Kumfuatisha Bwana Yesu Kristo: Nyaraka za Mtume Petro #17
Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa: https://ichthys.com
Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo
Ruksa ya Tafsiri Hii ya Kiswahili Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for This Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill
Kupevuka Kiroho ni Lazima Ili Kuishi Kama Kristo: Kufuatisha maisha ya Kristo kunataka tutembee kama Kristo alivyotembea. Kumfuatisha Kristo hakuwezi kufanikiwa bila kufikia kwanza kiwango cha kupevuka kiroho, na kwa upande mwingine kukua kiroho hakuwezi kufikiwa bila ya uelewa wa kina na kutumia kila wakati maadili ya maandiko katika maisha yetu. Maadili ni ile kweli, iliyochakatwa kutoka katika maandiko na kutumiwa na kila mmoja wetu. Yote tunayoyajua, yote tunayoyaelewa, yote tunayoyaamini kuhusiana na kweli za Biblia lazima yakusanywe pamoja katika mienendo ya kufikiri ambayo polepole inakuwa kawaida yetu ya kufikiri ikifuatiwa na namna tunavyoongea na namna tunavyoenenda pia. Hatujaachwa pekee katika lengo hili la kuelekea upevu wa kiroho na kufikia kiwango cha maisha cha kufikiri na kuenenda kwa uadilifu wa Kibiblia. Mungu ametupatia mtandao mpana wa msaada katika Kanisa, mfano wachungaji, wazee, waalimu, n.k.; lakini sio hao tu wanaotusaidia; tumepewa pia historia ya Bwana wetu Yesu Kristo, maisha yanayodhihirisha uadilifu wake Bwana wetu:
4.11 Naye [Kristo mwenyewe] aliwateua wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;
4.12 kwa kusudi la kuwakamilisha [kuwatayarisha] watakatifu [wote], hata kazi [yao] ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo [Kanisa Lake] ujengwe;
4.13 hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo [kiwango cha kupevuka ambacho kipimo chake ni Kristo];
4.14 ili tusiwe tena watoto wachanga [katika kuelewa kanuni za Biblia], tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.
4.15 Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.
4.16 Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili [Kanisa] upate kujijenga wenyewe katika upendo.
Waefeso: 4:11-16 SUV
Kristo Mfano Wetu: Maisha ya Mkristo, kutembea Kikristo, kunadhihirishwa na maadili yanayofundishwa katika Biblia. Tumesema kwamba upendo unajumuisha maadili haya yote, na kwamba maisha ya upendo uliotimilika yatakuwa ni ya kimaadili kabisa. Maisha kama hayo yalikuwa ni ya Bwana wetu Yesu Kristo. Katika maisha yake ya hapa duniani, alijumuisha na kuonyesha upendo wa Mungu, na kwa mfano wake mwenyewe, akikabiliwa na magumu kama tunayokabiliana nayo sisi (lakini/japo ni kwa kiasi kikubwa na kikali zaidi – Waebrania 4:15), alitupatia mwelekeo ambao sisi tunaweza kuufuata/kuuiga, nyayo za miguu Yake, ambazo kama tukiweza kuzifuata, tutaongozwa kwa njia iliyonyooka kuelekea kwenye maisha ya maadili, yanayomfurahisha Mungu (1Pet. 2:21-25; cf. Matt. 16:24; Yoh. 13:15).
Biblia ni ushuhuda juu ya Bwana Yesu Kristo (Yoh. 5:39), ushuhuda wa upendo wa Mungu unaodhihirishwa na Zawadi yake aliyotupatia, Mwana wake Yesu Kristo (Yoh. 3:16), kwani upendo unatoka kwa Mungu, na Mungu ni upendo (1Yoh. 4:7-8). Kwa maana hii basi, kila ukurasa wa Biblia unaakisi hulka ya Mungu na upendo wa Kristo, nasi tunapaswa kuwa na mtazamo huu tunaposoma maandiko. Kupevuka kiroho, kama tulivyoona, ni mchakato wa mabadiliko, na lengo kamilifu la mchakato huu ni muundo wa hulka ya Bwana Yesu Kristo ndani ya kila mmoja wetu (Wagal. 4:19). Ili kufanikisha lengo hili kuu, tunahitaji “kumfuatisha Kristo” (1Wakor. 11:1), na “kujivika Bwana Yesu Kristo” (War. 13:14) mpaka “Akae mioyoni mwetu” (Waefe. 3:16-17). Muktadha (context) wa kila aya hapa juu unaonyesha kwamba muundo huu wa hulka ya Kristo ndani yetu ni sehemu ya mabadiliko ya fikra zetu tunayoyazungumzia hapa. Katika 1Wakorintho 11:1, amri ya “kumfuatisha (kumu-iga) Kristo” inatolewa kwa maana ya kujitoa mhanga/sadaka, maana ya kuwajali wengine zaidi yetu sisi wenyewe katika kukua kiroho (1Wakor. 10:23-33). Amri ya “kujivika Kristo” katika Warumi 13:14 inatolewa katika maana ya kukataa maovu ya hulka yetu ya dhambi ili tuweze kuenenda kiroho kwa namna stahiki na njema. Mwisho, sala/ombi la Paulo kwa Kristo “akae mioyoni mwetu” (Waefe. 3:16-17) linafanikishwa “kwa imani” na sala hiyo inategemea kwamba “tumekwishatiwa nguvu mioyoni mwetu kwa njia ya Roho wake”, mchakato ambao kama tulivyoona unahusisha kurekebisha fikra zetu kwa misingi ya kweli kama inavyofundishwa katika Neno la Mungu. Kuiga tabia/moyo wa Bwana wetu inawezekana tu pale tunapoanza kufikiri kama Yeye alivyofikiri, tukiweka maslahi ya kiroho ya wengine mbele ya maslahi yetu, kuyakataa matakwa ya hulka yetu ya dhambi, na kugeukia Neno na Roho Mtakatifu kwa ajili ya kutiwa nguvu.
Kristo Mfano Wetu Katika Unyenyekevu: Kama tuna nia ya kweli ya kubadilisha fikra zetu, mmoja kati ya mipangilio ya kufikiri ambao tunapaswa kuuimarisha toka mwanzo kabisa ni ule wa unyenyekevu. Kama “tutamfuatisha Kristo” (1Wakor. 11:1), tunapaswa kuendeleza mtazamo wa unyenyekevu (kutotaka makuu) aliokuwa nao Yeye. Majivuno, kujikweza, kuweka nafsi juu ya mambo mengine yote, ilikuwa ndiyo dhambi ya kwanza ya Shetani na Adamu pia (Isa. 14:13-14; Mwa. 3:6). Kiburi, au ufidhuli, ni kinyume cha kujitoa mhanga na kuwajali wengine kwa upendo ambako kunahusiana kwa ukaribu na ule uadilifu wa unyenyekevu. Unyenyekevu ni fikra adilifu, hali ambayo tunatakiwa kuwa nayo wakati wote, na mfano wa tabia hii ni Bwana Yesu Kristo mwenyewe:
2.5 Kuweni na mwelekeo [fikra/mtazamo] ndani ya mioyo yenu ambao Kristo alikuwa nao ndani Yake;
2.6 Yeye ambaye hapo mwanzo alikuwa yu na namna ya [uwepo wa] Mungu, naye hakuona kuwa kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kushikamana nacho;
2.7 Lakini licha ya hadhi hii [ya usawa na Mungu aliyokuwa nayo], alijinyima hadhi Yake hii na kutwaa namna ya mtumwa, na akawa katika mfano wa mwanadamu;
2.8 Tena alipoonekana kama mwanadamu, alijinyenyekeza na akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Wafi. 2:5-8 SUV.
