Kanuni za Kimsingi za Kikristo za Maisha ya Duniani na Maisha ya Milele Mbinguni

Nyaraka za Mtume Petro #31

1Petro 1:17-21

Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for this Kiswahili Translation has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

1.17  Na ikiwa mnamwita [mnaomba msaada wa] Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu [ya hukumu Yake] katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni.
1.18  Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea [kutoka] kwa baba zenu;
1.19  bali [mlinunuliwa] kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa (doa), yaani, ya Kristo.
1.20  Ambaye ujio Wake ulijulikana kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa nyakati kwa ajili yenu [i.e. kwa ajili ya wokovu wenu];
1.21  ambao [kupitia kwake] Yeye (Kristo) mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu.
1Peter 1:17-21 SUV

Kitu cha kwanza tunachokiona katika nukuu hii ni kwamba inahitimisha mjadala wa Petro juu ya utakaso katika aya za 14-16. Baada ya kusisitiza pointi ya ulazima wa kila muumini kujizuia na dhambi na tamaa za kimwili kwa sababu ya uhitaji wa kuenenda kwa utakatifu kama vile Baba yetu wa mbinguni alivyo mtakatifu, Petro anarudia tena pointi hii katika aya ya 17 na anatupatia *urazini wa motisha (motivational rationale) wa kufanya hivyo zaidi ya kuogopa tu adhabu ya Mungu kutokana na kupaka matope ushuhuda wetu katika mwendo wetu wa Kikristo. Urazini au mantiki hii ni muhimu kuliko mitazamo yote ya Kikristo, ambayo
inapaswa kuwemo moyoni/akilini wakati wote na iwe imara wakati wote katika fikra

*Motivation[al] – -a motisha; rationale – urazini; mantiki; sababu ya msingi. Hivyo ninaitafsiri “motivational rationale” kama “urazini wa motisha” au “mantiki ya motisha” au “sababu ya msingi ya motisha”.
za kila Mkristo; urazini huu ni msalaba wa Bwana wetu. Pale tunapotambua gharama
aliyoingia Bwana wetu, na Baba yetu wa mbinguni katika kuosha dhambi zetu,
kujiingiza katika dhambi – kama vile ni jambo la kawaida tu – ni kupuuza kwa makusudi lile alilolifanya Bwana Yesu Kristo katika kufa kwa ajili yetu katika lile giza la Kalvari.

1.9  Maana yeye asiyekuwa na hayo [maadili anayoyataja katika aya za 5 - 7] ni kipofu, hawezi kuona vitu vilivyo mbali, amesahau kule kutakaswa dhambi zake za zamani.
2Pet. 1:9 (SUV)

Kwa maelezo rahisi, nukuu ya hapo juu ina lengo la kutupatia mtazamo muhimu sana wa kupata taswira ya ulimwengu na hasa mwenendo wetu ndani ya ulimwengu huu. Kila tunachokifanya, chema au kibaya, na kila tunachoshindwa kufanya, kinapimwa na damu ya Kristo. Kwa kiasi ambacho tunaiweka katika fikra zetu ile sadaka Yake kuu, tunakuwa na uwezekano mdogo wa kuikufuru kwa kutenda dhambi, na tunakuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kumwitikia katika namna chanya (positively) katika mwendo wetu wa kila siku, tukikua kiroho, tukiendelea kiroho, na tukizaa matunda mema tunapokumbuka upendo usiokuwa na kadiri wa Bwana wetu Yesu Kristo pale msalabani. Kama vile msalaba unavyoigawanya historia ya wanadamu katika pande mbili, kama vile unavyogawa maisha yetu katika pande mbili – kutoka kutoamini kwenda kwenye kuamini, vivyo hivyo msalaba unagawanya mioyo yetu na fikra zetu kama upanga mkali ukatavyo, kwani wenyewe (msalaba) ndio ile kweli ya muhimu ambayo juu yake kila kitu kimejengwa:

4.12  Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo [mifupa] na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li (Neno lililo ndani ya dhamiri zetu) jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
4.13  Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu [vi uchi] na kufunuliwa machoni pake Yeye tunayepaswa kujihusisha naye.
Waebr. 4:12-13

