Kanuni za Maadili Mema ya Kikristo: Nyaraka za Mtume Petro #34

Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa: https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo
Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for this Kiswahili Translation has been kindly granted by Dr. R. D. Luginbill
1Petro 2:11-25
2.11  Wapenzi, nawasihi kama wapita njia na wakazi wa muda tu hapa duniani, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo [kiuhalisia] na uzima wenu [wa kimwili na kiroho].
2.12  Mwe na mwenendo mzuri [mkingali] kati ya Mataifa (watu wasio Wakristo), ili, iwapo huwasingizia kuwa [mu] watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri (yaani maisha yenu mema na utumishi wenu kwa Kanisa la Kristo), wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa (ujio wa pili wa Kristo).
2.13  Tiini kila kiamriwacho na watu [wenye mamlaka] katika nchi mnamoishi, kwa ajili ya Bwana; ikiwa ni mfalme, kama [mtawala];
2.14  ikiwa ni wakubwa [wengine nchini], kama wanaotumwa Naye ili [kuwapa lawama wanayostahili na kuwaonya] watenda mabaya, na kuwasifu watenda mema.
2.15  Kwa sababu [haya] ndiyo mapenzi ya Mungu, kwamba kwa kutenda mema mzibe vinywa vya ujinga vya watu wapumbavu;
2.16  [mkiwa kama watu] walio huru, ila wasioutumia uhuru huo kwa kusitiri ubaya, bali kama watumwa wa Mungu.
2.17  Waheshimuni watu wote. Wapendeni ndugu (yaani Wakristo wenzenu). Mcheni Mungu. Mpeni heshima mfalme (yaani mtawala wa nchi mnamoishi).
2.18  Enyi watumishi, watiini bwana zenu kwa [heshima zote], sio wao walio wema na wenye upole tu, bali nao walio wakali [na waonevu].
2.19  Kwa maana ni jambo la sifa [mbele ya Mungu] kama mtu akivumilia [ili awe na dhamiri safi] anapoteswa kwa uonevu kwa ajili Yake.
2.20  Kwa maana mna sifa gani mkistahimili adhabu kwa sababu ya kutenda dhambi? Lakini kustahimili [mateso] mtendapo mema, huu ndio wema hasa mbele za Mungu.
2.21  Ninyi mliitwa kwa makusudi haya, kwa sababu Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akiwaachia kielelezo/mfano, ili mfuate nyayo zake.
2.22  “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake” (Isa 53:9b).
2.23  Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya (hakumtishia mtu); bali alijikabidhi (alimtumaini) kwake Yeye ahukumuye kwa haki.
2.24  Yeye mwenyewe alichukua/alibeba dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili sisi tukiwa wafu kwa dhambi, tuwe (tupate kuwa) hai kwa haki/uongofu; na kwa jeraha Lake mliponywa.
2.25  Kwa maana mlikuwa mnapotea kama kondoo; lakini sasa mmemrudia Yeye aliye Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu (uzima wenu).
1Petro 2:11-25

Utangulizi: Katika sehemu ya kwanza ya sura ya pili, Petro alitupatia analojia tatu ili kutuonyesha kwa mfano maisha ya Kikristo [yalivyo] baada ya kuzaliwa upya: kunywa maziwa ni analojia ya kujifunza kweli ya Biblia kwa makusudi ya kukua kiroho; kujenga nyumba juu ya mwamba ni analojia ya kupiga hatua chanya katika maendeleo yetu ya kiroho katika uhusiano wetu na Bwana Yesu Kristo; na ukuhani wetu wa kifalme ambamo tumeitwa na kuingizwa kunamaanisha utumishi wa kiroho kwa ajili ya Bwana ambao sote tumeitwa [tuutimize] – kila mmoja wetu kulingana na karama yake. Baada ya kuyaelezea mambo muhimu yaliyomo katika changamoto na fursa zinazowakabili waumini wote kufuatia tukio la kuzaliwa upya, Petro sasa anaendelea kwa kutupatia orodha ya matendo mema ambayo itakuwa muhimu sana kuifahamu katika vita tuliyomo ambayo ni ‘kuishi maisha yetu Kikristo’. Aya za 11 mpaka ile ya 25 ni, kimsingi, mfumo wa kanuni ambao waumini wote wenye nia ya kumpatia utukufu Bwana Yesu Kristo wanapaswa kuufuata, na Petro hapa anaujenga mfumo huu juu ya ule Mfano wa maisha ya Wakristo, na kwa hakika wanadamu wote, yaani Mwokozi wetu mpendwa:

Wapita njia na wakazi wa muda tu hapa duniani (aya ya 11):

2.11  Wapenzi, nawasihi kama wapita njia na wakazi wa muda tu hapa duniani, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo [kiuhalisia] na uzima wenu [wa kimwili na kiroho].

Ni muhimu kabisa kabisa kuwa mtazamo wetu kuhusiana na ulimwengu huu na maisha haya uwe kwamba vyote viwili – ulimwengu huu na maisha haya - ni vya muda na vya kupita tu. Tutakuwa hapa duniani kwa muda mfupi tu. Hatuna makazi ya kudumu katika huu ulimwengu ulioharibika na hii miili iliyoharibika ni ya muda tu. Tunatizamia kupewa miili ya milele (2Wakor. 5:1) na mahala tutakapoishi milele ambapo “mjenzi wake ni Mungu” (Waebr. 11:10). Hatujaleta chochote katika dunia hii, na hatutaondoka na kitu chochote (1Tim. 6:7) – isipokuwa zile thawabu tutakazopewa kutokana na juhudi zetu za kukua kiroho, kuishi Kikristo na kumtumikia Kristo na Kanisa lake.

Kwa hakika sisi [Wakristo] ni wapita njia tu hapa duniani (1Peter 1:1). Kama ambavyo Abrahamu na wazee wachamungu wenzake kama Isaka, Yakobo na wengine walivyoishi katika mahema, nasi pia tunaishi katika haya “mahema” ya muda ya mwili na damu, kwa shauku kubwa tukitazamia kutimizwa kwa lile tumaini letu (Tito 2:13), ufunuo wa Bwana wetu, wakati hii miili yetu ya uharibifu itakapobadilishwa (1Wakor. 15:51-54; 2Wakor. 5:1-8) nasi tutakuwa Naye milele (1Wathess. 4:17), tukimtazama kama alivyo [kiuhalisia] nasi tukiwa kama Yeye alivyo (1Yoh. 3:2). Kusahau msingi huu muhimu kunaweza kupelekea kwenye matatizo [ya kiroho] ikiwa matokeo ya kusahau huko ni sisi kuwa marafiki wa kupitiliza wa dunia hii na tunaanza kufurahia anasa zilizomo na kufanya urafiki nayo (linganisha na Zab. 90:9-12; 1Wakor. 7:29-31).

4.4  Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.
Yak. 4:4

2.15  Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba [kwa uhalisia] hakumo ndani yake.
2.16 Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima [yaani majigambo ya alicho nacho na anayoyafanya], havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.
2.17  Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu [akiwa hai] hata milele.
1Yoh. 2:15-17

Tamaa za mwili zipiganazo (kiuhalisia) na uzima wenu (aya ya 11):

2.11  Wapenzi, nawasihi kama wapita njia na wakazi wa muda tu hapa duniani, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo [kiuhalisia] na uzima wenu [wa kimwili na kiroho].
1Pet. 2:11

Maneno ya aya hii yanapaswa kuwa ya msaada mkubwa kwetu katika mapambano yetu dhidi ya dhambi – kwa kuwa yanatilia mkazo umuhimu mkubwa wa suala hili. Kwani “bila utakatifu, hakuna mtu atakayemwona Bwana” (Waebr. 12:14). Utakaso, kama tulivyoona [katika Nyaraka za Petro #13 na #30], ni utengano na dhambi na uovu, ukielezewa kuwa ni utakaso [wa mwanzo] katika Kristo pale tunapozaliwa upya, na pia utakaso-hitimisho (yaani katika ufufuo), pale itakapokuwa haiwezekani tena kwa sisi kutenda dhambi, tutakapokuwa katika miili yetu mipya. Kati ya utakaso wa mwanzo na utakaso-hitimisho, kuna ule utakaso mwingine, tukingali hapa duniani katika mwendo wetu wa Kikristo, ambapo tunafanya maamuzi wakati wote, ya kukataa kushindwa na vishawishi na kutenda dhambi. Tunapokuwa na nia ya kupambana na dhambi, Roho Mtakatifu yuko tayari wakati wote kutusaidia katika kufanya hivyo (kw. mf. Waga. 5:16-25; Yakobo 4:5-6). Tunaposhindwa katika vita hii, matokeo yake ni kwamba tunapoteza ushirika wetu na Bwana na hili linalazimu tumrudie Yeye na kumwomba msamaha kwa njia ya kukiri dhambi tuliyotenda (Zab. 32:5; 1Yoh. 1:9). Tunaposhindwa kumrudia na kutubu, hii husababisha, muda utakavyokwenda na dhambi zingine zitakavyoongezeka, kupungua kwa kasi yetu (kwa kiasi kikubwa) ya kukua na kuenenda kiroho, na hii yaweza kupelekea – katika baadhi ya Wakristo wenye mwenendo mbaya zaidi ambao wanashindwa kuuacha – kwenye apostasy, yaani kupoteza imani katika Bwana na hivyo kupoteza wokovu wao (kwa wale ambao wanageuka nyuma na kuukumbatia ulimwengu tena, wakimtelekeza Bwana) au kwenye ile “dhambi inayopelekea kwenye mauti” (kwa wale wanaoendelea kumwamini Bwana, lakini wakati huo huo hawataki kuyaacha maisha yao ya dhambi).1

Hii ndiyo maana “bila utakatifu”, hata wokovu wetu unaweza kuwa hatarini (Waebr. 12:14). Maneno ya Petro hapa kuhusu “tamaa za mwili zipiganazo na uzima wenu [wa kimwili na kiroho]” yanapaswa kuchukuliwa kwa umakini mkubwa, kwani ikiwa tunazungumzia “tu” uzima wetu wa kimwili (katika mfano wa wale Wakristo wanaochukuliwa na Mungu kwa njia ya “dhambi inayopelekea kwenye mauti” – wakipoteza nafasi/fursa yao kupata thawabu za ziada) au upotevu wa wokovu wao (katika mfano wa wale wanaochagua kuitelekeza imani yao katika

1Soma katika https://ichthys.com BB 3B: Harmatiology, section IV.6, “Apostasy and the Sin unto Death” kupata utondoti zaidi katika kanuni/fundisho hili.
Bwana, kuendelea na dhambi na kuukumbatia [tena] ulimwengu), katika mifano yote miwili hakuna jambo linaloweza kuwa baya zaidi. Hapa tunapaswa kuzingatia pia kwamba maendeleo ya kiroho, kiasi na kasi ya maendeleo hayo vitapungua sana kwa wale Wakristo wanaoyumba kati ya kuupenda ulimwengu [zaidi] na kumpenda Mungu [zaidi]. Kila mmoja wetu hutenda dhambi, lakini Wakristo wanaokuwa kiroho na wale Wakristo waliopevuka [kiroho] hutenda dhambi kwa kiasi kidogo zaidi na zaidi na dhambi mbaya zaidi siyo zile kubwa tu (hii haina maana kwamba dhambi siyo kitu kibaya, lakini kitendo cha ngono isiyo halali kwa wazi kabisa ni kibaya zaidi ya fikra ya kiburi dhidi ya mwenzako [au dhidi ya Mungu Mwenyewe]. Na mpaka tutakapofikia kiwango cha kuitawala miili yetu kwa ufanisi mkubwa, halafu tuweze kuitawala midomo yetu, na kisha mawazo yetu, maendeleo ya uhakika ya kiroho yatakuwa ni jambo la kubahatisha tu. Hivyo basi, katika utangulizi wa sehemu hii inayojadili mwenendo na maadili mema ya Wakristo, Petro anaanza kwa kutupatia msingi dhahiri na wa muhimu kabisa: kujilinda ndio msingi muhimu [na wa kwanza kabisa katika kupigana vita yenye ufanisi].

Tunaweza kulilinganisha fundisho hili na ule msingi wa vita unaoitwa “usalama” (security) ambao unalazimu kwamba matayarisho yafanywe, tena kwa uangalifu sana, dhidi ya mashambulizi yanayoweza kufanywa na adui hata wakati tunapoelekeza juhudi zetu katika mashambulizi yetu [dhidi ya adui huyo]. Kwani, ikiwa ugavi (supply) wetu wa mahitaji muhimu (kw. mf. maji, chakula, dawa, silaha, n.k.) unakatika, au kwa namna nyingine yoyote tunahatarishwa kwa sababu ya mashambulizi ya adui ambayo yanatukuta tukiwa hatujajitayarisha sawasawa, basi juhudi zetu zote tutakazozifanya za kusonga mbele vitani hazitakuwa na matokeo yoyote mazuri, na kwa kweli tutarudishwa nyuma na kupoteza muda wetu kwa sababu tulishindwa kujishughulisha na suala la kujilinda dhidi ya dhambi. Kwani, kwa kuwa bado tumo ndani ya miili hii ya dhambi na mauti (War. 7:24), dhambi itakuwa wakati wote “ikituvizia mlangoni” (Mwa. 4:7). Na kama ilivyo katika vita, tunaweza kupanga kila kitu, lakini adui naye hupata ushindi mara moja-moja, hivyo pia katika mwendo wetu wa Kikristo shetani na majeshi yake wanatuwekea upinzani katika kila kona, na kwa hakika wanatuwekea vishawishi mbele yetu katika namna na nyakati ambazo hatuwezi kutarajia [kabla]. Kwa kuwa vita yetu ndivyo ilivyo, kufanya mzaha na “tama za mwili” ambazo “zinapigana dhidi yetu” kutatufanya tuwe dhaifu mbele ya mashambulizi hayo ya kishetani – kinyume kabisa na kile kinachotarajiwa kutoka kwa kamanda yeyote wa kijeshi anayeijua kazi yake vizuri. Kiongozi wa kijeshi aliyefundishwa na anayeijua kazi yake vyema kamwe hatoacha maeneo muhimu aliyokabidhiwa bila ya ulinzi unaostahili – lakini Wakristo wanafanya hivyo, kwa kweli, pale wanapoupuuza uongozi wa kimungu ambao Petro anatupatia hapa.
Tukiendelea na mfano/analojia yetu ya kivita, ni jambo lisilowezekana “kuondoa” baadhi ya maeneo madogo-madogo (japo ni muhimu sana) kutoka katika eneo zima tulilokabidhiwa kulilinda, kwa kusudi la kuondokana na ulazima wa kulilinda eneo hilo [ati kwa sababu ni dogo tu]; vivyo hivyo inatupasa kuyalinda kwa makini yale maeneo ya tabia zetu ambamo tuna udhaifu unaotokana na hulka yetu ya dhambi kwa wakati wote tukingali katika ulimwengu huu na “tusifanye mipango ya kuridhisha uchu wa mwili” (War. 13:14; ling. na War. 6:11; War. 6:13; War. 6:19; War. 8:12; War. 12:1-2). Lakini pia si jambo jema kutumia muda mwingi tukifikiria namna ya kuyalinda maeneo hayo ya udhaifu wetu hata tukasahau kupeleka nguvu zetu katika lile jukumu nambari moja la maisha yetu ya Kikristo ambalo ni kukua kiroho – jambo ambalo litakuwa sawasawa na yule kamanda wetu kuweka askari wake wote katika kulinda yale maeneo muhimu na kusahau kupigana vita yenyewe! Kwa hiyo onyo la Petro la kujizuia kuridhisha tamaa za miili yetu halina kusudi la kuishia kwenye kujizuia huko tu, bali kusudi lake ni kutuweka sisi Wakristo katika hali ya utayari wa kuelekea kwenye mchakato wa kukua kiroho, kuendelea kuishi Kikristo na kulitumikia Kanisa la Kristo, ambayo ndiyo majukumu yetu makuu ya hapa duniani. Ikiwa tunataka kushinda yale mataji 3 ya ushindi yanayomletea heshima Bwana wetu na neema [za ziada] kwetu sisi katika milele yote, basi kujiingiza na kujihusisha katika mambo ya ulimwengu huu – na haswa katika yale mambo ya dhambi – ni kinyume kabisa na kusudi hilo.

2.3  Ushiriki taabu pamoja nami, kama askari mwema wa Kristo Yesu.
2.4  Hakuna mpiganaji wa vita ajitiaye katika shughuli za dunia, [kwa maana anajiepusha na hayo] ili ampendeze Yeye aliyemwandika awe askari.
2Tim. 2:3-4

Mwenendo wenu mzuri mkingali katikati ya mataifa (aya ya 12):

2.12  Mwe na mwenendo mzuri [mkingali] kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa [mu] watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri (yaani maisha yenu mema na utumishi wenu kwa Kanisa la Kristo), wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.
1Peter 2:12

Baada ya kuthibitisha katika aya iliyopita kwamba kuishi maisha yaliyotakasika ni jambo jema na la lazima ikiwa tunataka kuimarisha wokovu wetu, kukua kiroho na kupata thawabu kuu kabisa, Petro anaipanua kanuni hii kwa kutukumbusha kwamba matendo yetu – tunayoyafikiria, tunayoyasema na tunayoyafanya – pia yana athari kubwa kwa kila mtu tunayekutana naye, iwe kwa wale walio karibu sana nasi au wale walio mbali nasi. Kwani tumo katikati ya vita kuu na isiyoonekana kwa macho, kwa hiyo sisi hatuko huru kufanya yote tunayotaka hapa duniani. Mwenendo [wetu] mbaya unatuathiri sisi wenyewe katika maisha yetu ya kimwili na kiroho, lakini pia mwenendo wetu huu unaweza kuwaathiri wale wote tunaokutana nao (War. 2:24). Basi, badala ya kuwa mfano mbaya kwa wengine ambao Mungu hafurahishwi nao, tujitahidi [kwa mwenendo wetu] kuweka mfano mwema, si tu kwa sababu hili ni la faida kwetu (na kwa hakika mwenendo wetu mwema una faida kwetu, katika kuepuka adibisho/adhabu kutoka kwaMungu, na katika kupata thawabu njema za hapa duniani na zile thawabu za milele “kwa wale wanaomfurahisha Bwana”: Waebr. 11:5-6) lakini pia kwa sababu ya faida inayoweza kupatikana kwa wale wanaotuzunguka ambao wanatutazama, kwanza kwa waumini wenzetu (Waga. 6:10) na halafu kwa wale wasioamini ambao wanaweza kuamini kutokana na kuuona mfano wetu bora (1Wakor. 9:22). Kwani, ikiwa ni kweli tuna shauku ya kuwaona jirani zetu na wafanyakazi wenzetu wakiokolewa ili tufurahi pamoja nao “katika ile siku ya kujiliwa” - 1Pet. 2 aya ya 12 – yaani siku watakapohukumiwa kwa kusudi la kupata thawabu badala ya kupata adhabu ikiwa walifuata mfano wetu hapa duniani, basi ule mwenendo unaoharibu ushuhuda wetu wa Kikristo unapaswa kuachwa, na badala yake tunapaswa kuufanya mwanga wa taa yetu ya imani ung’are mbele yao katika namna ya kimungu.

