Nyaraka za Petro #24: Kujifunza Nguvu Zinazoendesha Imani
Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa: https://ichthys.com
Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo
Ruksa ya Tafsiri Hii ya Kiswahili Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for this Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill
Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga (ni nyembamba), iendayo kwenye uzima, nao waionayo ni wachache [mno].
Mathayo 7:14 SUV
1Petro 1:8-9:
[… hapo Bwana Yesu Kristo atakaporudi kwa utukufu.] Ijapokuwa hamjamwona, mnampenda tu. Ijapokuwa hamwezi kumwona kwa wakati huu, mna imani juu Yake. Kwa sababu hii mna furaha ambayo hamwezi hata kuieleza, ambayo inaonyesha ile milele ijayo yenye utukufu, pale mtakapokabidhiwa ule ushindi mkuu wa siku ya mwisho – wokovu wa maisha yenu – ambao ndiyo lengo na nia ya imani yenu hii.
Utangulizi: Tunakaribia kumaliza fundisho la maneno ya sifa ya utangulizi wa waraka wa kwanza wa Petro, yaani maneno ya kutoka moyoni mwake, ya sifa kwa Mungu Baba kwa neema zake zenye taswira nyingi anazompatia kila mmoja wetu. Tunavyofanya hivyo, suala linaloshika akili zetu mwishoni mwa aya ya 9 ni lile la ustahamilivu wa imani ya Mkristo akiwa katikati ya mitihani ya maisha. Mjadala wa Petro wa lile tumaini la uzima, matarajio ya ufufuo wa miili yetu na baraka zisizo kifani za milele ijayo, yanatokana na tathmini halisi ya maisha yetu kama tunavyoyajua hapa na kwa wakati huu: katika wakati wake hapa duniani, maisha ya Mkristo ni ya dhiki, taabu na mateso. Kwa hakika, kama waumini wa Bwana Yesu Kristo, tuna miadi ya kukabiliana na upinzani mkali kutoka kwa Shetani kiasi kwamba mafanikio ya ushindi wetu wa mwisho – kumaliza uhai wa sasa tukingali na imani yetu – yanaelezwa na Petro katika lugha ya shangwe: wokovu ni “tuzo ya ushindi” (kwa Kiyunani komizo: kuondoka na tuzo ya ushindi, kupata thawabu kutokana na juhudi; cf. Kama Petro anavyolitumia neno hili katika 1Pet. 5:4, na Paulo katika 2Wakor. 5:10; Waefe. 6:8). Zaidi ya hapo, wokovu huu wa siku ya mwisho ndilo lengo kuu la imani yetu, kwa sababu katika kufanikisha hili, tunakuwa salama, “tunaokolewa” katika namna ambayo haiwezi kubadilika kamwe. Hata hivyo, mpaka hapo tutakapoupata ushindi huu wa mwisho, tutakuwamo na tutaendelea kuwamo katikati ya vita kali inayohusu uzima wetu [wa milele].
Vita ya Imani: Katika kila taswira yake, thawabu yetu kwa imani yetu kwa Bwana Yesu Kristo ni kuu mno licha ya ukinzani wa Shetani na wafuasi wake wanaofanya juhudi kuu ili tushindwe. Tunatazamia kwa uhakika kuelekea maisha mapya, mwili mpya, na baraka zote za mbingu mpya na nchi mpya inayokuja. Hili ni tumani letu! Lakini bila ya imani binafsi endelevu katika Bwana Yesu Kristo, tumaini hili halitazaa chochote.
Madai ambayo mara nyingi yanasikika katika duru za kiinjilisti kwamba kusitirika na kustahamili kwa imani yetu ni “automatic”, kwamba imani yetu itaendelea, itasitawi bila [kujali] juhudia za kuitunza na kuiendeleza, si sahihi – kwa masikitiko makubwa sana. Mtazamo wa kimapokeo wa Ki-kalvinisti kwamba, kwa lugha rahisi, wale wanaoshindwa katika imani yao [basi] hawakuwa waumini halisi tangu hapo mwanzo nao pia si sahihi. Hapo nyuma tulipata fursa ya kujifunza kwa undani lile fundisho-fumbo la mpanzi (tizama Petro #12, #16, #18; Matt. 13:1-23; Marko 4:1-20; Lk. 8:4-15). Katika mjadala ule, itakumbukwa, mbegu ya Neno la Mungu iliangukia katika aina 4 za udongo: mgumu, wenye miamba, wenye magugu na miiba, na ule wenye rutuba. Hapa tutazungumzia mahususi ule mfano wa udongo wenye mawe/miamba, kwani aina hii ya udongo inawakilisha wale watu ambao mwanzoni wanakiri imani, lakini baadaye wanaanguka chini kwa sababu ya shinikizo – liwe la magumu au la utafutaji wa maisha na starehe za duniani. Imani kama hii haitoshi kufanikisha wokovu, kwa sababu mtu huyu “hakustahamili mpaka mwisho” (Matt. 24:13); maana yake, ingawa watu wa aina hii walimwamini Kristo wakati fulani, ulifika wakati mwingine imani yao ilipotea – wakarudi kwenye hali yao ya kutoamini.