Kuita Jina la Baba: Waumini huomba msaada wa Baba yao wa mbinguni kila siku – au wanapaswa kufanya hivyo. Tunafanya hivyo tunaposali sala aliyotufundisha Bwana wetu, na pia huenda wakati tunakiri na kutubu dhambi zetu, au wakati tunapofanya sala/maombi mengine katika wakati wowote wa siku. Kufanya hivi ni sahihi kabisa. Yeye ni Baba yetu aliye mbinguni, nasi ni watoto wake katika Kristo. Anaahidi kutusikiliza tunapoomba msaada (Luka 11:5-13), nasi tunamwomba wakati wowote tunapohitaji msaada – au tunapaswa kufanya hivyo. Hapa Petro anatukumbusha ni kiasi gani bado tunamhitaji Mungu baada ya wokovu, na anatusihi tufanye maamuzi stahiki: kama tunahitaji msaada Wake (na kwa hakika tunauhitaji), basi ni makosa kiasi gani hata kushawishika tu kuingia katika mfumo mbaya wa maisha ambao hatafurahishwa nao? Hiyo ndiyo hali ya “kutokuona mbali kiroho” anayoizungumzia Petro katika 2Petro 1:9, na hili ni jambo la hatari sana. Bila ya shaka ni kweli kwamba kukua kiroho kunapounganishwa na mwenendo uliotakaswa unaotokana nako kunatuleta karibu na Mungu na kunatia nguvu sala/maombi yetu (Zab. 34:17; Mitha. 15:29; 1Pet. 3:12), kinyume cha mwenendo huu huzaa matokeo kinyume pia (1Pet. 3:7). Hivyo basi, kuuweka utakaso katika mtazamo wake sahihi kunahitaji tukumbuke, kwanza, alichokifanya Kristo katika kutupatia msamaha tulio nao ndani Yake (ili tusitumie vibaya fadhila ya kitubio), na pili, kinachoweza kututokea ikiwa hatutoishi katika njia ya utakaso: msaada kutoka kwa Yeye aliye juu zaidi utakuja kwetu katika wakati mwafaka, na laana itabadilishwa na kuwa baraka, baada ya kukiri dhambi na kutubu kikwelikweli (yaani kuigeuka dhambi tuliyoitenda badala ya kuikumbatia), na bila ya shaka utaambatana na adhabu ya Mungu (kama Baba yetu wa mbinguni) ambayo ni muhimu katika kutukumbusha tuurudie na kukaa na ule mtazamo muhimu wa utakaso.

12.11  Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani [yaani, yanamfanya muumini aelekee kwenye ukamilifu].
Waebr. 12:11

Ambaye Anahukumu kwa Haki Mwenendo wa Kila Mtu: Kama waumini wa Bwana Yesu Kristo, hatutasimama mbele za mahakama ya Mungu katika ile hukumu ya Kiti Kikuu Cheupe cha Enzi. Sisi tumeokolewa, na hivyo hatuhusiki na Hukumu ya Mwisho [ya kuwatia hatiani wale wasioamini]:

3.18 Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini Jina [yaani Nafsi] la Mwana pekee wa Mungu.
Yoh. 3:18 SUV

Hata hivyo, kuna hukumu zingine, na hizi ndizo ambazo Petro anazizungumzia. Tukianza na ile ya mwanzo kabisa, sisi sote tutasimama mbele za kiti cha hukumu cha Bwana Yesu Kristo ili kila mtu “apokee ijara (mshahara) yake ya mambo aliyotenda katika/kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya”.

5.10  Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya [yasiyo na thamani].
2Wakor. 5:10 SUV

Hukumu hii ya Kanisa inahusisha mgawo wa thawabu za milele, lakini pia itahusisha tathmini ya maisha yetu itakayofanywa na Bwana wetu ambayo ni vyema kuikumbuka katika mwendo wetu wa hatua kwa hatua pamoja Naye.