5.16 Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
Matt. 5:16 SUV

Msemo unaotumiwa na Bwana wetu hapa juu (katika hati-mlazo, nzito) ni ule ule unaotumiwa na Petro katika aya tunayojifunza hapa: “kazi zilizo njema/matendo mema” (katika Kiyunani: kala erga / καλά έργα ). Kwa kuwa msemo huu, “matendo mema”, umeeleweka visivyo kwa kiasi kikubwa sana, tena na Wakristo pia, ni jambo linalofaa hapa kueleza kwamba “matendo / kazi” ni kila kitu tunachokifikiria, tunachokisema na tunachokifanya. Katika lile tukio kuu la hukumu ya mwisho, wale ambao hawakuamini watatathminiwa “kila mmoja wao kadiri ya matendo (kazi) yake” (Ufunuo 20:12-13) – na nukuu hii kutoka katika kitabu cha Ufunuo kwa dhahiri kabisa inaonyesha kwamba maisha yao yote yatatizamwa kwa utondoti mkubwa, na kuwekwa wazi. Kinyume na makisio ya wanateolojia wengi, na makisio yanayopendwa na watu wengine wengi, hukumu hii ya mwisho haitahusiana na kudhihirisha kwamba dhambi walizotenda wasioamini ndiyo sababu ya wao kuukosa uzima wa milele: hii si sahihi, kwa sababu Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zote na za wote, na hivyo hukumu ile haitahusiana na dhambi zao hata kidogo. Wasioamini wataonyeshwa kwa utondoti mkubwa kwamba hakuna kitu chochote walichofanya ambacho kilitosheleza kuwapatia wokovu. Hii ni kusema kwamba, itadhihirishwa kwamba hakuna “kazi au tendo” hata moja lililokuwa “jema” au “zuri” kwa namna yoyote ile – kwa sababu hakuna hata kitu kimoja “walichofanya” [kwa utashi wao] ambacho kilifanywa katika uweza wa Roho Mtakatifu.

6.29 Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini Yeye (Kristo) aliyetumwa na Yeye (Baba).
Yohana 6:29

Ni baada ya sisi “kuifanya” ile “kazi” ya kujiwekea msingi muhimu ambao Mungu ametuita tuifanye, yaani kuiweka imani yetu katika Bwana Yesu Kristo kwa ajili ya wokovu wetu, ndiyo tunakuwa waumini, na ni baada ya kuchukua hatua hii tu ndiyo tunakuwa na uwezo wa “kufanya matendo / kazi [njema]”. Kazi na matendo yote yanayofanywa na watu wasioamini, wasio Wakristo, ambao hawajazaliwa upya, [ijapokuwa machoni pao wenyewe na machoni pa ulimwengu yanaweza kuonekana kuwa ni “mema”] ni [kama] “nguo zilizotiwa unajisi” (Isa. 64:6 SUV), kwa sababu [kwa] mtazamo wa Mungu matendo hayo hayajafanywa na Roho wa Mungu katika Jina la Yesu Kristo. Hakuna kitu chochote ambacho mtu asiyeamini anakifanya kinaweza “kumfurahisha Mungu” (kw. mf. 1Wakor. 12:3). Mbele za macho ya Mungu, ni waumini katika Kristo pekee wana uwezo wa “kufanya matendo na/au kazi” ambazo ni “njema”. Kwa hiyo hakuna kitu chochote ambacho mtu asiyeamini atakifanya, hata kama ni cha kujitoa sadaka au cha kusifiwa kiasi gani mbele za macho ya ulimwengu, chenye uwezo wa kumpatia mtu huyo wokovu, isipokuwa tu ikiwa tendo / kazi hiyo ikifanywa ndani ya imani katika Kristo.

9.30  Tuseme nini, basi? Ya kwamba watu wa Mataifa, wasioifuata haki, walipata haki/uongofu; lakini ni ile haki (uongofu) itokanayo na imani;
9.31  bali Israeli wakiifuata sheria kama njia ya kufikia kiwango cha haki/uongofu, hawakufanikiwa katika hilo.
9.32  Kwa sababu gani? Kwa sababu hawakuifuata kwa njia ya imani, bali kana kwamba kwa njia ya matendo. Wakajikwaa juu ya jiwe lile likwazalo.
War. 9:30-32

2.8  Kwa maana mmeokolewa kwa neema [ya Mungu], kwa njia ya imani [yenu kwa Kristo]; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa [cha bure] cha Mungu;
2.9  [na] wala si kwa matendo [yenu], mtu awaye yote asije akajisifu.
2.10  Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza [tayari] ili tuenende nayo.
Waefe. 2:8-10

Mkanganyiko mwingi katika suala hili unatokana na kutafsiriwa vibaya kwa ile aya maarufu ya Yakobo inayosema kwamba “imani bila ya matendo imekufa” (Yak. 2:22; Yak. 2:26). Lakini ni jambo la wazi kabisa ambalo halina haja ya kusemwa kwamba Yakobo anaturejesha na kuzungumzia “kazi / matendo” ambayo ni “mema” kikwelikweli, [aina] ya matendo ambayo waumini wanaomwitikia Mungu na wanaouitikia ukweli Wake wanaweza kuyatenda, kama vile ile mifano anayoitoa [Yakobo] katika muktadha wa sura na aya zilizonukuliwa ya Abrahamu na Rahabu inavyoonyesha kwa wazi kabisa (Yak. 2:21-25): waumini wote halisi hufikiri na kusema na kufanya yale ambayo Mungu anafurahishwa nayo, na mwenendo huu wa kimungu, “kazi” au “matendo” haya ya kimungu, yanadhihirisha imani yao au yanawahalalisha. Huu ndio muktadha ambamo Petro anaitumia istilahi hii hapa: tunapoenenda vile Wakristo wanavyotakiwa kuenenda, tukiwaza mawazo ya kimungu ambayo husababisha [maneno], matendo na kazi za kimungu, tunakanusha kwa matendo na mazungumzo yetu ya kimungu, uzushi wa watu wasioamini wanaoweza kutupinga. Hivyo basi, jambo lolote ambalo watu wasioamini wanaweza kulisema kuhusu sisi, ikiwa tunatembea kama ambavyo Bwana Yesu anataka tutembee, basi uzushi wote huo kutoka kwa wasioamini utakuwa hauna uhalali wowote. Kama tutapitia mateso kwa sababu hiyo, basi tutakuwa hatustahili mateso hayo na hivyo Kristo anapata utukufu badala ya shutuma. Ikiwa tunakaza nia na kuendelea na kazi zetu njema, tunaweza kuwa na uhakika kwamba kila kitu tulichokifanya kwa ajili ya Bwana Yesu Kristo kitapata thawabu yake ya milele (Matt. 6:19-21; Matt. 10:42; Waga. 6:9-10; Waefe. 2:10).

Wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa (aya ya 12):

2.12  Mwe na mwenendo mzuri [mkingali] kati ya Mataifa (watu wasio Wakristo), ili, iwapo huwasingizia kuwa [mu] watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri (yaani maisha yenu mema na utumishi wenu kwa Kanisa la Kristo), wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa (ujio wa pili wa Kristo).
1Pet. 2:12

Akiwa chini ya ufunuo wa Roho Mtakatifu, Petro alifikiria kwamba ilikuwa ni muhimu kusisitiza kwamba ushuhuda mwema wa maisha yetu unatupa haki ya kutarajia thawabu kutoka kwa Bwana wetu. Ni kweli kwamba ni sahihi na vyema kwa Mkristo kuitumia motisha ya thawabu za milele ambazo Bwana wetu ameziahidi kwa wale wanaopambana vita ya Kikristo katika njia sahihi, ya

kimungu.2 Petro anaongeza na kukumbusha juu ya mafundisho yake ya kwa nini ushuhuda mwema una faida kwetu, kwamba hii ni sehemu tu ya taswira nzima, na kwamba ni halali kuwa na shabaha kama hii ingawa inaweza kuonekana kama vile ni ubinafsi. Kwa upande mwingine, tunapaswa pia kuhamasishwa kuishi maisha ya Kikristo kwa faida ya wale wanaotutazama – malaika na wanadamu wenzetu, walio hapa duniani na waliokwishaondoka – na kwa utukufu wa Mungu. Yesu Kristo alikufa kwa ajili ya kila mmoja wetu, ikiwa ni pamoja na wote wasioamini ambao wanatutazama katika mwendo wetu wa Kikristo. Kama kwa ukweli tunaufanya / tunauacha mwanga wa Mungu ukiangaze kila tunachokisema na kukifanya katika huu ulimwengu wa wasioamini, na kama hayo yanachangia katika kuokolewa kwa [hata] mmoja wao tu basi ile shabaha ambayo Petro anaisema hapa inafanikishwa, yaani kwamba wale wanaotufahamu kwa kututazama kwao waweze kuokolewa na kufikia, pamoja na sisi, “kumtukuza Mungu” katika siku ile ya kutathminiwa kwa Kanisa la Kristo – kwa sababu nao pia wameamini, na hili ni jambo la utukufu kwa Kristo pamoja na uzima [wa milele] kwao. Kwa kuwa basi tuna agizo [kutoka kwa Mungu] lenye taswira tatu, la kuutafuta utukufu wa Mungu katika yote tunayoyatenda, kuutafuta wokovu kwa ajili ya wanadamu wote, na kutafuta thawabu za milele kwa ajili yetu wenyewe,
basi ni kitu gani kitatuzuia tusijitahidi kutembea katika hii dunia kama Wakristo wema wasiokuwa na lawama katika kipindi hiki kifupi cha uhai wetu hapa duniani (1Pet. 2:11)? Tuna wito muhimu sana wa kutimiza – kwa hakika hakuna jambo muhimu zaidi ya hilo – na tutakuwa tumeutimiza wito huu kwa ukamilifu na kwa mafanikio ikiwa tunatii maelekezo ya Petro hapa, ya kujitenga na yote yanayoweza kuleta shutuma / lawama kwa ushuhuda wetu kama Wakristo na badala yake tuwe waangalifu katika kuakisi upendo na huruma ya Bwana Yesu Kristo katika yote tunayoyasema na tunayoyatenda.

Tiini kila kiamriwacho na wale wenye mamlaka katika nchi mnamoishi, kwa ajili ya Bwana (aya ya 13):

2.13  Tiini kila kiamriwacho na watu [wenye mamlaka] katika nchi mnamoishi, kwa ajili ya Bwana; ikiwa ni mfalme, kama [mtawala];
1Pet. 2:13

Kitu cha kuona kuwa ni cha umuhimu wa kwanza katika nukuu ya hapa juu ni sehemu yenye hati mlazo (italics): “kwa ajili ya Bwana”. Kama wawakilishi wa

2 Soma “The Judgement & Reward of the Church”, section I.7 in part 6 of Coming Tribulation katika https://ichthys.com
Bwana Yesu Kristo hapa duniani, ni muhimu sana kwa ajili ya ushuhuda tunaowajibika nao Kwake, kuwa watiifu kwa “wale wenye mamlaka katika nchi tunamoishi”.3 Hii ndiyo kusema, tunatii mamlaka za nchi / serikali kwa sababu ya Bwana Yesu Kristo. Haya ni matakwa Yake kwa ajili ya Kanisa Lake. Pili, tunapaswa kuwa waangalifu na kuona kwamba ni mamlaka halali pekee yanayopaswa kupewa utiifu na kuheshimiwa, yaani serikali iliyosimikwa katika nchi ambamo muumini husika anaishi. Maana ya hili ni kwamba tunaweza kusema kuwa kwa kipindi kirefu cha historia, serikali zilizokuwa [na zilizoko sasa] madarakani popote pale ambapo waumini wameishi, na wanaishi, ndipo penye “wale wenye mamlaka katika nchi”. Na mahali palipo na mamlaka yaliyosimikwa, basi mamlaka hayo yamesimikwa … na Mungu.

13.1  Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo inapaswa kumtii na inawajibishwa na Mungu.
13.2  Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu.
13.3  Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake;
13.4  kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu.
13.5  Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri.
War. 13:1-5

Maandiko yanatusimulia kwamba “wale wenye mamlaka” ambao chini ya mamlaka yao Paulo aliishi wakati anaandika waraka huu walimtia gerezani,
walimtesa na kumnyanyasa mara nyingi na waliendelea kumfanya hivyo kwa ukatili zaidi katika muda mfupi uliofuata, na mwisho wake wakamwua bila kufuata

3Hakuna utata [wowote] juu ya maana ya maandiko haya hapa kwani kitenzi cha Kiyunani hypotasso ni neno lile lile linalotumika kuelezea utovu wa utiifu kwa Mungu katika Waebrania 12:9, Yakobo 4:7, na kwa Bwana Yesu Kristo tukiwa kama Bibi Harusi Wake (waumini wote kiujumla) katika Waefeso 5:24. Zaidi ya hapo, asili ya etimolojia ya kitenzi hiki ni ya kijeshi, ambamo uvumilivu wa kutokutii ni mdogo sana; kitenzi-neno hiki kinamaanisha kujipanga katika msitari [wa kikosi cha jeshi] na kutii amri zitakazotolewa kwa ajili ya shughuli za kijeshi zinazofuata (katika War. 13:1; War. 13:5; Tito 3:1 pana kitenzi kile kile).
sheria zilizokuwako – na hivyo aya hii iko wazi kabisa. Hata zile serikali ambazo kwa mwenendo wao hazifanyi kazi yao katika kiwango stahiki cha haki na sheria (yaani serikali mbovu) hazipaswi kuchukuliwa – kwa sababu hiyo – kuwa siyo mamlaka ambayo Mungu mwenyewe ameyasimika. NB.: Tizama pia mfano wa utiifu wa Danieli na wenzake kwa mamlaka ya mfalme katika Babeli, licha ya kwamba Babeli iliivamia Yuda na kuwachukua mateka.

Sasa, je, serikali iliyoko madarakani ionyeshe uovu wa kiasi gani ndipo waumini wa Bwana waweze kuruhusiwa na [Mungu] kuacha kuitii? Katika enzi ya Kanisa inayoitwa Smirna Wakristo waliishi chini ya unyanyasaji na mateso yasiyokwisha kwa kipindi chote mpaka mwisho wa enzi hiyo, wakipitia mihula 10 mfululizo ya “dhiki” (Ufunuo 2:10). Zaidi ya hilo, waumini hawa hawakuwa tu wahanga wa serikali dhalimu au isiyofuata sheria – Wakristo hawa waliteseka kwa sababu tu walikuwa Wakristo. Sasa, Bwana wetu anawaelekeza wafanye nini katika mazingira hayo? “Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima”. Wanaagizwa wawe wastahamilivu katika mateso hayo, wakivumilia yote – na wasifanye upinzani wala uasi au kuyakimbia mateso hayo. Ni wazi kabisa kwamba waumini hawa hawakuacha kuamini wala hawakuacha kusali na kuomba wala hawakuacha utumishi wao kwa Kanisa – na hayo ndiyo yanayotutambulisha sisi sote kuwa ni Wakristo, na hayo ndiyo yaliyowaletea mateso. Wala hawakuiacha imani yao katika Kristo, na badala yake kumwabudu mfalme [wa Rumi kama sheria ya nchi ilivyoamrisha] pale walipotiwa nguvuni na kushitakiwa katika mahakama za Rumi; na msimamo huu uliwagharimu wengi wao uhai wao – lakini wakati huo huo msimamo wao huu uliwahakikishia uzima wao wa milele, na thawabu ambazo watapewa waliokufa kifo halisi cha kishahidi. Kutokana na aya hizi na mifano mingine katika Biblia, tunaweza kusema kwamba amri ya kuitii serikali iliyoko (ambayo tunaiona pia katika Tito 3:1) haitulazimu kuacha yale yote tuliyoamriwa kuyatenda (kama ambavyo Danieli hakuacha kuomba, na Mitume hawakuacha uinjilisti: Dan. 6:1ff; Matendo 4:18-20). Lakini tunaamriwa kutochukua silaha na kupambana na serikali ambayo ni wazi kabisa “imesimikwa na Mungu”. Soma pia “Kiongozi Bora wa Taifa Anapatikanaje?” katika https://sayuni.co.tz/masomo.mafupi/

Kama wanaotumwa Naye ili kuwapa lawama wanaostahili na kuwaonya wanaotenda mabaya, na kuwasifu watenda mema (aya ya 14):

2.14  ... wakubwa [wengine nchini], kama wanaotumwa Naye ili [kuwapa lawama wanayostahili na kuwaonya] watenda mabaya, na kuwasifu watenda mema.
1Pet. 2:14
Inaweza kuonekana kuwa ni vigumu kuzikubali serikali na tena inaweza kuwa ni vigumu zaidi kuwakubali maafisa wa serikali kwamba “wametumwa na Mungu” – haswa kwa mtu ambaye amesoma kiasi hata kidogo tu cha historia au mtu ambaye ana kiasi chochote cha uzoefu wa maisha. Lakini kauli hii ya Petro inapaswa kueleweka kwa urahisi sana na kuchukuliwa kwa makini, kama ile kanuni inayofanana [na hii] iliyotolewa na Paulo katika kitabu cha Warumi katika War. 13:1-5, ling. na Tito 3:1. Kama Paulo anavyosema katika aya ya kwanza ya kifungu hiki, “… hakuna mamlaka yasiyotoka kwa Mungu”, na mara baada ya kusema hivyo, anasema tena: “na ile [mamlaka] iliyopo inapaswa kumtii [Mungu], nayo inawajibishwa na Mungu” – akimaanisha kwamba uovu wowote unaofanywa na serikali si juu yetu kuuhukumu kwa sababu mamlaka hayo hayo yamo katika mikono ya Hakimu wa Mwisho. Haya [ya kuwajibishwa na Mungu] ni matarajio ya kutisha kwa afisa yoyote wa serikali yoyote ile [ikiwa atayatafakari] – au yanapaswa kuwa ya kutisha. Mafundisho haya yana shabaha pia ya kutupa faraja sisi Wakristo (waumini) kila mara tunaponyanyaswa au tunapoonewa au hata kuteswa na mamlaka yaliyosimikwa ya serikali: Mungu ndiye mwenye mamlaka halisi na ndiye atakayetudhihirisha sisi kuwa hatuna hatia – ikiwa tu hatutajichukulia sheria mkononi na kujaribu kujionyesha kuwa hatuna hatia.

13.2  Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao [na wenye mamlaka hayo] watajipatia hukumu.
War. 13:2

Kanuni hii haina maana kwamba sisi hatuna haki ya kujilinda na kujitetea tunapokuwa hatarini dhidi ya wahalifu (Bwana Yesu Kristo aliwaagiza wanafunzi wake wabebe majambia [ya kivita] kwa lengo la kujilinda: Luka 22:36). Pia kanuni hii haimaanishi kwamba hatuna ruksa ya kutumia njia halali za kisheria kujilinda dhidi ya unyanyasaji usio wa haki (kwa hakika Paulo alifanya hivyo: kw. mf. Matendo 25:11). Lakini kanuni hii inamaanisha kwamba msingi wa kufanya / kutimiza yale ambayo mamlaka halali yanatuamuru tufanye (kama vile kulipa kodi: Matt. 22:17-21; War. 13:6-7) na kujizuia kufanya yale yanayokatazwa na serikali hizo (Matt. 26:52; Tito 3:1; 1Pet. 4:15-16) ni msingi wa kimungu na umetoka kwa Mungu.