Hakuna jambo linalopaswa kushika moyo na akili yetu katika maisha ya Kikristo zaidi ya jambo hili. Kwani bila imani kwa Kristo, tunapotea, na ile mithali inakuwa kweli, “mwisho unakuwa mbaya kuliko mwanzo wake” (2Pet. 2:20-22). Kabla ya kulichambua kwa undani suala la kupoteza imani kwa Kristo, tunahitaji kwanza kuweka wazi maana ya kumwamini Kristo kwa ajili ya wokovu wetu.
Namna ya Kuwa Muumini: Kila mmoja wetu anafikishwa uso kwa uso na uhalisia na uwezo mkubwa wa Mungu katika wakati fulani wa maisha yake (War. 1:18-23; Mhu. 3:11). Kuitambua hali yetu ya dhambi na hatia inayoambatana na utambuzi huo tutakaposimama mbele za huyu Mungu mweza yote pia humtokea kila mwanadamu (War. 2:14-16; Waebr. 9:27). Hii ndiyo maana moja kati ya mambo ya kustaajabisha sana kuhusu zawadi hii ya bure kabisa kutoka kwa Mungu, yaani wokovu kupitia Mwanaye Yesu Kristo, ni kwamba wengi hawako tayari kuipokea. Waweza kufikiri kwamba ikiwa uhakika wa kifo cha mwili si sababu tosha au motisha ya kutosha ya kutuonyesha uhitaji wetu wa Mwokozi, basi angalau tumaini lakuokolewa kutoka kwa mkono wa Mungu atakayetaka haki itimizwe itakuwa motisha ya kutosha:
10.26 Maana, kama tukifanya dhambi kusudi [kwa kiburi] baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi [hizi];
10.27 bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wa[m]pingao [Bwana].
Waebr. 10:26-27 SUV.
Pamoja na ahadi ya Injili, ni ile habari njema kwamba tumewekwa huru kutokana na dhambi zetu kwa kifo cha Kristo alichokufa kwa ajili yetu, na hivyo, kwa kutumainia kazi Yake na siyo kazi yetu, tutaepuka hukumu ya siku za mwisho ambayo [bila imani kwa Kristo] ndiyo majaliwa (kudura) ya uzao wa Adamu. Hivyo, uwepo wa hukumu ya Mungu na wokovu kutoka hukumu hiyo ni sehemu halali katika mafundisho ya kuwavutia wasioamini ili wampokee/wamkubali Kristo kuwa Mwokozi wao (cf. Matendo 24:15 & 25).
Kwa uhakika ulikuwa woga wa hukumu ya Mungu katika mfumo wa tetemeko kuu ambalo alilishuhudia yule mkuu wa gereza ndio uliompa motisha ya kuutafuta wokovu. “Mabwana” aliwauliza kwa hofu Paulo na wenzake baada ya kuiona nguvu ya Mungu ikifungua milango ya gereza kwa tetemeko lile kuu na hapo hapo kuuona uhalisia wa uwezo wa Mungu, “nifanye nini ili nipate kuokolewa?” Jibu la Paulo lilikuja bila kusita wala utata:
“Mwamini Bwana Yesu Kristo nawe utaokoka.” Matendo 16:31.
Huu ni ujumbe wa Injili katika maneno rahisi sana. Unaokolewa kwa kumwamini Kristo, basi. Unakuwa Mkristo kwa kuweka imani yako katika Kristo. Biblia inaliweka hili wazi “katika njia na nyakati nyingi tofauti” - Waebr. 1:1.
Mwandishi Charles Ryrie katika kitabu chake “Survey of Bible Doctrine”, anahesabu zaidi ya aya 200 katika Agano Jipya pekee ambamo inaandikwa wazi kwamba wokovu unatokana na/unategemea imani pekee. Mtu anakuwaje basi, muumini katika Kristo, Mkristo na mfuasi wa Kristo? Kwa kuweka tu imani yako kwake, na katika muda huo unaingia katika jamaa ya Mungu, unakuwa sehemu ya mwili wa Kristo, unakuwa sehemu ya Kanisa Lake. Ujumbe huu mfupi na rahisi ambao unatakiwa kuwa nao katika muda ule unapookolewa, umefananishwa na punje ya haradali, ukilinganishwa na kiasi kikubwa cha mafundisho ambayo unayapata baada ya wokovu. Mpango mzima ni “Kristo”: kuikubali na kuipokea zawadi ya bure ya Mungu kwako kwa ajili ya uzima wa milele, unalazimika kwanza kumkubali na kumpokea Mwanaye, nafsi ya Kristo na kazi Yake:
Hakuna ajaye kwa Baba, bila kupitia kwa Mwana. Yoh. 14:6.
