Utakaso Katika Maisha ya Muumini Duniani: Kujilinda Kikristo Katika Vita ya Kiroho
Nyaraka za Mtume Petro #30
1Petro 1:14-16
Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa https://ichthys.com
Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo
Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for this Kiswahili Translation has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill
1Petro 1:14-16:
1.14 Kama watoto watiifu, msizifuate tamaa zenu za kale mlizozifuata [mlipokuwa] katika ujinga wenu [wa ile kweli];
1.15 bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;
1.16 kwa maana imeandikwa, Muwe watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu (Walawi 14:44).
Kama tulivyoona kabla, maneno katika Agano Jipya ambayo yanazungumzia dhana ya utakatifu yananyumbulishwa kutoka neno-mzizi (root) hag (cf. Hagia Sofia), na yalitafsiriwa [na kuingizwa] katika Vulgate (tafsiri ya Biblia katika Kilatini) pamoja na maneno ya Kilatini yanayohusiana na neno sanctus. Hivyo maneno “aliyetakaswa” na “mtakatifu” ni vivumishi kisawe (synonymous adjectives, au kwa maneno mengine ni maneno-sifa yanayokaribiana sana katika maana) lakini yote mawili yanawakilisha dhana moja katika maandiko. [NB: Katika Kiingereza, maneno “sanctification” na “holy” ni synonymous adjectives (yaani vivumishi kisawe) zilizonyumbulishwa kutoka lugha za Kilatini na Kijerumani, lakini maneno yote mawili yanawakilisha dhana ile ile Kibiblia]. Kwa maneno mengine, ijapokuwa katika matumizi ya kawaida maneno “utakaso” na “utakatifu” yanaweza kusababisha hisia tofauti au kupendekeza dhana tofauti kwa watu mbalimbali, kwa uhalisia yanamaanisha dhana moja katika maandiko ambayo ni “utengano na dhambi na uovu”. Tumekwishaona kuwa utakaso, kama ilivyo kwa wokovu, unafanywa na Mungu katika awamu tatu. Kama ilivyo kwamba kwa sasa “tumeokolewa” kwa maana ya hadhi (status) yetu mbele ya macho Yake ingawa hatujaanza kufurahia thawabu zetu wala ufufuo, vivyo hivyo waumini katika Kristo “wametakaswa” kwa sasa (au ni “watakatifu”) kama Mungu anavyotutazama au anavyotuchukulia, ingawa bado hatujapewa ile miili mitakatifu yenye uwezo wa kushinda dhambi. Kati ya hali hizi mbili za “utakaso wa mwanzo – positional sanctification” (na wokovu unaoambatana nao) na “utakaso wa siku ya mwisho – ultimate sanctification”: utakaso-hitimisho (na wokovu unaoambatana nao), tunajikuta tukitembea na kupita katika dunia hii katika nyayo za Bwana wetu, tukijaribu kufanya yale Anayotaka tuyafanye (na kuacha yale Anayotaka tuyaache). Huu utakaso “katika maisha ya muumini hapa duniani” ndio ambao Petro anauzungumzia katika aya ya 14-16 ya sura ya kwanza ya waraka wake wa kwanza hapo juu. Na kama ambavyo hapa duniani “tunatenda kazi” ya wokovu wetu (Wafi. 2:12) – kupitia vita hii ya kuimarisha imani yetu ambayo kwa wakati huu tumo katikati yake (1Pet. 1:5; 1:9) – vivyo hivyo, kwa hakika ikiwa ni sehemu ya vita hii hii, sisi waumini ni lazima tujitahidi kutembea mbele za Bwana wetu katika namna iliyotakaswa na iliyo takatifu.
4.3 Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu (yaani mjitenge na dhambi). [Yeye anataka] mwepukane na [dhambi];
4.4 kila mmoja wenu ajue kuuweza (kuutawala) mwili wake katika utakatifu na [mwenendo wa] heshima;
4.5 si [kuanguka] katika hali ya tamaa mbaya, kama [watu wa] Mataifa wasiomjua Mungu.
4.6 [Ili usifanye makosa na kumshawishi ndugu yako katika Kristo mkatenda naye dhambi] kwa sababu Bwana ndiye alipizaye kisasi cha haya yote; kama [nilivyowaonya mwanzo] na tukashuhudia sana [kuhusu hili].