1 Mungu asimama katika kusanyiko la Mungu; Katikati ya miungu anahukumu.
2 Hata lini mtahukumu kwa dhuluma, Na kuzikubali nyuso za wabaya?
3 Mfanyieni hukumu maskini na yatima; Mtendeeni haki aliyeonewa na fukara;
4 Mwokoeni maskini na mhitaji; Mwopoeni mikononi mwa wadhalimu.
5 Hawajui wala hawafahamu, hutembea gizani; Misingi yote ya nchi imetikisika.
6 Mimi nimesema, Ndinyi miungu, Na wana wa Aliye juu, nyote pia.
7 Lakini mtakufa kama wanadamu, Mtaanguka kama mmoja wa wakuu.
8 Ee Mungu, usimame, uihukumu nchi, Maana Wewe utawarithi mataifa yote.
Zab. 82:1-8

Sehemu kubwa sana ya ngao ambayo waumini wanapaswa kuwa nayo katika kukubali na kulitekeleza agizo hili la kutii mamlaka [za kiserikali zilizomo katika nchi wanamoishi] – hata kama kiwango cha utendaji haki cha serikali husika kiko chini sana – inatokana na ufahamu wa uhakika kabisa kwamba Mungu ndiye anayeendesha mambo yote katika ulimwengu, ikiwa ni pamoja na serikali zote – ambazo kiuhalisia Yeye ndiye anayezisimika na kuziendesha – na kwamba serikali hizi zinawajibishwa Naye, ingawa yawezekana watendaji waliomo serikalini wakalijua hili au la. Tunapaswa kukumbuka kwamba ruksa ya Mungu ya sisi viumbe Wake kuwa na utashi huru kabisa ina matokeo ya uwepo wa watendaji wenye dosari / mapungufu wanaounda mifumo ya kiutendaji yenye dosari / mapungufu ambayo pia inatumika katika namna ambazo zina dosari / mapungufu kwa kiasi kikubwa – lakini Yeye wakati wote anatutakia mema na ametutayarishia mahitaji yetu kwa utimilifu kutokana na ufahamu Wake tangu kabla ya kuumbwa ulimwengu. Yeye atatulinda pale mifumo hii ya kibinadamu inaposhindwa kufanya kazi sawa sawa, na atatuthibitisha kwamba hatuna hatia pale tutakapotendewa kinyume na haki.

32 Mtu asiye haki humvizia mwenye haki, Na kutafuta jinsi ya kumfisha.
33 Bwana hatamwacha mkononi mwake, Wala hatamlaumu atakapohukumiwa.
Zab. 37:32-33 SUV

17 Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu Mimi, asema Bwana.
Isa. 54:17 SUV

12.19  Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana.
War. 12”19 SUV

Wakristo wanapaswa pia kukumbuka kwamba haki iliyo timilifu inakuja hapo mwisho wa dahari. Wakati wa utawala wa Mileniamu wa Bwana wetu, ufalme Wake utakuwa ni wenye haki timilifu, ambayo itakuwa ikitolewa Naye kwa wakati, nasi tutakuwa na neema ya kushiriki katika utawala huo (Isa. 32:1-2; Ufu. 2:27; Ufu. 3:21).

6 Bwana uondoke kwa (katika) hasira yako; Ujiinue juu (dhidi) ya jeuri ya watesi wangu; Uamke kwa ajili yangu; Umeamuru (amuru) hukumu.
Zab. 7:6 SUV

6 Kiti chako cha enzi, Mungu (yaani Masihi, ling. na Waebr. 1:8), ni cha milele na milele, Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili
Zab. 45:6 (ling. na Zab. 71:1-2; Zab. 89:14; Zab. 97:2)

7 Ukuu wa enzi yake (yaani Masihi) na amani hautakuwa na mwisho kamwe, atakaa katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; atauthibitisha na kuutegemeza kwa haki na kwa uongofu, tangu sasa na hata milele. Ari ya Bwana wa majeshi ndiyo itakayotenda hayo.
Isa. 9:7

4 bali kwa haki [Masihi] atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya.
Isa. 11:4 SUV

5 Na kiti cha enzi kitasimikwa kwa upendo; na mmoja (yaani Masihi) ataketi juu yake katika kweli, [atakayetoka] katika hema ya Daudi; akifanya hukumu, akitaka sana yaliyo haki, mwepesi wa kutenda haki.
Isa. 16:5

6 Naye atakuwa roho ya hukumu kwake yeye aketiye katika kiti cha hukumu; naye atakuwa [chemchemi ya] nguvu kwao wapambanao na kuwarudisha nyuma adui walio langoni.
Isa. 28:6

1 Tazama, mfalme (yaani Masihi) atamiliki kwa uongofu, na wakuu watatawala kwa haki.
Isa. 32:1

5 Bwana ametukuka; kwa maana anakaa juu; amejaza Sayuni hukumu na haki.
Isa. 33:5

1 Tazama mtumishi wangu (yaani Masihi) nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia Roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu.
Isa. 42:1 SUV
5 Haki yangu i karibu, wokovu wangu umekuwa wazi, na mkono wangu (yaani Masihi) utawahukumu kabila za watu;
Isa. 51:5a

Katika utawala wa Mileniamu wa Bwana wetu, hakutakuwa na shaka yoyote kuhusu ukweli kwamba mamlaka yanayotawala ni halali na yamesimikwa na Mungu. Kwani Mwana wa Mungu atatawala kwa uongofu uliotimilika, akiamua kwa haki iliyotimilika, na neema za serikali hiyo timilifu zitakuwa tofauti kabisa na serikali zote zilizosimama kabla yake – haswa pale itakapolinganishwa na serikali ya mpinga-kristo ambayo itaitangulia kwa miaka michache tu (na ambayo itakuwa ni serikali yenye uovu mkubwa kuliko zote katika historia ya wanadamu).

Hata hivyo, ni kweli kwamba tofauti kati ya serikali mbalimbali zilizokuwako na zitakazokuwako kabla ya hizo serikali mbili zijazo haitakuwa kubwa sana kama ilivyo tofauti kati ya giza na usiku – serikali ya mpinga-kristo (mbaya sana) na mwanga wa mchana – serikali ya Mileniamu ya Kristo (njema sana). Pia kutakuwa – na kumekuwa – na nyakati katika historia ya wanadamu ambapo Wakristo wanajikuta wakiwa chini ya serikali kadhaa zinazoshindana katika nchi moja wanamoishi (kw. mf. Somalia, Sudan, D. R. Congo, baadhi ya nchi mpya za Balkans, n.k). Pia kipindi cha mapinduzi yaliyofanyika USA na pia wakati wa vita kati ya Kaskazini na Kusini mwa nchi hiyo kinatupatia mifano ya ziada ya hali hii; tunaweza kuona kwamba hali iko hivyo hivyo katika nchi yoyote ambamo serikali iliyomo iko katika mchakato wa kupinduliwa na kikundi kinachotaka kuunda serikali nyingine kutoka ndani au nje au iko katika hatari ya kupinduliwa kwa namna hiyo. Katika mazingira hayo – ambayo si kawaida sana lakini hutokea wakati fulani na hivyo suala hili halizungumzwi moja kwamoja katika maandiko – yaweza kumlazimu Mkristo kuamua yeye mwenyewe ni ipi kati ya serikali hizo ni halali. Mara nyingi, mabadiliko huja haraka na yanahitaji tu kubadilisha mtazamo kuhusiana na utawala mpya. Hata hivyo, wakati mwingine mchakato wa mapambano unaweza kuchukua muda mrefu [zaidi], kati ya kundi lililoko madarakani na lile linalotaka kutwaa madaraka.

Kuhusu maamuzi ya waumini katika nyakati kama hizi juu ya upande gani ambao muumini huyu atauunga mkono na kutii amri za upande huo, itakuwa ni matokeo ya uongozi wa dhamiri yake mwenyewe baada ya sala na maombi ya kupata uongozi wa Roho Mtakatifu. Na katika mifano mingi ya aina hii tunayoiona katika historia (yaani kama katika mifano miwili inayotajwa hapo juu), itakuwa si sahihi kuwakosoa bila kufahamu mazingira waliyomo wale wanaoamua kuitii serikali iliyopo au ile inayotaka kuwa mbadala wake. Tunachoweza kusema kwa uhakika, hata hivyo, ni kwamba waumini wanapaswa kuwa na ufahamu wa wazi kabisa wa matokeo yanayoweza kutukia kutokana na kuunga mkono kwa hali na mali kundi lolote la kisiasa kwa kiwango ambacho ni zaidi ya maelekezo yanayotolewa na maandiko. Kuchagua kuunga mkono upande fulani kati ya pande [kadhaa] zinazoshindana kisiasa kunaweza kuwa ni tendo la kishujaa na la heshima sana, na pia Mkristo mhusika anaweza kuepuka makosa ya kimaadili na kuendelea kuwa mtu mwema, lakini ni nadra sana kwa uchaguzi wa aina hii kutokuwa na matokeo mabaya kwa mhusika, familia yake na nchi yake. Na wakati “kutofanya uchaguzi / uamuzi” kuhusu jambo fulani pia ni kuamua, na ambako kuna uwezekano wa mhusika kuonekana mwoga mbele ya kadamnasi / raia wenzake, waumini wanapaswa kukumbuka sababu ya sisi kuwapo hapa duniani na ni Nani tunayemtumikia kwanza na juu ya wote kabla ya kujiingiza na kujiwajibisha na kundi lolote la kisiasa, hata kama wakati huo jambo hilo linaweza kuonekana kwamba ni la lazima na halizuiliki.

Mzibe vinywa vya ujinga vya watu wapumbavu kwa kutenda mema (aya ya 15):

Tumesema tangu hapo mwanzoni mwa mfululizo huu kwamba baadhi kati ya malengo makubwa ya Petro wakati anaandika waraka wake huu [wa kwanza] yalikuwa ni kufariji, kutia moyo, na kuwaandaa waumini aliokuwa akiwaandikia kutokana na mateso yaliyokuwa yakiwasibu. Kuacha mambo yote yanayoweza kuleta shutuma / lawama kwa ushuhuda wetu [wa Kikristo] na badala yake kuakisi upendo na huruma ya Bwana Yesu Kristo katika yote tunayoyasema na kuyatenda yaweza kuwa ni jambo gumu katika mazingira ya kawaida lakini yakafanywa kuwa magumu zaidi ikiwa wakati huo huo muumini anaonewa na wale walio madarakani, whether watesi hao ni watumishi wa serikali, waajiri mahala anapofanya kazi, au ndugu katika familia (kwa mfano waume, wake au wazazi), na ni kwa sababu hiyo, bila shaka, Petro anaanza mjadala wa suala hili muhimu kwa kuzungumzia ulazima wa kutii mamlaka yote halali. Lakini ni kweli pia kwamba kuwatendea Kikristo watu wote ni sehemu muhimu ya ushuhuda wetu, hata kwa wale ambao hawana mamlaka juu yetu. Hivyo basi, Petro sasa anarejea kwenye mada yake ya mwendo sahihi wa Kikristo katika nyanja zote za maisha, na siyo tu katika mahusiano yetu na mamlaka halali.

Kunyamazisha vinywa vya watu wasioamini, wanaosema mabaya kuhusu imani yetu, ndiyo “mapenzi ya Mungu” katika nyanja zote za maisha, na hili linaweza tu kufanikishwa “kwa kutenda mema”. Hii dhana ya “kutenda mema” ni, kwanza kabisa, “kuacha kutenda mabaya”, yaani kufanya au kusema, na pia, ili kufanikisha hayo yote mawili, “kufikiria au kuwaza” jambo lolote ambalo haliendani na hali ya kuwa mfuasi wa Bwana Yesu Kristo. Hii ni kusema, kujizuia kutenda (ikiwa ni pamoja na “kufikiri”) mambo yote yanayoweza kuchafua ushuhuda wetu wa Kikristo ndiyo namna bora zaidi ya “kufunga midomo” ya wale wanaotaka kuleta uzushi juu yetu na kwa namna hiyo kumkashifu Bwana wetu. Kwani sisi ndio mabalozi Wake katika hii dunia (2Wakor. 5:20; Waefe. 6:20; 1Pet. 2:21), na Yule mwovu na [ma]wakala wake siku zote wanatuchunguza, wakitaka kutuona tukitenda maovu, ili wakatushitaki mbele ya Bwana wetu (Ufu. 12:10; ling. na Zak. 3:1; 1Pet. 3:8), lakini pia kwa njia hiyo waweze kulitia ukakasi jina “Mkristo” katika mioyo ya wale wanaotutazama. Tunapoakisi mwanga wa Bwana wetu katika mwenendo wetu, ushuhuda wa maisha yetu unakuwa nguvu kuu, ukitia nuru katika ile kweli (Matt. 5:14-16; Waefe. 5:8; Wafi. 2:15), na kwa namna nyingi huu ndio uinjilisti wenye nguvu na uwezekano mkubwa wa mafanikio kuliko aina zote nyingine za uinjilisti – unapofanyika na kuonekana katika maisha yetu wakati wote na katika namna ya kimungu. Lakini ikiwa mwenendo wetu hauna tofauti sana – au siyo mwema zaidi – na mtu wa kawaida asiyeamini, basi ushuhuda wetu huu hautafikia malengo yake. Na kwa hakika, yeyote anayetutazama na mwenye shaka juu ya ukweli tunaotamka – au yeyote asiyeupenda ukweli huo kabisa – atatutathmini kwa matendo yetu mabaya na si kwa maneno / mafundisho yetu, hata kama maneno / mafundisho hayo yamejazwa neema ya kweli kiasi gani.

“Kutenda mema” katika namna iliyo chanya kunamaanisha kuusimamia na kuukuza mpango wa Mungu katika namna ambayo kila mmoja kati ya sisi Wakristo ameagizwa kufanya. Hii inalazimu mambo fulani ya msingi yanayohusisha Wakristo wote kuyatenda, yaani kukua kiroho, kumweka Kristo kwanza katika mwendo wetu, na kuzaa matunda kwa ajili ya Bwana wetu kwa kuzitumia karama tulizopewa na Roho Mtakatifu. Kama ni kwa njia ya sala, au [kutia] wenzetu moyo, au kuongoza kiroho kwa njia ya Neno / Biblia (kulingana na karama na fursa tunazopewa), au kwa njia ya kuwasaidia ndugu zetu katika Kristo kwa kuwapa misaada kulingana na mahitaji yao (ambayo ni ya lazima kwa ajili ya kukua kwao kiroho, kufanya maendeleo ya kiroho, na kulitumikia Kanisa), kwa namna hizi zote za kimungu tunaiga mfano wa upendo wa Kristo, na ushuhuda huo wa “matendo mema” pia ni vigumu kwa ulimwengu wa wasioamini kutouona na kuupuuza. Tunapaswa kukumbuka, hata hivyo, kwamba kwa sababu ya kiburi, wivu, ushawishi wa kishetani / ki-pepo, matendo haya mema ya Kikristo yanaweza kuwa chanzo cha upinzani zaidi kutoka kwa ulimwengu wa wasioamini. Kama hali inakuwa hivyo, tunaweza kutiwa moyo na ukweli kwamba huku “kushiriki katika mateso ya Kristo” kwa upande wetu kutachangia zaidi katika Bwana wetu kuwa na furaha na sisi na kutuongezea thawabu yetu ya milele (War. 8:17; 2Wakor. 1:5; Wafi. 1:29-30; Wafi. 3:10; Wakol. 1:24; 2Tim. 2:12; 1Pet. 4:12-13; ling. na Matt. 10:38; Matt. 16:24; Mrk. :8:34; Mrk. 10:21; Mrk. 10:38-39; Lk. 9:23; Lk. 14:27; Matendo 5:41; 2Wakor. 4:10-11; Waga. 6:17; 1Wathess. 1:6; 2Wathess. 1:4-5; 2Tim. 3:12). Kama tutatenda yaliyo mema, tuna haki zote za kujiamini kwamba, mwisho wa yote, tutahalalishwa na kuthibitishwa na Bwana, na kwa hakika hili litatokea (Zab. 112:1-10).

6 Ataitokeza haki yako kama nuru, Na hukumu yako kama adhuhuri.
Zab. 37:6 SUV

42 Wanyofu wa moyo wataona na kufurahi, Na uovu wa kila namna utajifumba kinywa.
Zab. 107:42

Wasioutumia uhuru … kwa kusitiri ubaya (aya ya 16):

2.16  [mkiwa kama watu] walio huru, ila wasioutumia uhuru huo kwa kusitiri ubaya, bali kama watumwa wa Mungu.
1Pet. 2:16

Kama waumini katika Bwana Yesu Kristo, tumekombolewa kutokana na Sheria ya Musa kwa sadaka ya Yesu Kristo ambayo iliridhisha kikamilifu matakwa yote ya Sheria ile [ya Musa] kwa njia ya damu Yake, kifo Chake msalabani kwa ajili yetu (War. 4:16; War. 6:14; War. 7:4; War. 8:2; War. 10:4; Waga. 2:19; Waga. 3:13; Waga. 4:3-7; Waga. 5:4; Waga. 5:18; Waebr. 7:12; Waebr. 10:1).

5.1 Kristo alifanya kazi ya kutuweka huru ili sisi wenyewe tuuchague uhuru huo; kwa hiyo kaeni imara katika uhuru huu, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa (yaani Sheria).
Waga. 5:1

Uhuru huu ni neema adhimu kabisa, ukitupatia sisi waumini wa leo fursa ya kumtumikia Bwana Yesu Kristo kama (jinsi) Roho Mtakatifu anavyotusukuma kufanya hivyo, bila ya masharti / vizuizi vya Sheria kutukawilisha. Lakini uhuru, wakati unatupatia fursa, unapaswa kutumiwa kwa uangalifu, katika namna ya kimungu, iliyotakaswa na katika unyofu, kama ambavyo Paulo alivyoweka wazi:

5.13  Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili (hulka ya dhambi), bali tumikianeni kwa upendo.
Waga. 5:13

Tunaitwa na Bwana wetu ili kumtukuzwa Kristo, na siyo kufuatilia anasa zinazopendwa na miili yetu (Matt. 5:24); siyo kuzidekeza hulka zetu (kila mmoja wetu) za dhambi, bali kumsikiliza na kumfuata Roho badala ya mwili (Waga. 5:15-25). Uhuru wetu wa Kikristo, kwa hiyo, ni rasilimali iliyokusudiwa kutumiwa katika utumishi wetu kwa Bwana Yesu Kristo badala ya kujiendekeza kusiko na maana. Kama ambavyo Petro anaweka wazi katika aya hii, kuwa “mtumishi wa Kristo” na “kuutumia uhuru katika kusitiri ubaya” ni mambo mawili yanayotengana – na yote mawili yanaelekea katika sehemu mbili zinazopingana kwa nyuzi 180. Hivyo basi, badala ya kuyafuata matamanio yetu wenyewe, tukiutumia uhuru tulio nao kuzifurahisha nafsi zetu, ikiwa tutatafuta kumfurahisha Nahodha wetu Yesu Kristo, tunalazimika kuwa watumishi Wake halisi (Matt. 16:24; Mrk. 8:34; Lk. 9:23). Hiyo ndiyo njia ya kuipokea ile kauli ya “umefanya vyema” ambayo sote tunaitaka na kuisubiri kwa hamu kubwa (Matt. 25:21-23; Lk. 19:17); hii ndiyo njia ya kupokea thawabu tele kutoka Kwake.

