Nyaraka za Petro #26: Dhiki na Taabu Binafsi na Athari Zake Mbalimabli Kwa Wakristo

Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for this Kiswahili Translation has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

Kielelezo: Imani inapopitia katika moto wa mitihani ya maisha ya Mkristo, matokeo ni ya namna mbili: Ushindi au Uasi

1Pet. 1:6-9:
Katika kutazamia kwa hamu wokovu wa siku ile ya mwisho, furaha yenu inazidi sana, japokuwa kwa sasa yaweza kuwa mnateseka kwa muda mkipitia mitihani ambayo malengo yake ni kwamba imani yenu idhihirike kuwa ni halisi. Uthibitisho huu wa imani yenu una thamani kuu zaidi ya dhahabu, kwani dhahabu, japo nayo hupimwa ubora wake kwa moto, mwisho wake huharibika. Bali imani yetu, inapohakikishwa kuwa ni halisi katika majaribio makali ya maisha, itawasababishia sifa, utukufu na heshima kwenu pale Bwana Yesu Kristo atakaporudi katika utukufu wake. Ijapokuwa hamjamwona, mnampenda tu. Ijapokuwa hamwezi kumwona kwa wakati huu, mna imani juu Yake. Kwa sababu hii mna furaha ambayo hamwezi hata kuielezea, ambayo inaonyesha ile milele ijayo yenye utukufu, pale mtakapokabidhiwa ule ushindi mkuu wa siku ya mwisho – wokovu wa maisha yenu – ambao ndiyo lengo na nia ya imani yenu hii.

Utangulizi: Mifano kutoka katika historia ya mateso ya Wakristo iliyozungumzwa katika sehemu iliyopita (pamoja na utabiri wa mateso makubwa yanayokuja siku za usoni katika kipindi cha Dhiki Kuu) inapaswa kutuwekea msisitizo katika ukweli kwamba imani yetu itapitia changamoto hapa duniani. Ikiwa dhiki tutakayopitia itakuwa ya ki-binafsi pekee, au tutapitia mateso kama sehemu ya kikundi chenye imani moja [ya Kikristo], yaani Kanisa, tunapaswa kwa gharama yoyote ile kushika imani yetu. Ni lazima kwa gharama yoyote ile tushikilie hii kamba [ya imani] ambayo ndiyo inatupatia usalama wa milele, kwani huo ndio ushindi pekee unaoweza kuzidi nguvu changamoto zote za maisha na kutufikisha salama nyumbani: yaani imani yetu katika Bwana Yesu Kristo (Waebr. 6:19; cf. War. 8:35-37; 1Yoh. 5:4-5).

Athari/Matokeo ya Aina Mbili ya Mateso/Dhiki Binafsi kwa Wakristo: Wakati wowote ule janga linapotokea (taabu na dhiki binafsi ya somo #25), husababisha athari fulani kwa wale wanaoguswa. Hulka ya athari hii ni ya umuhimu mkubwa sana pale ambapo mwathirika ni muumini wa Kristo. Katika mazingira haya, kiwango chetu cha kupevuka kiroho, kasi yetu ya maendeleo ya kiroho, na hali yetu ya kiroho ya wakati husika, vyote vinaathiriwa na namna tunavyopokea janga hilo, iwe kwa ubaya au kwa wema. Athari mbili za msingi za mateso makubwa au dhiki binafsi ni:

1) kulalamika: Tendo la kulalamika ni la kawaida kwa wanadamu wanaokumbwa na janga, sivyo? Je, ni kwa nini? Katika shida, ni rahisi sana kuwa na mwenendo mbaya – kuhusu maisha, kuhusu wewe mwenyewe, na hata kumhusu Mungu. Lakini kuwa na hisia mbaya, hisia hasi kuhusiana na taabu na dhiki binafsi, ijapokuwa mtu anaweza kuelewa sababu zake, ni njia iliyojaa hatari za kiroho. Hususan katika nyakati za magumu, Mungu anatarajia tumwamini Yeye, na siyo kumlaumu, na hiki ndicho kiini cha unyenyekevu halisi:

5.5  ... Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.
5.6  Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;
5.7  huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu. 1Pet. 5:5-7 SUV

10.9  Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu (yaani kizazi cha Kutoka Misri), wakaharibiwa [wakauwawa] na nyoka.
10.10  Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa [wakauwawa] na mharabu [Destroying Angel].
10.11  Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani [tunaoishi enzi za mwisho].
10.12  Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.
10.13  Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida [katika maisha] ya wanadamu; ila [zaidi ya hapo] Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo [kustahamili]; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea [namna ya kutatua tatizo], ili mweze kustahimili [shinikizo].
1Wakor. 10:9-13 SUV

2) kuyakumbatia: Kuyakumbatia mateso na majanga? Hii siyo reaction ya kawaida ya mwanadamu kwa majanga, sivyo? Kwa kweli ni reaction ya kiroho (super-natural), na ndiyo tunayoamriwa kuifanya. Badala ya kuwa na mtazamo hasi na kunung’unika (Yuda 16), tunapaswa kujitahidi katika nyakati za magumu kuishika imani yetu kwa nguvu zaidi na kuamini katika huruma ya Mungu na hulka yake ya kutoonea, tukitambua kwamba haiwezekani (sisi) kuzijua sababu zake zote zinazomfanya kuruhusu mateso yatusibu (War. 11:33; soma pia kitabu cha Ayubu). Kama tukipokea kwa moyo wa unyenyekevu yoyote yanayotoka katika mkono Wake (Ayubu 2:10), na kumtegemea katika nyakati hizi ambapo ni vigumu sana kumwamini, tunaongeza kasi yetu ya maendeleo ya kiroho:

Katika kutazamia kwa hamu wokovu wa siku ile ya mwisho, furaha yenu inazidi sana, ijapokuwa kwa sasa yaweza kuwa mnateseka kwa muda mkipitia mitihani ambayo malengo yake ni kwamba imani yenu idhihirike kuwa ni halisi.
1Pet. 1:6

5.3  Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi;
5.4  na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini [la thawabu ya milele];
5.5  na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.
War. 5:3-5

1.2  Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu [na mitihani] mbalimbali;
1.3  mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi [ustahamilivu].
1.4  [Basi acheni] Saburi na iwe na (ifanye) kazi [yake kwa u]kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno [kitu].
Yakobo 1:2-4