Uzima wa milele, wokovu kutoka kifo na hatia, haviwezi kununuliwa kwa kiasi chochote cha fedha za hapa duniani, lakini twaweza kujitwalia, bila ya kulipa chochote. Hii ni kwa sababu Bwana Yesu Kristo amekwishalipa kwa ajili yetu sote, kwa kifo chake msalabani kwa ajili yetu. Kwa sadaka Yake, ametugomboa, akilipa gharama zote za dhambi zetu tunazotenda, na hivyo kufungua mlango wa kuingia paradiso. Kama bado hujafanya hivyo, maji ya uzima yapo kwa ajili yako, unaweza kunywa bila malipo yoyote sasa hivi. Amini tu katika Bwana Yesu Kristo, nawe utaokolewa. “Tukiwa ni mabalozi wa Kristo, kama vile Mungu anakusihi nakukusitiza kupitia kwetu, tunakuomba, fanya mapatano na Mungu!” (2Wakor. 5:20).
14.1 Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.
14.2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.
14.3 Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.
Yoh. 14:1-3 SUV
3.16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
Yoh. 3:16 SUV
2.8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema [ya Mungu], kwa njia ya imani [yenu kwa Kristo]; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa [cha bure] cha Mungu;
2.9 [na] wala si kwa matendo [yenu], mtu awaye yote asije akajisifu.
Waefe. 2:8-9 SUV
16.31 Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.
Matendo 16:31
Ushuhuda wa maandiko uko wazi kabisa. Kinachohitajika kwa upande wako ni kupokea zawadi ya karama kutoka kwa Mungu mwenye upendo ambaye amekwisha fanya yote kwa ajili yako. Afanye nini zaidi ya lile lililokwishafanywa Naye la kumtuma Mwana wake wa pekee ampendaye, aje kufa kwa ajili yetu, ili wewe uweze kuishi milele Naye? Kinachohitajika ni wewe kukubali, kuweka imani yako katika Bwana Yesu Kristo, kumwamini, nao uzima wa milele utakuwa wako. Anachokitaka Mungu ni kwamba usikatae zawadi/karama hii Yake isiyo [na] kifani.
22.17 Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure.
Ufu. 22:17 SUV
Misingi ya Imani Katika Kristo:
אׇםַו 'aman πιστευω pisteuo
• Etimolojia ya Neno Imani: Japo Biblia inatumia msamiati mpana katika kuzungumzia mafundisho ya imani, dhana ya neno “imani” katika Kiswahili inanyumbulishwa kwa ukaribu zaidi na neno la Kiebrania ‘aman, neno la Kiarabu ‘iiman na neno la Kiyunani pisteuo (pamoja na maneno yanayohusiana nayo). Ikumbukwe hapa kwamba Biblia imeandikwa katika lugha za mwanzo (original languages) za Kiebrania (na Kiarami – Aramaic – kidogo) katika Agano la Kale, na Kiyunani katika Agano Jipya. Neno hili linapotumika kama kitenzi-neno (verb), hutafsiriwa kama kuamini (to believe). Kwa mfano, katika Mwanzo 15:6, ambapo tunaambiwa kwamba Abrahamu “akamwamini Bwana, naye kwake hili likahesabiwa kuwa haki”, ‘aman ndiyo neno linalotumika (katika Kiebrania). Mzizi wa kitenzi-neno (verb) unahusiana na dhana ya kuwa imara na wa kuaminika (hivyo ‘amunoth ni mihimili ya mjengo, wakati ‘amen inamaanisha “kwa kweli/uhakika au kwa kuaminika), hivyo kwamba katika Kiebrania, dhana ya kuamini[ka] inabeba pia msisitizo kwamba mlengwa wa imani hiyo (yaani Mungu) anaweza kuaminiwa na wote watakaoweka imani yao Kwake. Kama ilivyo nguzo imara, atatusaidia pale tutakapomwegemea, ‘aman inadokeza (na katika hilo sote tuseme amen!). Neno la Kiyunani pisteuo ndilo linalotumika katika Septuagint (tafsiri ya Bublia ya Kiebrania kwenda katika lugha ya Kiyunani iliyofanywa takriban 300BC ambayo ilikuwa na ushawishi mkubwa katika uandishi wa Agano Jipya kuhusiana na msamiati na mtindo wake wa uandishi) kutafsiri neno ‘aman, na hivyo wakati wote linabeba kiashiria cha utegemezi kwa Mungu. Katika Kiyunani, pisteuo maana yake ni kuwa na imani katika au kuamini kwa mlengwa fulani. Kama vile dhana hasi ya apistia (yaani kutokuwa na imani) inavyoweka wazi, “imani” inayoonyeshwa na pesteuo ni zaidi ya kukiona na kukielewa kitu kiakili tu (mfano Warumi 11:20-23, ambapo kutoamini ni mwenendo wa makusudi wa moyo wa mtu). Kwa kuongezea, waandishi mbalimbali wa Agano Jipya wamelitumia neno pisteuo katika tenzi endelevu (participles) wanapowazungumzia waumini (wakati uliopita/uliopo/ujao, unaoendelea). Hii ni muhimu, kwa sababu kwa waandishi wa Biblia, waumini ni watu ambao “walikuwa, wako na wataendelea kuwa katika hali ya kuamini”. Hivyo, wakati wowote unaozungumziwa, uliopita au wa sasa, unaoendelea, basi kitatumika kitenzi endelevu (participle) ambacho kitaweka wazi kabisa [kanuni] kwamba waumini ni watu ambao wanahusika wakati wote katika kitendo cha kuamini, iwe tendo hilo linaelezewa kwamba limekwishafanyika (Matendo 18:27; 19:18; 21:20,25; Tito 3:8), linaloendelea wakati wote (Waefe. 1:19), au limekwishafanikishwa (Waebr. 4:3).