6.9  Tena tusichoke katika kutenda [kazi njema ya Mungu]; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho (ikiwa hatutakata tama).
Waga. 6:9

Waheshimuni watu wote, wapendeni ndugu - yaani Wakristo wenzenu - (aya ya 17):

Waheshimuni watu wote, wapendeni ndugu (yaani Wakristo wenzenu), mcheni Mungu, mpeni heshima mfalme (yaani mtawala wa nchi mnamoishi).
1Pet. 2:17

Katika macho ya Mungu, kwa jinsi aya hii inavyofundisha, kila mwanadamu anastahili heshima zote za msingi. Sisi sote tumeumbwa katika mfano wa Mungu (Mwa. 1:26-27; ling. na 1Wakor. 11:7), na Bwana Yesu Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi za kila mwanadamu aliyeishi, anayeishi na atakayeishi hapa duniani (kw. mf. Yoh. 1:29; Yoh. 12:47; 2Wakor. 5:14-15; 2Wakor. 5:19; 1Tim. 2:4-6; Waebr. 2:9; Waebr. 7:27; 1Yoh. 2:2; 1Yoh. 3:5). Kwa kuwa Mungu anataka wote waokolewe (Eze. 18:23; Matt. 18:14; Yoh. 12:47; Matendo 17:27; 1Tim. 2:4; 2Pet. 3:9; ling. na Maombolezo 3:33), kitu kidogo kabisa ambacho waumini wanaweza kufanya ni kutoa hadhi na heshima kwa kila mwanadamu kwani wote hao ni wapendwa wa Mungu na waliumbwa na Kristo na kwa ajili yao Bwana Yesu alikufa.

6 Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu.
Mwa. 9:6

Heshima za msingi kama inavyoamriwa hapa juu (katika nukuu ya Mwa. 9:6), zinapatikana katika kutoingilia haki muhimu za wengine, haki ya kuishi ikiwa ni amri kuu na ya kwanza, na baada ya hapo zinafuata haki nyingine ambazo ni haki ya uhuru na haki ya kumiliki mali binafsi ambazo ni za lazimi ili kuishi (ambayo ndiyo lengo la amri ya 10 – kati ya zile amri 10 za Mungu) hii ni kusudi watu wote waweze kuwa na fursa ya kuitikia wito wa Mungu katika Bwana Yesu Kristo na kupata uzima wa milele ambao Bwana wetu alikufa ili sisi sote tuweze kuupata.

9 Bwana akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? 
Mwa. 4:9 SUV

Kama utaisoma aya hii hapa juu kwa umakini zaidi, utagundua kwamba heshima ya msingi kwa watu wengine hapa duniani inaonyeshwa siyo kwa kuwaingilia katika maisha yao (ambayo ni sawa na kuwa “mlinzi” wa ndugu yako), bali ni katika kutowanyima au kutoizuia haki yao ya kupata mahitaji muhimu ambayo Mungu amewapangia kwa muda [wao] ambao watakuwa wakiishi hapa duniani – katika matumaini kwamba watageuka Kwake na kuokolewa (soma Matendo 17:26-27). Hivyo basi, aya hii inayozungumzia heshima kwa watu wengine (na kuamuru hivyo) haihusiani na kutoa fadhila / hisani au kuwa “mtenda mema”; badala yake ni kuheshimu faragha ya watu wengine pamoja na haki zao za msingi kwa shabaha ya kuutunza uhuru wao wa kutenda wanavyotaka, na kuutunza uwezo wao wa kuchagua na kuamua – kama ambavyo tungependa wafanye hivyo hivyo kwetu sisi (yaani, hii ndiyo maana halisi ya ile inayoitwa “the golden rule”: Matt. 7:12).

Zaidi ya kujizuia kufanya kosa la kuingilia maisha ya watu wengine, taswira nyingine ya amri hii ya kuishi na wenzetu kwa heshima ni ulazima wa kujizuia kufanya upendeleo wa aina yoyote katika mtazamo na mwenendo wetu kwa wale tunaokutana na kuishi nao, na haswa kuhusiana na waumini wenzetu (Matendo 10:34; War. 2:11; Waefe. 6:9; Wakol. 3:25).

2.1  Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu.
Yak. 2:1

Katika mfano Wake wa yule masikini anayedharauliwa, na yule tajiri anayehudumiwa (Yak. 2:1-13), Yakobo anazungumzia kuhusu kuwapa heshima kuu na / au fadhila watu fulani kwa sababu tu ya hadhi yao katika maisha ya hapa duniani na kuwanyima heshima au kuwadharau wengine, haswa waumini wenzetu, kwa sababu tu hawana hadhi kama hiyo. Vivyo hivyo, Paulo anasema katika Warumi 12:16: “Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge” – NEN Bible. Kama ilivyo katika kadhia (case/jambo/suala) ya kuwaheshimu watu wote, na katika kadhia ya waumini wenzetu pia, jambo muhimu siyo kutafuta kushirikiana nao katika kila kitu, bali ni katika kuwakubali na kuwapokea wengine ambao hawana cheo kinachofanana na cha kwako, au hawana hadhi katika jamii inayofanana na ya kwako, au wanaoweza kuwa na kipato kidogo kuliko cha kwako, au wenye elimu na ustaarabu [unaoonekana] kuwa ni wa chini zaidi ya wa kwako, au kabila, au rangi tofauti, n.k., na kutowanyima zile huduma muhimu za kimungu ambazo Roho Mtakatifu ametuamini nazo [kila mmoja wetu] kwa sababu tu, kwa viwango vya kidunia, wenzetu hawa wanachukuliwa kuwa “hawastahili”.

5.14  Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako.
Waga. 5:14

“Majirani” maana yake ya kwanza kabisa ni waumini wenzetu / wengine (Waga. 5:13-14), na hapa ndipo kwenye tofauti kati ya amri ya “kuheshimu” na amri ya “kupenda” katika aya tunayoijadili (1Pet. 2:17). Wanadamu wote wanastahili heshima kutoka kwetu: tunataka wote waokolewe kama ambavyo Bwana wetu anavyotaka (na tuna shauku ya kuwapatia injili wale wote walio tayari kuipokea); lakini Wakristo wote wanastahili upendo kutoka kwetu: tunataka waumini hawa wote wakue kiroho, waendelee kupevuka kiroho na kuzaa matunda [ya kiroho] kwa faida yao binafsi, kwa ajili ya kukua kimaadili [ya Kikristo] kwa Kanisa la Bwana Yesu Kristo, na kwa ajili ya utukufu wa milele wa Bwana aliyekufa kwa ajili yetu. Bila shaka ni kwa sababu hii Petro analiweka tenzi-neno “heshima” katika wakati uliopita (aorist – katika Kiyunani), akionyesha kwamba ni uamuzi unaofanyika mara moja na hali hiyo haibadiliki, bali analiweka neno “upendo” katika taswira ya tendo linaloendelea (akionyesha kwamba hiki ni kitendo endelevu tunachopaswa kukifanya wakati wote). Kuwaheshimu watu wote inamaanisha kuwaacha wafanye maamuzi yao yanayotokana na utashi wao huru (tukishuhudia ukweli wa injili kwa matendo yetu na pia kwa maneno yetu kwa wale wenye shauku ya kuisikia: Matt. 7:6); kuwapenda ndugu zetu [katika Kristo] inamaanisha tunafanya kila kitu ili kuongeza nafasi na uwezekano wao wa kukua kiroho, kuendelea kupevuka, na kuzaa matunda, kwa kuzitumia karama tulizopewa na Roho Mtakatifu na kwa njia ya utumishi ambao Bwana wetu ametuita kuutimiza.

21.17 Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.
Yoh. 21:17

Mcheni Mungu, Mpeni Heshima Mfalme (yaani Mtawala wa Nchi Mnamoishi) (aya ya 17):

… mcheni Mungu, mpeni heshima mfalme (mtawala wa nchi mnamoishi)
1Petro 2:17b

Jozi hii ya amri inaenda sambamba na zile amri zilizotangulia (aya ya 17), lakini hapa mpangilio wake umekuwa kinyume (reverse order); hii inaitwa “chiastic” order, ambapo fundisho la kiroho linawekwa kwanza, na lile la kidunia likiwekwa katika nafasi ya pili. Mtindo huu wa mfuatano (sequency) una faida ya kuweka majukumu yetu ya kiroho kwa ndugu zetu katika Kristo pamoja na wajibu wetu kwa Mungu bega kwa bega (yaani ubavu kwa ubavu – side by side), na wakati huo huo ukiyaweka majukumu hayo pamoja na amri ambazo zinaainisha wajibu wetu katika kadhia za dunia hii, kwa watu wasioamini [wanaoishi hapa duniani] ambao tunakutana nao, na mamlaka zinazotawala ulimwenguni tunamoishi kwa sasa. Watu wengi wanaishia katika kuwaona watu wasioamini na mamlaka za nchi wanamoishi katika uwingi wao [na hawaendi mbele na kuona zaidi ya hapo]; lakini sisi tulio watu wa Bwana Yesu Kristo tunaelewa vyema kabisa kwamba ni katika ile jozi ya uwajibikaji (1Petro 2:17b) isiiyoonekana kwa urahisi lakini yenye thamani kubwa zaidi - kwa kiasi kisicho na mfano – ya kiroho ambamo kuna utukufu mkuu: kuwapenda ndugu zetu [katika Kristo] na kumtukuza Bwana wetu ndiyo malengo yetu halisi ya kiroho hapa duniani, na ndiyo sababu pekee ya sisi kuwapo hapa duniani ingawa ulimwengu una mawazo tofauti na haya.

10 Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima, Wote wafanyao hayo wana akili njema, sifa Zake zakaa milele.
Zab. 111:10 SUV

10 Kumcha Bwana ni mwanzo wa hekima; Na kumjua [Yeye aliye] Mtakatifu ni ufahamu.
Mithali 9:10

Upendo hutupatia motisha chanya: tunatiwa moyo kufanya yaliyo mema kutokana na shauku inayotoka moyoni kabisa ya kuwasaidia ndugu zetu; lakini woga / ucha Mungu unatutia motisha pia: tuko tayari kupatwa na jambo lolote [linalouma] kuliko kumuudhi Bwana wetu (na hivyo kumfanya aone ulazima wa kutupa adibisho Lake la upendo – japo linauma: Waebr. 12:5-13). Katika neema Zake kuu, Mungu wetu anatupatia vitu vyote viwili – shauku ya kuwapenda ndugu zetu na shauku ya kumpenda Yeye – ili tuendelee kutembea katika ile njia iliyonyooka inayoenda Sayuni (Zab. 84:5-7), bila ya kugeuka kulia au kushoto. Na ikiwa tunajipa motisha sahihi kwa kuwa na mtazamo wa upendo kwa Wakristo wenzetu kwa upande mmoja (unaodhihirika katika kuwapatia huduma za kiroho), na kumcha Mungu [kwa usahihi] kwa upande mwingine (kuenenda katika njia ya utakaso na kutenda yale anayotaka katika kukua kiroho, kuendelea na mchakato wa kupevuka kiroho na kuzaa matunda mema), basi kutimiza zile amri mbili za kuwaheshimu watu wote (ikiwa ni pamoja na wasioamini) na kumheshimu mfalme (neno “mfalme” likiwakilisha mamlaka yote halali nchini) kutatimizwa bila tatizo, na wakati huohuo tukielekeza fikra na nguvu zetu katika yale yaliyo muhimu kwa Mwokozi wetu.

5.14  Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako.
Waga. 5:14 SUV (linganisha na Matt. 22:36-40; War. 13:8-10)

Zinapochukuliwa kwa pamoja katika muktadha wa 1Pet. 2:17 amri hizi nne zinajumuisha wajibu wetu wote kama Wakristo katika ulimwengu huu … na kwa Bwana wetu, na kwa Mwili Wake, yaani Kanisa.

5.9  Kwa hiyo, tena, ikiwa tupo [katika miili ya] hapa [duniani], au ikiwa hatupo [katika miili hiyo], twajitahidi kumpendeza yeye.
5.10  Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri ya alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya [yasiyo na thamani].
5.11  Basi tukiijua hofu ya Bwana [katika matarajio ya hukumu hii], twawavuta wanadamu [ili waende mwendo sahii]; lakini tumedhihirishwa mbele za Mungu [jinsi mioyo yetu ilivyo]. Nami natumaini ya kuwa tumedhihirishwa katika dhamiri zenu pia.
2Wakor. 5:9-11

Enyi Watumishi, Watiini Bwana zenu kwa Heshima Zote (aya ya 18):

Enyi watumishi, watiini bwana zenu kwa heshima zote … 1Pet. 2:18a

Neno “mtumishi” hapa, katika Kiyunani ni oiketes, linamaanisha “mwanakaya”, na hiki ni kisawe (synonym) cha neno “mtumwa”, kwani katika ulimwengu [wa kale] wa Kiyunani na Kirumi katika karne ya kwanza, kaya kubwa – na wakati mwingine kaya hizi zilikuwa kubwa sana – zilijumuisha siyo tu wanafamilia, bali watumwa pia.

16.30 kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka?
16.31 Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na wanakaya wako.
16.32 Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake.
Matendo 16:30-32

Wasifu huu wa uinjilisti wa Paulo na Sila kwa Yule askari wa gereza la Filipi na wanakaya wake waweza kuonekana kama wa ajabu kidogo kwa watu wa karne hii ya sasa, lakini kwa kweli hata watu wa familia za kisasa huenenda hivi hivi: kaya (household) ilikuwa, na hata sasa ndiyo / ni, kikundi cha msingi cha jamii nzima (ling. na kuanzia nyumba 10 hadi kitongoji, kijiji, na kuendelea mpaka nchi nzima), na kikundi hiki cha msingi kilikuwa na tabia ya kufanya kazi kama ushirika mmoja, ukifuata maelekezo ya kiongozi wa kaya hiyo (ling. na Yer. 35:2-19). Hivyo si jambo la kushangaza kwamba kaya nzima ya yule askari gereza walimgeukia Mungu na kuokolewa kutokana na mahubiri ya mitume wale wawili, na hivyo tunaweza kuwa na matumaini kwamba wanakaya wa kaya nyingi za Kiyunani na Kirumi za wakati ule waliokolewa, au karibu wote. Kwa vyovyote vile, wengi kati ya waumini hawa wapya walikuwa watumwa, na tukio la kuokolewa kwao na kuwa wafuasi wa Kristo halikumaanisha kwamba waliacha / walikoma kuwa watumwa katika kaya hizo. [Hali ya] utumwa ni hali mbaya sana, lakini katika historia ya dunia hii ni katika karne za hivi karibuni tu ndiyo desturi hii ya kutisha imeanza kukomeshwa. Injili inaahidi ukombozi kutokana na kifo kwa wote, lakini haitoi ahadi ya kukombolewa kutoka katika madhila mengine ya dunia hii. Tunapookolewa (kwa kuamini ujumbe wa Injili), hatuponywi magonjwa yetu, na wala hatuwekwi huru kutokana na madeni [ya pesa] ambayo yawezekana kuwa tunayo. Tunapookolewa, hatuwekwi huru kutokana na majukumu yetu ya ndoa (ling. na 1Wakor. 7:12-16), na wala hatugombolewi kutoka katika utumwa ikiwa tulikuwa watumwa katika kaya fulani kabla ya kupewa wokovu ule mkuu utokao kwa Mungu. Katika hali hii, ilikuwa muhimu kwa Petro, akiwa katika hali ya kujazwa na Roho Mtakatifu, kutamka kwa dhati juu ya wajibu wa waumini wapya ambao walikuwa chini ya nira ya utumwa kuvumilia katika hali hiyo na kuonyesha heshima kubwa kwa mabwana zao na kuzipenda kazi zao walizopewa [ikiwezekana] zaidi hata ya hapo kabla. Kwa waumini, mabadiliko halisi katika hadhi zetu ambayo tunayapokea wakati ule tunapookolewa ni ya mbinguni, na si ya kidunia.

7.21  Je! Uliitwa ungali mtumwa [katika kaya fulani]? Usione ni vibaya lakini kama ukiweza kuwa na uhuru, afadhali uitumie fursa hiyo, ukawa huru.
7.22  Kwa maana yeye aliyeitwa katika Bwana [angali katika] hali ya utumwa, ni huru wa Bwana. Vivyo hivyo yeye naye aliyeitwa [angali katika] hali ya uhuru, ni mtumwa wa Kristo.
1Wakor. 21-22

Katika ulimwengu wa sasa, mfumo / desturi ya utumwa bado ipo (ingawa katika maeneo mengi imetangazwa kufanywa kuwa ni desturi iliyo kinyume na sheria ya nchi, na matokeo yake ni kwamba desturi hii imekuwa ikifanyika kwa kificho). Lakini kwa maana fulani sisi sote ambao tunalazimika kufanya kazi ya ajira ili tuweze kuishi ni “watumwa” wa malipo tunayopata ili tuweze kutunza afya zetu, nyumba zetu na familia zetu. Kama inavyosema methali moja katika Uyunani ya kale, masikini ni Yule anayelazimika afanye kazi ili aishi; fukara ni Yule anayelazimika kufanya kazi kwa mtu mwingine ili aishi. Na hii ndiyo hali ambayo wengi wetu tuko nayo. Kwa sababu hii, mwongozo unaotolewa katika Agano Jipya kuhusu mwenendo sahihi ambao watumwa walio Wakristo wanapaswa kuwa nao unafaa kufuatwa na wengi kati yetu ambao tuna waajiri: waajiri hawa, tukiongea ki-biblia, ni mabwana zetu –yaani sisi ni watumwa wao.

6.5  Enyi [mlio] watumwa, watiini wao walio bwana zenu kwa jinsi ya mwili, kwa hofu na kutetemeka, kwa unyofu wa moyo, kana kwamba ni mnamtii Kristo;
6.6  wala si kwa utumwa wa macho tu kama wajipendekezao kwa wanadamu bali kama watumwa wa Kristo, mkitenda yampendezayo Mungu kutoka moyoni;
6.7  kwa nia njema kama kumtumikia Bwana wala si mwanadamu;
6.8  mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapewa [thawabu kwa hilo] na Bwana, awe ni mtumwa au ni mtu huru.
Waefe. 6:5-8

3.22  Ninyi watumwa, watiini hao ambao kwa mwili ni bwana zenu, katika mambo yote, si kwa utumwa wa macho, kama wajipendekezao kwa wanadamu, bali kwa unyofu wa moyo, mkimcha Bwana.
3.23  Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu,
3.24  mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo.
3.25  Maana adhulumuye atapata mapato ya udhalimu wake, wala hakuna upendeleo.
Wakol. 3:22-25

6.1  Wo wote walio chini ya kongwa, hali ya utumwa, na wawahesabie bwana zao kuwa wamestahili heshima yote, jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yetu [ambayo yanatoka Kwake].
6.2  Na wale walio na bwana waaminio wasiwadharau kwa kuwa ni ndugu; bali afadhali wawatumikie, kwa sababu hao waishirikio faida ya kazi yao wamekuwa wenye imani na kupendwa. Mambo hayo uyafundishe na kuyasisitiza.
1Tim. 6:1-2

Kwa hakika, kati ya “watumwa” wa leo na wale wa kale kuna tofauti kubwa sana. Sisi wa leo tuko huru kuacha kazi moja na kuajiriwa mahala pengine, kama tunapata fursa hiyo, lakini kama ambavyo wengi kati yetu tumeona katika nyakati mbalimbali katika ajira zetu, kupata kazi nzuri na kudumu katika ajira hiyo – au kupata ajira bora zaidi – si rahisi [wakati wote]. Kwa vyovyote vile, wakati tukiwa katika ajira hizi, tunawajibika kufanya kazi kwa uaminifu na heshima, kama inavyostahili kwa sisi ambao Bwana wetu halisi ni Yesu Kristo, tukitumikia katika namna ambayo inamtukuza Yeye (na ambayo haitaleta lawama katika lile Jina tukufu ambalo kwalo tumebarikiwa kuitwa).

