni upotovu/mkengeuko/kasoro ambayo imetokana na dhambi ya Adamu na kusambazwa kupitia uzazi wa kimwili kwa wanadamu wote (Mwa. 2:16-17; 3:19; War. 2:12-21; 1Wakor. 15:21-22). Matokeo ya hali yetu ya dhambi na udhaifu wa miili yetu ya sasa ni kwamba hatuwezi kuishi kwa muda mrefu katika miili hii ya kifo. Lakini kifo cha miili hii ya sasa hakiathiri roho zetu, na roho zetu “zitavalishwa” mwili mwingine (kwanza wa mpito, ukifuatiwa na ule wa ufufuo) mara baada ya kifo cha mwili tulio nao sasa. Hivyo basi, suala muhimu kwa wanadamu siyo kifo, bali ni wapi tutaishi milele, na iwapo kuzaliwa upya (kiroho) kutaangamiza kifo katika maisha mapya ya milele (kupitia imani katika Kristo), au kuondoka kutoka maisha ya sasa kutafuatiwa na kifo cha pili (kutokana na kumkataa Kristo):

… mwanadamu alivyowekewa kufa [kimwili] mara moja tu na baada ya hapo anakabiliwa na hukumu. Waebr. 9:27

Kama tulivyosema, hakuna maelezo mengi katika maandiko kuhusu hali na mwili wa mpito, hali ambayo kizazi cha mwisho cha waumini hawatakutwa nayo, kwani wataenda moja kwa moja kutoka maisha haya mpaka uzima wa milele (japokuwa waumini wa mwanzo kabisa wamekuwa katika hali hii ya mpito kwa maelfu ya miaka sasa). Hata hivyo, tunajua kwamba hali ya mpito itakuwa na mwili wa mpito pamoja na roho yetu, na, la muhimu sana, mwili huu utatambulika kama tunavyotambulika sasa, siyo tu kwa kuonekana, bali kwa nafsi yetu pia (Lk. 16:19-31; 1Sam. 28:13-19; Ufu. 6:9; 7:9-17; 11:1-13).

Maandiko yanazungumzia zaidi ule mwili wa mwisho, wa milele, wa ufufuo, na tunapewa mafundisho ya uhakika katika Biblia kuhusu haya yaliyozungumzwa hapo juu. Tunaahidiwa kwa neno la uhakika kabisa katika 2Wakor. 5:1-3 kwamba hili “hema” la sasa likiharibiwa, roho zetu hazitatembea ovyo zikiwa uchi, bali zitapata makazi katika “nyumba ya milele”, na siyo gamba la dunia, bali la mbinguni ambalo limetayarishwa kwa ajili yetu na Mungu. Kwa Paulo, hili lilikuwa fundisho la kutia moyo sana. Kutokana na habari/fununu nyingi ambazo Paulo anazitoa kuhusu ufufuo, ebu tutumie wakati huu kutizama aya ambazo zina habari zinazotuelezea kwa undani kabisa kuhusu ufufuo:

15.35  Lakini labda mtu atasema, Wafufuliwaje wafu? Nao huja kwa mwili gani?
15.36  Ewe mpumbavu [Ebu tumia akili za kawaida tu]! [Mbegu] uipandayo haihuiki [haimei], isipokufa;
15.37  nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe (mbegu) tupu, ikiwa ni ya ngano au nyingineyo;
15.38  lakini Mungu huipa mwili kama apendavyo, na [huipa] kila mbegu mwili wake.
15.39  Nyama yote si nyama moja; ila nyingine ni ya wanadamu, nyingine ya hayawani, nyingine ya ndege, nyingine ya samaki.
15.40  Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali [tofauti], na fahari yake ile ya duniani ni mbali [tofauti].
15.41  Kuna fahari moja ya jua, na fahari nyingine ya mwezi, na fahari nyingine ya nyota; maana iko tofauti ya fahari hata kati ya nyota na nyota.
1Wakor. 15:35-41 SUV