• Maana ya Neno Imani: Imani, kama tulivyoona katika kitabu cha Waebrania, ni uhalisia wa yale tusiyoyaona: “Imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo; ni udhahiri wa mambo yasiyoonekana” (Waebr. 11:1; cf. 2Wakor. 4:18; 5:7). Mwandishi wa kitabu cha Waebrania halafu anaendelea kuonyesha jinsi imani ilivyo moja kati ya maadili muhimu ya maisha ya Kikristo, kwa sababu kwa kutumia imani, waumini maarufu wa kale walimfurahisha Mungu na wakamshuhudia Yeye mbele ya ulimwengu, wakienenda aghalabu bila kujali viwango na ‘maadili’ ya dunia hii (aya 2-40). Walienenda kwa imani, ambapo kulingana na aya ya kwanza, iliwapa uhalisia katika matumaini yao, na hivyo ikawapa uhakika ambao uliyafanya maoni ya dunia hii kuwa yasiyo na thamani (yanapolinganishwa na ule uhakika). Mwandishi huyu anayaweka mambo kinyume na vile yanavyoonekana. “Tuonyeshe ishara/mwujiza!” ni kilio na madai ya kizazi cha wakati wa Bwana Yesu na mpaka sasa. “Nipe uhakika kwamba wewe ni Mungu!” Lakini mwandishi wa waraka ule kwa Waebrania anatuambia kwamba kwa wale waumini waliotukuka wa kale, mambo yalikuwa kinyume kabisa na hivyo. Walikuwa na imani kwamba kile ambacho kwa wakati ule walikitumainia tu kukipata (ahadi ya thawabu kutoka kwa Mungu) kitafanyika kwa ukweli; kwamba kile ambacho kwa sasa hakionekani (uwepo na uongofu wa Mungu) hata hivyo kilikuwa halisi. Hii imani inaelezwa na mwandishi kwa Waebrania kuwa ndio msingi wa tumaini lao, kuwa ndiyo ithibati ya visivyoonekana. Kwani thawabu wanazotumaini kuzipata ziko, na yule Mungu asiyeonekana atakayewagawia thawabu hizo yuko. Kwa imani yao waumini wanaotajwa katika sura ya 11 wanatupa uthibitisho wa hili. Kama kusingekuwa na thawabu za kweli, kama kusingekuwa na Mungu mwenye haki, basi imani ya namna hii na matendo makuu yaliyotokana nayo yasingeonekana chini ya jua. Lakini kwa kweli ushuhuda mkuu wa hawa waumini shujaa ni uthibitisho wa kutosha wa uwezo na uwepo wa Mungu, na uwepo wa thawabu zilizotukuka alizoziweka salama matunzoni kwa ajili ya wale wanaostahamili katika imani. Hivyo, imani inajumuisha, inafunika Ukristo wetu katika marefu na mapana yake (Wagal. 1:23). Zaidi ya mtazamo au mwenendo wa moyoni, imani inaashiria kuaminika [kwa Mungu] (War. 3:3). Imani ni kitendo cha kukiri, kujisalimisha, kuacha kupinga na kuanza kujitoa, kuamua, ni kitendo cha unyenyekevu na heshima kwa mamlaka ya Mungu katika kumwogopa Mungu. Ni katika kujitoa kikamilifu na kuweka tumaini letu katika uadilifu wa Mungu ndipo tunauona uhalisia na uwepo wa yale maajabu yasiyoonekana yaliyoahidiwa kwetu [na Mungu].