5.11  Basi tukiijua hofu ya Bwana [katika matarajio ya hukumu hii], twawavuta wanadamu [ili waende mwendo sahihi]; lakini tumedhihirishwa mbele za Mungu [jinsi mioyo yetu ilivyo].
2Wakor. 5:11a

Ukweli kwamba Petro anamzungumzia Mungu Baba kuwa ndiye anayetathmini mwenendo wetu wa hapa duniani kwa sasa hauna mgongano kabisa/wowote na tunachokisoma katika Injili ya Yohana:

5.22 Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana [mamlaka ya] hukumu yote;
5.23 ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba.
Yoh. 5:22-23a

Hakuna haja ya kuurudia ukweli kwamba ule Utatu (The Trinity) ni Mmoja, na hii ina maana kwamba wana uadilifu uliotimilika, usio na mapungufu yoyote na wana azma moja kila wakati (kitu ambacho wanadamu hatuwezi kukielewa katika mapana na marefu yake). Hivyo “hukumu” itakayotolewa na Baba, na Mwana ataitoa hukumu hiyo hiyo. Kama Bwana wetu anavyotuambia katika aya zilizonukuliwa hapo juu, kusudi la kumkabidhi rasmi Mwana jukumu la kutoa hukumu ni ili “watu wote wamheshimu Mwana kama wanavyomheshimu Baba” – shabaha muhimu sana haswa tukikumbuka kwamba kizazi cha Bwana wetu kwa kiasi kikubwa (idadi kubwa) hawakutaka kumheshimu Yeye kabisa.

Kama wana wa Mungu katika umoja na Bwana Yesu Kristo aliyetununua kwa damu Yake, tunayo haki ya kuomba msaada wa Baba (War.8:15; Waga. 4:6), na kwa maneno haya katika 1Pet. 1:17, Petro anatuhakikishia kwamba tathmini ya mwenendo wetu inapofanywa na Baba itakuwa ya haki na bila upendeleo – kama vile Bwana wetu anavyotathmini mwenendo wetu hapa duniani. Hakuna tofauti kabisa kati ya tathmini hizi mbili. Kwa kuwa Baba amempa kibali Mwana kama Masihi, Kristo, Mpakwa Mafuta, ilikuwa muhimu kuonyesha kwamba katika hukumu Mwana amepokea mamlaka Yake moja kwa moja kutoka kwa Baba:

28.18 Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.
Matt. 28:18 SUV

Hivyo ijapokuwa Bwana Yesu ndiye anayetuhukumu, namna ambayo Petro anaieleza kanuni hii inaondoa mkanganyiko wowote wa dhana kwamba kwa namna fulani kunaweza kuwa na tofauti kati ya hao wawili. Woga [wa kimungu] na heshima tuliyo nayo kwa Baba inapaswa kuwa vile vile kwa Mwana, kwa sababu mamlaka yote yanamiminika kutoka kwa Baba na kwenda kwa Mwana katika ubinadamu Wake. Lakini katika hukumu mahususi, Utatu wakati wote huendana pamoja, hawatofautiani kamwe, iwe katika kututathmini wakati huu au siku tutakaposimama mbele ya mahakama ya Kristo katika siku ile kuu ijayo:

[Uchunguzi huu (unaozungumziwa katika Warumi 2:11-15) utafanyika] katika siku ile Mungu atakapoyahukumu mambo ya siri ya wanadamu sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu.
War. 2:16

Kinachofanikishwa na usemi wa namna hii ni kuhamisha uelekeo (focus) wa fikra zetu kutoka dunia hii na kukumbuka kwamba tunachokiona, tunachokisikia, na hisia zetu, havina umuhimu ule ule kama umuhimu wa jinsi tunavyofikiri, tunavyosema na tunavyotenda yanavyochukuliwa, yanavyotathminiwa katika ukumbi wa utawala wa Mungu Baba ulioko mbinguni. Bila ya shaka kama tunaweza kuuona, japo kwa kipindi kifupi tu, umati ulioko mbinguni katika uwepo wa Mungu Baba na Mungu Mwana wakielekeza macho yao hapa duniani na kututazama sisi kwa uelewa mtimilifu kabisa [walio nao] na tathmini ya yote ambayo sisi waumini tunayafanya, tutapata motisha zaidi ya kupita katika ile njia ya taabu na nyembamba, kwa maana ya mwenendo uliotakaswa, na pia kwa kutumia muda wetu vyema katika vita ya kukua kiroho, kuendelea kiroho na kuzaa matunda mema, vitu ambavyo vinapaswa kuwa ndivyo vyenye kipaumbele kwetu. Kila mtu hubadilisha mwenendo wake anapojua kuwa kuna watazamaji, na kama wale wanaotathmini mwenendo wetu ni watimilifu, basi huwa tunajitahidi kwa uwezo wetu wote.