Hivyo, katika kuyakabili mateso makali (taabu na dhiki binafsi), jambo la muhimu ni imani tu, kuitumia imani yako kwa subira, na kuitunza imani hiyo, hata mbele za magumu ambayo hatuyaelewi [chanzo na sababu yake] na ambayo ni magumu sana kwetu kuvumilia. Na ingawa tumelizungumzia suala la ustahamilivu wa imani (tizama masomo #13, #21, #24 na #25), tunalitizama tena suala hili hapa kwa kifupi, kwani “kurudia jambo lile lile kwenu”, kama mtume Paulo anavyosema katika muktadha (context) unaofanana, “si usumbufu kwangu, bali una faida ya kuwaletea usalama wa kiroho” (Wafi. 3:1; cf. 2Pet. 1:12-15). Dondoo kuhusu usalama wa kiroho ina ukweli wa kipekee katika suala letu, kwani suala tunalolizungumzia ni la kulinda imani yetu chini ya shinikizo kali. Kuwa na ‘reaction’ hasi kwa mateso, hata kumlaumu au kumtilia shaka Mungu ni hatari kwa imani yetu. Lakini bila ya imani endelevu kwa Kristo, hakuna kufika salama, hakuna wokovu, hakuna uzima baada ya kifo. Haya ni mambo muhimu sana – hakuna yaliyo muhimu zaidi yayo. Ndiyo maana hatuwezi kushakia umuhimu wa kustahamili na imani yetu au matokeo ya kuharibika kwa imani hiyo chini ya [ma]shinikizo ya taabu na dhiki binafsi katika maisha yetu.

Hatari ya Uasi: Hutokea vipi, basi, wale wanaompenda Bwana wanafikia hatua ya kumkana Yeye (Matt. 10:33; 2Tim. 2:12)? Inakuwaje waumini wanafikia hatua ya kujifanya “maadui wa msalaba wa Kristo” (Wafi. 3:18-19)? Haya ni maswali yanayotia hofu kweli kweli. Ni wazi kabisa kwamba waumini wa kweli wa Kristo hawageuki na kuwa waasi usiku mmoja tu. Lakini tukiwa Wakristo katika himaya ya Ibilisi, imani yetu itapata mitihani, tunayoyaamini yatawekwa chini ya shinikizo. Kwa kifupi, utashi wetu utaendelea kuulizwa maswali ambayo yatahitaji maamuzi hata baada ya kuokolewa. Vikwazo kwa imani yetu – uasi (apostasy – kuanguka kabisa kutoka katika imani kwa Mungu) ambao ni hatua ya mwisho ya vikwazo au kujikwaa - huanza na ‘reaction’ hasi kutokana na mtihani fulani. Iwe ni mtihani wa taabu fulani ambao muumini anashindwa (mfano wana wa Israeli pale Kadeshi – Hesabu 14), au kuanguka kutokana na shinikizo la kishawishi (mfano Adamu na Eva katika bustani: Mwa. 3), tukio fulani maalum linakuwa kikwazo na kumwangusha kutoka katika mwendo wake wa kiroho:

Mlikuwa mkipiga mbio vyema; ni nani aliyewakwaza hata mkaacha kuitii kweli? Waga. 5:7

Katika nukuu hapa juu, mtume Paulo anawakemea Wagalatia kwa kuacha Injili ya kweli ya Kristo na kukumbatia ‘injili’ ya uwongo ya wokovu kupitia matendo “mema” iliyokuwa ikihubiriwa Asia kote na wapinzani wake [Paulo] waliokuwa na mtazamo na agenda ya “Kuyahudisha” (yaani watu waliokuwa wakifundisha kwamba ni lazima kutii Sheria ya Musa ili kuokolewa – na hata leo wako). Ijapokuwa Paulo anasema wazi kabisa na kukitaja kilichowafanya “wajikwae katika mwendo wao” na kuvuruga imani yao, kuna dalili/fununu katika sehemu nyingi za waraka huu kwamba tatizo linaweza kuwa ni uhasama na mabishano ndani ya kanisa hilo ambayo chanzo chake hakijulikani (cf. Waga. 5:15; 5:19-21; 5:26; 6:1-5; 6:9). Kwa sababu yoyote ile iwayo, waumini wengi katika kanisa la Galatia walikuwa hatarini kupoteza imani yao: kwa sababu yoyote ile iwayo (au sababu kadhaa), walianza kuvutiwa na dhana ya kubadilisha imani rahisi ya Injili ya kweli na kuukumbatia mfumo wa imani ya wokovu kupitia matendo ‘mema’. Wakati wowote kweli inapotelekezwa (kwa sababu yoyote ile), mbadala wa uwongo hauko mbali:

Tazama, mimi Paulo nawaambia ya kwamba mkitahiriwa, Kristo hatawafaidia kitu!
Waga. 5:2

Hakuna kishawishi, hakuna mtihani wa dhiki tutakaokabiliana nao utakaokuwa nje ya uwezo wetu kushinda, kwa imani (1Wakor. 10:13). Na Mungu wetu ni mwenye huruma, ambaye atatutia moyo katika [ma]shikizo yote tutakayokabiliana nayo (2Wakor. 1:2-7). Hata hivyo, itakuwa vyema kwetu kuwakumbuka Wagalatia na kushindwa kwao, kwani mfano anaoutumia Paulo wa mashindano ya riadha bado ni halali leo hii. Ibilisi anaporusha kizuizi katika njia yetu (iwe kishawishi au dhiki), kama hatutaruka juu ya kizuizi hicho kwa imani, basi tunaruhusu hatua zetu tunazotembea kwa imani zivurugike. Sasa, mara nyingi kitu kama hiki kitakuwa ni kupitiwa kwa muda tu. Punde tutakiri kushindwa kwetu (kutubu dhambi yetu: Yoh. 1:9 – tazama somo #15), na tutarudi tena kwenye uwanja baada ya kusimama pale tulipoanguka (yaani baada ya kupokea adhabu yetu), ukichukulia kwamba hatutolaumu wala kukasirika kwa kushindwa kwetu au kwa hatua za kinidhamu ambazo Mungu atazichukua [kwa upendo] dhidi yetu. Mwandishi wa barua kwa Waebrania pia anatumia analojia ya mashindano ya riadha kama kielelezo cha ustahamilivu katika dhiki tunazopitia, akisisitiza umuhimu wa kujizuia ‘ku-react’ vibaya pale Mungu anapotupa nidhamu tunapojikwaa njiani:

12.1  Basi na sisi pia [kama waumini wanaotajwa katika sura ya 11], kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii [watu na malaika], na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi [maeneo ya tabia zetu ambamo tuna udhaifu mkubwa zaidi]; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,
12.2  tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
12.3  Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao [waliotenda] dhambi [dhidi ya nafsi yake] juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu [na kukata tamaa].
12.4  Hamjafanya vita hata kumwagika damu [yenu], mkishindana na dhambi;
12.5  tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia (adhabu)ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye;
12.6  Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye [na kumpokea kama mwana].
12.7  [Basi chukueni adhabu yenu kwa mtazamo huu] - Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye?
12.8  Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali.
12.9  Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na/[ili] kuishi?
12.10  Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake.
12.11  Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani [yanamfanya muumini aelekee kwenye ukamilifu].
12.12  Kwa hiyo [tukirudi kwenye analojia yetu ya mashindano ya mbio] inyosheni mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza,
12.13  mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete [kiungo kilichoumia] kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe. Waebr. 12:1-13 SUV
Huu ni ushauri mzuri sana – lakini kwa masikitiko makubwa hatuufuati ushauri huu mara nyingi “tunapoanguka” kutokana na kujikwaa kiroho. Hii huwatokea hata wale waumini wakuu, kama mfano wa nabii Eliyah unavyotuonyesha. Baada ya kuteseka kwa vipindi virefu vya dhiki binafsi kama mkimbizi kutoka kwa mfalme Ahabu na mkewe Jezebeli (1Wafa. 17), na mara baada ya kupata ushindi mkuu dhidi ya manabii wa mungu-sanamu Baali (Wafa. 18), Eliyah aka-react kwa woga badala ya imani kwa vitisho vya Jezebeli na kuingia katika hofu kubwa ya kiroho (1Wafa. 19). Inaonekana kwamba hata nabii mkuu huyu alifikia kiwango cha kuvunjika moyo, na vitisho vya Jezebeli vikamzidi nguvu. Ni jambo la kushangaza kiasi fulani katika hulka zetu wanadamu kwamba mara nyingi tunashinda mitihani mikubwa kisha tunajikwaa na vigingi vidogo tu. Reaction ya Eliyah ilimfikisha mahala ambapo akajiona anamlaumu Mungu. Ama kwa hakika alijirudi, lakini ikiwa tuta-react kama yeye katika mazingira yanayofanana na kukaa chini [tulipoangukia] kwa muda mrefu kupita kiasi (tukimlaumu Mungu kwa shida zetu – iwe shida hizo zetu zinatokana na mitihani au nidhamu ya Mungu kwa makosa yetu: Waebr. 12:1-13), basi hapo tunajiingiza katika hatari ya kuanguka katika korongo la uasi. Kwani mwenendo kama huu – kama utaachwa uendelee – unaweza kuashiria maangamizi kwa imani yetu.

Ingawa ni muhimu sana kwetu sisi kuwa macho na hatari zinazoikabili imani yetu, hatari ya uasi itazidi na kuongezeka kwa kiasi kikubwa sana katika kipindi tusichokijua [lini] hapo siku za usoni. Moja kati ya nyenendo za kipindi cha Dhiki na Dhiki Kuu (ile miaka 7 itakayotangulia ujio wa pili wa Kristo: Matt. 24:21; 24:29; Mrk. 13:19; 13:24; 2Tim. 3:1; Ufu. 3:10), ni kipindi cha “Uasi Mkuu” wa Wakristo dhidi ya imani yao ambao mfano wake haujawahi kutokea (Matt. 24:10-13; 2Wathes. 2:3; 1Tim. 4:1). Sababu ya msingi uasi huu [dhidi ya Mungu] unaotabiriwa na maandiko ni udanganyifu ambao haujawahi kutokea utakaofanywa na Ibilisi na watumishi wake, mpinga kristo na kuhani wake mkuu (Dan. 11:32-35; Matt. 24:11, 24; Mrk. 13:32; 2Wathes. 2:9-12; 1Tim. 4:1-5; 2Tim. 3:8-9 pamoja na Kutoka 7:11; 7:22; Ufu. 13:13-14; 19:20). Taswira – pattern - ya Uasi Mkuu (kiwango kikubwa cha dhiki binafsi pamoja na vishawishi vingi vyenye nguvu vitakavyolenga watu wajiunge na mfumo wa kumpinga Kristo) inafanana kwa kiasi fulani na taswira ya aina hiyo hiyo inayoonekana siku zote katika dunia hii ya Ibilisi, ingawa kiwango cha ugumu utakaowakabili Wakristo wakati huo ujao na mkazo wa vishawishi vya uwongo utakuwa mkubwa zaidi. Taswira hii ni:

1) reaction ya muumini kwa kikwazo fulani kinachomrudisha nyuma (taabu na dhiki binafsi, nidhamu kutoka kwa Mungu, vishawishi).

2) kupokea na kuukubali mfumo fulani wa imani ya uwongo badala ya imani ya kweli katika Kristo.

Sehemu zote mbili za taswira ya uasi (kupoteza imani kwa Kristo) ni muhimu kuzijadili. Tunaingia katika hatari ya kuupokea uwongo baada ya kuukataa ukweli, na, kwa upande mwingine, ikiwa – badala ya kukataa mitihani na dhiki ambazo sote kama waumini katika Kristo ni lazima tupitie hapa duniani katika mfumo wa Shetani – tunaendelea kumwamini Mungu katika hizo nyakati ngumu, hatutakuwa mateka wa Ibilisi kwa kubadilisha kweli ya Kristo na kuweka mfumo fulani wa uwongo mahala pake (2Tim. 2:26). Mifumo hii ya uwongo mara nyingi ni ile ile ambayo hapo siku za nyuma tuliikataa na badala yake tukaipokea Injili ya Kristo (kama vile wana wa Israeli walivyotamani kurudi Misri: Neh. 9:16-18):

2.20  Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa [kiroho], hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.
2.21  Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa [ya imani kwa Kristo].
2Petro 2:20-21 SUV

Mchakato wa Uasi: Kwa kawaida Mkristo hafanyi uasi [ndani ya] usiku mmoja tu. Kuna hatua anazopitia kati ya azimio la moyoni la kuwa Bwana Yesu Kristo ndiye Mwokozi wake, na pale mwishoni anapomkataa Bwana. Hivyo kutoka imani mpaka uasi, kuna hatua zifuatazo ambazo hupitiwa, kwa ujumla:

1) imani inakabiliwa na changamoto; muumini ana-react (anaonyesha athari).

2) moyo unakuwa mgumu.

3) mfumo mbadala unapokelewa na kuchukua nafasi ya imani sahihi.

4) imani sahihi inaharibiwa.