Sio tu wao walio wema na wapole, bali na wao walio wakali [na waonevu] (aya ya 18):

… sio tu wao walio wema na wapole, bali na wao walio wakali [na waonevu].
1Pet. 2:18b

Hii ni tahadhari nzuri na muhimu. Ni rahisi kwetu kudhani kwamba uonevu / kukosa haki katika maeneo yetu ya kazi kunatupa kisingizio cha kukwepa kufanya kazi kwa ufanisi na heshima. Biblia inatufundisha msimamo huu. Tunawajibika kwa Bwana Yesu Kristo, kufanya kazi ambayo kwayo tunalipwa ujira, kwa ufanisi na heshima hata kama hatuonyeshwi shukrani kwa kazi na mwenendo wetu – na hata kama tunaonewa / tunanyimwa haki katika sehemu zetu za ajira. Katika Kiyunani, kivumishi (adjective) kinachotafsiriwa kama “uonevu (kunyimwa haki - unfair)” hapo juu ni skolios, neno ambalo tafsiri yake sisisi ni “killichopinda, kisichonyooka” (linganisha na neno “scoliosis”), na linaonyesha hali ya kuwa kinyume na “wema”, na neno la Kiyunani linalomaanisha “wema” hapa ni agathos likionyesha siyo tu wema katika tabia na mwenendo, bali pia likionyesha “ufanisi katika kazi”, na pia ni kinyume cha “utayari wa kusikiliza hoja tofauti”, ambalo ni neno la Kiyunani epieikes, mara nyingi likimaanisha “-enye huruma”: hata kama wakuu wetu katika sehemu zetu za kazi hawako bora katika ufanisi wao wa kazi na wanatutendea kiholela na hivyo kutotundendea haki, hii haitupi sababu ya kutofanya kazi zetu kwa ufanisi na heshima kwani kiuhalisia sisi tunafanya kazi kwa ajili ya Bwana wetu (Wakolosai 3:24; ling. na Waefeso 6:7). Wakati tukizingatia ukweli huu, tunapaswa wakati wote kufanya kazi zetu “kama kwa [ajili ya] Bwana”, hata katika wakati ambao jambo hili ni gumu kwa sababu ya shida / magumu tunayopata kutokana na mwenendo wao huo. Katika nchi huru (au nchi yenye kiasi kikubwa cha uhuru), na ya kisasa ambamo utumwa umekomeshwa (au angalau umetangazwa kuwa ni kinyume cha sheria), tunayo haki ya kutafuta ajira nyingine kama hatuwezi au hatutaki kuvumilia manyanyaso katika mahala pa ajira yetu ya sasa. Kitu ambacho hatuna haki ya kufanya ni kuporomoka katika maadili ya Kikristo hata kufikia kuanza kurudisha visasi dhidi ya mabosi au/na waajiri wetu au waajiriwa wenzetu, au kusahau kwamba mwenendo wetu ni ushuhuda wa Bwana na Mwokozi wetu mpendwa Yesu Kristo. Watu wengi katika nchi mbalimbali wamefanya kazi chini ya mabosi au wasimamizi wabovu. Tunachotakiwa kukumbuka wakati wote, na haswa kama tunateseka chini ya bosi wa aina hii ni kwamba Bwana Yesu Kristo ndiye “bosi” wetu halisi, Naye ndiye tunayejitahidi kumfurahisha wakati wote.

Nanyi mabwana, watendeeni watumwa wenu kwa jinsi iyo hiyo. Msiwatishe, kwa kuwa mnajua ya kwamba yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, naye hana upendeleo.
Waefe. 6:9 NEN Biblia

NB.: Inaweza kuwa jambo bora kusoma aya hii katika muktadha wake, yaani kusoma mistari iliyo juu na chini yake, inayozungumzia somo hili lote ili kuipata maana halisi ya somo zima. Kwa hakika ni jambo bora kusoma mistari ya Biblia kwa desturi hii ili kupata maana nzima ya somo linalozungumziwa.
R. L. Kilambo.

Ni muhimu kueleza hapa kwamba waajiri pamoja na watu wote wenye mamlaka ya usimamizi, kama aya iliyonukuliwa hapo juu inavyodhihirisha, wanawajibika kwa Bwana kufanya kazi na wote walio chini yao katika namna njema na weledi wa hali ya juu unaotarajiwa kutoka kwa Wakristo wote katika sehemu yao ya kazi. Watu wasioamini yawezekana wakaendesha maisha yao katika kiwango hiki au la, lakini sisi tunajua kutokana na uzoefu wa maisha yetu kwamba wengi hawafanyi hivyo. Mjadala wa Petro katika aya zinazofuata ile aya ya 18 unatuongoza katika suala hili, lakini sisi pia tunapaswa kuweka wazi kwamba tunapozungumzia mwenendo mbaya dhidi yetu hatumaanishi kitu chochote ambacho kinavuka msitari wa kile ambacho kinakubalika kisheria na kimaadili. Waumini wana haki ya kufanya kile ambacho kinaruhusiwa na kanuni na sheria za kampuni au shirika wanamofanya kazi katika kupambana na mwenedno dhidi yao ambao unavunja kanuni na/au sheria hizo. Na kama mwenendo huo unavuka msitari na kuingia katika uvunjifu wa sheria au hata uhalifu, hakuna kitu hapa katika yale tunayoelekezwa na Petro [akiwa katika kujazwa na Roho Mtakatifu] kinachombana muumini asitafute ushauri na mwongozo wa sheria kwa upande mmoja au kufungua mashtaka dhidi ya mhusika kwa upande mwingine. Hata Sheria ya Musa inazungumzia aina hii ya tukio.

26 Mtu akimpiga mtumwa wake jicho, au jicho la kijakazi chake, na kuliharibu; atamwacha huru kwa ajili ya jicho lake.
27 Au akimpiga mtumwa wake jino likang'oka, au jino la kijakazi chake, atamwacha huru kwa ajili ya jino lake.
Kutoka 21:26-27 SUV

Vumilia mateso yanayotokana na uonevu (aya ya 19 -20):

2.19  Kwa maana ni jambo la sifa [mbele ya Mungu] kama mtu akivumilia [ili awe na dhamiri safi] anapoteswa kwa uonevu kwa ajili Yake.
2.20  Kwa maana mna sifa gani mkistahimili adhabu kwa sababu ya kutenda dhambi? Lakini kustahimili [mateso] mtendapo mema, huu ndio wema hasa mbele za Mungu.
1Pet. 2:19-20

Kufahamu kwamba uvumilivu wa mateso yasiyo ya haki unamfurahisha Bwana wetu Yesu Kristo kunapaswa kutupatia motisha ya nguvu ya sisi kutenda yaliyo haki na sahihi na mema katika maendeleo yetu ya kazi bila kujali mazingira yaliyopo katika maeneo hayo. Kwa hakika, ikiwa tunajikuta katika mazingira na hali ambamo tunanyanyaswa, kuteswa, n.k., iwe kwa kiasi kikubwa au kidogo, basi ni jambo muhimu sana kuikumbuka aya hii – kweli hii tuliyopewa na Roho Mtakatifu na kuifanya mwongozo wetu ulio imara. Kwani ni katika nyakati hizi, tunapohisi kwamba tunanyanyaswa, au, muhimu zaidi, tunapojua kwa uhakika kwamba tunachotendewa ni unyanyasaji, ndipo sisi, wanadamu tulio dhaifu, tunakuwa na uwezekano wa kuwakasirikia wale wanaotutesa (na hapo kuenenda katika namna zisizo za kimungu), au kushikwa na majonzi, mfadhaiko kupita kiasi (na hivyo kushindwa kufanya aina ya kazi tunayotakiwa kuifanya), au hata kumkasirikia Mungu (kama vile ni kosa Lake!), na hili ni kosa la kawaida ambalo hata waumini waliopevuka wana uwezekano wa kulifanya pale wanaposhambuliwa kwa ghafla / kwa mshitukizo (ambush) na pepo.

Kosa la kwanza hapo juu (kuwakasirikia wanaotutesa) linaweza kupewa jina la “kosa la Musa”. Alipokerwa na kizazi kipya cha wana wa Israeli katika namna ile ile ambayo baba zao walimkera, Musa alighadhibishwa na akakaidi maelekezo ya Mungu yaliyotolewa kwa utaratibu na utondoti mkubwa (Hes. 20:1-3). Kama mtu mkuu katika imani kadiri ya Musa anaweza kufanya kosa kama hili licha ya kwamba alifanya kazi chini ya “Bosi” mtimilifu kabisa – Bwana Yesu Mwenyewe - basi nasi tunaweza kusamehewa tunapokasirika pale bosi zetu wa hapa duniani wanapodhihirisha siyo tu kutokuwa na utimilifu, bali wanapotufanyia mateso yanayodhihirika kuwa ni ya uonevu. Katika nyakati kama hizi, tunapaswa kukumbuka ni Nani haswa ndiye Bosi wetu halisi, yaani Bwana Yesu Kristo, na kwamba sisi ni balozi Wake kwa watu wote anaoututuma kwao, aghalabu watu hao wakiwa ni wale wote tunaofanya nao kazi pamoja katika sehemu zetu za ajira.
Namna “tunavyojibu” aina hii ya mashambulizi ya Shetani itaonekana na wote wanaotuzunguka. Kama tutaendelea kuonyesha msimamo huu wa kimungu licha ya shinikizo la aina hii, kutokasirika dhidi ya watesi wetu bali kuendelea kufanya kazi zetu “kama vile tunamfanyia Mungu”, hili litaonekana na wafanyakazi wenzetu na mwisho wake hata wasimamizi wetu. Na Bwana wetu Yesu Kristo atafurahishwa nasi.

Kosa la pili hapo juu tunaweza kuliita “kosa la Eliya”. Baada ya mmoja kati ya ushindi mkubwa kabisa wa kiroho katika kumbukumbu za Biblia, Eliya akajisahau na hivyo akashitukizwa na shambulizi la ghafla la vitisho vya Yezebeli juu ya uhai wake na akakimbia kwa hofu, akautelekeza wajibu aliopewa kama nabii wa Mungu (1Wafalme 19:1-18). Kama muumini mkuu kama Eliya aliweza kufanya kitu cha namna hii ingawa alipaswa kujua kwamba “Bosi” wake halisi asingeweza kuacha kitu chochote kibaya kimtokee (kama ambavyo “Bosi” wake huyu alivyodhihirisha hapo baadaye: soma 1Wafalme 1:10-12), sisi leo hii tunaweza kusamehewa kwa kushikwa na hisia za mfadhaiko na kushawishika kukata tama ikiwa, na wakati, tunajikuta tukilengwa na unyanyasaji mkali katika maeneo yetu ya kazi. Katika nyakati kama hizi tunapaswa kukumbuka kwamba Yeye ambaye ndiye mwajiri wetu halisi ameshika kila kitu katika mikono Yake – ikiwa ni pamoja na uhai wetu na uhai wa wale wanaotutesa. Kama ni mapenzi Yake kuwa sisi tupitie mateso hayo, basi bila ya shaka kuna sababu nzuri kabisa, ijapokuwa hatuwezi (na huenda hatuna uwezo) kuziona sababu hizi kwa wakati huo (kama ilivyokuwa kwa Ayubu). Hivyo basi, badala ya kufa moyo wakati matatizo kama haya yanatukumba, tunahitaji kujipa moyo katika Bwana, tukijikumbusha kwamba Yeye yuko pamoja nasi, na kwamba atatuvusha katika bahari hii ya mateso bila ya sisi kuguswa hata na tone moja [la maji], kama tu tutausubiri wokovu Wake katika namna ya kimungu, tukiendelea kuenenda katika namna inayoonyesha heshima Kwake licha ya manyanyaso yote tunayopitia.

Kosa la tatu hapo juu tunaweza kulipa jina la “kosa la Yona”. Tunajua kutokana na hasira alizozionyesha baadaye kwamba sababu yake ya kukimbilia Tarshishi ilikuwa ni kwamba aliona kuwa Mungu “alikosea” pale Alipotaka kuwapelekea wokovu maadui wakubwa wa Israeli ambao walikuwa ni Siria (Yona 4:1-4). Ni jambo linalotokea wakati fulani kwamba watu kwa ujumla, na hata walio waumini wakati mwingine, humlaumu Mungu badala ya kuamini kwamba Yeye atatuokoa wakati wa shida. Matukio magumu au mabaya ambayo mtu anayaogopa au anayachukia yanapomtokea, swali la kawaida lisilostahili kuulizwa ambalo kwa kweli ni swali la ki-ovu ni: “Mungu aliachaje jambo hili litokee?” Kwa kweli, kuchukua hatua hii isiyofaa ya kukosa imani kwa Mungu na kuonyesha ukosefu wa heshima kwa hulka Yake timilifu ni sababu mojawapo ya uasi kwa Mungu, yaani kutelekeza imani kabisa kwa Kristo (Matt. 13:21; Marko 4:17; Lika 8:13). Wakati makosa yale mawili ya mwanzo yanaweza ‘kueleweka’ ijapokuwa yanasikitisha na ni ya kujutia sana, hakuna kisingizio cha aina yoyote cha kutuwezesha kumlaumu Mungu. Hili ni kosa la kimsingi kabisa katika kusoma maana ya kila tukio lililotokea au litakalotokea katika ulimwengu huu, mtazamo wa ki-shetani ambao uko mbali kabisa na ule wa kimungu, ni kushindwa kabisa kuelewa misingi ya kwanza kabisa ya kweli: kwamba Mungu anatupenda na amefanya na anaendelea kufanya kila kitu kwa faida yetu sisi waumini ambao tumesafishwa na damu ya Kristo, akifanyia kazi mambo yote kwa ajili ya mema yetu (Warumi 8:28). Kwani kama ambavyo Petro atatukumbusha katika aya zinazofuata, Mungu Baba alimtoa Mwana wake mpendwa ili atuokoe na atuepushe na ziwa la moto, na Yesu Bwana wetu alikufa katika giza pale msalabani pale Kalvari ili alipie gharama ya moto kwa ajili ya kila mmoja wetu. Huu ni upendo – na kumlaumu Yeye ambaye anatutakia mema tu ni kusahau wokovu wetu mkuu … na kuurusha usoni Mwake.

Kushindwa katika maeneo yote haya matatu katika historia ya waumini hakukutukia bila matokeo ya maumivu kwa waumini hao watatu. Lakini katika matukio yote haya matatu, wanaume hawa wakuu wa Mungu walipewa nafasi / fursa ya pili ya kurekebisha makosa yao, Yona alipewa nafasi ya pili kwa kuokolewa kutoka baharini kimuujiza na baadaye aliwafanyia uinjilisti na kuwaongoza Wasiriya wengi kwenye wokovu; Musa na Eliya watapata nafasi / fursa yao ya pili katika siku za usoni za vipindi vya Dhiki na Dhiki Kuu (kila kipindi kimoja ni miaka 3.5, vikifanya kipindi kizima cha miaka 7) watakaporudishiwa uhai wao wa kibinadamu na kuletwa katika ardhi ya Israeli ambapo watasimamia na kuongoza uhuisho wa imani ya wana wa Israeli, nao wengi wao watamrudia / watamwamini Kristo kabla ya, na wakati wa unyakuo / ujio wa pili wa Kristo. Hata hivyo, ni nani ambaye hawezi kuona kwamba ingelikuwa bora zaidi kama ndugu zetu hawa watatu wasingefanya makosa yale na badala yake kumtegemea Mungu wakati wa adha yao? Mfano mzuri wa fundisho hili unapatikana katika 1Sam. 30:1-20; soma mahususi ile aya ya 6 ya sura hii ya 30. Hivyo, wakati tunaifurahia ile huruma na msamaha mkuu wa Mungu, na tunajiamini kwamba Atatusamehe na kutuokoa ikiwa tumedhamiria kuendelea kuwa watoto Wake, Yeye “anafurahi” pale ambapo badala ya kukasirika, kufadhaika, au kumlaumu Yeye, sisi tunasimama imara chini ya shinikizo na kufanya yale aliyotupangia kufanya: kuendelea kufanya kazi nzuri itakayomletea heshima kwa sababu sisi ndio tunayemwakilisha Yeye. Kama tunateseka kwa “kufanya yaliyo sahihi” na si kwa sababu tuna-react visivyo sahihi pale “tunapotendewa vibaya”, hapo tunamtukuza Mwokozi wetu mpendwa kwa kufanya hivyo na matokeo yake ni kwamba Yeye anafurahi.

Tutakuwa tunafanya ajizi ikiwa hatutaeleza hapa kwamba kuvumilia manyanyaso katika sehemu zetu za kazi si kitu kile kile kama kuvumilia adhabu, maonyo, kushushwa cheo, kupunguzwa mshahara, n.k., kunakotolewa dhidi ya Mkristo kwa uvunjaji wa sheria. Ndiyo maana Petro anauliza swali linalochoma mpaka moyoni: “mna sifa gani kustahimili adhabu kwa sababu ya kutenda dhambi?” Kama tumekuwa wavivu au wazembe au kwa namna yoyote ile tumeshindwa kutekeleza au kutimiza wajibu kazini kama ambavyo mwajiri wetu anatarajia, basi matokeo ya mwenendo mbovu kama huo kazini kwetu hayafanani kabisa na “mateso tusiyostahili” ambayo Petro anayaelezea katika sehemu hii. Kwa hakika, adhabu hiyo ni matokeo ya haki ya mwenendo wa kipuuzi kama huo kuhusiana na majukumu yetu – kwa Bwana wetu na pia kwa waajiri wetu.

Lakini kama hatuna hatia ya kutokuwa makini, na hata hivyo kupata mateso (jambo linalowezekana kabisa kama inavyoelezwa hapa, na linalotutokea wengi wetu kama siyo karibu sisi wote), basi tunaweza kutiwa moyo katika kufahamu kwamba tunaenenda “ili tuwe na dhamiri safi tunapoteswa kwa uonevu kwa ajili ya Mungu” (aya ya 19), na kwamba mwenendo wetu huu dhidi ya mateso tusiyostahili ambayo tunayavumilia una matokeo ya “kumfurahisha Mungu”. Kwani sababu pekee inayotufanya tuendelee kubaki hapa hapa ulimwenguni baada ya wokovu ndiyo hii, kwamba tumfurahishe Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo kwa kufanya mapenzi Yake.

Tumekwishajadili kwamba ni halali kwa Mkristo kuchukua hatua pale tunapotendewa visivyo kazini, iwe kwa njia ya malalamiko ndani ya shirika au kampuni au katika vyombo vya sheria vya kiserikali ikiwa tutaona mateso tunayopitia yanastahili hatua hiyo. Lakini hatutaonekana waoga mbele za Mungu na Wakristo wenzetu ikiwa tutateseka bila malalamiko wakati tumetimiza wajibu wetu kazini kwa ajili ya Kristo. Kwa hakika, kuvumilia ni kitendo cha ujasiri zaidi kuliko kulipiza kisasi au kulalamika kwa namna moja au nyingine.