Analojia ya Paulo ya mbegu inayopandwa inasaidia sana kuuelezea mwili wa ufufuo ni mwili gani kwa kuutofautisha na mwili wetu wa sasa. Ili mwili mpya “uchipue au umee”, ule mwili wa zamani ni lazima “upandwe” au ufukiwe ardhini, hivyo kwamba kifo chetu kama Wakristo siyo mwisho wa tumaini, bali ni takwa la lazima kutoka kwenye hali yetu ya udhaifu ya sasa kuelekea kwenye makazi yaliyotukuka, yasiyoharibika, ya mbinguni. Zaidi ya hapo, kama vile mmea unaochipua unahusiana na ile mbegu iliyopandwa na wakati huohuo ni tofauti sana na mbegu hiyo, vivyo hivyo mwili wetu wa mbinguni utakuwa unafanana na mwili wetu wa sasa, lakini pia utakuwa tofauti sana na huu mwili wa sasa. Jambo hili liko wazi kwa kutumia akili ya kawaida tu, kwani miili yetu ya sasa ina mapungufu makubwa katika urefu wa uhai wake, lakini miili yetu ya ufufuo [ya kiroho] itaweza kuishi milele. Zaidi ya hayo, upeo wa “utukufu” au ufahari wa miili hii utatofautiana (kutokana na tofauti ya thawabu), kama vile sayari zinavyotofautiana katika kiwango cha mng’ao.

15.42  Kadhalika na [ufufuo wa wafu] kiyama ya watu. [Mwii wetu] Hupandwa katika uharibifu; [na mwilli mpya] hufufuliwa katika kutokuharibika;
15.43  hupandwa katika aibu; hufufuliwa katika fahari [utukufu]; hupandwa katika udhaifu; hufufuliwa katika nguvu;
15.44  hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa roho. Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko.
15.45  Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho, Kristo, ni roho yenye kuhuisha.
15.46  Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho.
15.47  Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni.
15.48  Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni.
15.49  Na kama tulivyoichukua sura yake [mfano wake] yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake [mfano wake] yeye aliye wa mbinguni. 1Wakor. 15:42-49 SUV

Hivyo, mwili wetu mpya hautakuwa wa uharibifu: badala ya kukaliwa na dhambi, utakuwa hauna doa, wenye utakaso, na mng’avu; badala ya kuzongwa na udhaifu na magonjwa, utakuwa wenye nguvu na uwezo mkubwa; kwa kifupi, mwili huo, badala ya kufaa kwa maisha ya kimwili tunayoishi hapa duniani, utakuwa kwa namna zote unafaa kuishi maisha ya kiroho tutakayokuwa tunaishi hapo milele. Zaidi ya hapo, ni jambo la uhakika kwamba tutafanikiwa kuwa na mwili huu wa kiroho, na Kristo amehalalisha ule mpangilio wake kwa ajili yetu: kwanza mwili wa duniani, halafu mwili wa kiroho. Aya hii ya 2 kutoka 1Wakor. 15 inaweka wazi kwamba mwili huu wa kiroho tutakaoupokea utakuwa katika mfano wa mwili wa Kristo [aliokuwa nao] baada ya ufufuo kama vile mwili wetu wa sasa ulivyo katika mfano wa mwili wa baba yetu Adamu. Hivyo basi, hulka ya mwili wa ufufuo inaweza kueleweka tu kwa kujifunza zile aya zinazosimulia ufufuo wa Kristo na matukio yaliyofuata hadi kupaa kwake, kwani “atakapokuja tena, tutakuwa kama Yeye” (1Yoh. 3:2).