1. Imani inapata changamoto; muumini ana-react (anaonyesha athari): Kama tulivyoona hapo juu, vikwazo vya aina mbalimbali vinaweza kumwangusha muumini, vikakatisha mwendo wake kwa muda, vikavuruga hatua zake anapopiga mbio kuelekea lengo lake. Wakati mwingine vikwazo hivi ni kushindwa kwa nafsi kwa kiasi kikubwa au kidogo (yaani dhambi binafsi ambazo huleta adhabu ya nidhamu kutoka kwa Mungu ambayo nayo muumini anaikasirikia badala ya kukiri na kutubu, na kumrudia Mungu). Wakati mwingine vikwazo hivi ni mitihani na magumu yenye malengo ya kuimarisha imani na kuupa kasi mwendo wa kukua kiroho (kushindwa mitihani katika hali hii, ambapo muumini anakasirika au analaumu anaonyesha kuchoka badala ya kumwamini Mungu kwamba atamvusha katikati ya magumu hayo kwa usalama). Vyovyote vile itakavyokuwa, na kikwazo chochote kile kinacholeta changamoto ambayo inasababisha muumini kukasirika, kukata tamaa, na kupoteza imani (kuasi), bila shaka kila mmoja wetu anamfahamu mtu/watu ambao wamejikwaa kwa namna hii. Mara nyingi kuna tukio moja baya na la kutisha lililomtokea muumini, ambalo kwalo muumini huyu anamlaumu Mungu (ijapokuwa anaweza asiseme hilo). Ni lazima tukumbuke kuwa mtazamo wa namna hii sio sahihi kabisa: tatizo si Mungu hapa, wala Yeye hajaonyesha kuwa si mwaminifu, na kwa kweli hawezi kuwa si mwaminifu (2Tim. 2:11-13). Hata kama mazingira yetu ya shida yanaonekana kuwa ni “ya uonevu” kiasi gani, ni muhimu kutosahau kwamba sisi wanadamau hatufahamu na hatuna fununu zote za yanayoendelea katika ulimwengu wa hapa duniani na wa kiroho (yaani hatuoni na hatuwezi kuona picha kamili – Ayubu 38-41), na kwamba Mungu yuko sahihi katika kila analofanya na mwongofu, ingawa hatuwezi kueleza kwa nini kila tukio linalotupata linatupata kwa sababu gani, na kila kikwazo kinachotokea ni kwa sababu na kwa malengo gani, kwetu sisi wenyewe na kwa wengine pia.

Tunaporuhusu changamoto za imani yetu zitutingishe na kutuvuruga, tutasahau mema yote ambayo Mungu ametufanyia. Ingawa Aliwakomboa kutoka utumwani, akawaonyesha uweza wake na upendo wake kwao katika miujiza mingi, aliwalisha kwa “mkate wa mbinguni” na akawanywesha kwa “maji kutoka katika mwamba”, aliwalinda na kuwalea katika jangwa, lakini bado wana wa Israeli wa kizazi cha kutoka Misri hawakufanikiwa kufaulu mtihani wa imani. Mara kumi “walimjaribu Mungu kwa dharau” waki-react mara hii kwa mitihani kutoka kwa Mungu, mara hii kwa vishawishi vya tamaa zao wenyewe, mpaka mwishoni wakaitupilia mbali nafasi yao ya kuiona nchi ya ahadi, naye Mungu badala yake “akawaua kule mwituni” (Hesabu 14:20-23; 1Wakor. 10:1-13):

3.12  Angalieni [tahadharini], ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu [mwovu] wa kutokuamini, kwa kujitenga [kuasi kutoka kwa] na Mungu aliye hai.
3.13  Lakini mwonyane [na kutiana moyo] kila siku, maadamu iitwapo leo [tunapoendelea kuwa duniani]; ili mmoja wenu asifanywe mgumu [moyoni] kwa udanganyifu wa dhambi.
3.14  Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu [wa imani] kwa nguvu mpaka mwisho;
3.15  hapo inenwapo:

Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa [ule walipomkasirisha] kukasirisha [pale Meribah].

3.16  Maana ni akina nani walio[m]kasirisha, waliposikia? Si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa?
3.17  Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arobaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka [ilizagaa] katika jangwa?
3.18  Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika raha yake, ila wale walioasi?
3.19  Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.
Ndiyo, kizazi hiki cha Israeli walisahau yote mazuri ambayo Mungu aliwafanyia kabla. Wakaruhusu shida za kila siku na hamu za hapa na pale kuwa changamoto kwa imani yao, na wakavuna walichopanda. Tunapaswa kujifunza kutoka kwa mfano wao hasi, na kamwe tusisahau yote mema ambayo Mungu ametufanyia, ingawa hata sisi tutapitia hali ngumu ya maisha. Sasa, “kitu kikuu kizuri” ambacho Mungu amefanya kwa ajili yetu ni kutupa zawadi ya Mwanaye, Bwana Yesu Kristo – yaani Yeye afe ili sisi tuweze kuishi milele naye. Hakuna mateso, hakuna vikwazo, hakuna dharau tutakayoonyeshwa, hakuna tamaa, hakuna hamu, hakuna faida ya mali tunayoweza kupata - hata kama ni kupata dunia nzima, yenye thamani ya kutufanya tuharibu urithi wetu wa uzima wa milele tulio nao kupitia imani katika Bwana Yesu Kristo. Hatuwezi kujiacha tuwe na machungu, kuvunjika moyo, au kuchoshwa, au kuacha kujali, au mwisho kuruhusu hisia yoyote au athari iingilie maisha yetu na kututenganisha na Yeye tunayepaswa kumpenda zaidi ya wote wengine. Na tunapaswa kuutunza uhusiano huu tulionao Naye kwa gharama yoyote ile. Na changamoto hii ni vigumu kuipambanua (na wakati mwingine inanyemelea bila sisi wenyewe kuitambua haraka!) tukiwa katikati ya nyendo zinazokanganya za maisha. Haitoshi [kwamba] ati “tuna ufahamu akilini mwetu” juu ya FULANI anayeitwa Kristo ambaye mara moja moja “tunakumbuka” kumwabudu. Kwani hata pepo wanatambua uwepo wa Mungu, lakini uelewa huu hautowaweka nje ya jehanamu (Yoh. 2:19)! Ni lazima, kwa gharama yoyote ile, tuendeleze uhusiano wetu na Bwana Yesu Kristo – utii wetu, uaminifu wetu, upendo wetu, kujiwajibisha kwetu, ufuasi wetu, tumaini letu, imani yetu isiyotikisika, katika Yeye.