Mwisho, aina mojawapo ya unyanyasaji, ingawa ni unyanyasaji baridi, ni kushindwa kwa uongozi wa makampuni na mashirika kutoa sifa stahiki kwa wale ambao ndio wanafanya kazi kwa bidii, wakilifaidisha shirika au kampuni kwa kiasi kikubwa na hata kuokoa jahazi katika nyakati za shida, lakini [viongozi hao] wanatoa thawabu na kuwapa heshima watu wengine ambao mchango wao (kama upo!) si mkubwa kiasi hicho (na wakati mwingine huleta matatizo tu!). Kama jambo hili ni matokeo ya upendeleo, kutokuwa na sifa za uongozi, au kupitiwa tu, sisi Wakristo tunahitaji kukumbuka wakati wote kwamba sifa pekee zenye umuhimu ni zile zinazoenda kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwamba mwenendo wetu unapomfurahisha Yeye, basi thawabu yetu kutoka Kwake ina thamani kubwa kuliko sifa zote [tunazoweza kupewa] hapa duniani.

2.19  Kwa maana ni jambo la sifa [mbele ya Mungu] kama mtu akivumilia [ili awe na dhamiri safi] anapoteswa kwa uonevu kwa ajili Yake.
2.20  Kwa maana mna sifa gani mkistahimili adhabu kwa sababu ya kutenda dhambi? Lakini kustahimili [mateso] mtendapo mema, huu ndio wema hasa mbele za Mungu.
1Peter 2:19-20

Mliitwa kwa Makusudi haya (aya ya 21):

2.21  Ninyi mliitwa kwa makusudi haya, kwa sababu Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akiwaachia kielelezo/mfano, ili mfuate nyayo zake.
2.22  “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake” (Isa 53:9b).
2.23  Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya (hakumtishia mtu); bali alijikabidhi (alimtumaini) kwake Yeye ahukumuye kwa haki.
1Peter 2:21-23

Kuteseka kwa niaba ya Bwana Yesu Kristo si jambo linalotokea “kama ajali” lakini, kama vile aya ya 21 inavyotamka, hii ni sehemu muhimu sana ya Ukristo wetu: “ninyi mliitwa kwa makusudi haya”.

5.11 Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu.
5.12 Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.
Matt. 5:11-12 SUV

1.29  Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake;
Wafi. 1:29 SUV

3.12  Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa.
2Tim. 3:12 SUV

4.14  Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia.
1Pet. 4:14 SUV

Wito huu wa “kupitia mateso” hapa ulimwenguni tumepewa sisi kwa sababu ya ushuhuda ambao uvumilivu wetu imara unadhihirisha kwa wengine, ukithibitisha kwao 1) nguvu ya kweli ambayo inatufanya tuweze kuhimili wakati tukipitia mateso hayo, 2) uaminifu wa Mungu katika kutuvusha salama katikati ya mateso hayo, 3) upendeleo wetu wa kupata kibali cha Mungu badala ya kupata ahueni ya muda mfupi au faida ya muda tu katika dunia hii. Tunatarajia ufalme ambao “si wa dunia hii” (Yoh. 18:36), tunautafuta “mji ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu” (Waebr. 11:10), thawabu ambayo ni kuu kuliko “hazina zote za Misri” (Waebr. 11:26), na ufufuo ambao ni “bora” zaidi ya faida za hapa duniani na ahueni ya maisha haya (Waebr. 11:35). Tunapovumilia mateso ya aina yoyote katika namna ambayo ni ya kimungu, kuonewa na kunyimwa haki kazini kukiwa ni aina mojawapo ya mateso hayo, tunaonyesha kwamba Bwana Yesu Kristo na maoni Yake juu yetu ni suala lenye umuhimu kwetu kuliko kitu chochote katika maisha yetu, na kwamba sisi hatuko tayari kubadilisha thawabu yetu ya mbinguni kwa ajili ya kuupata “mchuzi mwekundu wa dengu” kama ambavyo Esau ambaye hakumcha Mungu alifanya (Waebr. 12:16). Mwenendo wetu huu katika kutojali matamanio ya kimwili na yale ya kidunia unadhihirisha kwa uwazi zaidi kuliko maneno tu, uthabiti na uhalisia wa imani yetu, na hivyo unakuwa, kwa wote wanaoutazama mfano wetu, ushuhuda wenye nguvu na unaoonekana, wa Mungu tunayemtumikia ambaye haonekani lakini aliye mwaminifu siku na wakati wote.

1.27  Lakini mwenendo wenu na uwe kama inavyoipasa Injili ya Kristo, ili, nikija na kuwaona ninyi, au nisipokuwapo (nisipokuja), niyasikie mambo yenu, kama mnasimama imara katika roho moja, kwa moyo mmoja mkiishindania imani ya Injili;
1.28  wala hamwaogopi adui zenu, katika neno lo lote; kwao hao ni ishara mathubuti ya kupotea, bali kwenu ninyi ni ishara ya wokovu, huo utokao kwa Mungu.
Wafi. 1:27-28

Mfano adhimu unaofaa kuigwa wa jinsi tunavyotakiwa kujistahi pindi tunapokuwa chini ya matendo yasiyo ya haki si mwingine bali ni ule wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo na mateso aliyoyavumilia ili aweze kufika msalabani. Kwa kuwa Alikufa kwa ajili yetu – na akatugomboa kwa damu Yake (sadaka Yake kwa ajili ya dhambi zetu) – tunachoweza kufanya kwa upande wetu ni kufuata mfano Wake aliotuachia, kama yalivyo mapenzi Yake. Na kwa kuwa sasa sisi ni watu Wake, ni jambo la wazi kwamba yule mwovu na mfumo wa ulimwengu aliouasisi watatuchukia na kutuwekea upinzani kwa kadiri wanavyoweza.

15.18 Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.
15.19 Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua [kutoka] katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia.
15.20 Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu.
Yoh. 15:18-20 SUV

Tunaongeza kwa haraka kabisa hapa kwamba hakuna mateso yoyote ambayo tunaweza kuitwa kuyastahamili yanayoweza kufanana kwa kiwango na hata sehemu ndogo tu ya mateso ambayo Bwana wetu aliteseka kwa niaba yetu, bila kusahau kwamba sadaka Yake msalabani katika kufa kwa ajili ya dhambi zetu ilikuwa isiyo na kifani na hakuna ya kufanana nayo, ikingali kuu katika sehemu yake ndogo kabisa kuliko sadaka zote zilizokwishatolewa na zitakazotolewa [milele]. Hata hivyo, maandiko yanazungumzia “sisi kushiriki katika mateso ya Kristo”, tukiiga uvumilivu Wake wa kishujaa wa yote aliyoyakabili kabla ya lile giza kuingia / kushuka, na ni msingi huu Petro anaurejea hapa (War. 8:17; 2Wakor. 1:5; Wafi. 1:29-30; Wafi. 3:10; Wakol. 1:24; 1Pet. 4:12-13; Ufu. 1:9; linganisha na Marko 10:38-39; Matendo 5:41; 2Wakor. 4:10-11; Waga. 6:17; 1Wathes. 1:6; 2Wathes. 1:4-5; 2Tim. 3:12), yaani kuidhihirisha imani yetu na uaminifu wetu kwa ulimwengu wa wanadamu na malaika kwa kuhimili mateso kimungu. Mliitwa kwa ajili ya hayo [mateso] (1Pet. 2:21) …

14.22 wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya (wakiwatia moyo) wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.
Matendo 14:22

3.4  Kwa kuwa tulipokuwapo kwenu tulitangulia kuwaambia kwamba tutapata dhiki (sisi Wakristo), kama ilivyotukia, nanyi mwajua.
1Wathes. 3:4

… kama wawakilishi wa Bwana aliyetugomboa.

12.3  Mtafakarini sana Yeye (Bwana wetu) aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya waliotenda dhambi [dhidi ya nafsi yake] msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu [na kukata tamaa].
Waebr. 12:3

2.11  Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia;
2.12  Kama tukistahimili, tutatawala pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi;
2.13  Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.
2.14  Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao.
2Tim. 2:11-13

Kufuata mfano wa Bwana wetu, aliyekufa kwa niaba yetu, katika mambo yote lakini haswa katika jambo la ustahamilivu wakati wa kutendewa mabaya, ni jambo la msingi kwa Mkristo. Msemo unaopendwa sana na watu siku hizi ni, “Bwana Yesu angefanya nini [katika mazingira ya leo hii]? – (“What would Jesus do?”) una dosari kubwa, kwani haujalenga shabaha. Sisi siyo Bwana Yesu Kristo na hatukabiliani na yale aliyokabiliana nayo Yeye, hata kidunchu! (haswa katika kufa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote). Badala yake, tunapaswa kujiuliza sisi wenyewe, “Bwana Yesu anataka mimi nifanye nini?”, halafu tukifanye kitu hicho. Yeye ndiye aliyetugomboa, Yeye ndiye aliyeulipia uhuru wetu kutoka katika dhambi na kifo kwa gharama ya damu Yake, Yeye ndiye aliyepitia kifo chake cha kiroho msalabani kwa ajili ya dhambi zetu zote, na hivyo Bwana wetu ana haki ya kutarajia mwenendo huu kutoka kwetu, yaani uvumilivu wa manyanyaso kwa upande wetu katika namna ambayo inamletea Yeye utukufu. Kila tulicho nacho kinatokana Naye, tuna madeni kwake, na hakuna kilicho na thamani kwetu kama Yeye kufurahishwa na mwenendo wetu.

25.21 Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.
Matt. 25:21

Kufaulu mtihani wa mateso tusiyostahili (ya uonevu) si jambo linalowezekana kwa wale Wakristo ambao bado ni wachanga kiroho, yaani hawajafikia kiwango cha kupevuka kiroho. Kunahitaji kiasi cha juu kabisa kabisa cha ile kweli ya Biblia ndani ya mioyo yetu, iliyoaminiwa na kushikiliwa imara, tayari ikingojea Roho Mtakatifu aitumie pale dhoruba za maisha zitakapojitokeza. Biblia ndiyo “nia (mind, thinking) ya Kristo” (1Wakor. 2:16), kwa hiyo ili tuweze kujua kile ambacho Bwana wetu anakitaka kutoka kwetu kunalazimu kwanza tusome na kujifunza kila kitu alichotupatia katika Neno Lake la kweli (Biblia). Hapo ndipo sisi tutakuwa na nafasi ya kutimiza kwa ufanisi amri, zilizo wazi na zilizofichika, zilizomo katika ibara hii ya maandiko. Hivyo basi, upevu wa kiroho ni sharti la lazima [kutimiza] kabla ya kuweza kufanikiwa kutimiza maagizo yanayotolewa hapa. Bwana wetu ni mfano timilifu wa kanuni hii, kwani alifanikiwa kujifunza na kuitumia kweli yote ya maandiko [katika] kuukanusha uwongo wa kijanja wa Shetani: Matt. 4:1-11; Lk 4:1-13). Ingawa kamwe hatutafikia kilele kile cha mafanikio cha Bwana wetu katika mwendo wetu wa Kikristo, hii ndiyo (angalau) shabaha tuliyopewa tuifikie, kwani huu ndio mfano tunaoamriwa bayana tuufuate hapa.

4.1  Basi kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, sisi nasi tujivike silaha ya nia ile ile (yaani mtazamo wa aina hiyo hiyo); kwa maana yeye aliyeteswa katika mwili wake (kama Bwana Yesu alivyoteseka) ameachana na dhambi.
1Peter 4:1

Kwa kuwa Bwana wetu “hakutenda dhambi” (1Pet. 2:22), katika namna hiyo hiyo nasi tunapaswa kugeuza sura zetu kutoka yote yaliyo ya dhambi, tukifanya hivyo zaidi na zaidi kadiri tunavyokua [kiroho] – tukihakikisha tunaungama na kutubu dhambi zetu mara tunapogundua tumetenda dhambi hizo kwa makusudi (ukaidi) au la. Hii inatokea haswa katika eneo la dhambi za moyoni na zile za ulimi / mdomo katika muktadha wa kuvumilia unyanyasaji, ambapo kishawishi cha kurudisha kisasi kwa kutoa kauli kali inayoumiza ni kikubwa sana. Rejea mfano mahususi ambao Petro anautumia katika kutupatia kielelezo cha mfano wa Kristo, yaani Bwana wetu alijizuia kabisa kurudisha kisasi kutokana na kashfa / uzushi Aliosingiziwa na pia Alijizuia kutoa vitisho kwa wale waliokuwa wanamtukana. Sasa, katika muktadha wa utumwa, na katika muktadha wa kuajiriwa – yaani mfumo wa kale na wa sasa – hili ni suala muafaka ambalo Petro analizungumzia hapa. Tunajua, kwa mfano kutoka Yakobo (Yak. 3:2-12; Yak. 1:19) – na uzoefu kutoka katika maisha yetu ya Kikristo – kwamba dhambi za ulimi / mdomo / maneno ni kati ya dhambi ngumu sana kujiepusha nazo.

1 Nalisema, Nitazitunza njia zangu Nisije nikakosa kwa ulimi wangu; Nitajitia lijamu kinywani, Maadamu mtu mbaya yupo mbele yangu.
2 Nalikuwa sisemi, nalinyamaa kimya, Sina faraja, maumivu yangu yakazidi.
3 Moyo wangu ukawa moto ndani yangu, Na katika kuwaza kwangu moto ukawaka; Nalisema kwa ulimi wangu,
Zab. 39:1-3 SUV

Kishawishi cha kulipiza kisasi dhidi ya wale tunaohisi wametufanyia mabaya huja kwa kunyemelea, na mara nyingi huamsha hisia kali sana. Hivyo, hata tukijizuia kuwakabili mabosi wetu uso kwa uso na kuwaeleza makosa yao pamoja na malalamiko yetu, mara nyingi tunaingia katika kishawishi cha “kuteta” pamoja na wafanyakazi wengine tulio nao chini ya mabosi hao, na hivyo kuwafanya mabosi hao waonekane wabaya kabisa. Aina hii ya kashfa (kuteta dhidi ya mtu ni kashfa – slander) ni mfano kamili wa jinsi wafanyakazi wa chini wanavyolipiza kisasi dhidi ya mabosi wao, au “wanavyojilinda” dhidi ya mabosi wenye kinaya (kiburi / majivuno). Kashfa hii [kutoka kwa wafanyakazi wa chini] pia ina udanganyifu uliofichika kwa maana ya kwamba inaweza kuonekana kama siyo dhambi, kutegemea na kile tunachosema. Lakini hata kama tunachosema siyo uwongo wa moja kwa moja, kutegemea na motisha zetu na maneno tunayotumia, siku zote tunaingia katika hatari ya kutenda dhambi ya kashfa – slander – pale tunaposema jambo hasi juu ya mtu yeyote yule – na hususan wale wenye mamlaka juu yetu. Kukaa kimya kabisa ni kiwango kigumu sana kukifikia (kama ambavyo aya kutoka Zaburi zilizonukuliwa hapo juu zinavyodhihirisha), lakini Wakristo wana ulazima wa kuukumbuka msingi wa kujizuia na kashfa (ingawa kwa hakika Yeye alikuwa na kila sababu ya kulipiza kisasi – 1Pet. 2:22) katika kila sehemu ya kazi na maisha yetu ambapo tunafanyiwa mabaya, kwa jinsi tunavyoona.

Na kuna tatizo lingine linaloambatana na hii tabia ya kujionyesha kwamba hatuna lawama na kulipiza kisasi: Wakristo wana ulazima wa kumwamini Mungu, kumtegemea Yeye, kumngojea Yeye kwa ajili ya ufumbuzi wa shida zao, kuweka wokovu (deliverance) wetu katika mikono Yake, na siyo kuchukua hatua sisi wenyewe. Lakini tukianza kufanya kashfa, na kama tunashawishika kwenda hatua moja mbele na kujihusisha kwenye ujanja-ujanja au hila za aina yoyote, au njama, au siasa za maofisini zenye nia ya kuwahujumu wale tunaoona kuwa wanatuonea, basi hapo tutakuwa tumelitoa suala hilo katika mikono ya Bwana na kuliweka katika mikono yetu wenyewe. Matokeo ya jambo hili na mwenendo huu kamwe hayatakuwa na neema kama ambavyo yangekuwa nayo ikiwa tungengojea kwa subira kuuona wokovu (deliverance) wa Bwana.

Wakristo wana ulazima wa kukumbuka kwamba siku zote mambo yao yataenda vyema ikiwa watamtegemea Bwana, na siku zote yataenda mrama wanapotegemea juhudi zao wenyewe. Hivyo, wakati haiwezekani kufikia kiwango cha kutokuwa na mushkeli wa aina yoyote – hata kidogo tu – na pia haiwezekani kutokuwa na malalamiko ya msingi ya aina yoyote, jinsi tunavyozidi kutotilia maanani manyanyaso ya mahala petu pa kazi, na jinsi tunavyopunguza malalamiko, ndivyo jinsi itakavyokuwa bora kwetu kwa mtazamo wa kiroho. Njia na mtazamo huu bora, kwa hakika, ndio ambao Bwana wetu siku zote aliuchukua na kuufuata – Naye ndiye mfano tunaotakiwa kuufuata siku zote.

2 Ulimi wa mwenye hekima hu[tumiwa na ku]tamka maarifa vizuri; Bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu
Mithali 15:2 SUV

Kishawishi cha kuwatisha watesi Wake kwa hakika kilikuwa kikubwa sana. Yeye ndiye aliyewaumba! Na katika wakati huo alikuwa anakaribia kufa kama sadaka kwa ajili yao! Na pia Yeye ndiye atakayekuwa Hakimu atakayewahukumu! Lakini hakushindwa mbele ya kishawishi hicho. Hakuna kishawishi chochote cha kutoa vitisho ambacho sisi tutakabiliana nacho kinachoweza kuwa kikubwa kama kishawishi kile alichokabiliana nacho Yeye. Nasi tunajua kwamba Hakimu Mwenyewe yuko pamoja nasi katika manyanyaso yote tutakayolazimika kuyapitia. Kisasi chochote kile tutakachojaribu kulipiza ili tuweze kuthibitisha uonevu tunaoteswa nao hakiwezi kufanana na hukumu ya haki ambayo Bwana wetu anaweza na atawapatia wale ambao wamethubutu kuwanyanyasa watakatifu Wake. Katika nyakati hizo [za uonevu], badala ya kulipiza kisasi, inatupasa “tujikabidhi kwa Muumba wetu aliye mwaminifu huku tukizidi kutenda mema” (1Pet. 4:19).

15 Basi Bwana atuamue, akatuhukumu mimi na wewe, akaone, akanitetee neno langu, akaniokoe na mkono wako.
1Sam. 24:15 SUV

1 Ee Bwana, unihukumu [na unithibitishe], unitetee kwa (dhidi ya) taifa lisilo haki, Uniokoe na mtu wa hila asiye haki.
Zab. 43:1 SUV (ling. na Zab. 7:8; 26:1; 35:24; 54:1; 138:8).

Kwani ni bora kumtumainia Bwana kuliko kuwatumainia watawala (Zab. 118:9) – na kwa hakika ni bora kumtumainia Bwana kuliko kujitegemea sisi wenyewe tulio dhaifu. Kwani wakati mara nyingi hatuwezi kufanya chochote kikubwa (haswa pale tunaponyanyaswa na wakubwa kazini mwetu), hakuna ambacho Bwana hawezi kufanya.