3.1  Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na (au kutokana na nafasi yenu katika) Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
Wakol. 3:1 SUV

Ishi siku zako zilizobaki hapa ugenini duniani kwa kumwogopa Mungu:

4 Bwana, unijulishe mwisho [wa uhai] wangu, Na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani; Nijuze jinsi [maisha yangu yalivyo ya muda mfupi tu].
5 Tazama, umefanya siku zangu kuwa mashubiri (ni urefu wa kiganja tu); [urefu wa] Maisha yangu ni kama si kitu mbele zako. Kila mwanadamu, ingawa amesitawi, ni [upepo tu].
6 Binadamu huenda tu huko na huko kama kivuli; Hufanya ghasia tu kwa ajili ya ubatili; Huweka akiba wala hajui ni nani atakayeichukua.
Zab. 39:4-6 (cf. Zab. 89:47)

Kama tukiweza kupata nafasi ya “kuonyeshwa” na Mungu siku hata siku na hatua kwa hatua jinsi muda ulivyo mfupi mpaka pale tutakaposimama mbele Yake (Waebr. 10:37; cf. Zab. 44:2), hatungewazia sana siku za maisha yetu pale tunapomalizia muda mfupi uliobakia na tunapoulinganisha na utukufu wa milele ijayo (Mhu. 5:20). Kama vile Petro alivyotukumbusha hapo mapema kwamba wakati wote tunatizamwa kwa makini (nasi tunaenda vyema zaidi tunapojua kwamba tunatizamwa), vivyo hivyo sasa anatukumbusha kwamba tuna muda mfupi sana hapa duniani (War. 13:11; Wafi. 4:5; Yak. 5:8; 1Pet. 4:7; Ufu. 1:3; 22:10; cf. Luka 21:8), hasa tunapolinganisha na milele tutakayoishi na Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa kujua hali hiyo basi, ni vema zaidi “kumngojea Bwana” katika kila kitu, hasa tunapokuwa na hisia kwamba tunakikosa kile tunachokiona kuwa ni hitaji kwa upande mmoja au tunaposhawishika katika jambo/starehe fulani ambayo si ya muhimu au hata yenye madhara kwa upande mwingine. Hivyo kuelekeza macho yetu bila kutetereka kwenye tumaini ambalo muda si mrefu litafunuliwa kwetu (1Pet. 1:13) ni jambo jema zaidi kuliko kung’ang’ana na dunia hii na masikitiko na majuto yake; basi kwa wakati huu tuzitumie fursa ambazo Bwana ametupatia kuzalisha mazao mema ambayo yatatupatia thawabu pale atakaporudi (Waefe. 5:16; Wakol. 4:5).

24 Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana [yaani siku ya ujio Wake wa 2], Tutashangilia na kuifurahia.
Zab. 118:24 SUV

2.12  Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyoitii [ile kweli] sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu [pamoja nanyi], bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.
Wafi. 2:12 SUV

Ubatili wa maisha kama ulivyorithishwa na wahenga wako:

2 Mhubiri [Mwalimu] asema, Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili.
Mhu. 1:2 SUV

Wakati Petro anazungumzia mahususi desturi za mwanzo/kale za kipagani za watu wa mataifa ambao ni kati ya walengwa wa waraka wake huu wa kitume, ukweli ni kwamba mapokeo yote yakiwa tofauti kikanuni na kweli ya Neno la Mungu basi yanakuwa batili na yasiyofaa chochote, hii ikiwa ni pamoja na kufuata Sheria ya Musa kinyume na kusudi, maana & malengo ya Sheria hiyo – kwa kimombo, legalism. Juhudi za wanadamu hazina maana kwani sote hufa na hakuna anayeweza kuwa na uhakika ni nani atakayepata faida za juhudi hizo zetu batili chini ya jua (Zab. 39:6; Mhu. 2:17-18). Yote tunayofanya na kufanikisha katika maisha yetu kwa nguvu na uwezo wa mwili hupita na kufifia mara, kama sisi wenyewe (Wagal. 6:8). Kama vile wimbo wa sifa za Mungu (wa zamani sana) unavyosema: of a truth we have only one life, will soon be passed; only what’s done for Christ will last”. Kwa kulinganisha ubatili wa juhudi za wanadamu hapa duniani – juhudi ambazo ukiziunganisha pamoja, tangu mwanzo (kuumbwa) wa wanadamu haziwezi kumwokoa mwanadamu hata mmoja wetu kutoka maangamizi – na wokovu usio na kifani ambao sisi waumini tunao kupitia damu ya Kristo, Petro anafikisha ujumbe wake: uhalisia huu wa kiroho unapaswa kutuongoza au kupelekea kuelekeza juhudi zetu kwa kile kilicho cha milele, kile kinachodumu, na si kile cha kupita, ambacho muda si mrefu kitafifia.