• Imani ni Zaidi Sana ya Mwenendo na Mchakato wa Kufikiri Tu: Imani ni zaidi ya uelewa au kukubali uwepo wa Mungu au Uungu wa Kristo. Kama Yakobo anavyosema, “Je, unaamini kwamba Mungu yuko? Hiyo ni vyema sana. Lakini hata pepo wanaamini hivyo na kutetemeka [kwani wanaijua hatma ya kutisha ya uasi wao]” (Yak. 2:19). Ujumbe wa Yakobo hapa ni kwamba imani siyo tu zoezi la kiakili juu ya uwepo wa Mungu au hata kutambua kwamba Kristo ni Mwana wa kweli wa Mungu. Imani inavuka mpaka wa kutambua tu habari fulani. Imani inazitambua na kuzikumbatia kweli hizi. Pale mtu anapoamini katika Bwana Yesu Kristo kuwa ndiye njia pekee ya kufika kwa Baba, njia pekee ya kuokolewa kutoka katika hukumu na kifo, mtu huyu hapo hapo anabadilishwa milele, na hakuna uelewa wa kiakili tu wenye uwezo wa kufanikisha mwujiza mkuu kama huu. Hivyo, pamoja na uelewa wetu wa kiakili kuhusu kweli zilizoko katika Injili ([uelewa huu ukitiwa] nguvu na Roho Mtakatifu), imani yetu inapaswa pia kuhusisha kujitoa na kujiwajibisha katika kumfuata Bwana Yesu Kristo. Hii dhana imo pia katika neno la Kiyunani epignosis. Neno hili hutumika mara nyingi (pamoja na kitenzi-neno kinachohusiana nalo epigignosko) kuelezea “elimu” ya Mungu katika mazingira ya wokovu, epignosis inahusisha dhana ya kufahamu, kukubali, na hivyo kutii ukweli wa Mungu na Utashi Wake (War. 1:28; 1Tim. 2:4; 2Tim. 2:25).
• Muundo na Jinsi ya Kutenda kwa Imani: Katika maandiko, masimulizi ya kwanza kabisa, ya undani kuhusiana na wokovu wa nafsi yanapatikana katika Mwa. 15:6, ambapo tunasoma kwamba Abrahamu “alimtumainia Bwana, naye Bwana akamhesabia haki kutokana na imani hiyo.” Katika nyakati za Agano la Kale, waumini walielekeza macho yao kwenye msalaba, kwenye siku ambayo kwa namna moja ama ingine, Mungu atafuta dhambi na kufungua mlango wa wokovu (cf. War. 3:25b). Siku zote Mungu amejiwekea mashahidi wa matendo makuu ya wokovu atakayoonyesha ulimwengu kupitia dhabihu ya Mwana Wake. Kutoka yale mavazi ya ngozi za wanyama aliyowapa Adamu na Eva (ambayo yalihusisha kuchinjwa kwa wanyama wale), kupitia hata mfumo mzima wa sadaka wa Walawi, mpaka ile siku yenyewe ya msalaba, Mungu ameweka wazi kwa mtu yeyote mwenye shauku ya kujua, kwamba WOKOVU UNAPATIKANA KUPITIA KUTOLEWA SADAKA KWA MWINGINE MAHALA PETU ili kulipia ile adhabu ya dhambi zetu. Abrahamu alimtumainia Mungu – si kwake yeye mwenyewe au katika uongofu wake – kwa ajili ya wokovu wake wa siku ya mwisho, na tumaini hilo, alilokuwa akiliimarisha siku zote za maisha yake, ndilo lilikuwa njia ya wokovu kwake. Katika Warumi 10:9-10, Paulo anatuambia kwamba hata leo njia ya wokovu ni ile ile: ikiwa “tutakiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana kwa midomo yetu, na kuamini katika mioyo yetu kwamba Mungu alimfufua kutoka katika wafu” basi tutaokolewa. Yakobo anaweka wazi kwamba Paulo “haongezi” kitu chochote katika njia na utendaji wa imani. Huwezi kuwa muumini, anadhihirisha, bila ya imani hiyo kudhihirishwa katika maisha yako (Yak. 2:18-26). Kama ushahidi, ananukuu kufaulu kwa Abrahamu katika mtihani [wake] ule mgumu wa imani, amri kutoka kwa Mungu kwamba amtoe sadaka ya kuchinja mwanawe Isaka. Badala ya kusuasua, Abrahamu aliamini kwamba Mungu anayemtumainia atafanya yote kuwa mema, na wokovu wa Isaka kupitia kwa mbadala aliyetolewa na Mungu mwenyewe imekuwa taswira ya dhabihu ya Kristo kwa ajili yetu mpaka leo. Ikiwa tunamwamini Mungu mioyoni mwetu, basi na “kukiri ukweli huo kwa midomo yetu” kutafuata, pamoja na ushuhuda wa imani yetu kimatendo ambao Mungu ataufanya kupitia sisi katika maisha yetu ya Kikristo tutakayoishi. Basi, mbali na taswira ya wazi tuliyo nayo ya kazi inayookoa iliyofanywa na Nafsi ya Mwokozi wetu Yesu Kristo tunapotizama nyuma kwenye msalaba, njia ya wokovu inabaki ile ile kwa Paulo kama ilivyokuwa kwa Abrahamu: amini. Na wakati Abrahamu alitazama mbele kwa matuamini kwa ile dhabihu ambayo Mungu ameitoa kwa ajili yetu, sisi tuna uhakika wa ufahamu wa kazi iliyofanywa na Bwana wetu Yesu Kristo msalabani, ufahamu ambao kama mtume Petro anavyotuambia, “manabii waliuulizia na kuutafuta” (1Pet. 1:10-12). Hivyo basi, “kukiri” [kwa mdomo] kama inavyofundishwa katika War. 10:9-10 si sharti katika mchakato wa kuwa muumini, bali ni namna Paulo anayoitumia ya kututhibitishia (kama vile Mungu alivyothibitisha kwa Abrahamu, na kama Yakobo anavyoweka wazi kwa mtindo wake wa uandishi) kwamba waumini wote wa kweli wanaonekana kwa kazi wanazozifanya: yaani katika mfano huu, hakuna mtu ambaye kikweli (moyoni) ameweka imani yake katika Kristo atakataa au hatokuwa tayari kukiri kwamba Yesu ni Bwana.