Bila ya kuwa na imani endelevu, tutatenganishwa na familia ya Mungu, kama ambavyo kutokuwa na imani kunamweka mtu nje ya familia hiyo (War. 11:20-21). Tuna fursa nyingi kama Wakristo, za kutufanya tuache kumfuata Bwana wetu, kugeuka na kuelekea/kurudi katika “nchi ya kutoamini” (Waebr. 11:15). Changamoto iliyoko ni kuendelea kumfuata Yeye wakati imani yetu imewekwa chini ya shinikizo. Na hakuna njia nyingine. Hatuwezi kutelekeza imani yetu kwa Kristo na tukabaki kuwa wa Kristo, kwani maana ya neno ‘Wakristo’ katika Biblia ni “wale wanaoamini” (kw. mf. War. 3:22). Hivyo ni lazima tuwe macho na kujichunga tusigeuke kulia wala kushoto, bali tumfuate Bwana wetu katika njia iliyonyooka, tukijichunguza ili tuone ikiwa bado tuko “katika imani” (2Wakor. 13:5). Baadhi ya mbegu za imani (soma Matt. 13:1-23; Mrk. 4:1-20; Lk. 8:4-15 & 10:23-24; na Petro Somo #12) hazichipui kwa sababu zinaghilibiwa [na uwongo], lakini tunapaswa kuamini neno la Mungu; mbegu zingine hazioti mizizi, kwa sababu zinakaushwa na shida, bali tunapaswa kumwamini Yeye wakati wa shida; nyingine hazizai matunda, kwa sababu zinasongwa/zinashinikizwa na hofu na udanganyifu wa maisha hapa duniani, lakini tunapaswa kushinda na kupanda juu ya ukinzani wa dunia ya Shetani. Sasa, Ibilisi kwa uhakika anajua wakati ambao imani yetu inaweza kushambuliwa kwa mafanikio, na wakati ambapo kuna ‘udhaifu’ anaoweza kuutumia kushambulia uaminifu wetu. Tunaweza kuona “sampuli” ya mbinu za Shetani katika majaribu ya Bwana wetu Yesu Kristo, na tunapaswa kufuata mfano wake katika kuyakabili na kuyashinda:

4.1 Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi.
4.2 Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona [akiwa na] njaa.
4.3 Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate.
4.4 Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
4.5 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu,
4.6 akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.
4.7 Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.
4.8 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno [vantage point], akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake,
4.9 akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia.
4.10 Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.
4.11 Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia.
Matthew 4:1-11 SUV

• anashambulia imani yetu wakati anapoona yawezekana tukawa dhaifu kwa sababu ya shinikizo au ufukara: Ibilisi alimshawishi Kristo (aya ya 3) ili atumie uweza Wake kwa faida yake mwenyewe (yaani, ageuze mawe kuwa mkate), kunyume na mpango wa Mungu. Tunapokabiliwa na magumu na ufukara, tusiruhusu imani yetu kushindwa na shinikizo hilo. Ijapokuwa hatuwezi kufanya mawe yawe mkate, tutashawishika ili tuvunje amri ya Mungu, kutenda dhambi, kwa mfano, tunaposhinikizwa na matukio (kwa mfano uhitaji mkuu na ufukara). Badala ya kushindwa na shinikizo hilo na kulitumia kama kisingizio kufanya mambo kinyume na imani, tunapaswa kulinda imani yetu na kumtegemea Mungu kama Kristo alivyofanya, tukikumbuka kwamba “mtu haishi kwa mkate pekee, bali kwa kila Neno litokalo kinywani mwa Mungu”.

• anashambulia imani yetu wakati anapoona tunaweza kuwa dhaifu kwa sababu ya majaribu au tamaa: Ibilisi alimjaribu Kristo (aya za 5-6) kwa kumshawishi atende bila hadhari na kuamua haraka bila kufikiri kwa kumweka Mungu katika hali ya kulazimika kumwokoa kutoka katika mazingira magumu. Tunapoona “fursa” ya dhambi ya msukumo wa haraka , ni lazima tutambue kwamba hiyo “fursa” ni mtego na kuikataa kama Kristo alivyokataa, tukikumbuka “usimjaribu Bwana Mungu wako”.

• anashambulia imani yetu wakati anapoona kuwa tunaweza kuwa dhaifu kwa sababu ya kutojua (ujinga) na kupoteza mwelekeo wa kiroho: Ibilisi alimjaribu Kristo (aya za 8-9) apokee kutoka kwake (Ibilisi) kitu ambacho mwisho wa dahari kitakuwa mali ya Kristo, yaani utawala wa dunia. Mara nyingi nasi pia tutakabiliwa na majaribu ya kijanja sana ambapo mahitaji yetu sahihi yatapata ufumbuzi kwa njia zisizo sahihi. Kristo ndiye mtawala ajaye wa ulimwengu, lakini kumwabudu Shetani ili apate utawala huo si sahihi. Nasi pia tunaweza kukabiliwa na jaribu la kupewa “vitu halali tunavyohitaji au kuvitaka” lakini katika “namna isiyo halali”. Ni elimu na ufahamu kamilifu wa maandiko, kuendelea kukua kiroho, na uangalifu mwingi ndio kutapunguza hatari ya kuanguka katika mitego ya kijanja ya namna hiyo, ili nasi tuweze kusema, kama Kristo alivyosema: “Ondoka mbele yangu Shetani. Kwani imeandikwa: ‘Mwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie Yeye tu’”.

2. Moyo Unakuwa Mgumu(1): Kati ya kuonyesha athari [hasi] za mwanzo (hasira, kulaumu, kukata tamaa, kuchoka, n.k.) kwa sababu ya mateso, majaribu fulani, iwe mhusika anastahili (nidhamu kutoka kwa Mungu) au hastahili (mitihani), na kuasi au kumkataa Kristo, kuna mchakato wa kisaikolojia ambao Biblia inauita “moyo kuwa mgumu”. Moyo kuwa mgumu ni mchakato wa upofu wa kiroho unaoongezeka polepole ambao dalili yake siku zote ni kuongezeka kwa dhambi na kupungua kwa imani – vikienda sambamba. “Moyo kuwa mgumu” katika kiini chake ni kurejea katika mitazamo [iliyoachwa wakati mtu anazaliwa upya] iliyo kinyume na Mungu na mapenzi Yake, na mwisho wake inapelekea mtu anayehusika kurudi katika hali yake ya kwanza ya kutoamini. Hata katika hatua zake za mwanzoni, “moyo kuwa mgumu” huleta vurugu katika maisha yetu ya kiroho na ni tishio la kweli kwa wokovu wetu. Kama vile ugumu wa mishipa ya damu ya mwili hubana mtiririko wa damu na kuhatarisha moyo wa mwanadamu, na mara nyingi hupelekea kwenye kifo cha mtu huyo, vivyo hivyo moyo wa kiroho unapokuwa mgumu unabana mtiririko wa ile kweli ndani yake na inaleta hatari kubwa katika maisha ya kiroho ya Mkristo huyu. Katika kadhia (case) kali kabisa [ya jambo hili], huweza kupelekea kwenye kifo cha kiroho kinachoitwa uasi (apostasy), ambapo kweli inatupwa kabisa na aina fulani ya uwongo inakubaliwa/inapokelewa mahala pake, na ambapo mtu huyu aliyekuwa Mkristo hapo mwanzo anakuwa [sasa] hana tena imani hiyo kwa Kristo.