Mfano huu anaoutumia Paulo, wa kujitoa mhanga kwa Kristo katika upendo wake kwetu sisi, ni mfano mzuri kwetu; je, waweza kulinganisha kujitoa huku kwake na shida [ndogo ndogo] tunazopata sisi katika maisha yetu ya kila siku? Wakati neno ufidhuli (katika etimolojia yake) linamaanisha kujitakia (kutoka kwa watu) heshima ambayo hatustahili, Kristo alikuwa na haki zote za kuabudiwa kama Mungu – kwani Yeye ni Mungu. Lakini katika upendo mkuu, alijitoa na kuwa mtumwa kwa ajili yetu na kufa kwa ajili yetu. Tukiwa Wakristo ambao tunakubaliana na msingi wa kumfuata Bwana wetu, tunapaswa “kufikiri na kuenenda kimaadili” kama Kristo alivyofanya, na kuendelea na mtazamo wa unyenyekevu. Yawezekana hatutolazimika kutoa uhai wetu kwa ajili ya wengine, lakini tunapaswa kuwa na mtazamo kwamba Bwana Yesu Kristo alikufa kwa ajili ya wengine na kwa ajili yetu pia. Kama Mchungaji wetu Mkuu, alitoa mhanga uhai wake kwa ajili yetu, basi nasi tuna wajibu angalau wa kuishi na wenzetu kwa uvumilivu na kusamehe. Mwenendo wa huduma kwa wengine badala ya ubinafsi ni sehemu muhimu katika mchakato wa fikra adilifu. Unyenyekevu, basi, ni moja kati ya maadili au mwenendo ambao ni tabia ya kila siku ya Mkristo aliyepevuka. Kukosekana kwa unyenyekevu au kuwepo kwa kiburi (na majivuno) ni dalili kwamba Mkristo huyu hajaweka akili yake katika misingi ya kweli, hatimizi amri ya kumfuatisha Kristo, na kufikiri kimaadili.
Kristo, Mfano Wetu Katika Majaribu: Tunapoanza juhudi za kubadilisha mtindo wa maisha yetu kwa kubadilisha fikra zetu, tusisahau kwamba Ibilisi na umati wa watumishi wake hawakai tu na kututizama tukipiga hatua chanya katika maendeleo yetu ya kiroho bila ya wao kutupinga vikali. Kama vile Kristo alivyoyakabili majaribu ya Shetani kule nyikani kwa misingi ya Biblia (Matt. 4:4-19), vivyo hivyo nasi tunapaswa kuwa tayari wakati wote. Hii haina maana kuwa tunapaswa kuwa na aya ya maandiko kwa kila tukio la maisha, bali ni kwamba hii tabia au desturi ya kuelekeza fikra zetu kwenye uadilifu tuliojifunza kuiga kutoka kwa Bwana wetu itatusaidia sana katika saa yetu ya majaribu kama ilivyokuwa kwake. Zaidi ya hapo, mitihani na majaribu siku zote ina sehemu mbili: tukio la nje/la kimazingira ambalo linaleta shikizo, na yule rafiki ya Shetani ambaye siku zote humsaidia katika kutuangusha chini, yaani hulka yetu sisi wenyewe ya dhambi.
Kufaulu mitihani na kushinda majaribu ambayo humkabili kila muumini katika maisha yake (na kwa kweli ni sehemu muhimu katika kupiga hatua kiroho) kunapaswa kutazamwa kwa namna mbili. Kwanza, kufaulu/kufanikiwa katika mtihani mgumu ni dalili ya maendeleo, kwani umefaulu kuwa mfuasi wa Bwana licha ya shinikizo. Pili, mwenendo huo ni kupinga na kushinda hulka yetu ya dhambi ambayo tabia yake ni kwenda kinyume na matakwa ya Mungu. Ikiwa “tutajivika Kristo” (War. 13:14) na kuenenda kama Yeye alivyofanya kule nyikani, ni lazima wakati huo huo “tumvue yule mtu wa kale” (hulka yetu ya dhambi) ambaye hutushawishi kufuata tamaa zetu badala ya matakwa ya Mungu (Wakol. 3:9-10). Tunapaswa kuelekeza macho yetu kwenye kweli ya Neno la Mungu, na hilo ndilo jambo muhimu katika fikra adilifu.
Ni lazima tujifunze kuyaona na kuyaelewa matukio ya maisha yetu kwa kutumia misingi ya kweli ambayo Mungu ametupatia tuifanamu na kuitumia. Kwa maneno mengine, tunapaswa “kuyasoma” na kuyaelewa mazingira tuliyomo kwa kutumia kanuni za Neno la Mungu, lengo likiwa ni kuipata dira au mwelekeo ambamo humo tutapita kwa uadilifu hapa duniani. Kama Shetani alivyojaribu kuivuruga kweli wakati wa majaribu ya Bwana wetu kule nyikani, vivyo hivyo ameunda mfumo wa kidunia wenye vurugu, vishawishi, vivutio vyenye lengo la kuwapotezea watu mwelekeo, na magumu ili yatupotoshe kutoka kwenye ukweli. Kristo alifaulu mitihani yake kwa kuelekeza akili yake kwenye Neno na matakwa ya Baba Yake. Alipojaribiwa na Shetani kule nyikani, Kristo aliyajibu majaribu ya Shetani kwa kutumia kweli. Ili nasi tumfuatishe Bwana wetu katika wakati wetu wa majaribu, tunapaswa kufanya hivyo hivyo, na ili tuweze kukabiliana na hali yoyote kwa kutumia ile kweli, tunapaswa kwanza kuwa tunafikiri kwa misingi ya kweli. Haiwezekani kuanza kusoma Biblia baada ya kupata magumu! Ili tuwe na ufanisi siku hadi siku hapa katika himaya ya Shetani, ni lazima tuwe na kweli ya Mungu ambayo tumeiweka mioyoni mwetu katika mfumo unaoweza kutumika mara moja. Ni lazima tuwe na tabia ya kutafakari maadili ya maandiko (yaani misingi ya mwenendo sahihi/adilifu na mtazamo sahihi) wakati wote.
Kristo Ndani ya Mioyo Yetu: Ni baada ya “kutiwa nguvu yule mtu wa ndani yetu” ndipo tunafanikisha ndani ya nafsi zetu ule uelekeo wa macho yetu kwa Bwana wetu ambapo inaweza kusemwa kwamba “Anakaa ndani ya mioyo yetu” (Waefe. 3:16-17). Mchakato huu wa kutiwa nguvu (kama Waefeso sura ya 3 inavyofundisha) unafanikiwa kwa njia ya imani, kwa msaada wa Roho Mtakatifu, na msingi wake ni “upendo”. Mtiririko wake uko wazi: kukua kwa imani na upendo (kwa msaada wa Mungu) kunatia nguvu ule mchakato wa kukua kiroho mpaka tunafikia kiwango cha Kristo kuwa kila kitu kwetu. Hivyo, kukomaa kwa nafsi zetu kiimani hakuwezi kutenganishwa na maendeleo ya uadilifu, tafakuri juu ya uadilifu, na kutumia uadilifu katika maisha yetu. Ndipo hapo tutakapokuwa na matumaini ya kufika pale mahala ambapo, kama Mtume Paulo, Kristo anakuwa katikati ya maisha yetu, na kuingia katika uzima wa milele ni faida kwetu (Wafilipi 1:21). Ili tuwe aina ya Wakristo ambao Mungu wetu anafurahishwa nao, tunahitaji kukua wakati wote ili kwamba tufikie kiwango hiki cha kupevuka ambapo macho yetu yatakuwa yanaelekezwa kwa Bwana Yesu tu, na kukaribia kile kiwango chake cha kutembea kwa uadilifu.