4.7 Maana Mungu hakutuitia uchafu, bali tuwe katika utakaso.
1Wathess. 4:3-7
Katika somo letu lililopita (Petro #29), tumeona Petro akisisitiza katika aya zinazotangulia aya zetu hizi hapa juu kuhusu umuhimu wa kuimarisha msimamo wa mashambulizi katika vita yetu ya kiroho tulimo kama askari wa Bwana wetu Yesu Kristo. Lakini kwa nini Petro anazungumzia mashambulizi yetu ya kiroho dhidi ya adui – ambayo yanafanyika katika uwanja wa vita wa mioyo yetu au yule mtu wetu wa ndani – kabla ya kutoa wito wa kujitakasa na kuishi maisha matakatifu hapa katika 1Pet. 1:14-16? Hili ni jambo ambalo hutegemei kuliona katika makanisa ya leo, ambamo kukemea dhambi kwa sauti kali ndilo jambo linaloongoza (ikiwa wanawazia kufundisha, jambo la nadra sana!), wakati kukua kiroho na kuendelea kiroho na njia zinazohusiana na kukua kiroho kavifundishwi kabisa! Sababu ya Petro kufanya hivi ni kwamba kukua na kujiimarisha kwanza katika kanuni za kweli ya Biblia ni jambo la lazima kabisa kabla ya mwenendo mwema kuanza kuonekana: utakatifu halisi, msingi wake ni kuwa na mwitikio/kiitikio chanya kwa ule wito wa kweli ya Biblia (na siyo kuosha na kupaka rangi ya kupendeza nje ya chombo kwa sababu ya kuogopa bila ya kuwa na mabadiliko halisi ya ndani – Matt. 23:27-28). Paulo anaweka masuala haya katika mpangilio huu huu sahihi. Katika nukuu ya hapo juu (1Wathess. 4:3-7) tunaona kwamba kujua na kutenda mapenzi ya Mungu ni msingi wa kwanza wa maisha matakatifu (Waebr. 10:35-39; 1Pet. 4:1-2; 1Yoh. 2:16-17). Yaani, tunatumaini, siyo mambo ya utoto/uchanga wa kiroho. Ili kujua mapenzi ya Mungu katika ujumla wake, na kuhusiana na maisha yako wewe kama Mkristo, ni lazima ufikie kiwango cha kupevuka kiroho. Hivyo, ingawa kujiweka mbali na aina fulani za dhambi yaweza kuwa ni utekelezaji wa wazi wa amri za Biblia za “kuwa watakatifu” ( na hata katika hili, kufanya hivyo kutokana na nia sahihi kunalazimu kiwango cha juu cha kupevuka kiroho), ni dhahiri kwamba kuna mengi zaidi yanayohusishwa na utakaso katika muktadha ambao Petro anauzungumzia hapa. Utakatifu halisi, kuenenda katika njia ya utakatifu wakati mambo ni magumu na siyo rahisi kupambanua njia ipi ya kupita ni sahihi, inataka kiwango cha upevu wa kiroho ambacho hakipatikani haraka-haraka tu:
5.14 Lakini chakula kigumu [cha kiroho] huliwa na watu waliopevuka kiroho, ambao dira zao za uadilifu – dhamiri zao, kwa kutumiwa kwa uadilifu, zimezoezwa kupambanua [kati ya] mema na mabaya.
Waebr. 5:14
1.9 Na hii ndiyo dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana, mnavyozidi kukua katika imani na kweli, na katika kutumia [imani na kweli hiyo] katika mazingira yote ya maisha yenu;
1.10 mpate kuyafahamu yaliyo mema; ili mpate kuwa na mioyo safi, bila kosa, mpaka siku ya Kristo (siku ya thawabu);
1.11 hali mmejazwa matunda ya haki [au uongofu], kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu.
Wafi. 1:9-11
12.1 Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu [kama makuhani] yenye [kumfurahisha Mungu, mnayoifanya kiroho].
12.2 Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua [kwa] uhakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.
War. 12:1-2 (cf. War. 2:17-18)
6.5 Enyi [mlio] watumwa, watiini wao walio bwana zenu kwa jinsi ya mwili, kwa hofu na kutetemeka, kwa unyofu wa moyo, kana kwamba ni kumtii Kristo;
6.6 wala si kwa utumwa wa macho tu kama wajipendekezao kwa wanadamu bali kama watumwa wa Kristo, mkitenda yampendezayo Mungu kwa [kutoka] moyo[ni];
6.7 kwa nia njema kama kumtumikia Bwana wala si mwanadamu;
6.8 mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapewa [thawabu kwa hilo] na Bwana kwamba (awe) ni mtumwa au kwamba (awe) ni huru.
Waefe. 6:5-8 SUV
Hivyo kuijua ile kweli, kuiamini, ni muhimu sana katika kutimiza amri za Biblia za “kuwa watakatifu”:
17.17 Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.