16 Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi.
17 Maana atakapokufa hatachukua cho chote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata.
Zab. 49:16-17 SUV

6.19 Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba;
6.20 bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi;
6.21 kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.
Matt. 6:19-21 SUV

Tumeokolewa, si kwa vitu vinavyochakaa … bali kwa damu yenye tunu ya Kristo:

Alichokifanya Bwana wetu Yesu Kristo katika giza la msalaba wa Kalvari, akifa kwa ajili ya dhambi zetu zote, ni jambo ambalo haiwezekani kulipa umuhimu zaidi ya ule ulio nalo. Ni jambo kuu kuliko ulimwengu, na ni jambo la ajabu kuliko jambo lolote kutoka mwanzo wa historia ya malaika hadi mwisho wa historia ya wanadamu linaloweza kufikirika na malaika na wanadamu wote [Ikumbukwe, malaika walianza kuumbwa, halafu wanadamu wakafuata]. Mungu akawa mtu (japo alibaki kama Mungu pia), akachanganyika nasi, akatembea katika dunia hii kama mmoja wetu, aliteseka zaidi ya uwezo wetu wa kuelewa au kufahamu – na alipaa/alipanda katika miali ya moto pale msalabani [kwa saa tatu] mpaka dhambi zote za wanadamu zilipolipwa. Hakuna mtazamo wa Kikristo juu ya maisha haya au ulimwengu huu yaweza kuwa kamili au sahihi bila kuwa na msingi wake katika sadaka ya mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo. Ili tuishi kwa ajili Yake kama tunavyotakiwa, tunapaswa kuelewa kwa usahihi Alichokifanya kwa ajili yetu.1 Dhahabu, madini ya fedha , vito, pesa na mali vyaweza kuwa na thamani katika maisha haya dhalili na ya muda mfupi, lakini utajiri wote wa dunia hii hauwezi kulipia hata dhambi moja ya mtu mmoja – na ukithubutu kufanya (kudai) hivyo utakuwa umemfedhehi Mungu. Ili kununuliwa kutoka chini ya utumwa wa dhambi, ili “kugombolewa”, bei yenye tunu ilitakiwa [kulipwa] ambayo hakuna aliyeweza kuilipa isipokuwa Mmoja – Bwana wetu Yesu Kristo. Naye alifanya hivyo alipobeba dhambi zote za wanadamu katika mwili Wake wa kibinadamu pale msalabani. Hii ndiyo sarafu ya ukombozi ambayo kwayo pekee sisi waumini tumenunuliwa kutoka katika utumwa wa dhambi na kuwekwa huru katika uzima wa milele – damu ya Bwana Yesu Kristo mwokozi wetu wa pekee.2

Hivyo tunapaswa kutambua kwamba deni halisi tulidaiwa na Mungu, lakini ni Yeye ndiye aliyelilipa.

Hivyo tunapaswa kukumbuka kwamba mali za kidunia haziwezi kutukomboa, na hivyo tunapaswa kuondoa macho yetu na fikra zetu kutoka kwenye mali.

Hivyo tunapaswa kushukuru kwa kile Bwana wetu alichokifanya ili tuishi maisha yetu kwa ajili Yake kama tunavyopaswa: hili ndilo fundisho tunalopaswa kujifunza, ili tulitumie, kutoka katika aya hii. Tunapaswa kuwa na deni la shukrani kwa Bwana wetu kutokana na ukombozi wetu kutoka katika dhambi na kifo, kifo chake cha kiroho kwa ajili yetu pale msalabani alipohukumiwa kwa ajili ya dhambi zetu zote. Ni kosa kubwa kabisa, basi, kung’ang’ana kwenye mali za uharibifu za dunia hii ambazo kitambo kidogo tu zitaondolewa, wakati kwa ukweli tunapaswa kuweka fikra zetu katika wokovu wetu kutoka katika kifo na hukumu ambamo Kristo ametununua kwa gharama ya uhai Wake.