Mbinu za Fikra Adilifu: Maandiko yana mifano mingi ya waumini ambao mwenendo wao adilifu unaonekana kuwa ni MKUU na ni vigumu kufikia kiwango chake. Ni Mkristo gani ambaye hataki kuwa na SUBIRA ya Ayubu, FURAHA KATIKA BWANA ya Daudi, IMANI ya Danieli, au AMANI ya Paulo? Maadili haya na mengine yanaweza kufikiwa na kila mmoja wetu. Lile “wingu kubwa la mashahidi” wa kale (Waebr. 12:1) walikuwa na uwezo wa kupenyeza uono wao hadi ukavuka ukungu wa maisha ya duniani na kuona mbali zaidi ya hapo kwa macho ya IMANI. Waliweza kuwa na subira, imani, furaha na amani kwa sababu “waliona” ile taswira kuu na bora iliyoko mbele ya mateso na masikitiko ya maisha ya sasa, kwamba hofu na vurugu za maisha haya ambazo wakati wote zinatupiga vita na kutupotezea mwelekeo ni mambo ya kupita tu, na kwamba ule uwepo wa Mungu, uwepo wa makazi yetu ya milele ijayo, wajibu wetu wa kiraia katika makazi hayo ya milele, unazidi kwa kiasi kisichopimika matatizo yetu ya hapa duniani. Mtazamo huu uko wazi kwa waumini wote, lakini hautokei wenyewe na hautowezekana kwa urahisi tu. Inataka juhudi za makusudi kuzitumia fikra adilifu tunazojifunza katika maandiko. Kwa lengo hilo, ebu basi tutizame misingi michache hapa:
1. Dira: Kama tunajaribu kuvuka msitu mnene kwa kutumia ramani, maelekezo yaliyo katika ramani hiyo yatakuwa na faida kidogo sana ikiwa hatuwezi kujua kaskazini ni wapi ili tuweze kuisoma kwa usahihi; ukishajua kaskazini ni uelekeo upi ndipo utaweza kuiweka ramani yako katika uelekeo stahiki na utajua mahali ulipo, na hivyo utajua uelekee wapi ili ufike ng’ambo ya msitu. Kwa namna hiyo hiyo, maadili yanayofundishwa katika maandiko yanatumika kama dira ya ndani ya mioyo yetu. Yanatusaidia katika kutupatia mwelekeo katika maisha yetu ya hapa duniani, yakitengeneza daraja linalounganisha kweli ya Biblia na mazingira yanayotukabili. Kabla ya kuchambua maadili haya moja baada ya lingine, ebu tukumbuke kuwa maandiko yanatupatia miongozo ya maadili ili iwe dira ya fikra zetu katika kuelekea kwa Mungu na mapenzi Yake:
• Tupeleke fikra zetu kwa mambo ya mbinguni na siyo ya duniani (Wakol. 3:2; Wafi. 3:19-20; 4:8).
• Tuache kujiona bora kuliko wengine, tuwe na mtazamo wa unyenyekevu (War. 12:2-3).
• Tuweke fikra zetu katika mambo yanayowaunganisha waumini wenzetu, siyo yale yanayowatenganisha (War. 12:16; 15:5; 2Wakor. 13:11; 1Pet. 3:8).
• Fikra zetu ni lazima zifanane na zile fikra za Baba, siyo za mwanadamu na za Shetani (Matt. 16:23).
• Fikra zetu ziwe kama za Mwana, na siyo kama za wabinafsi (Wafi. 2:2-4).
• Fikra zetu ziwe kama za Roho Mtakatifu, na siyo za kimwili (War. 8:6).
• Fikra zetu ziwe kama za watu waliopevuka, siyo kama za watoto (1Wakor. 13:11; Wafi. 3:15).
Haya ni maelekezo ya wazi kabisa ambayo yanaonyesha uelekeo stahiki wa fikra zetu kama Wakristo. Kuyaweka maelekezo haya katika akili zetu kwa imara kutatusaidia kuwa na hakika na dira yetu, tukitafakari juu ya yale yanayomfurahisha Mungu na kwenda mbele kwa kuutumia ule uelekeo adilifu na sahihi.
2. Kuendelea Mbele kwa Maadili: Mara nyingi kuitizama picha iliyokuzwa na ikawa kubwa sana ni vigumu. Kama tulivyoona, maadili yote yanajumuishwa na kuwa amri moja, ya UPENDO (upendo wa Mungu kwetu sisi unaodhihirishwa na Bwana Yesu Kristo na itikio la wito wa upendo kwa upande wetu, kwake Yeye na kwa viumbe wake), na Biblia yote inaweza kuchukuliwa na kuwa ni uwanja wa mafunzo kwa ajili ya ile fikra adilifu kuu: UPENDO. Tunapoiweka hii fikra adilifu kuu kabisa katika vitendo, tunaona kwamba sisi wanadamu wenye mapungufu na wenye uelewa/ufahamu mdogo tunahitaji mambo yanyumbulishwe hatua kwa hatua ndipo tuelewe kwa usahihi. Hii huwa wazi zaidi katika hatua za mwanzo za kukua kiroho. Tunaweza kupata msaada wa mwanzo katika shauku yetu ya kulielewa hili kwa undani zaidi katika barua ya pili ya Petro ambamo anatupa orodha ya baadhi ya maadili ya msingi kabisa ya Mkristo. Petro anatupangia maadili haya, si kwa umuhimu wake kutoka juu mpaka chini, bali kwa mpangilio/orodha ya mwendelezo wake asilia, kama vile matofali ya kujengea yanavyopangwa, kila moja likiwa ni msingi wa tofali linalofuata juu yake, nalo pia likitegemea tofali lililotangulia …:
1.5 Na kwa lengo hilo hilo, pamoja na imani yenu, kwa ari kuu endelezeni wema na ufahamu/maarifa, na pamoja na ufahamu/maarifa [wa/ya kanuni za Biblia], kiasi [kujitawala nafsi]; 1.6 Na pamoja na kiasi, saburi [uvumilivu], na pamoja na saburi, uchamungu (utauwa); 1.7 Na pamoja na uchamungu, endelezeni upendo kwa ndugu zenu, na pamoja na upendo kwa ndugu, endelezeni upendo. 1.8 Maana mkiwa na maadili hayo, na ikiwa mnayaongeza kila siku, yatawafanya ninyi kuwa mnaofaa na wenye kuzaa matunda, katika kumjua na kumtii kwenu Bwana wetu Yesu Kristo.
2Peter 1:5-8 SUV (nyongeza yangu ya msamiati)
Hivyo basi, mwendelezo wa maadili katika 2Pet. 1:5-8 umepangwa kama ifuatavyo: imani, wema, ufahamu/maarifa ya Neno, kiasi/kujitawala nafsi, saburi/uvumilivu, uchamungu, upendo kwa ndugu, na upendo. Maadili haya siyo kwamba yanasimama kila moja peke yake, bali yanaingiliana kwa kiasi fulani. Hata hivyo, mwendelezo anaotupatia Petro una maana nzuri na unatusaidia katika kuelezea namna tunavyoweza kujijenga kuelekea kwenye maisha adilifu ya Kikristo. Hata katika ile “orodha fupi” ya Paulo (1Wakor. 13:13), orodha ya mwendelezo wa uadilifu inaanza na IMANI na inaishia na UPENDO.