• Yaliyomo Katika Injili: Kristo ndiye aliyemo katika “habari njema (Kiyunani euangelia), taarifa nzuri kutoka kwa Mungu kuhusu wokovu kutoka dhambi na kifo kwa wale wote wanaomwamini Mwana wake na hakuna msingi mwingine kwa imani yetu (1Wakor. 3:11). Baada ya kusema hili, ebu tujiulize swali lifuatalo: ni kiasi gani cha taarifa au elimu juu ya Kristo ambacho mtu anahitaji kujifunza/kujua ili tu aweze kuokolewa, kwani ni wazi kwamba sisi sote tunaoamini tulijifunza mengi zaidi kuhusu Mwokozi wetu baada ya kuweka imani yetu katika Kristo kuliko tuliyoyajua saa ile tulipozaliwa upya. Tuchukue mfano wa Abrahamu tena; baba yetu katika imani hakuyajua yote ambayo sisi tunayajua sasa kuhusu tukio kuu la kutwaa mwili kwa Kristo, kwani nyingi kati ya tondoti (details) za kutwaa mwili kwa Bwana Yesu ili afe mahala petu zilikuwa zimefichwa zisionekane mpaka zilipofikia uhalisia wake (2Wakor. 3:12-18). Lakini tangu msalaba, Kristo mwenyewe, na si kanuni ya sadaka ya Mungu kwa niaba yetu (kama ilivyokuwa katika Agano la Kale), ndiye suala muhimu na la wazi katika wokovu, na hivyo Nafsi na kazi ya Kristo ndivyo vinapaswa kuaminiwa au kutambuliwa na kukubaliwa (Kiyunani epignosis: siyo tu kuelewa bali kukubali pia). Mungu Baba amemfanya Mwanaye, Bwana Yesu Kristo, kuwa ndiye msingi wa wokovu, na hivyo kwa sasa hakuna namna nyingine ya kuokolewa (Yoh. 5:23; 12:44; 14:6; Matendo 4:12).
• Tendo la Imani Inayookoa: Kimsingi, kumwamini Kristo ni kitendo cha kukubali na kupokea mbadala wa Nafsi ya Kristo mahala petu, yaani kutambua kwamba sisi wenyewe tunastahili tu kifo na hatia, na hatuwezi hata kidogo kuepuka kaburi. Hata hivyo, mara tusikiapo habari njema kwamba Mungu ametupatia njia ya kuokolewa kutoka kifo na hatia ambavyo huwakumba wanadamu wote, tunaikumbatia hii “habari njema” ya Bwana Yesu Kristo na kifo chake kwa ajili yetu. Kinapochukuliwa kwa mtazamo huu, kitendo cha kuamini ni, kimsingi, kufanya uchaguzi wa kusimama kwa uongofu wa Kristo badala ya uongofu wetu sisi wenyewe (cf. Mwa. 15:6; War. 3:21-26; na Aaron kama taswira ya Kristo “atabeba hatia”: Kutoka 28:38). Tunaweka imani yetu katika Kristo kwa ajili ya wokovu wetu kutoka dhambi na kifo. Kanuni hii ni muhimu sana. Habari njema ya Injili ni tamko kwamba tumesamehewa kwa msingi wa kazi ya Kristo, tunapata msamaha huu kupitia imani [tuliyo nayo] katika Yeye aliyefanikisha kazi hii [kwa faida yetu]. Hivyo, katika kiwango fulani, utambuzi [wetu] wa uhitaji wa msamaha na wokovu kutoka dhambi na kifo ni sehemu muhimu ya imani inayookoa. Kama Bwana wetu anavyosema, “yeye aliyesamehewa kidogo, hupenda kidogo”. Zaidi ya hapo, kama hatuamini kikweli na kuona waziwazi kwamba tuna uhitaji mkubwa wa kuokolewa kutoka kifo na dhambi, basi tutakuwaje na motisha ya kutosha kupokea karama hii kutoka kwa Mungu? Hivyo uhitaji na fursa kwa ajili ya wokovu ni sehemu mbili za sarafu moja. Unaamini kwamba kuna umuhimu wa wokovu (kitubio), hivyo unamtegemea Kristo kwa ajili ya kufanikisha wokovu (kuweka imani katika Kristo). Kwa namna hii matendo mawili yanayoelezwa katika War. 10:9-10 ya kmwamini na kum-kiri Kristo yanaunganishwa na hayawezi kuachanishwa.