27 Tazama, mimi ni Bwana, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza?
Yer. 32:27 SUV

Hii haina maana ya kwamba sisi waumini tunalazimika kuwa watu wasiojilinda, watu wanaokubali tu kunyanyaswa bila ya kutoa ukinzani. Alipotishiwa uhai wake na Sauli, Daudi alikimbilia jangwani – lakini wakati wote alikuwa mwangalifu katika kuhakikisha hafanyi jaribio la kumwua mpakwa mafuta wa Bwana – Sauli – badala yake alimtumainia Bwana kuthibitisha kwamba yeye hana hatia, wakati Wake utakapowadia. Vivyo hivyo, tunaweza kuamua kubadilisha ajira zetu, au kutumia njia halali, za ndani au nje ya kampuni au shirika, ikiwa manyanyaso tunayoyakabili yatavuka msitari wa mwenendo unaokubalika katika sera za kampuni au shirika, au yatavuka msitari wa sheria za nchi. Lakini katika mambo yote, ni busara kwa waumini kuyaweka matatizo haya katika mikono imara ya Bwana wetu kwa kadiri inavyowezekana, hata pale tunapolazimika kuchukua hatua ya aina moja au nyingine. Na katika mambo yote ni jambo la busara kujizuia kulipiza kisasi kwa mdomo / maneno – siyo kwa sababu tunawaogopa wanaotunyanyasa, … bali ni kwa sababu tunamwogopa Yeye ambaye tumeweka tumaini letu kwake kutuokoa.

25 Bwana ni mwema kwa hao wamngojeao, Kwa hiyo nafsi imtafutayo.
26 Ni vema mtu autarajie wokovu wa Bwana Na kumngojea kwa utulivu.
Maombolezo 3:25-26 SUV

Huu ndio ufunguo – ndio ufunguo wa kila kitu katika maisha ya Kikristo. Tunapaswa kujifunza mazoea ya kumtumainia Mungu, kwamba atafanya kila kitu kuwa mema kwa ajili yetu, hata kama tunachokabiliana nacho wakati ule kinaonekana kuwa cha kutisha, cha uonevu na hakiwezekani kabisa kuvumiliwa.

8.28  Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu huwafanyia kazi wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani wale walioitwa kwa kusudi lake.
War. 8:28

Mpango wa Mungu, aliouunda kabla ya kuumba ulimwengu, umejumuisha kila kitu kitakachotokea (rejea War. 8:29-30; Waefe. 1:4-5; etc; soma pia Kanuni ya Kudura ya Mungu (Predestination) kama inavyofundishwa katika Biblia kutoka https://sayuni.co.tz/ ) Wakati wowote tunapokabiliwa na tatizo [gumu] ambalo sisi wenyewe hatuwezi kulitatua, huo ndio wakati muhimu na mwafaka wa kuweka mambo yetu katika mikono Yake thabiti na kuyaacha hapo mpaka anapotukomboa.

Mtwike Bwana fadhaa zako, naye atakutegemeza, hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke. Zab. 55:22. NEN Biblia.

Nyakati fulani tunapaswa kukubali kwamba hatuwezi kufanya na kufanikisha kitu fulani sisi wenyewe, na hapo tunapaswa kuazimu kumsubiria Mungu; “tusijishughulishe na mambo makubwa kuliko sisi wenyewe (mambo yanayotuzidi nguvu)” (Zab. 131:1); tusiweke nia ya kujithibitisha “kuwa [sisi] hatuna hatia” sisi wenyewe; badala yake tunapaswa kutumaini kwamba Bwana atafanya mambo yote kuwa mema kwa ajili yetu, hata kama kwa wakati huo jambo hili linaonekana kuwa halielekei kufanikiwa au haliwezekani kabisa – na kwa hakika haswa jambo hilo linapoonekana kuwa ni gumu mno au lisilowezekana. Kwani tunajua – au tunapaswa kujua – kwamba Bwana wetu anatuchunga wakati wote na kwamba Yeye anahukumu katika njia iliyo sahihi na ya haki wakati wote. Kama Ayubu, tunapaswa kuelewa kwamba pale tunapopitia mateso tusiyostahili na yasiyo ya haki, basi hii ni kwa sababu hayo ni “mapenzi ya Mungu” (1Pet. 2:15). Tunapaswa kutokuwa na shaka kwamba Bwana wetu mpendwa Yesu Kristo anajua fika kile anachokifanya na kwa nini, ingawa sisi wenyewe yawezekana tusiujue mpango Wake. Kazi yetu kama wafuasi Wake ni kutouliza kwa nini, bali ni kumtumainia na kutokuwa na mashaka Naye. Kama tutakuwa na mtazamo huu wa Kibiblia, mwisho wa yote hatutasikitishwa – hata kama tunalazimika kusubiri kwa ajili ya wokovu (deliverance) Wake (na hili hutokea mara nyingi tu katika maisha ya Mkristo!).

9 Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure?
10 Wewe hukumzingira kwa ukingo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi.
11 Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.
Ayubu 1:9-11 SUV

4 Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake.
5 Lakini sasa nyosha mkono wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele za uso wako.
Ayubu 2:4-5 SUV

Tunapoitazama vita inayoendelea ulimwenguni, vita ambayo nasi tunashiriki kama askari [kwa ukaribu kabisa], je, ni jambo la kushangaza kwamba sisi waumini tunapitia katika shida na mateso yanayosababishwa na yule mwovu, watumishi wake, na mfumo wa ulimwengu aliouasisi na kuusimika pamoja na watendaji wake (wanadamu na malaika)? Kwa hakika, ni jambo la kushangaza sana – na pia ni matokeo ya neema isiyo kifani ya Mungu wetu – kwamba hatupitii mateso kwa kiwango kikubwa zaidi ya kile tunachopitia.

15.18 Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.
15.19 Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua [kutoka] katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia.
15.20 Likumbukeni lile neno [la msingi] nililowafundisha, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa walininyanyasa mimi, watawanyanyasa ninyi [pia]; ikiwa walilishika neno langu, watalishika na lenu.
Yoh. 15:1-20

Tunapozidi kusogea karibu ya Bwana wetu na mwanga wa utukufu Wake tunaouakisi unavyozidi kuwa mng’avu hapa ulimwenguni, ndipo, tunapaswa kujua, kwamba zile nguvu za uovu zitatushambulia zaidi. Hii ni sehemu muhimu ya vita hii isiyoonekana ambayo sisi ni askari tunaopigana ndani yake kwa ukaribu sana. Lakini badala ya kuingiwa na hofu, tuna kila haki ya kuwa “hodari na wenye moyo wa ushujaa” (Kumb. 31:6-7; 31:23; Yoshua 1:6-9; 1:18; 1:25; 1Mambo ya Nyakati 32:7), kwa sababu tunamtegemea Yeye ambaye dhidi Yake hakuna mwenye nguvu zaidi. Na kwa wale miongoni mwetu wanaoweka tumaini lao, imani yao na utegemezi kamili Kwake …

1) Watapata faraja na kutiwa moyo katika mitihani na mateso yao.

16.33 Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mtapitia dhiki (tribulation); lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu!
Yoh. 16:33

1.3  Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote;
1.4  atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu.
1.5  Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu (katika huduma yetu kwenu), vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo.
1.6  Lakini ikiwa sisi tu katika dhiki, ni kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu; au ikiwa twafarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu [mnayoipokea]; ambayo hutenda kazi yake kwa [ninyi] kustahimili mateso [kama] yale tuteswayo na sisi.
1.7  Na [hivyo] tumaini letu kwa ajili yenu ni imara, tukijua ya kuwa kama vile mlivyo washiriki wa yale mateso, vivyo hivyo mmekuwa washiriki wa zile faraja.
2Wakor. 1:3-7

4.14  Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo basi hiyo ni baraka ya kweli kwenu, kwa kuwa Roho wa utukufu, yaani Roho wa Mungu, anawakalia (ili mumtegemee katika mtihani huo mnaopitia).
1Pet. 4:14

2) Kuna wokovu na msaada tunapokuwa katika mitihani na dhiki zetu.

9 Bwana atakuwa ngome kwake aliyeonewa, Naam, ngome kwa nyakati za shida.
10 Nao wakujuao jina lako wakutumaini Wewe, Maana Wewe, Bwana hukuwaacha wakutafutao.
Zab. 9:9-10 SUV

18 Kwa maana mhitaji hatasahauliwa daima; Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele.
Zab. 9:1 SUV

8.35  Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au kukosa mahitaji, au adha, au njaa, au ufukara, au hatari, au upanga?
8.36  Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa.
8.37  Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa [njia ya] Yeye aliyetupenda.
8.38  Kwa maana nimekwisha kujua [kwa] hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka [demons/pepo] , wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,
8.39  wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.
War. 8:35-39

10.13  Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida [katika maisha] ya wanadamu; ila [zaidi ya hapo] Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo [kustahamili]; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea (namna ya kutatua tatizo), ili mweze kustahimili [shinikizo hilo].
1Wakor. 10:13

4.7  Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu.
4.8  Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa;
4.9  twaudhiwa, bali hatuachwi (hatutelekezwi); twapigwa na kutupwa chini, bali hatuangamizwi;
2Wakor. 4:7-9

1.6  Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu na mitihani ya namna mbalimbali;
1.7  ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo (haidumu, huisha), ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima,
1Pet. 1:6-7a

3) Hivyo tunapaswa kuwa waangalifu katika kuwa na mwenendo sahihi wa kuendelea kuwa na amani mioyoni mwetu tukingali katikati ya mitihani na dhiki, tukielekeza macho yetu katika faraja ambayo tunayo haki ya kuipokea kwa sasa, na tukielekeza macho yetu mbele kwenye wokovu tunaoujua kwa imani kwamba unakuja.

3 Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu (“amani mara dufu”), kwa kuwa anakutumaini.
Isa. 25:3

15 Kwa maana Bwana MUNGU, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi, Kwa kutubu na kustarehe [katika Mimi] mtaokolewa; nguvu zenu zitakuwa katika kutulia na kutumaini; lakini hamkukubali [haya yote].
Isa. 30:15

1.6  Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu na mitihani ya namna mbalimbali;
1.7  ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo [haidumu, huisha], ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika [ile siku ya] kufunuliwa kwake Yesu Kristo.
1Pet. 1:6-7

Kwa kuwa sisi waumini tuliitwa “kwa makusudi haya”, yaani kushiriki katika mateso ya Kristo, tukimshuhudia katika ulimwengu kwa njia ya uvumilivu wetu wa kimungu katika mitihani na dhiki zetu, ambazo ni ndogo sana zinapowekwa sambamba na kulinganishwa na yale [mateso] ambayo Bwana wetu alilazimika kuyapitia na kuyavumilia kabla ya msalaba, sisi Wakristo hatuwezi kuiachia amani ambayo ni yetu kwa sababu sisi ni [watu] wa Kristo – kwani huu ndio mtazamo na mwenendo tunaopaswa kuwa nao bila kujali mawimbi makubwa yanayounguruma kwa nguvu katika maeneo tunamoishi. Na pale tunapofanya hivyo, na Mungu akiendelea kutusaidia, tutachomoza juu ya shida zetu (kama mtu aliyekuwa akizama majini anavyochomoza juu ya maji hayo), tukipiga hatua kutoka amani [moyoni] hadi furaha [moyoni] kwa njia ya matumaini ya utukufu mkuu ambao utakuwa wetu muda mfupi ijao.

1.2  Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali;
1.3  mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.
1.4  [Basi acheni] saburi na [ifanye] kazi [yake kwa] ukamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kuonekana wenye mapungufu.
Yak. 1:2-4

4.12  Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba (siyo kifo) ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.
4.13  Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.
1Pet. 4:12-13

Kama ambavyo Bwana wetu aliweza kuvumilia mateso ambayo sisi hatuwezi hata kukisia ukali wake kwa “kujikabidhi katika mikono yenye upendo ya Mungu Baba (1Pet. 1:23), vivyo hivyo nasi tunapaswa kujifunza kuweka mambo yetu yote katika mikono imara ya Mungu wetu, tukimwamini kwamba atatuvusha – kwani imani hiyo na uhakika huo ndio msingi wa amani iliyo mioyoni mwetu. Shida yoyote inayotukabili tunaitoa kwa Baba yetu aliye mbinguni katika sala, “tukimtwika fadhaa zetu zote, kwani Yeye anatujali” (Zab. 55:22; 1Pet. 5:7), na tukimtumainia kuwa atafanya mambo yote kuwa mema kwetu, kama Alivyotuahidi (War. 8:28). Yeye ni mwaminifu kabisa na kamwe hajawahi kutuangusha, hata mara moja, ikiwa tu tuko tayari kuusubiria wokovu Wake. Hivyo basi, Yeye anastahili matumaini yetu yote. Alimvusha Bwana wetu Yesu Kristo katika majaribu magumu zaidi ya yale ambayo mwanadamu yeyote amepitia, na kumfikisha salama kwenye ushindi upande wa pili. Na hivyo Bwana Yesu Kristo ndiye mfano wetu, kwani ndiye aliyetupatia kigezo ili tuweze “kufuata / kutembea katika nyayo Zake” (1Pet. 1:21). Kwa hakika ni mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo ambaye anatutathmini na kutuhukumu, na wala si mwanadamu yeyote ambaye tunaweza kumwona na kumsikia, hata wale ambao [kwa sasa] wanaonekana kuwa na madaraka ya muda mfupi tu juu yetu. Hivyo, kama tuko sawa mbele za Hakimu wetu, hatuna haja ya kumwogopa mwanadamu yeyote au mahakama yoyote ya wanadamu au mashambulizi yoyote kutoka kwa wanadamu au mchakato wowote wa kututathmini unaotokana na wanadamu … kwa sababu Yeye atatuokoa, ikiwa tu tutaendesha maisha yetu vile anavyotaka (Zab. 118:6-9).

22 Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.
Zab. 55:22 SUV

Yeye Mwenyewe Alizichukua Dhambi Zetu Katika Mwili Wake Juu ya Mti (aya ya 24):

2.24  Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili tukiwa wafu kwa sababu ya dhambi, tupate kuwa hai kwa sababu ya haki; na kwa kupigwa kwake [mijeledi] mliponywa.
1Pet. 2:24

Sentensi hii hapa juu inaanza na kiwakilishi (pronoun) katika Kiyunani: “Yeye aliyechukua dhambi zetu katika mwili Wake juu ya mti”. Hili ni jambo muhimu kuliona hapa kwa sababu Petro anaunganisha kanuni hii muhimu sana ya kifo cha kiroho (spiritual death) cha Bwana wetu msalabani na haki Yake ya kuwa Hakimu wetu katika kila jambo kama ambavyo Yeye mwenyewe “alivyojikabidhi kwa Yeye anayehukumu kwa haki” (1Pet. 2:23). Bwana Yesu Kristo ni Bwana wetu kwa sababu Yeye ndiye aliyetuumba – lakini pia alipata heshima hii kama Mwana wa Adamu kutokana na kufa Kwake pale msalabani kwa ajili yetu.

5.22 Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana [cheo cha ku]hukumu yote;
5.23 ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka.
Yoh. 5:22-23

Kwa kuwa Mungu Baba alikabidhi hukumu yote kwa Mungu Mwana [ambaye ndiye Mwokozi wetu], matokeo yake, kama Bwana wetu anavyoonyesha papo hapo (immediately), ni kwamba “yeye alisikiaye neno Langu na kumwamini Yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka hukumuni na kuingia uzimani” (Yoh. 5:24 SUV). Hivyo basi, kama ambavyo Bwana wetu katika uanadamu Wake alijiweka chini ya mamlaka ya Baba katika mambo yote, akimtumainia Yeye kama Hakimu Wake, vivyo hivyo na sisi waumini ambao sasa [ni watu] Wake tunapaswa kuwa waangalifu wakati wote – na haswa wakati wa shinikizo – kujitumainisha sisi wenyewe kwa Hakimu wetu, Yesu Kristo, ambaye ameshinda haki ya kuwa na mamlaka hayo ya kutuhukumu sisi kwa njia ya uvumilivu Wake pale msalabani, kifo Chake cha kiroho ambapo alilipia dhambi zote za ulimwengu.

6.37 Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msitie [mtu] hatiani, nanyi hamtatiwa hatiani; sameheni, nanyi mtasamehewa.
Luka 6:37

Kitendo cha Petro cha kuunganisha dhana hizi mbili, yaani 1) ulazima wetu wa kustahamili mateso yasiyo ya haki, na 2) mfano wa Bwana wetu katika kufanya hivyo – ila tu Yeye alifanikisha jambo hili katika kiwango timilifu katika kipindi chote cha maisha Yake hapa duniani na, tukitizama matukio muhimu yanayohusu wokovu wetu, kabla tu, na wakati wa matukio yote ya wiki ile ya kufa Kwake ambayo uelewa wetu [wa tukio hilo] si mkubwa sana – ni kitendo cha makusudi: kazi au wajibu wetu katika kushiriki katika mateso ya Kristo bila ulalamishi ni kujitumainisha Kwake kwa ajili ya wokovu wetu, tukiingojea tathmini ya Hakimu wetu … kama ambavyo Yeye mwenyewe alivyojitumainisha kwa Baba.

5 Mikononi mwako naiweka roho yangu; Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.
Zab. 31:5 (ling. na Lk. 23:46)

Pamoja na kipigo, kutemewa mate, kudhihakiwa, kushuhudiwa uwongo, kutukanwa, kusalitiwa, kukanwa, na mateso mengine yote ambayo Bwana wetu alilazika kuvumilia, na kusulubiwa ikiwa ni njia ya maumivu sana ya kuuwawa, ukweli kwamba Bwana wetu alisulubiwa (kinyume na kupigwa mawe au kukatwa shingo), ulikuwa ni sehemu ya kumuaibisha pia. Kwani kulikuwa na kiasi fulani cha aibu kilichohusishwa na aina hii ya kuuwawa (ling. na Waebr. 12:2), kwa sababu kifo hiki kilimwonyesha mhusika “katika hali ya kulaaniwa” (Waga. 3:13).

23 mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utamzika siku iyo hiyo; kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu; usije ukatia unajisi katika nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi wako.
Kumb. 21:23 SUV

3.13  Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti;
Waga. 3:13 SUV

Pasipo na shaka yoyote ni kwa sababu hii Petro anauita msalaba “mti” hapa, kwa makusudi ya kutukumbusha pia kwamba Bwana wetu Yesu Kristo alipitia fedheha kwa ajili yetu (ikiwa ni pamoja na mateso mengi aliyopitia wakati wa kifo Chake kwa ajili ya dhambi zote za wanadamu).