• Imani, tegemeo thabiti kwa Mungu Baba na Mwanaye, Bwana wetu Yesu Kristo, ndio mwamba ambao juu yake kukua kote kunajengwa. Tunapaswa kwanza kumwamini Yeye, kumwamini Mwanaye na kazi aliyoifanya Mwanaye ya kuwezesha wokovu wetu, katika unyofu wa maneno Yake na katika ukweli wa ahadi Zake kwetu za ufufuo na thawabu, ili tuweze kufanikisha maendeleo ya kiroho (Waebr. 11:6).
• Wema (morality) ni tafsiri inayofaa ya neno la Kiyunani arete kama Petro anavyolitumia katika muktadha huu. Japokuwa kwa kawaida hutafsiriwa kama “uadilifu” au “ubora”, katika Thucydides (mwandishi wa historia wa kale wa Kiyunani) na waandishi wengine, neno hili linamaanisha “kilicho sahihi na kinachofaa” katika mazingira fulani. “Kufanya kilicho sahihi” ndio ubora unaomaanishwa na Petro hapa, na dhana yetu ya unyoofu, mwenendo adilifu (katika maeneo yote ya maisha) ndiyo kinachomaanishwa hapa.
• Maarifa yanafuata katika orodha ya Petro. Mara baada ya kujifunza kumtegemea Mungu na Kristo, na “kusafisha maisha yetu”, hatua inayofuata ni kupanua uelewa, ufahamu na elimu ya mafundisho na misingi ya Neno la Mungu. Hii haina maana ya kwamba tusitafute maarifa haya tangu mwanzo, bali inamaanisha kwamba tunasisitizwa juu ya umuhimu wa kuimarisha kiasi fulani cha uadilifu katika maisha yetu mara baada ya kuweka imani yetu katika Kristo: tunapaswa kuweza kufanya marekebisho ya msingi katika mwenendo wetu ambayo hata akili ya kawaida tu inatuonyesha kwamba hayaendani na mwenendo wa Kikristo. Maendeleo endelevu ya kiroho, lakini, yanahitaji kiasi kukubwa cha misingi ya maarifa katika Neno la Mungu, ambayo tunalishwa kutoka katika chanzo cha Neno la Mungu.
• Kiasi/kuitawala nafsi ni muhimu sana katika maendeleo ya mwenendo stahiki wa Kikristo, hata Mtume Paulo alifanya fundisho hili kuwa ni moja kati ya mafundisho muhimu ya Injili aliyompatia Felix (pamoja na mafundisho ya uongofu na hukumu inayokuja: Matendo 24:25). Kiasi au kuitawala nafsi ni tafsiri ya neno la Kiyunani engkrateia, na katika Agano Jipya linatumika kumaanisha taswira/pande zote zinazohusika katika kuidhibiti hulka yetu ya dhambi pamoja na tamaa na uchu wa hulka hiyo wa namna nyingi. Neno hili lina wigo mkubwa, kutoka dhambi za ulimi/maneno na mawazo mpaka dhambi za wazi [na zile] zilizo nzito. Japo tumeokolewa, bado tungali na hulka ya dhambi ndani ya miili yetu hapa duniani, na hivyo ni katika kuwa na msimamo thabiti katika kuitawala nafsi ndipo tunaweza kujiweka mbali na aibu na matatizo mengi yanayoambatana na dhambi, na kuwa na matumaini ya kufanya maendeleo katika uadilifu na kupevuka kiroho.
• Uvumilivu/saburi ni sifa ambayo tunaihitaji sana katika majaribu ya maisha yetu ya Kikristo (Yak. 1:3-4; Waebr. 12:1). Na mara tu baada ya kuanza kuishi maisha mema ya Kikristo tukipiga hatua katika kujifunza juu ya Mungu wetu na matakwa Yake kwa maisha yetu na wakati huo huo tukijitahidi katika kutawala mwenendo wetu, tutegemee kufanyiwa majaribu na mitihani. Uvumilivu na matumaini ni maadili yanayohusishwa kwa karibu sana na Mtume Paulo (Warumi 8:25), na katika uvumilivu (ambao maana yake halisi ni “kukaa chini ya” shinikizo la mtihani), tunakuwa karibu sana na uadilifu wa tumaini katika orodha ya Petro. Uvumilivu/saburi ni kushika imani na mwendo wetu (kama vile kuendelea kujifunza Neno la Mungu) hata katika wakati ambao shinikizo na mtihani vinazidi. Tumaini ni upande wa pili wa sarafu ambayo upande wake wa kwanza ni uvumilivu. Tegemeo la uhakika kwamba baada ya kifo tutakuwa na Bwana milele, kwamba tutapitia ufufuko uliotukuka kutoka katika mwili huu wa sasa ulio dhaifu, na kwamba tutapata thawabu kwa ajili ya utumishi wetu na uaminifu kwa Bwana wetu tunaouonyesha katika maisha yetu ya sasa hapa duniani, yote yanachangia katika kutupa mtazamo unaovuka wakati wa sasa na badala yake unayapeleka macho yetu yaone uhalisia wa milele ambao una mng’ao kuliko magumu ya sasa. Hili ndilo tumaini linalotupa nguvu ya kuvumilia na kustahamili.
• Uchamungu (utauwa katika SUV) ni uadilifu mwingine wenye maana mahususi katika muktadha (context) huu. Neno uchamungu tunalitoa kwenye neno la Kiingereza “godliness”. Lakini Petro aliandika nyaraka zake kwa Kiyunani. Hivyo tutatumia historia kidogo katika kunyumbulisha neno hili uchamungu/utauwa. Wayunani waliamua kumpa majina ya sifa mfalme wao Octavian, wakamwita eusebeia na “Augustus” yaliyo na maana moja katika etimolojia zake, na yanahusiana na dhana ya heshima kuu, kutukuza, kuabudu. Hivyo basi, katika maana yake halisi neno “uchamungu” halimaanishi “uungu” [hakuna maana ya neno “Mungu” katika neno “uchamungu” - godliness], bali linamaanisha uchaji Mungu, ibada au kuabudu. Sasa, lenye uzito zaidi hapa ni “uchaji Mungu” (pious, piety kwa maneno mengine ya Kiingereza). Katika Kirumi, kwa mfano, kuwa pius, ni kutimiza wajibu wako kwa familia, nchi yako na miungu (Warumi walikuwa wapagani). Hivyo basi, kutimiza wajibu wako, mahususi katika utumishi ambao msingi wake ni kipaji au vipaji ambavyo Roho Mtakatifu alikupatia wakati unazaliwa upya, ni sehemu kubwa ya anachomaanisha Petro hapa katika mwendelezo wa maadili. Mara baada ya kujenga maisha ya Kikristo yenye mwenendo wa imani, unyofu, kujifunza Biblia, kuitawala hulka yetu ya dhambi, na kuendeleza uwezo wetu wa kuhimili majaribu ya maisha, hapo unafika ule wakati wa kujitoa kwa Wakristo wenzetu katika Kanisa kwa kuitumia imani yetu kivitendo; yaani kwa kutoa huduma (utumishi) kwa njia ambayo Mungu ametupatia. Haya yanakuwa ndiyo matumizi stahiki na ya ki-uchamungu (ki-utauwa) ya maadili baada ya kufikia hatua hii ya kukua.