• Imani Ndiyo Fikra Adilifu ya Msingi ya Mkristo: Kama tulivyoona mara nyingi katika masomo yetu haya ya 1Petro, imani ndiyo fikra adilifu ya msingi ya maisha ya Kikristo, ikiorodheshwa kwanza kabisa (na hivyo ni ya msingi) katika 1Wakorintho 13, na kama kanuni ya msingi ambayo Wakristo wote wanapaswa kuielewa, katika Waebrania 6:1 (pia imeorodheshwa mwanzoni katika orodha ya Petro: 2Pet. 1:5). Haiwezekani kufanya/kufanikisha maendeleo yoyote katika maisha ya Mkristo, au, kwa hakika, kufanya chochote katika mpango na matakwa ya Mungu juu ya maisha yetu bila imani (Waebr. 11:6). Imani ndiyo fikra adilifu ya msingi , ndilo tofali la msingi ambalo juu yake fikra adilifu zote nyingine zinajengwa (kw. mf. tumaini: Waebr. 11:1; upendo: 1Wakor. 13).
• Imani Katika Kristo Ndiyo Njia Pekee ya Wokovu: Bwana Yesu Kristo ndiye kiini na ndiye kitovu cha maisha yetu ya Kikristo (Waebr. 12:2). Kwa kazi aliyofanya msalabani, Yeye ndiye Mwokozi wa ulimwengu (1Yoh. 2:2; 1Tim. 4:10), na hakuna anayeweza kumjongelea Baba au kupata msamaha Wake wa dhambi au kibali Chake kupitia msuluhishi mwingine yeyote (1Yoh. 14:6; Waefe. 2:18). Kristo ndiye mlengwa pekee anayefaa wa imani yetu, yaani Nafsi pekee ambayo kwake tunaweza kuweka imani yetu na kupata wokovu kutoka hukumu na hatia inayokuja kama Petro anavyoweka wazi katika Matendo 4:12:
4.12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.
Mlango ni mwembamba na barabara inayoelekea huko ni ngumu, lakini hakuna njia nyingine ambayo kwayo tunaweza kupokea uzima wa milele zaidi ya kumpokea Bwana Yesu Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wetu (Matt. 7:13; Lk. 13:24). Haijalishi maisha ya mtu ni magumu kiasi gani au eneo analoishi ni mbali na gumu kufika kiasi gani, Mungu ameyaweka yote hayo katika Mpango Wake, na kiwango tangu msalaba ni kile kile: imani katika Kristo. Hakuna kiasi chochote cha ‘matendo mema’ wala ‘kujitoa’ kinachoweza kutosha mbele za Mungu Baba kuchukua nafasi ya Mwanaye pale msalabani (Waefe. 2:8-9).
• Imani Huleta Utengano: Injili inapatikana bure, haihitaji stahiki ya namna yoyote kwa upande wetu, na inapatikana kwa wote. Katika upotofu wa fikra za wanadamu, wengi wanajikwaa katika urahisi, wepesi na ukarimu wa ujumbe huu kutoka kwa Mungu. Kwa baadhi yao, Injili ni “rahisi mno”, kwa wengine “haijakaa kitaaluma kwa kiasi cha kutosha kuwaridhisha wao” (1Wakor. 1:23; 2Wafalme. 5:1-14). Wengine wanaudhika na kukasirishwa na dhana ya hukumu na kutiwa hatiani na Mungu kwa sababu ya matendo yao maovu, wakikana uhalisia wa dhambi zao, wakichukia mwanga wa ile kweli kwa sababu ya matendo yao ya giza (Yoh. 3:19-21). Lakini tunapaswa kusimama kwenye kweli, bila kujali ushawishi wa fikra na hoja za kibinadamu za wakati huu: hakuna njia nyingine ya kuokolewa mbadala na kupitia imani kwa Bwana Yesu Kristo. Msimamo usiobadilika kama huu mara nyingi hutenganisha watu, lakini hii ndiyo kudura, haya ndiyo majaliwa (destiny) ya kweli. Kama vile Mungu alivyotenganisha ardhi na maji (Zab. 104:9), na kama alivyomtuma Abrahamu atenganishe miili ya wanyama na kuweka njia katikati yayo (Mwa. 15:8-17), kama Alivyotenganisha kati ya mwanga na giza (Mwa. 1:3-4; cf. Yoh. 1:5), vivyo hivyo Anatenganisha kati ya wazima na wafu, kinachotenganisha kati ya uzima wa milele na hukumu ya milele ikiwa ni imani katika Mwanaye. Mpaka hapo Bwana wetu atakaporudi, tujue kwamba suala la imani katika Yeye, yaani Injili, kuwa ndiyo upanga unaotenganisha wanadamu katika makundi mawili yanayopingana na yaliyo kinyume: wanaoamini na wasioamini (Matt.10:34; cf. War. 2:8).