5.6 Kwa hakika Kristo alikufa kwa ajili yetu wakati tukiwa hatuna msaada wetu wenyewe – na alifanya hivyo katika wakati mwafaka, akifa kwa ajili yetu, ingawa tulikuwa waovu.
5.7 Kwani ni vigumu kwa mtu kutoa uhai wake kwa ajili ya mwingine mwenye haki; lakini yawezekana mtu akatoa uhai wake kwa ajili ya mwingine aliye mwema.
5.8 Bali Mungu ameonyesha upendo Wake kwetu sisi, kwani wakati tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.
War. 5:6-8

Mwanakondoo asiye na doa wala dosari:

Kichwa cha ibara hii kinatilia mkazo utimilifu wa ubinadamu wa Bwana wetu. Alizaliwa bila ya hulka ya dhambi (ambayo ndiyo sababu ya kwa nini alipaswa kuzaliwa na bikira, yaani ili kuzuia Yeye kurithi hulka ya dhambi inayopititishwa au inayorithishwa ki-genetiki kupitia baba wa kibinadamu, na si mzazi wa kike), aliishi maisha [ma]timilifu pasipo kutenda dhambi – mwanadamu pekee katika historia aliyeweza kufanya hivyo (hakuna mwingine aliyekaribia kiwango hicho) – Yesu Kristo alihitimu kuwa anayeweza kubeba dhambi zetu. Kama vile Sheria ya Musa ililazimu dhabihu ya mwanakondoo asiye na doa wala dosari nje ya mwili wake, vivyo hivyo Bwana wetu, Mwanakondoo wa Mungu, alikuwa mtimilifu moyoni Mwake na hivyo akahitimu kubeba dhambi za dunia katika mwili Wake pale msalabani katika giza na kuhukumiwa badala yetu (1Pet. 2:24; cf. 2Wakor. 5:26).

1.29 Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!
Yoh. 1:29 (cf. Yoh. 1:36) SUV

Ambaye ujio Wake ulifahamika kabla ya kuumbwa ulimwengu:

Petro anaongeza maneno haya ili kutukumbusha kwamba msalaba, mwamba ambao mpango mzima wa Mungu na historia yote vina msingi juu yake, haukua *”ajali” wala wazo la kukisia baada ya uumbaji, bali ni sehemu muhimu na ndio msingi wa kila kitu ambacho kimetokea na kitatokea, iliyopangwa hata kabla ya amri ya Mungu ya kuumba ulimwengu. Usemi huu unaweka wazi kwamba kabla Mungu hajaanzisha uumbaji alilazimika kuweka ahadi/mpango wa ile sadaka/dhabihu tunu ya Bwana Yesu Kristo, namna pekee ambayo ilihakikisha kwamba viumbe wangepewa utashi (free will), na bado hatma ya viumbe hao ni kuishi milele na Mungu atakayewaumba (kwani “wote hutenda dhambi” - War. 3:23). Kuweka hili katika fikra zetu ni jambo la lazima kwa Wakristo wote ili kuendelea kuwemo katika msitari wa lengo na mpango wa Mungu – ambamo Bwana Yesu Kristo na kazi Yake pale msalabani ndiye Nafsi muhimu kabisa na ndiye msingi wake.

lakini sasa, mara moja tu, katika utimilifu wa nyakati [conjunction of the ages], amefunuliwa, azitangue dhambi kwa dhabihu ya nafsi Yake.
Waebr. 9:26b SUV

Yeye aliyekuja [kimwili] mwisho wa nyakati kwa ajili yenu:

Bwana Yesu Kristo amekuja hapa duniani kwa ajili yetu. Ujio Wake ulikuwa ni wa kujitoa sadaka katika kila namna. Mungu hana uhitaji wowote. Na kwa Mungu kutwaa mwili wa kibinadamu ilikuwa ni kujitoa sadaka isiyo na kifani – ambayo hatuwezi kuelewa katika mapana na marefu yake mpaka tutakapofika mbinguni. Lakini [kwa Mungu] kuja hapa duniani katika hali isiyo ya utukufu, kupata mateso ya “upinzani kutoka kwa wenye dhambi dhidi Yake” wakati wote wa maisha Yake hapa duniani (Waebr. 12:3), kufanikisha utumishi mkuu kuliko [utumishi] wetu sote katikati ya upinzani [mkubwa kuliko wote] wa Shetani na majeshi yake ambao dunia imewahi kuushuhudia, (e.g. Matt. 4:1-11), kuikabili hofu ya mahakama saba ili tu afike kwenye msalaba na kusulibiwa (tazama BB 4A) – halafu kuhukumiwa katika giza kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, kubeba dhambi zote katika mwili Wake akiwa msalabani (1Pet. 2:24) … hakuna haja ya kusema, shukrani tunazotakiwa kuwa nazo kwa mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo kwa mateso yote aliyoyapata kwa ajili yetu, na kwa Mungu Baba kwa kumtoa hata afe kwa ajili yetu ili tuokolewe, haina kiasi. Kama anachokitaka kutoka kwetu ni [sisi] kuishi maisha ya utakaso, na moyo wa shauku ya kutaka kumjua Yeye, na kuwasaidia ndugu zetu Wakristo kufanikisha lengo hilo hilo, je, hilo ni jambo kubwa/gumu kweli?!

*Accident: jambo la “kubahatisha” - kwa hakika, hakuna “ajali”, hakuna “bahati” katika uumbaji/ulimwengu. Ajali, bahati, nasibu ni mafundisho ya Shetani.
Ninyi ambao kupitia Kwake mmekuwa waumini wa Mungu:

Maisha ya hapa duniani yana lengo moja tu: kuutumia utashi tuliopewa na Mungu katika kuamua; na uamuzi muhimu kuliko maamuzi yote kwa kiumbe mwenye “mfano wa Mungu” ambao anaweza kuufanya ni kukubali au kukataa mamlaka ya
Mungu. Kwa wanadamu wote tunaoishi baada ya msalaba, Nafsi iliyofunuliwa ya Bwana Yesu Kristo aliyekufa msalabani kwa ajili ya dhambi za ulimwengu ndiye mlengwa pekee wa uamuzi huu; Mwokozi wetu, Nafsi Yake na kazi Yake, vinapokelewa tu kwa kuweka imani yetu kwa ajili ya wokovu wetu, Kwake. Hivyo ndivyo tunavyomchagua Mungu na kumkataa Shetani na ulimwengu anaoutawala. Tunapomkubali Bwana Yesu Kristo kuwa Mwokozi wetu, tunaonyesha kwamba tunayakubali mamlaka ya Mungu Baba. Dhana ya “waumini” inaelezwa katika Kiyunani (lugha asilia ya Agano Jipya) kwa kutumia neno “pisteuontas” ambalo linamaanisha “[wale ambao] wanaamini”; utaona kwamba neno hili liko katika wakati-uliopo-unaoendelea (present participle tense). Dhana iliyoko ni ya tendo linalofanyika sasa – kuamini – na linaloendelea. Tukiwa kama wale walioweka imani yao katika Bwana Yesu Kristo, tuko katika hali inayoendelea ya imani katika Yeye”, na tunapoingia katika uhusiano huu wa imani na Kristo tunapewa pia uhusiano wa milele na Baba: “kupitia Yeye” tunakuwa pia “wale wanaomwamini Mungu Baba” (cf. Matendo 16:34; War. 4:24).

6.29 Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini Yeye [Kristo] aliyetumwa na Yeye [Baba].
Yoh. 6:29 SUV

12.44 Naye Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi [tu] bali Yeye aliyenipeleka [pia].
Yoh. 12:44 SUV

14.1 Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.
Yoh. 14:1 SUV

14.6 Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Yoh. 14:6 SUV

Aliyemfufua kutoka katika wafu na kumpa utukufu:

Kwa kufufuka na kutukuzwa kwa Kristo tunadhihirishiwa ushuhuda wa aina mbili wa ushindi Wake dhidi ya dhambi na mara mbili ya dhamana ya uzima wetu wa milele ijayo ulio na shani kuu. Kwani tu wamoja na Kristo, na kwa hivyo, tukiwa Mwili Wake na Bi Harusi Wake, tutashiriki katika kudura (destiny) Yake milele.