• Upendo kwa ndugu katika Bwana (philadelphia, katika Kiyunani, yaani upendo kwa Wakristo wenzetu) na upendo (agape, katika Kiyunani, yaani upendo wa Kikristo kwa watu wote) ndiyo maadili mawili ya mwisho katika orodha yetu. Inatia shauku kujua kwa nini Petro amegawa upendo katika sehemu hizi mbili. Hii inamaanisha kuwa, japokuwa tunapaswa kuwapenda watu wote, kipaumbele chetu kama Wakristo ni kuwapenda Wakristo wenzetu kwanza. Hii haina maana ya kwamba sisi Wakristo tuwe wachoyo au wabinafsi katika huduma zetu za Kikristo kwa wasioamini, bali kwamba tuna ulazima wa kuijali “familia yetu ya kiroho kwanza”. Hivyo, kama ule uadilifu mkuu, upendo-agape unatawala maisha yetu, hiyo ni dalili ya uhakika ya kwamba uadilifu wa aina nyingine nao upo na unafanya kazi.
Petro anakamilisha orodha yake kwa kusema kwamba kama tunayo na tunayakuza maadili haya yote, basi tutakuwa wenye mafanikio na wenye kuzaa matunda katika kumjua kikamilifu Bwana wetu Yesu Kristo (2Petro 1:8). “Kumjua kikamilifu” kunakozungumziwa hapa kunatokana na neno la Kiyunani epignosis, ambalo linamaanisha zaidi ya kujua (gnosis) kutoka katika orodha hapo juu: epignosis inamaanisha elimu/ufahamu kamili, fanikishi, elekevu; kutambua, kutii, kuelewa kikamilifu ambako kunakuwa ni msingi wa matendo au mwenendo unaofuata, kwa maneno mengine, matumizi adilifu ya ufahamu wa maandiko tulio nao.
3. Imani, tumaini na upendo: Orodha maarufu ya Paulo ya maadili ya msingi katika 1Wakor. 13:13 inahusisha imani, tumaini na upendo. Kama ilivyo kwa orodha ya Petro, orodha ya Paulo pia ni endelevu. Upendo ndio ile amri kuu, lakini, katika utendaji wake, huwezi kufanikisha fikra adilifu ya upendo bila kukua kiroho, yaani kuendeleza na kukuza kwanza imani na matumaini. “Mambo haya matatu” ndiyo ambayo Paulo anatuambia yatabakia kwetu baada ya vile vipaji vya kustaajabisha, vya shani, vya kipindi kile cha Mitume wa Bwana Yesu cha waanzilishi wa Kanisa Lake kupita na vipaji vile kukoma (1Wakor. 13:8-10). Sisi, Mwili wa Kristo, tunakuwa na maadili badala ya maajabu na shani za kunena kwa lugha za kigeni, uponyaji, unabii na mengineyo. Ni maadili, yatakayodhihirishwa kimatendo na kila Mkristo ndiyo yatatutambulisha sisi kuwa ni Wakristo mpaka tutakapomwona uso Wake pale atakaporudi:
• Imani ndiyo jicho la maisha yetu mapya ya Kikristo ambalo litatuongoza katika njia yetu tuliyopewa na Mungu tupite katika maisha yetu (2Wakor. 4:18; 5:7). Kama waumini wa Bwana Yesu Kristo, tunategemea, tunatumainia, tuna imani kwamba yale tuliyoahidiwa na Mungu ni kweli licha ya kwamba dunia inashuhudia kinyume chake/tofauti (1Wakor. 1:21). Dunia wakati wote inahujumu imani yetu, lakini sisi tunaziamini ahadi tulizopewa na Mungu (2Wakor. 7:1). Tunaamini kwamba dhambi zetu zimesamehewa na Mungu kwa sababu Kristo alikufa kwa ajili yetu kwa maondoleo ya dhambi hizo. Tunaamini kwamba kwa imani yetu Kwake na katika kazi Yake tutaishi milele. Tunaamini kwamba mwili huu tulio nao ni wa muda tu, hivyo utabadilishwa, japo kwanza utarudi kuwa [ma]vumbi, na utakuwa mwili wa utukufu, utakaoishi milele, ambao hautaharibika kamwe. Tunaamini kwamba huzuni, machozi na magumu ya maisha haya yatakwisha kabisa katika uhai wa milele unaokuja (Ufu. 21:4). Tunaamini kwamba Kristo ameenda kabla yetu kutayarisha mahala kwa ajili yetu ili tuwe Naye milele – Yoh. 14:2-3. Tunaamini haya yote na zaidi ya haya kwa sababu Mungu ametuahidi hivyo (Waebr. 11:6). Tunaamini katika hulka Yake, na katika ukweli, unyofu wa Neno lake. Licha ya mapigo ya maisha, tunaendelea katika imani, tunaijenga imani yetu, na tunajaribiwa kwa mitihani ambayo ina matokeo ya kututia nguvu (Yak. 1:2-4; 1Peter 1:6-7). Tunaijua kweli, si kwa sababu tunaweza kuipima hesabu yake, si kwa sababu tunaweza kuithibitisha, si kwa sababu tunaweza kuonyesha uhakiki wa kisayansi – kwa kweli ni kinyume kabisa na hayo (Waebr. 11:1). Imani yetu ndiyo uhakiki pekee tunaouhitaji, siyo kwamba inajitosheleza, bali ni kwa sababu msingi wake ni hulka ya Mungu mwenyewe (1Pet. 1:21). Tuna imani – kwa Mungu, kwa Bwana Yesu Kristo mwanawe, na katika ahadi tulizopewa zilizo katika maandiko. Imani inatupa nguvu ya kuhimili masikitiko na maumivu ya maisha, kwani tunamtegemea Mungu, kwamba anapanga kila tukio la maisha yetu kwa faida yetu (Warumi 8:28).
• Tumaini huchanganyika moja kwa moja na imani pale mioyo yetu inaponyoosha mikono na kukumbatia maisha matakatifu, yasiyoonekana, ya baadaye, ya milele ambayo Mungu wetu ametuahidi. Kama vile imani inavyoweka tegemeo (na tumaini) katika nafsi na hulka ya Mungu na Mwanaye Bwana Yesu Kristo, vivyo hivyo tumaini linaelekeza macho ya tegemeo hilo katika milele ijayo, katika ahadi za kustaajabisha za maisha ya milele ijayo. Mwanga wa matumaini unapasua giza la masikitiko, na kuelekea kwenye furaha isiyoelezeka ya kuwa pamoja na Bwana wetu milele tukiwa katika mwili mtimilifu, pamoja na watakatifu wote. Tumaini ni jicho la ile imani yetu ambalo uono wake unapenya mpaka milele ijayo na kutuhakikishia uwepo wa maajabu haya yasiyoonekana kwa sasa (War. 8:23-25). Tumaini letu si ndoto ya Alinacha, bali ni uhalisia usioonekana kwa sasa, nasi tuna shauku ya kuondoka duniani na kufufuka katika ule mwili mpya ambao tutakuwa nao milele pamoja na Bwana wetu (2Wakor. 5:1-9), hatutafuti mali za kupita za dunia hii, bali, kama Musa, tunapeleka macho yetu kwenye thawabu ambayo Mungu atatupatia (Waebr. 11:26). Tumaini hili letu, kujiamini kwetu kwamba Mungu atatutimizia ahadi hizi zote za kustaajabisha, linaweka fikra zetu katika mbingu, ambako Bwana wetu ametangulia kututayarishia kila kitu (Waebr. 6:18-20; Yoh. 14:2-3).