Yoh. 17:17 SUV
Hivyo basi, kupevuka kiroho ndio ufunguo wa kuishi maisha yaliyotakaswa vile Bwana wetu anavyotaka tuishi. Hii siyo tu kwa sababu kwa kujifunza maandiko na kusikiliza na kuamini kweli ya mafundisho ya maandiko kutoka kwa mwalimu stadi basi tutajua kutenda na kupambanua yaliyo sahihi na yale yasiyo sahihi. Mara nyingi hili litakuwa wazi hata kwa waumini wachanga kabisa. Ila, kwa kukua kiroho tunaendeleza uwezo wa kutambua na kuepuka vishawishi na kukamilisha majukumu mengine yanayohusiana na amri tunazopewa katika maandiko, pamoja na kujipa motisha kutokana na uhusiano wetu unaozidi kupevuka na Bwana Yesu Kristo. Hatutakuwa rahisi kudanganyika na tutakuwa na uwezo mkubwa wa kutumia busara ya [maandiko] katika maamuzi yetu yanayopelekea kwenye maeneo ya maisha yetu na nyakati mbalimbali za majaribu, lakini pia tutakuwa tunaendeleza na kudhihirisha unyofu wetu wa kiroho, msingi ulioimarishwa na kweli ya Neno la Mungu ambao unatupa uwezo mkubwa zaidi katika kupinga, na kutupa busara inayoongezeka katika mbinu za kupinga, jambo lolote ambalo linaonekana kuwa linaweza kutishia mwenendo wetu uliotakaswa pamoja na Bwana Yesu Kristo – Yeye ambaye siku hadi siku tuna nia ya kumfurahisha.
Mjitenge na kitu chochote ambacho kina [hata mwonekano tu au “harufu”] wa uovu.
Wathess. 5:22
Itakumbukwa kwamba Eva alitetereka kwa sababu ya kudanganywa. Tunavyoongeza ufahamu wetu na tunavyozidi kuamini yale tunayojifunza katika maandiko, ndivyo uwezekano wa kuanguka katika vishawishi kwa sababu ya kutojua, unapungua. Kweli inatuweka huru kutoka katika aina hii ya ujinga – siyo tu ujinga wa hulka ya dhambi lakini pia hulka ya adui na mbinu zake ambazo zinafanya majaribu kuwa ni hatari zaidi. Uhuru huu nao unatupa uwezo kwa njia ya Roho Mtakatifu wa kupinga kwa ufanisi zaidi, kama tuna nia imara ya kusimama katika kweli tuliyoielewa, kuiamini na kuiweka moyoni kwa imani.
8.31 Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli;
8.32 tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.
Yoh. 8:31-32 SUV
Kwani tunapokua kiroho, tunajifunza siyo tu nini cha kuepuka, bali pia tunajifunza juu ya Yeye ambaye tunapaswa kushikamana Naye wakati wote, mpendwa Bwana wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Muda unavyozidi kwenda, mambo yote makuu tunayojifunza na kuamini kumhusu Yeye na Neno alilotupatia, yatabadilisha fikra zetu zote kuhusu maisha ya duniani na ulimwengu mzima na mwenendo wetu ndani yake. Kwa hakika, ni kweli ya Neno la Mungu pekee inayoweza kutubadilisha katika namna halisi na yenye faida kwetu. Mabadiliko halisi ya kiroho hayawezi kufanyika kutoka nje na kwenda ndani ya moyo. Hatuwezi kuwa “watakatifu” kwa kujilazimisha kufuata (au kumruhusu mtu mwingine atulazimishe kufuata) mfumo wa sheria na amri fulani. Amri au sheria zitatungwa na zitavunjwa – na hulka yetu ya dhambi – na mfumo wa aina hiyo wa sheria, hata ukiundwa kwa uangalifu namna gani utafanikiwa ‘kuwabana’ tu watu wanaoishi chini yake, na hautaweza kuwabadilisha mioyo yao. Kupaka rangi nyeupe nje ya mwili hakuwezi kubadilisha kinachoendelea ndani, rohoni. Matilaba/motisha ya kuwa “watakatifu” yaweza kuwa safi kabisa, lakini utekelezaji wa agizo/jukumu hilo hauwezi kufanikishwa kwa juhudi za kimwili pekee (War. 7:7-25). Muumini atafanikisha jukumu la kutembea na Bwana Yesu Kristo kwa kubadilika moyoni katika namna chanya ambayo kwa asili yake inaepuka njia ya kimwili (yaani ni mabadiliko ya kiroho), na hivyo inatekeleza amri ya upendo (War. 13:10).