Maandiko yanayozungumzia muonekano wa Bwana wetu baada ya ufufuko na kabla ya utukufu wake, na kupaa mbinguni, yanapatikana katika Matt. 28, Marko 16, Lk. 24, Yoh. 20-21, na Matendo 1:6-11. Tunaweza kuandika muhtasari wa baadhi ya dondoo za wazi zinazohusiana na tabia na uwezo wa mwili wake mpya (na hivyo miili ile mipya tutakayopewa sisi) kama ifuatavyo:

1. Mwili wa ufufuo wa Kristo unatambulika kwa namna zote kwamba ni mwili halisi wa binadamu:
a. Unashikika, unaonekana (Matt. 28:9; Lk. 24:39; Yoh. 20:17; 20:27).
b. Anatambulika kuwa ni [wa] mtu (Lk. 24:31; Yoh. 20:16; 20:20; 20:26-28; 21:12).

2. Mwili wake wa ufufuo uliweza kutimiza matendo ya kawaida ya kibinadamu:
a. Alisema, aliongea (Matt. 28:10; 28:18-20).
b. Alitembea (Lk. 24:15).
c. Alikula (Lk. 24:43; Yoh. 21:13-15).

3. Katika mwili wake wa ufufuo, Kristo ana uwezo wa kuonekana na kutoonekana ghafla, anavyotaka:
a. Kutokea ghafla (Lk. 24:36).
b. Kutoweka ghafla (Lk. 24:31).

4. Katika mwili wake wa ufufuo, Kristo aliweza kusafiri kwa mwendo wa haraka sana, na pia kupita vizingiti visivyopitika kwa kawaida:
a. Kristo alitoka kaburini kabla malaika hajaondoa jiwe (Matt. 28:1-3).
b. Aliingia ndani ya chumba bila kufungua milango (Yoh. 20:19).
c. Alipaa mbinguni (Matendo 1:9-10).

Tunatarajia kikamilifu, sisi wenyewe na wale tuwapendao, walioondoka katika Kristo na walioko, kwamba tutapokea mwili kama wa Kristo katika ufufuo wetu. Kitu muhimu cha kukumbuka ni kwamba, nyingi kati ya aya zinazohusiana na Kristo baada ya ufufuo wake zinamwonyesha jinsi alivyo kabla ya kupaa mbinguni, kabla hajakaa katika mkono wa kuume wa Baba na kabla ya kutukuzwa kwake, hivyo kwamba japokuwa mwili aliokuwa nao katika ufufuo ni ule ule kabla na baada ya matukio haya, mwonekano wake ni tofauti kabisa baada ya kutukuzwa kwake (Ufu. 1:12-16; Matendo 9:1-6; 22:6-11; 26:12-18). Kwa namna hiyo hiyo, tunaweza kutarajia miili yetu ya ufufuo itakuwa na utukufu huo huo (1Wakor. 15:43).

Hivyo, baada ya ufufuo, miili yetu mipya itaendelea kufanana na hii ya sasa katika nyanja kadhaa muhimu, isipokuwa itakuwa bora zaidi katika namna ambazo tunaweza kufikiria tu kwa sasa. Tutakuwa watu walewale, bali hatutakuwa na dhambi, na hatutakuwa na tabia nyingi hasi zinazotuathiri katika maisha yetu ya sasa (Ufu. 21:3-4).

Ufufuo ndiyo hali ya mwisho ya wanadamu wote. Hata wale wasio waongofu, yaani wale wanaomkataa Kristo hapa duniani watafufuliwa pia (bali ufufuo wao unawapeleka kwenye hukumu na laana: Ufu. 20:11-15; cf. Dan. 12:2; Matt. 25:31-46;). Muungano wa roho-mwili ni wa milele. Kifo ni kasoro, hukumu iliyotokana na dhambi ya wazazi wetu wa mwanzo. Kama waumini, tunatarajia milele yenye amani na raha, [ikitanguliwa na] hali ya mpito kabla ya hapo (2Wakor. 5:1-10; Ufu. 6:9), ikifuatiwa na mwili mkamilifu wa milele katika mfano wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Wakati wa Ufufuo: Ufufuo ni kudura/majaliwa ya kila mwanadamu. Hivyo, ufufuo unatokea katika makundi mawili tofauti: ufufuo wa wasio waongofu na ufufuo wa walio waongofu (Dan. 12:2; Waebr. 9:27).