• Imani si Mwisho, ni Mwanzo Tu: Kwa wale wanaoamini, maisha ya Kikristo ndiyo kwanza yanaanza. Baada ya kuunyanyua na kuubeba msalaba wetu kwa imani, Kristo anatupa amri ya kumfuata (Matt. 16:24; Mk. 8:34). Kama ambavyo tumekuwa wanajumuiya wa familia ya Mungu kwa imani, vivyo hivyo sasa ni lazima tutembee kwa imani kama tunavyofanya juhudi za kumfuata Bwana wetu katika maisha yetu yote (2Wakor. 5:7). Zaidi ya hapo, Luka anaongeza dondoo mbili muhimu kwenye amri hii ya Bwana wetu ya kumfuata, kwa upande mmoja akisema kwamba hili ni jambo tunalopaswa kufanya kila siku (Lk. 9:23), na kwa upande mwingine, kwamba bila hii “imani ya ufuasi”, hatuwezi hata kufikiriwa kwamba sisi ni wanafunzi Wake (Luka 14:27). Neno la Kiyunani linalomaanisha “mwanafunzi” ni mathetes, neno linalotokana na mzizi wa neno la Kiyunani linalomaanisha “kujifunza”. Hivyo, kumfuata Kristo na kujifunza kweli aliyoturithisha katika Neno Lake takatifu vimeungana kimsingi kabisa na haviwezi kutenganishwa. Kumfuata Kristo ni kujifunza Neno Lake, kulielewa, na kulitimiza kwa matendo (Yak. 1:22).
Maisha ya Mkristo
kusikia (kwa imani)> NENO LINAPOAMINIWA <(kwa matendo) kutenda
• Matokeo ya Imani: Kuna faida nyingi sana katika kuwa muumini katika Kristo (katika kitabu cha tatu (3) cha mfululizo wa vitabu vyake vya “Systematic Theology”, Lewis Sperry Schafer anaorodhesha faida 33 zinazojitegemea ambazo huongezeka katika hesabu ya muumini kutokana na neema za Mungu). Lakini, kwa hakika, moja kati ya karama muhimu na inayopendwa ambayo huja kwa tendo la imani ni kuhalalishwa kwetu (War. 5:1). Hii ni kwa sababu kuhalalishwa (kufanywa waongofu mbele za macho ya Mungu kwa sababu ya tumaini letu kwa kazi ya Kristo kwa imani) kunasababisha wokovu wetu kutoka kifo cha kiroho na kuingia kwenye uzima wa milele (War. 3:21-22; 1Yoh. 5:11). Sisi tulio ndani ya Kristo kupitia imani yetu Kwake hatutaingia tena katika hukumu ya kutisha ya Mungu ambayo ni kile kifo cha pili (War. 8:1; Ufu. 20:11-15), bali “tumeingia kwenye uzima tukitoka kwenye kifo” (1Yoh. 3:14).
• Imani ni Lazima Ijengwe: Mwisho, baada ya kuwa na imani inayookoa, hatuwezi kukaa tu na kuwa na mtazamo kuwa imani itajiendeleza na kujijenga yenyewe. “Mjichunguze wenyewe ili muone kama mko katika imani”, Paulo anawaasa Wakorintho (2Wakor. 13:5). Huu ni ushauri mzuri, haswa tunapokumbuka ile tuzo kuu itakayotokana na kuimarisha imani yetu: ufufuo na uzima wa milele. Twaweza kuwa na uhakika kwamba Mungu atakuwa mwaminifu kwao watakaomtegemea (2Tim. 2:12-13). Hii ina maana ya kwamba tuishike imani tunayokiri mpaka mwisho, kwani ni imani yetu itakayotupatia ushindi:
Kwani huu ndio ushindi unaozidi nguvu ulimwengu: imani yetu!
1Yoh. 5:4
Hitimisho: Haijalishi maisha yetu ni magumu kiasi gani, haijalishi mlima (mpando) ni mkali kiasi gani, haijalishi njia na lango ni jembamba kiasi gani, ustahamilivu wetu katika imani yetu kwa Bwana Yesu Kristo si bure (1Wakor. 15:58; Wagal. 6:8). Kwani upande wa pili wa lile lango kuna MILELE pamoja na baraka na faraja ambazo kwa sasa hatuwezi kuzielewa:
10.37 Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia.
10.38 Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye. Waebr. 10:37-38 SUV.
=0=
Imetafsiriwa kutoka: Faith Dynamics: Peter’s Epistles #24
=0=
Basi, na tuonane katika somo #25 la mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!