Yote haya ni kweli, siyo tu kwa ujumla bali pia katika utaratibu wa mwendo wa Kikristo. Tunavyozidi kuwa karibu na Bwana, ndivyo Naye anavyokuwa na uwepo halisi zaidi ndani yetu, katika maisha yetu, ndivyo tunavyompenda zaidi na kumfurahisha Yeye kunakuwa ni kipaumbele katika kila hatua tunayopiga hapa duniani (badala ya kuwa maneno tu), na ndivyo tunaweza kusaidiwa na mtazamo huu na nia hii njema wakati shinikizo na kishawishi vinapotukabili. Hakuna aliye mkamilifu, na hakuna muumini atakayefanikisha ukamilifu/utimilifu wa kutotenda dhambi hapa duniani (mafundisho kinyume na hapo ni kanuni za uwongo zilizo hatari sana: War. 3:23; Yak. 3:2; 1Yoh. 1:6-10), lakini tunaweza, tunapaswa, na ni lazima tuwe na maendeleo siku hadi siku katika kutimiza jukumu la “kuwa watakatifu, kwani mimi ni mtakatifu” (1Pet. 1:16). Na njia pekee iliyohakikiwa na ya kimaandiko, Kibiblia, ya kufanya hivyo ni kuendelea kukua kiroho siku hadi siku kwa kusikiliza, kujifunza, kuamini na kulitumia Neno la Kweli.
Uwatakase kwa ile kweli (yaani, uwaeleke kwenye utakatifu); Neno lako ndiyo kweli. Yoh. 17:17
1.22 Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, basi jitahidini kupendana kwa moyo [wa kindugu], hata kuufikilia upendano wa [ki]ndugu usio na unafiki.
1Pet. 1:22 SUV
Hivyo utakaso wa kweli, utakatifu wa kweli, utatokana na kuiamini kweli, halafu kuenenda kutokana na kweli hiyo katika utiifu. Hayo ndiyo mabadiliko halisi ambayo maandiko yanaagiza, mabadiliko ya ndani (moyoni) yanayopelekea kubadilika kwa mwenendo wetu wa nje – badala ya kupaka rangi [ya kupendeza machoni] mwilini au kuenenda kwa mfumo fulani wa sheria ili kulazimisha “utakatifu” bandia:
Nimelificha Neno lako ndani ya moyo wangu, nisije nikatenda dhambi dhidi yako.
Zab. 119:11
Kama tulivyoona mara ya mwisho katika majadiliano ya mbinu ambazo Wakristo wanafundishwa ili wapate ushindi katika vita ya kiroho, kujilinda kiroho kwa ufanisi (yaani kuepuka vishawishi) ni jambo gumu sana kufanikisha bila kupeleka mashambulizi kwa adui (yaani kukua katika Kristo kwa kusikiliza mafundisho ya kweli, kuiamini hiyo kweli, na kuitumia kweli hii wakati wote katika uwezo wa Roho Mtakatifu). Kwa hakika, kukua kiroho na kuishi katika utakatifu ni shughuli zinazotegemeana na kushirikiana, kwani kushambulia kunasaidia ulinzi, na kulinda kunasaidia mashambulizi – tunatumia lugha ya kivita kwa sababu maisha ya Kikristo ni mapambano wakati wote (cf. Waefe. 6:12-17). Tunapojifunza na kuamini ile kweli zaidi na zaidi, udanganyifu wa vishawishi (na yule mwovu anayetuletea udanganyifu huo) vinaonekana kwa urahisi zaidi katika uhalisia wake, wakati huo huo upendo wetu kwa Mungu (ambao unakua sambamba na ufahamu wetu juu yake, sadaka Yake, wema Wake, na mpango Wake unaoendelea kufunuliwa, unaofanyika kwa ajili yetu) na kiu yetu ya kumfurahisha Yeye vinafanya upinzani [dhidi ya adui yetu] wenye mafanikio kuwa na uwezekana mkubwa. Vivyo hivyo, ushindi tunaoanza kuupata dhidi ya dhambi unaongeza nguvu katika kujiamini kwetu kiroho na unapunguza uharibifu ambao vinginevyo tungeuleta/tungeufanya katika uhusiano wetu na Bwana wetu ambaye tunampenda kuliko uhai wetu.