1. Wasio waongofu: Ufufuo wa wale wasiookolewa unafanyika mwisho wa historia ya wanadamu kabla tu ya tathmini yao mbele ya “kiti kikuu cheupe cha enzi” (Ufu. 20:11-15). Hivyo ufufuo huu ni sehemu mahususi ya kuwashughulikia wale waliomkataa Kristo katika maisha yao, na hivyo ni sehemu kuhimu ya Injili (Matt. 17:31; 24:25).

2. Kutokana na 1Wakor. 15:20-28, ufufuo wa waumini unafanyika katika hatua au awamu tatu, “Kristo tunda la kwanza, halafu wale walio wa Kristo atakapokuja, na mwisho atakapomkabidhi Mungu Baba ufalme”. Ufufuo wa Kristo ni tukio la kihistoria, limekwisha tokea. Awamu zile mbili zilizobaki za ufufuo zinatuhusu hapa:

a. “Wale walio wake Kristo siku ile atakaporudi”: Hii, awamu ya pili, inatukia pale Kristo anapokuja mara ya pili (1Wathess. 4:15ff). Waumini wote waliotangulia kwa Bwana na wale watakaokuwa hai wakati ule Kristo anarudi kuuchukua ufalme wake ujao wa miaka 1,000.

b. “Halafu ule mwisho”: Mwisho wa utawala wa mileniamu (miaka 1,000) wa Kristo, Bwana wetu “ataukabidhi” ufalme kwa Baba yetu (1Wakor. 15:24), na “mauti yatamezwa na ushindi” (1Wakor. 15:53-57).

Hitimisho: Kama waumini, tunatarajia, kwa tumaini la uhakika na matazamio kwa ile siku ambapo, kama Bwana wetu, nasi tutaishi katika/na ule mwili mpya wenye nguvu, uwezo, utukufu ambamo milele tutakaa na Mungu wetu. Maisha ya sasa yanaweza kutupa simanzi, lakini ufufuo utazidi na kuvuka mipaka ya ubunifu wa mioyo yetu. Hakuna hata sehemu moja ya utu wetu itakayofutika (ukiondoa dhambi ambayo itakoma). Ufufuo hautapunguza chochote kutoka katika mazuri ya maisha haya (japo “mazuri” hayo mengine yanatia shaka!), bali utayaongeza, utayazidisha kwa kiasi tusichokijua sasa, mabadiliko ya hali duni tuliyo nayo sasa kwenda katika hali ng’avu, ya kumeremeta, adhimu, tukufu, bora sana ya baadaye itakayodumu milele. Ulimwengu unatuambia kwamba tunangojea kaburi tu, bali sisi tunajua kwa kujiamini katika imani yetu kusikotetereka kwamba kama vile kaburi lilivyoshindwa kumzuia Yeye, vivyo hivyo litashindwa kutushikilia sisi; tutapata ushindi dhidi ya kaburi, dhidi ya kifo, kwa nguvu na sadaka ya Bwana wetu Yesu Kristo, tutakuwa na milele ya raha isiyokwisha Naye, katika mwili mpya, mwili wa ufufuo, ambao hautaharibika. Hivyo, ufufuo kiukweli ni “tumaini lenye uzima” analolizungumzia Petro na ambalo sisi Wakristo tunalikumbatia: tegemeo, tazamio la uhakika kwa njia ya imani yetu, na la kuishi milele kupitia ufufuo wa miili yetu; tazamio, tumaini lenye nguvu, kwamba uzima wa milele ulio ndani yetu kutokana na kuzaliwa upya, siku ile kuu ya ujio wake itamea, itachipua, itasitawi na kuwa uhai mpya, uwepo halisi wa uzima wa milele tukiwa uso kwa uso na Mwokozi wetu na Bwana wetu Yesu Kristo.

=0=

Translated From: The Resurrection: Peter’s Epistles #20

=0=

Basi, na tuonane katika sehemu #21 ya mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amen!