• Upendo, katika mwendo wetu kuelekea upevu, unajengwa katika msingi wa tumaini (Wakol. 1:4-5). Tukiwa na imani kamilifu katika Mungu wetu, macho yetu yakielekezwa kwa uthabiti katika ule uhalisia wa milele, tuko tayari kumfurahia na kumpenda Bwana wetu kwa nafsi yetu yote, na kuwapenda wengine pia (Matt. 5:14-16). Kwetu sisi, upendo unaanza kwa Mungu (1Yoh. 4:19). Mungu ni upendo, nasi tuna uwezo wa kupenda kwa sababu Yeye ametupatia uwezo huo (1Yoh. 4:7-8). Upendo wake kwetu uko katika zawadi ya Mwanaye aliyekufa badala yetu ili tuweze kuokolewa (Yoh. 3:16). Je, sasa, yawezekana vipi tukashindwa kumpenda Yeye aliyetuokoa kutoka katika mamlaka ya dhambi katika wakati ambao tulikuwa adui zake (War. 5:8)? Kwa sababu hiyo tunasikia shukrani na furaha kwa ajili ya wokovu ambao Mungu katika rehema zake nyingi ametupatia kupitia ile sadaka ya upendo ya Bwana Yesu Kristo (Yoh. 15:13). Amri yetu kuu kama waumini wake ni kuakisi upendo huu wa ajabu ambao Mungu ametumiminia kwa sisi kuonyesha upendo huohuo kwa waumini wenzetu (Yoh. 15:12). Upendo ndio MKUU katika maadili yote (1Wakor. 13:13); upendo ndio “gundi” ya upevu ambayo inashikilia kwa pamoja maadili yote mengine na unahakikisha kwamba tunatembea kama Kristo anavyotaka tutembee (Wakol. 3:12-14).
Imani inapeleka macho yake katika uaminifu wa Mungu; katika imani tunamfuata Yeye kwa sababu tunamtegemea.
Tumaini linapeleka macho yake katika ahadi Alizotupatia; tunavumilia maisha haya kwa furaha, kwa sababu tumeahidiwa maisha mema milele.
Upendo unaona yale ambayo Mungu ametufanyia katika Yesu Kristo na unamulika shukrani hii kwa wengine; tunamtumikia Yeye na Kanisa Lake kwa sababu Yeye alitupenda kwanza.
Maadili haya matatu yasiwe mbali na mawazo yetu. Kwa kutumia maadili haya nyoyo zetu zinaweza kusogeza pembeni pazia la magumu ya maisha haya na kuona wazi uhalisia muhimu uliofichika kwa macho yetu, uhalisia wa hulka ya Mungu, ahadi zake zisizoharibika, na upendo wake usiomithilika. Imani, tumaini na upendo ndiyo mifereji ambamo wakati wote tunapaswa kupitisha fikra zetu. Maadili haya ndiyo vipimo vinavyotumika kutathmini mwenendo wetu wa Kikristo.
4. Nguzo Elekezi Katika Maisha ya Mkristo: Tunapoanza kutembea katika ile barabara nyembamba, iliyonyooka, inayoelekea kwenye wokovu (Mathew 7:14), Neno la Mungu linatupatia nguzo-elekezi zinazotusaidia kuenenda ndani ya barabara, “vizuio”, kwa lugha ingine, ambavyo kazi yake ni kutukumbusha kuendelea katika eneo la kati ya barabara, pale tunaposogea kushoto au kulia zaidi mwa barabara. Nguzo-elekezi hasi/kanushi ni yale makatazo ya wazi kutoka kwa Mungu (kwa mfano “usiibe”, Kut. 20:15); na ile nguzo-elekezi kuu chanya ni ile amri ya kupendana (Yoh. 13:34). Lakini kuna viashiria vingine vingi tulivyopewa pia. Hapa kuna mifano michache ya nguzo-elekezi aina ya hasi/kanushi na aina ya chanya katika maandiko ambazo tumepewa ili kurekebisha mwenendo wetu:
• (+) tunaambiwa tuwe na furaha katika Bwana (Wafi. 4:4); (-) tunaambiwa tusinung’unike (Wafi. 2:14).
• (+) tuwe na huruma (Yak. 2:13); (-) tusihukumu (Matt. 7:1-2).
• (+) tuwe wastahamilivu (Wafi. 4:5); (-) tudhibiti hasira yetu (Waefe. 4:26).
Nguzo-elekezi hasi/kanushi na chanya za aina hii hupatikana katika sehemu kubwa ya maandiko. Tunapewa hata orodha kadhaa ambazo zinatusaidia katika kulinganisha mwenendo wetu wa Kikristo na orodha hizo. Yakobo, kwa mfano, katika kuelezea hekima zitokazo juu, anatupatia sifa chanya za maisha adilifu: “matakatifu, yenye kupenda amani, yenye upole, yaliyo tayari kusikiliza maneno ya wengine, yaliyojaa huruma na yenye kuzaa matunda mema, yasiyopendelea na yasiyo na unafiki” - Yak. 3:17. Paulo, kwa upande mwingine, katika kuelezea hulka ya watu watakaoishi siku za mwisho, anaorodhesha baadhi ya maovu tunayopaswa kujizuia kuyafanya:
3.2 Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,
3.3 wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,
3.4 wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;
3.5 wenye mfano wa utauwa [uchamungu] lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.
2Tim. 3:2-5
Tunapopima mwenendo wetu kwa kuulinganisha na orodha hizi, hasi/kanushi na chanya, ni lazima tupate kujitia moyo kujitahidi kuiga zile sifa chanya na kuacha zile hasi/kanushi.
Karibu kila ukurasa wa Biblia una hizi nguzo-elekezi ambazo, zikitazamwa kwa unyenyekevu, zinaweza kusaidia katika kuongoza na kunyoosha mwenendo wetu wa Kikristo na kuendeleza maisha ambayo Mungu wetu anataka tuwe nayo. Amri bayana kama hizi, ziwe hasi/kanushi au chanya, ni muhimu sana, kwa sababu (ukichunguza orodha hizo mbili hapo juu utaona) “upendo” na “usitende dhambi” ni amri jumuishi kwa kiasi kikubwa [zina wigo mpana sana] hivyo kwamba sisi Wakristo tunaweza kujipa imani kwamba tunaenenda vyema zaidi ya vile tunavyoenenda kiuhalisia. Kila tunaposoma aya hizi, amri hizi, tunapaswa kuwa na tabia ya kutafakari maana yake, na baada ya hapo kujiuliza kama mwenendo wetu unafuatana na amri hizi au la.
Hivyo, kwa mfano, katika Tito 2:12, pale Paulo anavyotuambia tuishi maisha yenye busara, utaratibu, ya uongofu na ya kumcha Mungu, tunapaswa kuchunguza sifa hizi zina maana gani haswa:
• busara: tahadhari inayoongozwa na hekima kuhusiana na matendo ya dhambi au yaliyo hatari kiroho.
• uongofu: mwenendo wa unyofu, uadilifu na wenye haki.
• uchamungu: kutimiza majukumu ya kiroho katika namna ya kweli.
Kwa namna hii, tutakuwa tumetumia fursa kamili ya kuchunguza mwenendo wetu, tukijirekebisha kulingana na viwango alivyoviweka Mungu katika Neno lake.
5. Tunapoanguka: Katika hali kamilifu, tunapaswa, kwa juhudi zote, kutumia misingi ya maadili kila tunapopata nafasi. Hata hivyo, kwa kuwa maisha ya siku hizi huenda kwa kasi na pia matukio yanaweza kututoa katika msitari wetu wa Kikristo, inasaidia kutosahau kwamba fikra-adilifu zitaturudisha katika msitari huo pale tunapoanguka kiroho.