a. Moyo na maana yake Ki-biblia: Kama tulivyoona katika somo la hapo nyuma (somo #16), katika Biblia, moyo unawakilisha yule mtu wa ndani. Haswa haswa, moyoni ni mahala tofauti na 1) sehemu ya kiroho, 2) sehemu ya kimwili ya asili yetu. Kwa maelezo mahususi, moyoni ni pale mahala ambapo mwili wetu na roho yetu [ya milele] vinapounganishwa (1Wakor. 14:14; cf. 1Wakor. 2:12; kwa aya zinazoainisha mwingiliano huu, tizama kwa mfano Kumb. 2:30; Zab. 7:9; cf. Matt. 18:55; Wafi. 4:7). Pakiwa ndiyo “kiungo” cha mwili wetu wa sasa na roho yetu ya milele [ambayo katika ufufuo itavishwa na mwili mpya mkamilifu, usioharibika), moyoni ndipo ambapo fikra na hisia, ziwe mbaya au nzuri, hufanyika (Mithali 23:7). Moyoni ndipo tunapomtukuza Mungu, lakini pia ndipo panapotokea “fikra za uovu, mauaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushuhuda wa uwongo na matusi” (Matt. 15:18-19). Ni waumini wa Kristo pekee wenye uwezekano wa kweli wa kushinda, kuizidi nguvu ile tabia ya zamani [kabla ya kuzaliwa upya] ya fikra za kidunia ambazo moyo umezoea (1Wakor. 2:14-15), na kwa hakika tumeamriwa hivyo (War. 12:2). Kwa kifupi, moyo wetu [ulivyo], ndivyo “nasi tulivyo kiuhalisia”, mtu [wote] wa ndani, ukijumuisha fikra, matumaini na ndoto zetu, hisia, madhaifu na mapungufu. Siku zote roho zetu zinapokuwa ndani ya mwili huu na tabia zake potofu, hatuwezi kutenganisha [kwa kiwango cha ukamilifu] zoho zetu hizi kutoka kwenye majaribu na udhaifu (Matt. 26:41; War. 7:14-25; tizama somo #15 juu ya dhambi na kitubio), lakini tunaweza kubadilisha nafsi zetu za ndani, yaani mioyo yetu, kwa uweza wa Roho ya Mungu na Neno la Mungu (War. 12:2; Waefe. 4:21-24; tizama haswa somo#17).

b. Moyo asilia: Tulipokuwa tusioamini, tuliamua kutomsikiliza Mungu, na matokeo yake “moyo wetu mgumu usio na toba” ulituingiza katika ghadhabu ya Mungu (War. 2:5). Mioyo yetu iliumbwa ili kupokea mwanga wa Mungu, lakini [mioyo hii] ilijaa giza (Matt. 6:22-23); iliumbwa kuelewa kweli ya Mungu, lakini ikawa migumu (War. 2:5). Tulikuwa “katika ujinga uliojaa kiburi wa akili zetu, uelewa wetu ukaingia giza na kutengwa kutoka uzima wa Mungu” na mioyo yetu ikawa migumu (Waefe. 4:18; tizama pia War. 11:7; 11:25). Tukawa vipofu katika roho zetu (Marko 6:52; 8:17-21). Ijapokuwa ugumu huu ulikuwa na (na bado unao) viwango vyake (Kutoka 4:21; 7:13; 8:15), kwa kiasi hiki au kile, sisi sote tulikuwa na mioyo migumu, tukiwa hatuwezi kuona wala kuelewa kweli ya Mungu – mpaka Roho wake Mtakatifu alipotuletea Injili inayotia mwanga ya Bwana Yesu Kristo, na macho ya mioyo yetu yakafunguliwa na tukamwona Yeye na tukampokea kama Mwokozi wetu (Yoh. 1:8-9; 2Wakor. 4:4; 2Tim. 1:10).

c. Mwanzo mpya wa moyo: Tunapookolewa, kila kitu kinakuwa kipya. Ugumu na giza na usugu wa mioyo unaondolewa papo hapo tunapompokea Kristo kuwa ndiye Mwokozi wetu. Tunapata nguvu mpya katika maisha yetu ya kiroho – papo hapo. Mioyo yetu “inasafishwa kwa imani” (Mat. 15:9), na sasa tunaweza kuuona ukweli wa Mungu. Tunapata, kwa maana fulani, “mioyo mipya” (Eze. 11:18-21). Hali ya zamani ya kutoamini imeondoka, na katika Kristo sasa tumekuwa “viumbe vipya” na mioyo yetu imekuwa huru kutoka ule ugumu na upofu wa zamani (2Wakor. 5:17; Wagal. 6:15). Hii katika kiini chake inamaanisha kwamba ile nguvu ya mienendo ya upinzani dhidi ya Mungu, pingu zote zilizofunga uelewa wetu wa kiroho zinavunjwa, na sisi, imani yetu, inakuwa huru kumfuata Mungu bila vizuizi. Pamoja na zawadi ya uzima wa milele, tunapewa fursa na nafasi ya kuwa na fikra safi zilizotakaswa kulingana na hayo maisha mapya yaliyotakaswa. Hii haina maana kwamba sasa hivi tunajua kila kitu tunachohitaji kujua kama waumini – hata kidogo: bado tunahitaji kukua kiroho. Bali inamaanisha kwamba sasa hivi hatuna kizuizi. Mungu ametupatia mwanzo mpya moyoni. Tunapaswa wakati wote kuwa na tahadhari, hata hivyo, dhidi ya kujirudia kwa mienendo mibaya ya zamani iliyotutenga na Mungu katika hali yetu [ya zamani] ya kutoamini.
d. Usiufanye moyo wako kuwa mgumu: Hata hivyo, wokovu ni mwanzo tu wa safari yako. Unabaki na uwezekano wa kuufanya moyo wako kuwa mgumu katika siku za usoni, hata kwa waumini. Chanzo katika matukio yote ya kurudi tena katika upofu wa kiroho, upinzani dhidi ya Mungu na kutomsikiliza Mungu ni dhambi binafsi. Ni jambo la wazi kwamba dhambi, ambayo maana yake ni kumkataa Mungu na mamlaka Yake juu yetu, inatutenganisha Naye na kupunguza usikivu wetu wa mapenzi Yake (“masikio” ya mioyo yetu yanaingia sugu) na uongozi wa Roho wake Mtakatifu (tizama somo #15 na somo #16). Sasa, sisi sote hukabiliwa na majaribu na sote hutenda dhambi (Mithali 20:9) – kwa sababu bado tunaishi ndani ya mwili wa/wenye dhambi, tutatenda dhambi wakati fulani, baada ya kuzidiwa na majaribu hayo (War. 7). Lakini kuna tofauti kubwa sana kati ya kuteleza au kuanguka mara moja moja (ambapo Mungu hutupa adhabu ya nidhamu kama Baba, na inatarajiwa kwamba tutasikia, tutatubu na tutajirekebisha) kwa muumini anayejiendeleza kiroho na yule aliyejiachia jumla katika dhambi bila kitubio. Tunapozikabili dhambi zetu, tunapokiri kwa Mungu na kugeuka, tunaweza kutumainia kupata kuponywa kutoka dhambi hizo pamoja na adhabu, na kutakaswa mioyo yetu. Lakini kama, kwa upande mwingine, tunaacha dhambi iendelee katika maisha yetu na tunaiacha ikue na kuongezeka mioyoni mwetu, itaanza kuisonga imani yetu, maotokeo yake ni mioyo yetu kuwa migumu zaidi. Kwa sababu hii maandiko yanatuonya: “msifanye mioyo yenu kuwa migumu ...” kama walivyofanya wana wa Israeli wa kile kizazi cha kutoka Misri (Waebr. 3:8; 3:15; 4:7), kwani mwisho wao unaosikitisha ni mfano kwa sisi wote wa hatari ya mwenendo wa namna hiyo (1Wakor. 10:11). Kufanywa upya au kuhuishwa wakati wote kunawezekana tunapomrudia Mungu na kukiri dhambi zetu, lakini tukiendelea kuwa wagumu katika ukinzani wetu dhidi ya Mungu, matokeo yake ni mioyo yetu kuwa migumu.