Kama watoto watiifu, msiozifuata tamaa zenu za awali mlizokuwa mkizifuata katika ujinga wenu [wa kale, wa ile kweli] …
1Pet. 1:14
Tofauti na Platonism, Ukristo wa Kibiblia unafundisha ukweli kwamba ufahamu (knowledge) pekee hauwezi kuleta mwenendo sahihi. Lakini kwa hakika ni kweli, kama Petro anavyosema katika aya hii, kwamba kutoijua kweli kunahusika kwa kiasi kikubwa na kuanguka kwa mtu katika majaribu, tamaa, na dhambi (za aina zote). Tunavyozidi kutambua dhambi ni nini, ndivyo tunazidi kuongeza uwezo wetu wa kuiepuka. Tunavyozidi kufahamu kuhusu adhabu kutoka kwa Mungu tutakazopata kama matokeo ya kuvunja amri Zake, ndivyo tunazidi kuongeza uwezo wetu wa kuenenda kwa uangalifu tunapokabiliwa na vishawishi vya namna hii. Tunavyozidi kufahamu juu ya thawabu kuu za milele walizoahidiwa wale wanaopigana vita hii kwa mafanikio, ndivyo tunazidi kuwa na kiu ya kuepuka chochote kinachoweza kuathiri ufanisi wetu kama wapiganaji wa Kikristo au kutupunguzia kasi ya mbio zetu kuelekea katika utepe (1Wakor. 9:24-27). Na tunavyozidi kuongeza ufahamu kuhusu Bwana wetu mpendwa na Mwokozi wetu Yesu Kristo, ndivyo tutakavyozidi kutembea karibu Naye, ndivyo tutazidi kumshukuru kwa kile alichokifanya katika kubeba dhambi zetu na kutukomboa kutoka katika kifo kwa damu Yake, na ndivyo tutazidi kupenda kufanya kila kitu ili kumfurahisha Yeye na kutofanya yale yanayomuudhi Yeye – tunaweza kuwa na hilo tumaini! Ama kwa hakika, tunapaswa kujifunza kweli ambazo juu yake misingi hii imeegemezwa (na misingi mingine pia) kwa undani na kwa kinaganaga, na tunapaswa kuamini kweli hizi kwa moyo wote. Tunapofanya hivyo, utakaso katika maisha yetu, kuishi na kutenda kama mabalozi wa kweli wa Kristo kutaanza kufanyika kwa urahisi zaidi na tutaanza kudhihirisha mara nyingi zaidi utakatifu katika mwendo wetu na Bwana.
7.1 Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza (tukitimilisha - perfecting) [utakaso wetu] katika kumwogopa Mungu.
2Wakor. 7:1
Katika aya hii, “ahadi” za uzima wa milele na thawabu kuu katika siku ile ya ufufuo ndizo motisha tunazofundishwa kuzitumia katika kufuatilia utakatifu. Zaidi ya hapo, “kumwogopa Mungu” kunakotajwa, ijapokuwa kunamaanisha pia kuogopa kutofurahishwa Kwake na dhambi zetu pamoja na kuogopa adhabu Yake, hii isieleweke kabisa kuogopa kutengwa na Mungu. Sisi waumini tuko salama kabisa katika wokovu wetu – ikiwa tunaendelea kuwa waumini (kitu cha kuogopa hapa ni kuacha kuamini {apostasy} kwa kuacha kabisa imani tuliyo nayo katika Kristo). Kuna mahala pengine ambapo mtume Paulo anaelezea kwa undani zaidi huu woga wa Mungu tunaotakiwa kuutumia ili utusaidie kuendelea katika msitari na kuupa utakatifu kipaumbele katika maisha yetu:
5.10 Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara (recompense) ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.
5.11 Basi tukiijua hofu ya Bwana [katika matarajio ya hukumu hii], twawavuta wanadamu [ili waende mwendo sahihi]; lakini tumedhihirishwa mbele za Mungu [jinsi mioyo yetu ilivyo]. Nami natumaini ya kuwa tumedhihirishwa katika dhamiri zenu pia.
1Wakor. 5:10-11
Tukiwa kama waumini tuliozaliwa upya “katika Kristo”, tunachokiogopa katika kushindwa kutembea katika njia ya utakaso ni kushutumiwa mbele ya kiti cha hukumu kwa “mwenendo” usio na faida: kuishi katika njia isiyo na utakaso kunaathiri na hakuendani na kupevuka kiroho, kuenenda kiroho, na kuzaa matunda [mema] ya kiroho, kama vile ilivyo kwamba kupevuka kiroho ni kiambato (ingredient) cha lazima na hutoa motisha ya nguvu katika mwenendo uliotakaswa, mwenendo mtakatifu pamoja na Mungu. Kutizamia ule wakati ambapo tutathawabiwa kwa yale tuliyoyafanya “katika mwili” (2Wakor. 5:10) ni jambo ambalo waumini wanaoendelea, wanaotembea katika njia ya utakaso wanapaswa kufanya wakati wote. Kwa upande mwingine, kama hatufanyi maendeleo ya kiroho na hatuendelei katika mwendo uliotakaswa pamoja na Bwana, tunafahamu kwa hisia [kupitia Roho Mtakatifu] kwamba shutuma badala ya thawabu ndiyo matokeo ya kushindwa huko kwa jinsi tunavyoonyesha namna tulivyotumia wakati wetu hapa duniani. Kushindwa au kuanguka mara moja hakusababishi kukosa thawabu kama ilivyo kwamba ushindi mmoja hausababishi kupata thawabu; lakini kushindwa kokote kule kunatuathiri katika vita hii, kama vile ambavyo kila ushindi unachangia katika thawabu yetu ya milele. Kama tulivyojadili hapo juu, utakaso (kujilinda kiroho dhidi ya adui) hauwezi kutenganishwa na kukua kiroho, kuendelea kiroho na kuzaa matunda ya kiroho (mashambulizi ya kiroho dhidi ya adui). Kwa upande mmoja, kama muumini anajilinda zaidi kuliko kushambulia, uhaba wa kasi ya kwenda mbele utamweka katika hali ya kukosa ulinzi zaidi na zaidi kwa jinsi muda unavyozidi kwenda kutokana na kuikosa kweli, na anakuwa dhaifu na rahisi kuanguka kutokana na kutokuwa na kasi hiyo. Kwa upande mwingine, kama muumini anafuatilia kwa nguvu zote kukua kiroho kwa kujifunza na kuiamini kweli, mtazamo hobelahobela kwa dhambi utaathiri juhudi hiyo njema, utaathiri ushuhuda wake, utatatiza maendeleo yake kutokana na kulazimika kubeba mzigo wa adhabu ya/za Mungu, na kufanya suala la kufaulu mitihani migumu kuwa jambo lisilowezekana mpaka dosari hii itakaponyooshwa. Ulinzi uliotakasika dhidi ya dhambi ukiunganishwa na kuikumbatia kwa furaha ile kweli ya Mungu na kuitumia katika mitihani yote ya maisha ya duniani (kuwasaidia wengine kufanya hivyo pia pale nafasi inapojitokeza) kutamwezesha muumini yeyote kutimiza wito anaopewa na Kristo, na ataingia katika orodha ya watakaopewa thawabu kuu Aliyoiweka kwa ajili ya wote wanaoyasikia maneno Yake na kuyapa heshima yanayostahili.