12.1  Basi na sisi pia [kama waumini wanaotajwa katika sura ya 11], kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii (watu na malaika), na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi (maeneo ya tabia zetu ambamo tuna udhaifu mkubwa zaidi); na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,
12.2  tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
Waebr. 12:1-2 (ling. na Waebr. 11:11-26)

13.13  Basi na tutoke, tumwendee nje ya kambi (yaani kama Yeye, tukimchagua Mungu badala ya ulimwengu), tukichukua (yaani tukibeba) shutumu lake (yaani kama alivyobeba Yeye).
Waebr. 13:13

Mahala pengine katika tovuti ya https://ichthys.com tumejadili kifo cha kiroho cha Bwana wetu, malipo aliyoyafanya kwa ajili ya ulimwengu wote katika yale masaa matatu wakati akisulubiwa msalabani (mara nyingi katika Biblia ikitumika istilahi “damu ya Kristo” kuelezea tukio hilo kuu)4. Kama ambavyo Petro anathibitisha katika aya hii, Bwana wetu “alizibeba dhambi zetu zote” katika mwili Wake – maana yake dhambi hizi zote “zilimiminwa” juu Yake katika lile giza na kwamba Yeye alilipa gharama yote [ya dhambi hizo] katika kuvumilia ile hukumu ya moto iliyotakiwa ili kuiridhisha ile haki (justice) ya Mungu katika kila dhambi mojawapo. Hivyo basi, sadaka ya Bwana wetu ni jambo / tukio kuu kuliko yote katika historia ya ulimwengu, kwa kiwango kisichoweza kufikirika na sisi. Sehemu ndogo kabisa ya kile Alichokifanya kwa ajili yetu – kwa ajili ya ulimwengu wote – ni kubwa kuliko chochote kilichokuwako, kilicho sasa hivi, na kitakachokuwako. Haiwezekani kabisa kuupa msalaba thamani kubwa zaidi ya ile ulio nao (yaani over-estimate) – na kwa kweli haiwezekani kuelewa thamani yake halisi wakati tukingali katika hii miili yetu ya sasa, hapa duniani. Lakini sisi Wakristo tuna ulazima wa kuweka akilini ukweli kwamba kifo cha Bwana wetu kwa ajili yetu, kifo Chake cha kiroho, katika kulipia gharama ya wokovu kwa ajili yetu kwa kufa kwa ajili ya kila dhambi yetu, ndiyo sarafu halisi ambayo imetumika katika kuununua uhuru wetu kutoka katika kudura (destiny) ya kifo ambayo ndiyo ingekuwa majaliwa yetu – na kwamba hakuna kilicho na thamani zaidi ya sadaka ile katika ulimwengu mzima.

1.18  Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea [kutoka] kwa baba zenu;
1.19  bali [mlinunuliwa] kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa (doa), yaani, [damu] ya Kristo.
1Pet. 1:18-19

“Damu” hii haikuwa damu halisi katika maana sisisi (literal) ya neno damu (kwani Bwana wetu hakufa kwa sababu ya kutokwa damu, mwili Wake ulibakiwa na damu ndani yake hata baada ya Yeye kwa hiari Yake mwenyewe ‘alipoipumua

4 Tizama haswa: section II, “The Saving Work of Jesus Christ”, in Bible Basics 4A: Christology.
nje’ roho Yake baada ya kifo Chake cha kiroho: Yoh. 19:30-35). Hii “damu ya Kristo” ni sitiari (metaphor), ikimfananisha Kristo na kondoo wa sadaka ambaye kifo cha mwili wake (kilichoonekana wazi wakati koo lake lilipokatwa) kinawakilisha kifo Chake cha kiroho (kilichofunikwa na lile giza na tangu hapo kujulikana na kueleweka kutoka katika maandiko tu). Kifo Chake cha kimwili kinaashiria kile alichokifanya kwa ajili yetu katika namna dhahiri / bayana kabisa – lakini hakuna hata mtu mmoja hapa duniani anayeweza kuelewa uhalisia na ukubwa wa gharama ambayo Bwana wetu amelipa kwa ajili yetu, akitesekea hukumu ya moto kwa kila moja kati ya dhambi zetu zote na dhambi za ulimwengu wote – vinginevyo hakuna anayeweza kuokoka / kuokolewa kutoka kwa haki (justice) ya Mungu wetu isiyo na upendeleo wowote.

5.21  Yeye asiyejua (asiyetenda) dhambi alimfanya kuwa [sadaka ya] dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa [na] haki (uongofu) ya Mungu katika Yeye.
2Wakor. 5:21

Yesu Kristo alifanya hili kwa ajili yetu. Na wakati hatuwezi kuelewa kikamilifu urefu, upana, na kina cha sadaka Aliyoitoa kwa ajili yetu, kwa hakika tunapaswa kuuweka mioyoni mwetu na kamwe tusiuachie ukweli kwamba wokovu wetu, wokovu kutoka shimo la mauti, kutoka kifo, na kutoka laana ya milele, ni kutokana na sadaka ile pekee. Kwa hali hiyo basi, kwa nini tusiweke kipaumbele cha maisha yetu kuwa ni kuitikia wito Wake na kufanya yale Anayotuamuru tuyafanye, yaani “tuwe wafu kwa dhambi bali tuwe hai kwa haki”?

Kuweni Wafu kwa Dhambi ili Muwe Hai kwa Haki (aya ya 24):

Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu katika mwili Wake ili sisi, baada ya kuwa wafu kwa dhambi, tuweze kuishi kwa haki / uongofu. Kwa majeraha Yake sisi tumepona. {Kwa kupigwa Kwake mijeledi mmepona}.
1Pet. 2:24

Sadaka ya Bwana Yesu imetuokoa, lakini bado tungali hapa duniani baada ya wokovu huo. Hii ndiyo dondoo (point) ya Petro katika kuuzungumzia msalaba hapa, baada ya kutufundisha kwamba Bwana wetu ndiye mfano mkuu tunaopaswa kuufuata – kabla tu ya dondoo hii (katika aya ya 21). Bwana wetu hajatupatia tu mwongozo tunaopaswa kuufuata, bali amefanikiwa pia kushinda na kuipata heshima kutoka kwetu na kutufanya tuwe wafuasi Wake kwa hiari yetu wenyewe na tunapita katika njia aliyotutengenezea kwa kutulipia gharama inayotuweka huru na kifo na laana kwa njia ya damu Yake, yaani mateso ya adhabu ya dhambi zetu zote katika lile giza pale msalabani. Na Yeye alifanya hivyo, kama aya inayonukuliwa hapo juu inavyotamka, “ili sisi, baada ya kuwa wafu kuhusiana na dhambi, tuweze kuishi katika uongofu”. Kama waumini waliozaliwa upya katika Kristo, tumo “katika umoja na Kristo”; yaani, tumo “ndani Yake” (kwa mfano, Yoh. 14:20; Yoh. 15:1*ff.; War. 16:7; 2Wakor. 5:17; Waefe. 2:6; Waefe. 2:10; Waebr. 3:14; 1Pet. 5:14), na hivyo tunashirikiana Naye kwa ukaribu kabisa katika kila kitu. Katika Kristo tumekuwa “wafu kwa ulimwengu”, baada ya kuwa tumesulubiwa Naye kimsingi na hivyo tumeachana na mambo yote ya kidunia na ya dhambi milele.

6.6  mkijua neno hili, ya kuwa mtu wetu wa kale / asili alisulubishwa pamoja Naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusiwe watumwa wa dhambi tena;
War. 6:6

2.20  Nimesulubiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.
Waga. 2:20

5.24  Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.
Waga. 5:24 SUV

6.14  Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu.
Waga. 6:24 SUV

5.14  Maana, upendo wa Kristo unatushurutisha, na hivyo tuna uhakika huu, ya kwamba ikiwa mmoja alikufa kwa ajili ya sisi wote, basi wote walikufa [katika
Yeye];
5.15  tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake Yeye aliyekufa na akafufuka kwa ajili yao.
2Wakor. 5:14-15

6.4  Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo

*ff maana yake: and following (na aya zinazofuata)
na sisi tuenende katika maisha mapya.
War. 6:4 (ling. na War. 7:4-6; War. 8:10)

3.3  Kwa maana mlikufa [kwayo yaliyo chini – hapa duniani], na uzima wenu [halisi, wa milele] umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.
Wakol. 3:3 (ling. na Wakol. 2:20)

Kama ambavyo aya tunayoijadili katika muktadha huu (1Pet. 2:24) pamoja na aya nyingine zilizonukuliwa hapa juu zinavyodhihirisha wazi, hiki kifo ambacho sisi waumini tunashiriki pamoja na Bwana wetu kutokana na sisi kuwa katika umoja Naye, kinatokana na utakaso wetu kama mmoja kati ya malengo yetu ya msingi, yaani kujitenga kwetu na mambo yote ya dhambi katika maisha yetu ya Kikristo [mara] baada ya kuzaliwa upya.

3.3  Kwa maana mlikufa [kwayo yaliyo chini – hapa duniani], na uzima wenu [halisi, wa milele] umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.
War. 8:13

Jambo ambalo halina hata haja ya kusemwa ni kwamba, wakati kufa kwetu kwa dhambi na tamaa ya anasa za ulimwengu huu ni suala lililo kamili [na lisilo na masharti wala mipaka], utakaso wetu katika maisha ya dunia hii mara nyingi ni jambo lenye taswira nyingine kabisa. Ingawa tumeitwa tuwe watakatifu kwa kiwango timilifu (1Pet. 1:15-16), hakuna hata mmoja wetu “anayeishi ndani ya mwili” atakayeweza kufanikiwa kufikia kiwango hicho cha utimilifu … lakini tunatarajiwa siyo tu kujiwajibisha kwa shabaha hiyo ya kimungu, lakini pia kupiga hatua kila siku katika kujitenga kwetu na dhambi na tamaa za ulimwengu huu katika kila kitu tunachokiwaza, tunachokisema na tunachokitenda. Ni vita – katika hili hakuna shaka. Lakini ni vita ambayo Bwana wetu mpendwa Yesu Kristo anatutarajia tuipigane kwa moyo wote – na Ana haki zote za kutarajia mwenendo huo kutoka kwetu kutokana na kile alichokifanya kwa niaba yetu katika kutugomboa ya kutarajia kwamba tutajitahidi kufanya hivyo. Tunaposhindwa kufikia shabaha hii, kama ambavyo sote tuna udhaifu huu, Yeye anakuwa Wakili wetu, pamoja na Roho Mtakatifu, katika kutusamehe pale tunapokiri dhambi zetu zote, dhambi ambazo Yeye alikwishakufa kwa ajili yake na kuzilipia gharama yote ya hukumu (Zab. 32:5; War. 8:26-27; 1Yoh. 1:9; 1Yoh. 2:1).

Hivyo kwa waumini wote, “kufa kwa dhambi” siyo msemo wa kawaida tu. Ni agizo muhimu, yaani kuuleta mwenendo wetu katika kiwango cha kuoana kabisa na hadhi tuliyo nayo: kutokana na hali / nafasi yetu ya kuwa katika Kristo, sisi ni watimilifu; hivyo basi, tunapaswa kuenenda katika namna timilifu. Hii ndiyo maana halisi ya “kuishi kwa haki / uongofu”. Uongofu unaoelezwa katika muktadha wetu hapa ni ule ambao sisi waumini tunapewa pale tunapoweka imani yetu katika Bwana Yesu Kristo (War. 3:23-26; War. 4:1-5; War. 4:25; War. 5:1; War. 8:28-30).

6 [Abrahamu] akamwamini Bwana, Naye akamhesabia jambo hili kuwa haki / uongofu
Mwa. 15:6.

Kwa kuwa tunao uongofu wa Mungu, basi tuko huru na lawama / shutuma zote, ingawa tungali hapa duniani, na hivyo, tunarudia tena kusema, tunatarajiwa kufanya kila juhudi ya kimungu kuuweka mwenendo wetu hapa duniani katika msitari mmoja na ule uongofu mtimilifu ambao ni wa kwetu kutokana na kuwa wamoja na Bwana Yesu Kristo. “Kuishi” hivyo kunamaanisha kile kinachosemwa: “jinsi tunavyoendesha maisha yetu ya Kikristo hapa duniani. Kama “tunautafuta utakatifu” (Waebr. 12:14), tukijitahidi kuwa watakatifu na kuishi katika uongofu wakati wote na katika taswira zote za maisha yetu, basi hapo tutakuwa tunaishi kutokana na agizo hili. Lakini kama si hivyo …

2.11  Hili ni neno la kuaminiwa: kama tukifa pamoja Naye, tutaishi pamoja Naye pia;
2.12  Kama tukistahimili [katika mateso na mitihani], tutamiliki [tutatawala] pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi;
2.13  Kama sisi hatuamini, Yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.
2Tim. 2:11-13

Mwisho kuhusiana na suala hili, haifai kabisa kusahau kwamba kuishi kwa shabaha ya kumfurahisha Bwana Yesu Kristo siyo tu ni suala la kujizuia kutenda kitu chochote kibaya, wala hii siyo sehemu kubwa ya shabaha hiyo. Kumfurahisha Bwana wetu, kuufanyia kazi (kuutimiza) uongofu wetu unaotokana na imani yetu katika Yeye, kunamaanisha kufanya yale matendo chanya ambayo Yeye anataka tuyafanye.

16.24 Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, [kwanza] na ajikane mwenyewe (aache matamanio yake binafsi), ajitwike msalaba wake, anifuate.
Matt. 16:24

Kuishi kwa ajili ya Bwana Yesu Kristo kunamaanisha kuzikana tamaa zetu katika kuzigeuka dhambi na pia kuukubali ukweli kwamba sasa tunaishi kwa ajili Yake na tuko tayari kufa kwa ajili Yake wakati wowote (na tunaubeba msalaba huo wakati wote). Lakini pia inamaanisha kimsingi kwamba tunapaswa kumfuata Yeye, yaani kufanya kama alivyofanya Yeye katika kukua kiroho katika namna timilifu (Luka. 2:40; Luka 2:46-49) hadi kufikia kupevuka kiroho, kufaulu mitihani yote Aliyopitia katika namna timilifu (na hivyo kuonyesha maendeleo timilifu ya kiroho), na kuzaa matunda [ya kiroho] kwa utimilifu katika kutimiza utumishi mkuu kuliko huduma / utumishi wote katika historia, kabla ya kupitia mateso makali ya msalaba na kifo cha kiroho kilichofuata. Sisi, kwa kweli, hatuwezi kuwa watimilifu katika dunia hii, lakini tunapewa thawabu kulingana na juhudi zetu zinazofanywa kimungu katika kutimiza majukumu yetu chanya ambayo Bwana wetu ametuita ili tuyatimize – na hii inapaswa kuwa motisha ya kutosha ya ziada ya sisi kufanya hivyo, shauku kubwa kabisa kwa ajili ya furaha Yake na sisi, pamoja na woga wa Yeye kutofurahishwa nasi.

5.10  Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya [yasiyo na thamani].
5.11  Basi tukiijua hofu ya Bwana [katika matarajio ya hukumu hii], twawavuta wanadamu [ili waende mwendo sahihi]; lakini tumedhihirishwa mbele za Mungu [jinsi mioyo yetu ilivyo]. Nami natumaini ya kuwa tumedhihirishwa katika dhamiri zenu pia.
2Wakor. 5:10-11

Hivyo basi, na tufanye azma ya kugeuka kutoka yote yasiyo ya kimungu na badala yake tuikumbatie kwa shauku yote changamoto yetu ya kufanikisha kila jambo ambalo Bwana wetu anataka tufanye hapa duniani, shabaha yetu ikiwa ni kukua, kuendelea na kuzaa matunda [ya kiroho] kwa ajili Yake, licha ya mateso yote na ukinzani tutakaokabiliana nao katika njia yetu, iwe katika ajira zetu au sehemu nyingine yoyote katika maisha yetu.

Na kwa Jeraha Lake Mliponywa {Tafsiri nyingine: Na kwa Kupigwa Kwake Mijeledi Mliponywa} (aya ya 24):

2.24  Yeye mwenyewe alichukua/alibeba dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili sisi tukiwa wafu kwa dhambi, tuwe (tupate kuwa) hai kwa haki/uongofu; na kwa jeraha Lake mliponywa.
1Pet. 2:24

Jeraha linalozungumziwa hapa ni kile kifo Chake msalabani kwa ajili ya dhambi zetu. Yote tuliyo nayo kama waumini, matarajio ya ufufuo na uzima wa milele ambapo mateso yote ya kimwili yataisha milele, yanategemea na kitendo cha Bwana wetu cha “kubeba dhambi zetu katika mwili Wake pale msalabani”. Hii ndiyo namna “tulivyoponywa” kutoka katika dhambi ambayo vinginevyo ingetuangamiza katika ziwa la moto milele, na hii ndiyo sababu tunatazamia furaha ya milele. Hii ni sababu tosha ya kutoruhusu shukrani kwa Bwana wetu kwa ajili ya yale Aliyoyafanya kwa ajili yetu iondoke katika mioyo yetu na akili zetu.

6.14  Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu.
Waga. 6:14 SUV

Kondoo Waliopotea Lakini Sasa Wamerejea (aya ya 25):

2.25  Kwa maana mlikuwa mnapotea kama kondoo; lakini sasa mmemrudia Yeye aliye Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu (uzima wenu).
1Pet. 2:25

Ili kutusaidia kuuimarisha mtazamo huu wa kuachana na mambo ya zamani na kuukumbatia kwa moyo wote uzima mpya tulio nao katika Bwana Yesu Kristo, Petro anatualika tukumbuke – kwa muda mfupi tu – jinsi tulivyokosa maana katika maisha yetu na jinsi tulivyokuwa na huzuni katika maisha yetu kabla ya kutwaliwa na Bwana wetu mpendwa. Kama ambavyo hakuna kitu kibaya zaidi ya kondoo kuwa bila ya mchungaji mzuri, vivyo hivyo mambo yote yalikuwa ubatili na kufa moyo kabla hatujaokolewa. Hatukuwa na mwelekeo maalum, na ule mwelekeo tuliokuwa nao ulikuwa unatupeleka kwenye giza na kifo. Lakini sasa, kwa kuwa mwanga wa wokovu umepambazuka juu yetu katika Bwana Yesu Kristo, tunaye Mchungaji Mwema, kwa hakika Mchungaji mtimilifu kabisa (Zab. 23:1ff; Zab. 80:1; Isa. 40:11; Eze. 34:11-16; Matt. 2:6; Luka 12:32; Yoh. 10:11-16; Waebr. 13:20; 1Pet. 5:4; Ufu. 7:17). Wakati wote Yeye alikuwa ndiye Mchungaji wetu stahiki, baada ya kuwagharamia watu wote kwa damu Yake katika kufa kwa ajili ya dhambi zetu msalabani. Na sisi, ambao ndio kusanyiko Lake “tumegeuka” kwa hakika kutoka ulimwenguni na kutoka katika ile njia pana inayoelekea kwenye laana na badala yake kumfuata Yeye ambaye anatutakia mema wakati wote (War. 8:28). Yeye ndiye anayetulea wakati wote, na Atasimamia maisha yetu mpaka mwisho, mpaka siku ile ya mwisho tutakapomwona Mwokozi wetu mpendwa Yesu Kristo uso kwa uso [hatimaye].

Kwani huyu ndiye Mungu, Mungu wetu milele na milele. Atakuwa kiongozi wetu, hata kifo chetu.
Zab. 48:14 SUV

15 Ina thamani [kuu] machoni pa Bwana, Mauti ya wacha Mungu wake.
Zab. 116:15

4.18  Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina.
2Tim. 4:18 SUV

Hivyo haijalishi nani ni mfalme wetu wa sasa wa hapa duniani (au mchungaji) au ‘bosi’ wetu kazini kwetu, au msimamizi wetu ni nani: Yeye ambaye ndiye anaendesha maisha yetu sasa na milele ni Bwana Yesu Kristo – na imetupasa kuishi maisha yetu ya sasa kwa kuutambua ukweli huo, tukivumilia katika namna inayomfurahisha Yeye mateso yoyote ya Kristo tutakayoitwa kuyashiriki … bila kukata tama kamwe.

12.2  tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
12.3  Mtafakarini sana Yeye (Bwana wetu) aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya waliotenda dhambi [dhidi ya nafsi yake] msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu [na kukata tamaa].
Waebr. 12:2-3

=0=

Translated from: A Christian Code of Conduct: Peter’s Epistles #34.

=0=

Basi na tuonane katika somo #35 la mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!