e. Moyo kuwa mgumu: Tunauona mchakato wa moyo kuwa mgumu wazi kabisa katika kitabu/waraka cha Waebrania (nukuu ya hapo juu) ambapo mwandishi wake asiyejulikana anajadili hatua za mchakato huo:

3.12  Angalieni [tahadharini], ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu [mwovu] wa kutokuamini, kwa kujitenga [kuasi kutoka kwa] na Mungu aliye hai.
3.13  Lakini mwonyane [na kutiana moyo] kila siku, maadamu iitwapo leo [tunapoendelea kuwa duniani]; ili mmoja wenu asifanywe mgumu [moyoni] kwa udanganyifu wa dhambi.
Waebr. 3:12-13 SUV

Katika uchambuzi wa mwandishi, uasi (kumgeuka Mungu) unamatokeo angamizi katika moyo, unaufanya moyo kuwa “mwovu”. Na nguvu inayoendesha mchakato wa kuufanya moyo kuwa mgumu ni “udanganyifu wa [matendo ya] dhambi”. Suala hili liko wazi. Maisha katika dhambi (siyo kuanguka mara moja moja, bali kuendelea kutenda dhambi bila kikomo au bila kitubio) hayaendani na imani, kwani kuamini au imani haiwezi kutenganishwa na utiifu. Hatuwezi kutumikia dhambi na Mungu kwa wakati mmoja, au hata nyakati mbalimbali katika maisha yetu kama Wakristo, kwani kama tukikumbatia dhambi na kumwacha Mungu, tutaacha kuwamini Kristo, tutaacha kumtii Kristo. Kama Yohana anavyotuambia, “yule aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi” 1Yoh. 5:18. Yaani, maisha ya dhambi ni dalili kwamba dhambi imezidi imani, na kwamba mtu huyu si muumini wa Kristo tena (au yuko katika hatari kubwa ya kuasi).

f. Moyo ulio mgumu: Na hivyo, tukiendelea katika njia isiyofaa kwa muda mrefu, tutafikia wakati katika kuporomoka kwetu kiroho ambapo hatutamtazama (au hatutaweza tena kumtazama) Mungu usoni, kwa lugha nyepesi. Sababu yoyote ile au kikwazo chochote kile kilichotufanya tukeuge kutoka kwa Mungu, tukatoka katika njia ya uzima wa milele, dhamiri sasa zimeungua kufikia kiwango cha kuhalalisha kufanya kitu chocho tunachotaka (2Tim. 3:8; Tito 1:15), mioyo yetu imeingia giza (Waefe. 4:18-19), na hatuna shauku tena ya kuwa na uhusiano wa maana na Mungu kwa masharti Yake – ambayo ni kumfuata Bwana Yesu Kristo kwa uaminifu (War. 1:18-21).

3. Mfumo mbadala wa imani unapokelewa: Tunapoamua kumtelekeza Mungu na njia ya wokovu aliyoamuru tuitumie, yaani imani kwa Mwanaye, Bwana Yesu Kristo, vivyo hivyo Mungu naye anatutelekeza, anatuacha na mihemuko yetu ya asili ya dhambi tuliyoamua kuifuata badala ya Mwana wake aliyetupatia kwa gharama Yake mwenyewe (War. 1:24; 1:26,28; Waefe. 4:19). Ni kejeli inayotia uchungu kwamba badala ya kuwa huru (kutoka katika “pingu” za kufanya mapenzi ya Mungu, wale wanaochagua njia isiyoaminika ya uasi wanajikuta badala yake wakiwa watumwa wa bwana mwingine: dhambi (Yoh. 8:34;2Pet. 2:19; cf. 4:8-11). Kwani ni kweli ya hulka yetu ya kibinadamu kwamba ni lazima tuchague kumtumikia bwana mmoja au mwingine, na kama tunachagua kumkataa Mungu, ni lazima tuchague kukubali mbadala Wake ambao asili yake ni ya dhambi na huo mbadala ndio utakuwa “Mungu”, hata kama sisi wenyewe tutauita au hatutauita huo mbadala “mungu” (ni kwa sababu hii, kwa mfano, maandiko yanatufundisha kwamba tamaa (ya mali au/na ya madaraka, n.k.) kuwa ni ibada ya sanamu (idolatry) – Wakol. 3:5; cf. Waefe. 5:5. Hili haliepukiki kwani ni lazima tuchague kati ya kuwa na Kristo au kutokuwa Naye (Matt. 12:30); hatuwezi kumtumikia Mungu na pia kumtumikia Mammon (‘mungu’ wa kipagani wa ulafi na uchoyo) kwa wakati mmoja (Matt. 6:24; Lk. 16:13); tutavutwa kwenda Mlima Sinai au kwenda iliko Yerusalemu ya mbinguni, na siyo vyote (Wagal. 4:21 – 5:1). Kama vile wana wa Israeli walivyowageukia miungu wa uwongo (Kumb. 8:10-20), Wagalatia walivyoyageukia mafundisho ya uwongo ya Wayahudishi (Judaizers – Waga. 1:6-9), kanisa la mwanzo lilivyowageukia Wanostiki na Wanikolai (Nicolaitans) – kwa mfano Ufunuo 2:6, na wale wanaomwasi Mungu leo wanavyogeukia mambo yao wenyewe (iwe ni kujiunga na “cult” mpya, ya kisasa au matamanio yao wenyewe) na hivyo kufanya uchaguzi ambao ni kinyume na Mungu, Kinyume na Kristo, maana yake ni kuchagua kitu kingine na kukifanya kuwa ndiyo “sanamu” yako ya ibada, iwe inafanywa waziwazi au la. Mwisho wake, kama tukimgeuka Mungu na imani katika Kristo ambayo tulikuwa nayo hapo mwanzo, ni kwamba nasi tunageukia Misri, tunarudi kwenye lile giza la zamani la mioyo yetu, tunarudi kwa kile tulichokitapika kwa sababu hakikuwa na faida za kiroho, na hivyo tunakuwa na hali mbaya zaidi kuliko ile ya zamani (2Pet. 2:20-21; cf. Eze. 16).