Dhambi za aina yoyote zinaturudisha nyuma kiroho, na hata kujisahau “kidogo” katika mtazamo wetu kunataka kitubio (katika sala ya faragha kwa Mungu: 1Yoh. 1:9). Hata hivyo, kujisahau huku kunaweza kutupa fursa ya kuelekeza upya fikra zetu katika uadilifu (haswa katika yale matendo adilifu ambayo ni kinyume na ile dhambi iliyotukwaza na tukaanguka).
Sehemu ya maumbile yetu kama wanadamu ambayo inahusika moja kwa moja na usimamizi wa mwenendo wetu wa kiroho ni dhamiri, kabla ya [tendo] baya ili kulizuia, na baada ya [tendo] baya ili kulisahihisha/kujirekebisha. “Dhambi” inatushitua tukumbuke lililo sahihi katika mazingira mbalimbali ya maisha yetu. Wakati hata wasioamini wanayo dira ya ndani inayowaonyesha jema na baya (War. 2:15), sisi kama Wakristo kila siku tunaiunda upya, tunaisahihisha, na tunaiboresha dhamiri yetu (1Wakor. 8:7-12; 10:25-29).
Pia tuna neema ya Roho Mtakatifu aliye ndani yetu kama Msaidizi wa dhamiri yetu. Ama kwa hakika tunaamriwa kutoipinga huduma hii Yake kwa ajili yetu sisi (Waefe. 4:30; 1Wathess. 5:19).
Hivyo, tunapoona mwenendo hasi katika maisha yetu, ni wajibu wetu siyo tu kuukataa mwenendo huu mbaya, bali pia kuitumia fursa hiyo kuzirudisha fikra zetu kwenye mwenendo chanya. Kwani kwa hakika, “dhamiri njema” ni sehemu muhimu ya upendo “utokao katika moyo safi”, na “imani isiyokuwa na unafiki” ambayo tunatakiwa kuwa nayo (1Tim. 1:5).
6. Uadilifu Chini ya Shinikizo: Mateso ndiyo njia kuu ya kusitawisha uadilifu (War. 5:3-5; Yak.1:2-4; 1Pet. 1:6-7). Ili kufanikiwa kama Mkristo, ni lazima tujifunze kuyapa maana mpya kabisa mateso na magumu ambayo ni tofauti kabisa na maana ambayo dunia inayapa, “twafurahi na kusikia fahari katika mateso”, “twahesabu kuwa ni furaha tupu”, na kutambua kuwa “kujaribiwa kwa imani yetu kuna thamani kuliko ile dhahabu yenye ubora sana”. Ukweli ni kwamba, hatuna wito wa kuishi katika starehe na anasa, utulivu na ustawi wa kiuchumi (utajiri). Kwa hakika, tunavyozidi kupevuka, basi na tutegemee kutahiniwa (kupimwa) zaidi na kuboreshwa na Mungu. Kama Bwana wetu alivyosema, “kila tawi lililo langu linalozaa, Baba yangu hulipogoa (prunes) ili liweze kuzaa matunda zaidi (Yohana 15:2).
Haiwezekani kutokuwa na shughuli katika maisha ya Mkristo: usalama wa kiroho unaenda sambamba na maendeleo ya kiroho (Wafi. 2:12; 2Pet. 1:10; 1Yoh. 2:24; 2Yoh. 1:8). Kuishi miaka mingi kama Mkristo hakumaanishi kukua kiroho (Waebr. 5:12). Kupevuka [kiroho] kunatokana na mitihani, na tunavyozidi kukua ndivyo tunavyozidi kupata mitihani (1Wakor. 4:9-13; 2Wakor. 6:1-13; 11:16-33). Hiki ni kitu kinachoeleweka kwa urahisi hasa pale tunapofikiria kidogo, kwamba tunavyozidi kujifunza ile kweli, basi na wajibu wetu wa kuitumia kweli hiyo katika maisha yetu unaongezeka (Yak. 4:17). Kama tukilinganisha mafunzo ya misingi muhimu ya kweli na lishe tunayoitumia kwa ajili ya miili yetu, basi tunaweza kuiendeleza anolojia hiyo kwa kulinganisha tunavyolitumia Neno katika maisha yetu (kuitumia misingi ya kweli katika maisha yetu ya kila siku, haswa katika wakati wa magumu, majaribu) na mazoezi ya viungo/kimwili. Kama vile kunyanyua kitu kizito kunaipa kazi misuli yetu, na, ukipata lishe bora, pamoja vinasababisha misuli hiyo kukua, vivyo hivyo Mungu anatufanya tunyanyue mizigo ya kiroho katika mfumo wa mitihani/mazoezi (maamuzi magumu, mateso, hasara, kukawia kujibu sala zetu, n.k.). Kama tukivumilia katika kunyanyua mizigo hii ya kiroho, na huku tukipata lishe ya kiroho (Neno la Mungu) wakati wote, tutapata maendeleo katika kukua kiroho na imani yetu itajenga misuli (1Tim. 4:7-8).
Ni jambo la kawaida kwa Wakristo, hasa Wakristo ambao kwa dhati kabisa wanaendelea kukua kiroho, kukabiliwa na majaribu makali, mitihani migumu kiasi kwamba inawapa shinikizo katika imani yao. Ebu tujikumbushe mfano wa Abrahamu, ambaye mwanzoni alikuwa na wakati mgumu kwa ajili ya kupata mtoto wa kiume wa kumrithi ambaye alimhitaji sana, lakini ambaye, mwisho wa siku, alikuwa tayari kumwua mrithi huyo huyo kama dhabihu kwa Mungu, kwa amri ya Mungu, kwa sababu aliamini kwamba, kwa namna moja ama nyingine, Mungu atalifanya jambo hilo kuwa jema. Ebu tukumbuke pia mfano wa Ayubu, ambaye, baada ya kuvumilia magumu mengi kwa muda mrefu, akapoteza subira/saburi yake na akaishia kukemewa na Mungu na kukumbushwa juu ya kutokuijua kwake ile nguvu ya Mungu: tunaweza tusielewe ni kwa nini tunateseka, lakini tunapaswa kumwamini Mungu kwamba kuna sababu ya maana ya kwa nini tunateseka, na kutegemea kwamba atafanya mambo yote kwa ajili yetu kuwa mema katika wakati wake na katika namna/njia yake. Mwisho, ebu tujikumbushe ile ahadi mahususi ya Mungu kwetu aliyotupatia katika 1Wakorintho 10:13, ambapo tunaambiwa kwamba hatutapewa magumu/mitihani tusiyoiweza (kumudu), na kwamba mwisho wa yote atatupatia ufumbuzi: katika kilindi cha huzuni, masikitiko, kukatishwa tamaa, hasara na kushindwa, tunaweza kuhisi kama vile hatuwezi kuendelea, lakini tunapaswa kumwamini kwamba Atatusaidia, na kwamba Atafanya mambo yote kuwa mema kwetu (War. 8:28).