7 Kama ukitenda vyema, hutapata kibali (hutakubaliwa)? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea (inakunyemelea) mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.
Mwanzo 4:7
Bwana wetu aliyasema maneno haya kwa Kaini wakati Kaini hajaokolewa, wakati alipokuwa hana heshima yoyote kwa Bwana (kama ambavyo tendo lake la kumwua ndugu yake Abel baadaye lilivyoweka wazi). Kisa hiki kina lengo la kutufundisha hapa kwamba hata wasioamini (Bwana wetu anatuhakikishia) wanaweza kuishinda au kuitawala shawishi ya kutenda dhambi (ingawa Kaini alishindwa kufanya hivyo). Ni suala la kuamua. Na kwa hakika tunaliona jambo hili likidhihirishwa wakati wote katika matendo ya wasioamini ambao ni raia wema, wasiovunja sheria, wenye hulka adilifu. Kwa hakika, kwa kiasi fulani ni rahisi kwa wasioamini kuwa wema na waadilifu na kujizuia na mwenendo wa dhambi kwa sababu wao si walengwa mahususi wa Ibilisi kama ambavyo waumini walivyo. Kitu ambacho msingi huu unatufundisha, ijapokuwa Kaini mwenyewe alishindwa kuitikia kwa usahihi ni kwamba kwa uhakika tunaweza kujilinda dhidi ya vishawishi na tunaweza kujizuia kutenda dhambi, hata kama inaonekana kuwa ni vigumu sana kufanikisha hilo. Kama mtu asiyeamini ambaye hana heshima kwa ile kweli – na hana msaada kutoka kwa Roho Mtakatifu – anaweza kuishi katika namna ya utakaso (na maandiko, pamoja na uzoefu wetu unaonyesha kwamba hili linawezekana), basi kwa hakika sisi ambao tuna Roho Mtakatifu aishiye ndani yetu tunaweza kufanya hivyo pia. Kwa sababu hiyo, wakati wowote inapokuwa ni suala la kishawishi mahususi au kutawaliwa na tamaa fulani kama pombe, ngono isiyo halali, n.k. au mwenendo fulani wa dhambi, waumini wanapaswa kuwa wakweli katika nafsi zao, wakubali tatizo, na kulikabili uso kwa uso. Ni lazima tutambue na kukubali ukweli kwamba kwa hakika tuna mamlaka juu ya utashi wetu, na kwamba kwa msaada wa Roho Mtakatifu siyo tu kwamba tunaweza, bali ni lazima tuseme “hapana!” kwa dhambi, kishawishi, kutawaliwa na tamaa/ulevi (ulevi si lazima uwe wa pombe tu!) na mwenendo wowote mwingine ambao ni kinyume na Neno la Mungu na mapenzi ya Mungu.
5.17 Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.
5.18 Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria [ya Musa].
5.19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu [mwenendo wa aibu], ufisadi,
5.20 ibada ya sanamu [madawa ya kulevya, kutegemea watu, malaika], uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,
5.21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia (nawaonya) mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.
5.22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
5.23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.
5.24 Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.
5.25 Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.