4. Imani inaharibika: Kuwa mwanafunzi wa Bwana Yesu si jambo rahisi. Mwokozi wetu alituambia “tuhesabu gharama” kabla ya kubeba jukumu la maisha la kumfuata Yeye katika dunia hii (Lk. 14:26-35). Taswira aliyoionyesha ina changamoto nyingi kiasi kwamba wengi wameepa kuwa wanafunzi Wake (Yoh. 6:60-66; cf. Matt. 10:32-39), hata hivyo Anatuhakikishia kwamba nira Yake ni rahisi (yaani inafaa kwa ajili yetu: Matt. 11:29-30), kwamba ikiwa tutakuwa na imani, yote yawezekana tukiwa Naye (Matt. 19:23-26). Mara tukishaingia katika makubaliano, tukipokea ahadi yake ya uzima wa milele kupitia imani kwake Yeye, suala linakuwa la imani endelevu Kwake, la kuishi kwa imani (War. 1:17; Waebr. 10:38), na linakuwa la uaminifu, la kumfuata kwa utiifu (1Pet. 1:2; 4:17).

Mwisho wa mchakato wa uasi, wa imani chini ya shinikizo, hali inapelekea katika ugumu wa moyo, ambao nao unapelekea katika kukubali mbadala wa Mungu na mwanaye, ni kifo cha imani ya mhusika. Yule muumini-wa-wakati-fulani ambaye anaruhusu shinikizo juu ya imani yake kumwondoa kutoka kwa Mungu na kumpeleka katika dhambi, ambaye anaanguka kando ya njia na kuuacha moyo wake kuwa mgumu dhidi ya kweli ya Mungu, anapitia kitu kile kile kilichowatokea waumini-wa-wakati-fulani wa kizazi cha kutoka Misri. Hawakuingia katika nchi ya ahadi kwa sababu 1) Hawakuendelea katika imani kwa Mungu pale mambo yalipokwama na kutoenda kama walivyotarajia (Waebr. 3:19); 2) hawakumtii Mungu pale Alipowapima ili kuona kama imani yao ilikuwa halisi (Waebr. 4:6). Katika kiini chake, imani na utii ni kitu kimoja (Yoh. 3:36). Kama kweli unaamini, utatii; na unatii kwa sababu unaamini kwelikweli. Una uzima wa milele katika Bwana Yesu Kristo kupitia imani katika Injili, lakini kama tu “utaishika imani yako bila kuiacha au kulegeza mkono” katika utii wako kwa Kristo (Matt. 10:33; Lk. 12:9; 1Wakor. 15:2; cf. Pia Wakol. 1:23; 2Tim. 2:11-13). Kama vile sisi tunaomwamini Bwana Yesu Kristo tunasimama kwa sababu ya imani yetu, basi na wale wanaoanguka wanaanguka kwa sababu ya kutoamini (War. 11:20-23), lakini kama mtume Paulo anavyotuambia, hili laweza kubadilika. Moyo kuwa mgumu, upofu wa kiroho unaoendelea ambao huambatana na dhambi na kutokumtii Mungu, kama hakutadhibitiwa, kutaizima imani yetu. Na hivyo tunatahadharishwa:

3.7  Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mtaisikia sauti yake,
3.8  Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha [wakati wa Kutoka Misri], Siku ya kujaribiwa katika jangwa,
3.9  Hapo baba zenu waliponijaribu,
Waebr. 3:7-9a

Haya basi, na tuwe na tahadhari, na togope hata “kivuli tu cha kumgeuka Mungu”. Na tuchukue hatua, hata kama zinauma, ili tukae karibu na Mungu wetu, tukikiri na kutubu dhambi zetu kila zinapotokea, na kupokea yote yanayotoka katika mkono Wake, yawe matamu au machungu, tukijua kwamba kwa uwezo Wake yote yanafanywa kuwa mema kwa ajili yetu (War. 8:28). Na tuepukane na njia yoyote inayoteleza inayoelekea kwenye uasi, ambako kunatufanya tumgeuke Mungu wetu, kwa kujifunza na kutafakari namna uasi unavyotokea:

4.17  Basi nasema neno hili, tena nashuhudia [nasisitiza] katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao [za kutoamini];
4.18  ambao; akili zao zimetiwa [uelewa wao umeingia] giza, nao wamefarikishwa [wametengwa] na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao;
4.19  ambao wakiisha kufa ganzi [wamepoteza dira ya kilicho chema] wanajitia katika mambo ya ufisadi [kuridhisha nafsi] wapate kufanyiza kila namna ya uchafu kwa kutamani [tamaa isiyo kikomo] (yaani wamepata mbadala wa Mungu).
4.20  Bali ninyi, sivyo mlivyojifunza Kristo;
Waefe. 4:17-20

Notes:

1. Ili kusoma kwa undani na kupata mifano katika maandiko, soma “Exodus 14: Hardening Pharao’s Heart”.

=0=

Imetafsiriwa kutoka: Reactions to Personal Tribulation: Peter’s Epistles #26

=0=

Basi, na tuonane katika somo #27 la mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!