Ama kwa hakika, mateso ni mtihani wa mwisho na mkuu wa imani yetu kwa Mungu, wa kujiamini kwetu katika tumaini letu la kuokolewa na Mungu, na upendo wetu Kwake, licha ya mazingira yetu. Tunapopita katika maisha haya ya machozi na suluba, tunaweza kumwamini tukiwa katikati ya huzuni, tunaweza kuona mbali zaidi ya maumivu ya muda huu na kuona utukufu ujao, tunaweza kumpenda katika maumivu yetu, tukimshika mkono na kuamini kwamba maumivu yote yana lengo lake, yakituzalishia “utukufu mkuu usio kiasi”, usiofanana na mateso ya sasa (2Wakor. 4:17)? Wakristo wengi wanaweza “kuwa na imani”, wakaweka tumaini lao kwa Mungu wakati mambo ni mazuri, lakini tumaini lisilotetereka, tumaini katika ahadi yake ya milele, na upendo kwake na vyote vilivyo vyake, ni vigumu kuwa nao wakati dhoruba za maisha zimetupa pigo kali. Hizi, hata hivyo, ndizo nyakati ambazo hulka yetu ya kiroho inapata mitihani halisi, na tunagundua kina cha maadili yetu ya Kikristo ni kirefu kiasi gani.
7. Sala na Maombi: Sala, mazungumzo yetu ya kudumu na Mungu (1Wathess. 5:17), ni sehemu muhimu ya kutumia maadili ya Kikristo katika maisha yetu. Katika Wafi. 4:6-8, Paulo anatuambia kwamba ikiwa tutaacha kuogopa na ikiwa tutapeleka hofu zetu kwa Mungu katika sala, amani Yake, amani iliyo na nguvu za kutosha kutuliza wasiwasi wetu, atatulinda, atalinda hisia na fikra zetu. Katika amani Yake, inayopatikana kwa njia ya sala, tegemeo letu kwake, upendo wetu kwake, na tumaini la kutimiza ahadi zake kwetu, vinachanganyika na kuwa kitu kimoja, na tunathibitisha pamoja Naye kwamba ikiwa tuliutafuta kwanza ufalme wa Mungu, mahitaji yetu yote ya kidunia yatashughulikiwa (Matt. 6:25-34). Sala, isiyokoma, ya kila wakati, ni muhimu kwa matumizi ya maadili ya Kikristo, kwa sababu sala inapeleka fikra zetu kwa Mungu. Sala inapaswa kuwa njia yetu ya kwanza ya kuelekeza fikra zetu kwa Mungu, kwa uweza wake na ufumbuzi wake wa matatizo yetu. Tunaposali, tunajikumbusha uhitaji wetu kwake na msaada wake, na hivyo tunapeleka fikra zetu kwake ili ziwe na uelekeo mmoja na fikra zake.
8. Tafakuri: Zaburi 1 inatufundisha kuwa “yeye aliyebarikiwa” hufurahia katika mafundisho ya Bwana na katika hayo “hutafakari usiku na mchana” (aya ya 2). Kila kipande cha maandiko, kila chembe ya mafundisho ya Biblia (mara nyingi katika namna ambayo siyo bayana kwa kutazama mara moja), inasaidia kuunda mfumo wa uelewa na mtazamo pevu ambao hukua kila uchwao. Hatuwezi kutumia kila dakika kujifunza kuhusu Mungu na mafundisho Yake, lakini katika siku nzima sisi hupata wakati wa kuwaza. Mawazo yetu huelekea wapi katika wasaa huu wa mpito? Je, tunafikiria tu hofu zetu na matatizo yetu? Siyo kwamba tuutumie muda huu na fursa hizi kwa kufariji roho zetu kwa kukumbuka kweli ambazo ni muhimu sana kwetu?
Kama vile miili yetu inavyohitaji damu izunguuke katika mishipa yake wakati wote ili ifanye kazi [sawasawa], pia roho zetu ni lazima zilishwe wakati wote na ile kweli ya Mungu. Kuelekeza fikra zetu katika misingi ya maadili, mitazamo ya upendo na shukrani kwa Mungu, imani katika ahadi zake, na tumaini katika thawabu ya milele, kwa mfano, ni njia nzuri ya kuanza mchakato huu, na kuutumia “mtaji wa kiroho” wa ile kweli iliyowekwa ndani ya mioyo yetu. Na tuendelee kuifanya kweli “izunguke” [kama damu mwilini] katika fikra zetu mara nyingi tunavyoweza ili tuweze kutimiza amri ya kutafuta “yaliyo juu” kule Kristo Bwana wetu aliko (Wakol. 3:1-2).
Tamati: Kuwa na tabia ya kuelekeza fikra katika maadili ya Kikristo (mafundisho yanayohusiana na sehemu mbalimbali muhimu za mwenendo wetu wa kila siku) ni mbinu muhimu katika kutukumbusha nafasi yetu ndani ya mpango wa Mungu, na sehemu muhimu ya kupevuka kiroho. Kujua na kutimiza mapenzi ya Mungu kwa maisha yetu ndilo lengo kuu la fikra adilifu (Wakol. 1:9-10; War. 12:2), na tunapotafakari katika maadili yanayoendesha matendo yetu, hatuwezi kuacha kutathmini mwenendo wetu wa Kikristo na kutiwa motisha ya kuuweka mwenendo huo katika msitari mmoja na mapenzi hayo/mpango huo wa Mungu (Waefe. 5:18).
Tunavyozidi kuwa na uthabiti katika kuelekeza tumaini letu kwa Mungu, upendo alio nao kwetu (ambao tunapaswa kuuakisi/kuuonyesha), na tumaini la ajabu la kuwa naye milele, tunakuwa na ridhaa na furaha ambayo si tu ni tiba/ufumbuzi wa tatizo la tamaa, mashaka, na mitihani ya maisha, bali pia ni hali/kiwango kinachowezekana kufikiwa tu na Wakristo walioweka imani yao, tumaini na upendo katika uwezo na nafsi ya Mungu (2Wakor. 9:8; Wafi. 4:10-14; 1Tim. 6:8-10; Waebr. 13:5-6):
• Tunaelekeza fikra zetu katika imani pale tunapomtumaini Mungu kutusaidia katika magumu yetu yote; tunamwacha atushike mkono na kutuongoza; hatuogopi, japokuwa inawezekana tusijue anakotupeeka, kwa sababu tuna imani naye kwamba anafanya yaliyo mema kwa ajili yetu (Zab. 23; War.8:28).
• Tunaelekeza fikra zetu katika upendo pale tunapokumbuka anatujali kiasi gani – hata akamtoa Mwanaye awe dhabihu kwa ajili yetu (Yoh. 3:16), na hivyo tunajua ya kwamba Mungu aliyelipa gharama kubwa kiasi hiki katika upendo wake kwetu kwa hakika hatotutelekeza (War. 8:31-39); na hivyo, katika kujiamini na upendo huu, tunafanya bidii ya kuuakisi/kuuonyesha kwa wenzetu kwa ajili ya utukufu wake.
• Tunaelekeza fikra zetu katika tumaini tunapokumbuka kwamba maisha yetu hapa duniani ni ya kupita tu, lakini kuna maisha yasiyoisha tutakapokuwa na Mungu, yenye utukufu na furaha, milele isiyokuwa na mateso katika mwili wa ajabu, na maskani yetu wenyewe yaliyo ya shani isiyopimika ndani ya Yerusalemu Mpya.
Katika uhalisia wake, maadili ya Kikristo ni KWELI, kweli ambazo tunapaswa kujifunza na kuzi-ishi ili kupevuka, kweli ambazo ni muhimu kwetu kuzitafakari kila siku, na ambazo tunapoweka akili zetu zitafakari juu yake, zinatuweka katika msitari ambao ni muhimu kwetu kama Wakristo.
=0=
Translated from: Imitating Christ: Peter’s Epistles #17
=0=
Basi, na tuonane katika somo #18 la mfululizo huu, kwa neema za Mungu, Amina!