Waga.5:16-25 SUV
Kufanikisha haya – kujifunza namna ya kutembea katika njia takatifu [na iliyotakaswa] si suala la kufanikishwa usiku mmoja na si mchakato usiohitaji juhudi. Inataka kuingia katika vita siku hadi siku na hatua kwa hatua. Kwa kuwa sisi ni wanadamu, tutakuwa na siku za kushindwa, tutarudia makosa, lakini kwa msaada wa Roho Mtakatifu tutaendelea kufanya maendeleo katika kutimiza amri ya “kuweni watakatifu, kama mimi nilivyo mtakatifu”, hata kama utimilifu katika hili hauwezi kufikika. Hivyo basi, ni lazima tuendelee “kuutafuta utakaso” (Waebr. 12:14), hata wakati ikiwa ni vigumu kufanya hivyo, hata tunapojikwaa, tunapoanguka na kutenda dhambi (War. 3:23; Yako. 3:2; 1Yoh. 1:9) katika kufuata mfano wa Bwana wetu tujitahidi kuwa watakatifu “katika mwenendo wenu wote” (1Pet. 1:15b).
Kama Watoto Watiifu: Tumeacha mpaka mwisho wasifu anaoutumia Petro kutuelezea sisi kuwa ni waumini. Kama Wakristo, “tusizifuate tena tamaa [zetu za awali/mwanzo/zamani] tulizozifuata katika ujinga wetu [wa ile kweli]”, bali tutafute utakaso badala yake. Kwa kuwa sasa tumezaliwa upya, *[mtazamo, mwenendo, na tabia] yoyote ya maisha yetu ya awali, desturi zetu zote za dhambi za mwanzo,
taswira yoyote ya maisha yetu kama watu wasioamini na wasiostahili kusimama mbele za Mungu, yote hayo sasa yanapaswa kuwekwa pembeni. Sasa ni wakati wa kuyakumbatia mabadiliko kutoka kuishi kama wasioamini na kuenda kuishi kama waumini wanavyotakiwa kuishi. Hicho ndicho kiini cha “utakatifu” kama Petro anavyokielezea kwa kutumia lugha ya kutofautisha. Kuwa mtakatifu maana yake nini? Kwa hakika tunajua kinyume chake ni nini, yaani “kuzifuata tamaa” za aina zozote ambazo tulizifuata katika wakati ule tulipokuwa si waumini. Utakatifu basi, kwanza kabisa, ni kugeuka kutoka ulimwengu na kuelekea kwa Bwana – kitu ambacho kinaweza kufanikishwa kikwelikweli kwa kutumia tendo chanya la kuweka fikra zetu katika kweli Yake na wakati huohuo inahitaji juhudi ya makusudi ya “kutozifuata” tamaa za dhambi kama ulimwengu unavyotarajia na unovyoona kuwa ni kawaida.
2.15 Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba [kwa uhalisia] hakumo ndani yake.
2.16 Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima [yaani majigambo ya alicho nacho na anayoyafanya], havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.
2.17 Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu [akiwa hai] hata milele.
1Yoh. 2:15-17 SUV
Katika kutusihi namna hii akiwa katika Roho Mtakatifu, Petro anatuita “watoto watiifu”, na katika kufanya hivyo anatupatia motisha na kututia moyo ili tuikabili ile changamoto ya kuishi maisha matakatifu kwa ajili ya Bwana Yesu Kristo: kututia moyo, kwa sababu kama watoto, wana wa Mungu aliye hai, sehemu ya Mwili wa Kristo, tunao wokovu ambao ni salama na wa uhakika kama ilivyo imani yetu katika Bwana Yesu Kristo; motisha, kwa sababu wakati utiifu si tabia “inayojipa yenyewe” (automatic), kutambua kwamba utakaso ni hali ambayo Bwana wetu aliyekufa kwa ajili yetu anaitaka kutoka kwetu sasa hivi ni suala linalodai mwamko wa fikra zetu na kutusaidia kufanya mabadiliko yoyote yanayotakiwa katika mtazamo wetu ili kutimiza amri za kutuwezesha kuishi katika utakatifu zilizo katika aya hizi. Petro hatutishi na upotevu wa wokovu ikiwa tutashindwa kuishi (kwa hakika wokovu wetu unategemea imani yetu kwa Kristo, na si rekodi yetu, iwe nzuri ama mbaya, kuhusiana na dhambi).1 Petro hatutishi na adhabu kali ya Mungu ikiwa tutashindwa kuishi kama tunavyotakiwa kuishi kama vile tuko katika hali ya utakaso (ijapokuwa tunapaswa kuelewa kwamba kuna athari nzito tu kwa waumini wanaoshindwa kutii amri ya “kutozifuata” tamaa na shauku za uovu za dunia hii).2 Bali Petro
*Mabano ya square: maneno yote 3 yametafsiriwa kutoka neno moja, texture.