3.2  Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado [jinsi] tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa (revealed) [Kristo], tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.
1Yoh. 3:2 SUV

Na kama vile Kristo alivyotukuzwa na Baba baada ya ufufuo Wake na kukaa mkono wa kuume wa Baba katika kudhihirisha uhalali wa sadaka Yake na ushindi Wake msalabani (Zab. 2:7-8; 110:1; Waebr. 1:13; 12:2; 1Pet. 3:22; cf. Yoh. 13:31-32; 17:5; Wakol. 3:1), vivyo hivyo nasi tutashiriki katika utukufu huo (War. 5:1-2; Wakol. 1:27; Tito 2:13) – siyo aina fulani ya uhai wa kufifia na/au uhai wa mpito, bali ni uzima halisi na wenye neema tele katika miili mipya na isiyoharibika, tukiishi katika ushirika na Bwana wetu mpendwa na Mwokozi wetu milele.

8.17  na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.
8.18  Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu.
War. 17-18 SUV

Na matokeo yake ni kwamba unakuwa na imani na [ma]tumaini katika Bwana:

Matokeo ya Ujio wa Kwanza wa Kristo, kifo Chake cha kiroho kwa ajili yetu, na ufufuo Wake, kupaa mbinguni na kukaa kuume kwa Baba, sisi ambao tumemwamini Yeye pia “tuna imani na [ma]tumaini katika Mungu [Baba]”, kwani yeyote aliyeweka imani yake katika Kristo ni wa Baba pia.

10.38 lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba.
Yoh. 10:38 SUV

14.9 Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?
Yoh. 14:9 SUV

16.27 kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba.
Yoh. 16:27 SUV

Kwa msemo-hitimisho huu, Petro anatuleta katika kukamilisha mduara wa mchakato wa wokovu kwa kutuondolea shaka kwamba siyo tu sisi ni watu wa Kristo kwa imani yetu Kwake, bali sisi ni watu wa Mungu Baba pia – kwani hakuna tofauti yoyote baina ya mapenzi ya Baba na mapenzi ya Mwana (Yoh. 10:30). Hivyo, matokeo ya kuwa wana wa Mungu, tukipendwa sawasawa na Baba na Mwana, tunayo imani katika Baba na vivyo hivyo katika Mwana, na tumaini katika Baba kama tulivyo na tumaini katika Mwana, Bwana wetu mpendwa Yesu Kristo, tukitazamia wakati ambao tutakuwa nao wote pamoja mbinguni juu na, baada ya mwisho wa historia, katika nchi mpya hapa duniani. Tukijiamini katika wokovu wetu kama watoto wanaopendwa na Baba na Mwana Wake Bwana wetu Yesu Kristo, tumejazwa na Roho Mtakatifu tuliyeletewa Awe ndani yetu, tuna kila motisha ya kuitikia wito wa kuishi maisha ya utakaso kama Petro anavyotuhimiza katika sehemu hii ya Neno. Majaliwa au kudura (destiny) yetu ya milele iko salama katika Bwana kwa neema kupitia imani yetu. Ebu basi na tufanye kila juhudi tuitikie ile changamoto ya kuishi maisha yetu ya Kikristo kama vile Mwokozi wetu anavyotaka tuishi, bila kujali upinzani wowote au mateso tutakayolazimika kuyakabili, kwa ajili ya utukufu wa Bwana wetu mpendwa Yesu Kristo, tukikumbuka wakati wote kile alichokifanya kwa ajili yetu.

12.1  Basi na sisi pia [kama waumini wanaotajwa katika sura ya 11], kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii [watu na malaika], na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi [maeneo ya tabia zetu ambamo tuna udhaifu mkubwa zaidi]; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,
12.2  tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
12.3  Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya [waliotenda] dhambi [dhidi ya nafsi yake], msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu [na kukata tamaa].
Waebr. 12:1-3 SUV

Notes:

1. Tafadhali tizama Bible Basics Part 4A: “Christology”, Section II.5, “The Spiritual Death of Christ”.
2. Tafadhali tizama Bible Basics Part 4A: “Christology”, Section II.7, Redemption”.
=0=

Imetafsiriwa kutoka: Basic Christian Orientation to Life and Eternity: Peter’s Epistles Part 31

=0=

Basi, na tuonane katika somo #32 la mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amen!