anatukumbusha kwamba Mungu ni mtakatifu, na kwamba sisi ni Wake kama watoto
Wake. Kama tunataka kuwa watoto ambao Baba anafurahishwa nao, basi jinsi ya kuenenda na kuupokea ujumbe huu ni wazi kabisa. Kwa kutumia mfano ambao Petro anatuonyesha, tunajua kwamba watoto ambao si watiifu kwa baba zao wa kimwili hupata shida hapa duniani, na hili ni kosa lao wenyewe. Hawakomi kuwa watoto kwa sababu ya kutotii kwao huku, lakini ni lazima wanapata adhabu, na mwenendo huu kwa hakika si njia ya kuelekea kwenye furaha, kwani furaha na ushirikianao utarudi tu baada ya adhabu na ule mwenendo mbaya umekwishasahihishwa. Ni vyema kuwa mwana mtiifu badala ya kuwa si mtiifu, na kwa kuwa hakuna asiye mkamilifu, ni vyema kupunguza idadi ya makosa tunayotenda na tujitahidi tusitende zile dhambi nzito nzito. Lakini hata kama kosa kubwa linafanyika kwa mwenendo wa ujeuri na kiburi, tunajua kwamba sisi ni watoto wao tu, ijapokuwa tutafanya maisha yetu kuwa machungu na kutia “asidi” - acid – katika uhusiano wetu na wazazi wetu kwa muda kwa sababu ya matendo mabaya tunayoyafanya katika kushindwa kutii mamalaka yao halali.
Kwa namna hiyo hiyo, Petro anatusaidia hapa kuona thamani ya hadhi yetu kama watoto wa Mungu waliozaliwa upya, na wakati huohuo akitutia moyo kwa mkazo kabisa tulichukue jukumu la kuishi katika utakatifu bila kufanya mchezo. Kuiona thamani ya hadhi yetu ya kuwa sisi ni watu wa Mungu Baba na Yesu Kristo Bwana wetu ndio msingi na ndio mwanzo wa kutimiza agizo la kuwa watakatifu: tunapaswa “kuwa watakatifu”, si kwa sababu ya woga, bali ni kutokana na heshima na staha na upendo tulio nao kwake Yeye aliyemtoa Mwana wake kwa ajili yetu, na Yeye aliyetugomboa kutoka katika utumwa wa dhambi zetu zote kwa damu Yake mwenyewe – kifo Chake [cha kiroho] msalabani katika kulipia kila moja ya dhambi zetu. Ulimwengu hautafikia mwisho wake kwa sababu tunafanya kosa, tunapotoka, tunatenda dhambi. Lakini kama kweli tunampenda Bwana wetu Yesu Kristo zaidi ya uhai wetu (kama tunavyodai), kumsikitisha na kushindwa kufanya Anachokitaka tufanye vinapaswa kuwa motisha ya nguvu kwetu, zaidi ya adhabu tunayoweza kuipata kwa kushindwa mtihani wa utiifu. Tunavyozidi kusogea karibu Naye katika mwendo wetu wa kiroho siku hadi siku, ndivyo furaha Yake kwetu inakuwa na maana kuu [kwetu], na tutaitikia wito Wake kwa sauti kuu zaidi, tunapoanza kumwona Yeye asiyeonekana kwa uwazi zaidi kwa kutumia macho yetu ya imani, imani ambayo msingi wake ni mwamba wa kweli/kanuni za Neno la Mungu. Tunavyozidi kujifunza na kuamini yamhusuyo Bwana Yesu Kristo na kweli Yake, ndivyo tunazidi kuishi maisha ya utakaso wa kweli, siyo tu kufanya mabadiliko ya nje ya kitabia, bali kufanya mabadiliko halisi ndani ya mioyo yetu, na kudhihirisha utakaso huo katika ulimwengu kwa ajili ya utukufu na heshima ya Bwana aliyetununua na aliyetuita tuwe watakatifu kama Yeye alivyo Mtakatifu, Yesu Kristo Mwokozi wetu. Ni Yeye tunayetaka kumwitikia; ni katika uso Wake ambapo mwenendo na maadili yetu mema yanaakisiwa/yanaonekana.
Nena na mkutano [kusanyiko] wote wa wana wa Israeli, uwaambie, mtakuwa watakatifu, kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni Mtakatifu.
Mambo ya Walawi 19:2
Notes:
1. Kuacha imani (apostasy) kunatokea tu kupitia kuikana kabisa imani katika Kristo na kurudi kwenye hali ya kutoamini. Tazama “Apostasy and the Sin Unto Death” katika BB 3B.
2. Katika mifano ya waumini ambao wanakataa kabisa kabisa kuitikia wito wa Mungu ambaye anawapa adhabu endelevu ili wajirudi wenyewe na kurudi Kwake, basi “dhambi iliyo [inayopelekea kwenye] ya mauti” kutokea. Tazama “Apostasy and the Sin Unto Death” katika BB 3B.
=0=
Imetafsiriwa kutoka: Sanctification in Time: Christian Defense in our Spiritual Warfare
=0=
Basi, na tuonane katika somo #31 la mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!