KUMWABUDU MUNGU / IBADA SAHIHI KWA MUNGU

Wakristo halisi hujifunza mafundisho kutoka katika Biblia, ambalo ndilo Neno halisi la Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi, na vyote vilivyomo. Kujifunza Biblia ni sehemu mojawapo ya kumwabudu Mungu; ziko sehemu nyingine za ibada kwa Mungu kama kuishi kutokana na misingi ya Biblia – sala, kuacha dhambi, n.k., kupambana na matatizo tunayopitia hapa duniani kwa kutumia misingi ya Kikristo – inayofundishwa katika Biblia, kulitumikia Kanisa la Bwana wetu – kufundisha, kuonyesha mfano, kusaidia, n.k. Wakristo halisi wanatakiwa kufanya kila juhudi ili kufikia kiwango cha kupevuka kiroho, ambapo Bwana wetu Yesu Kristo anaweza kuwatumia kwa utumishi wa aina mbali mbali katika Kanisa Lake. Katika mchakato huu [wa kukua kiroho], haiwezekani kwa Mkristo kufanikisha kusudi hili kwa kusikiliza mafundisho ya kutunga kutoka kwa wanadamu na / au pepo. Kuhusiana na hili, maandiko yanafundisha kama ifuatavyo:

4.23 Lakini saa inakuja, nayo saa hiyo imekwishafika, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho (yaani kiroho) na kweli (yaani roho zetu na mioyo yetu ikiitikia wito wa Roho Wake na kweli Yake). Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao [ili] wamwabudu.
4.24 Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na [katika kweli Yake].
Yohana 4:23-24

Wapo walimu wanaofundisha mafundisho ya kutunga wao wenyewe au ambayo chanzo chake ni Shetani, ijapokuwa wanadai kwamba mafundisho yao hayo yanatoka katika Biblia, Neno la Mungu. Ebu tutizame mfano hai kutoka katika maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo na huduma Yake hapa duniani miaka mingi iliyopita:

7.1 Kisha Mafarisayo, na baadhi ya waandishi waliotoka Yerusalemu, wakakusanyika mbele yake,
7.2 wakaona wengine katika wanafunzi wake wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani, isiyonawiwa.
7.3 Kwa maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao;
7.4 tena wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea kuyashika, kama kuosha vikombe, na madumu, na vyombo vya shaba.
7.5 Basi wale Mafarisayo na waandishi wakamwuliza, Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono najisi?
7.6 Akawaambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami (nukuu kutoka Isaya 29:13);
7.7 Nao waniabudu bure (bila tija), Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu,
7.8 Ninyi mwaiacha amri ya Mungu (Sheria), na kuyashika mapokeo ya wanadamu.
7.9 Akawaambia, Vema! Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu.
7.10 Maana Musa alisema, Waheshimu baba yako na mama yako, na, Amtukanaye babaye au mamaye kufa na afe.
7.11 Bali ninyi husema, Mtu akimwambia babaye au mamaye, [mali yangu] Ni Korbani, yaani, [nimeiweka] wakfu, kitu changu cho chote kikupasacho kufaidiwa nacho, huwa basi {maana yake ni kwamba walipoweka mali zao Korbani basi ile ZAKA / TITHE ya 10% inayotozwa kwa mali hiyo inakuwa ndogo sana bali THAMANI ya mali hiyo inaongezeka na Mafarisayo hao wanazidi kuwa matajiri, LAKINI wazazi wao hawatafaidika na mali hiyo, kwani imewekwa wakfu!! Ndiyo sababu hapa Bwana wetu anawaita wanafiki};
7.12 wala hammruhusu baada ya hayo kumtendea neno (kumfaidisha) babaye au mamaye;
7.13 huku mkilitangua neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyopokezana; tena mwafanya mambo mengi yaliyo sawasawa na hayo.
Marko 7:1-13 (Soma pia Matt. 15:1-9)

15.12 Ndipo wanafunzi wake walipomwendea, wakamwambia, Wajua ya kuwa Mafarisayo walipolisikia neno lile (yaani Matt. 15:1-9) walichukizwa?
15.13 Akajibu, akasema, Kila pando (mmea) asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang'olewa.
15.14 Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili.
Matt. 15:12-14

Ili kudhihirisha kwamba mafundisho ya Mungu ndiyo ya kweli, ndiyo yenye kweli inayotuelekeza sisi juu ya namna ya kumwabudu Yeye, ebu tusome aya zifuatazo:

16.13 Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?
16.14 Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.
16.15 Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?
16.16 Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.
16.17 Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.
Matt. 16:13-17

Anasema Bwana wetu, akimwambia Petro, kwamba “… kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni”. Kwa maneno mengine, si mwanadamu anayefunua kweli kwetu sisi, bali ni Mungu Mwenyewe. Hili linapaswa kutupatia uhakika wa ahadi zote zinazotolewa katika maandiko kwa ajili yetu, kwa ajili ya wokovu wetu, kwa ajili ya ufufuo wa miili yetu, n.k., ikiwa tu tutatumia ile hulka tuliyopewa Naye ya utashi, ya kuamua kumwamini Mwanaye ambaye kwa Yeye ulimwengu huu unaokolewa kutoka mauti ya milele.

Akiizungumzia Injili aliyoifundisha na chanzo cha Injili hiyo, Paulo aliwaambia Wakristo wa Galatia kwamba:

1.11  Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu.
1.12  Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.
Waga. 1:11-12

Hapo tunaendelea kuona kwamba kwa hakika Neno la Mungu ndiyo chanzo chetu cha ile kweli, haswa ile Injili ambayo kwayo sisi sote tunaokolewa kutoka mauti na utengano wa milele na Mungu.

2.20  Basi ikiwa mlikufa pamoja na Kristo mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, kwa nini kujitia chini ya amri, kama wenye kuishi duniani,
2.21  Msishike, msionje, msiguse;
2.22  (mambo hayo yote huharibika wakati wa kutumiwa); hali mkifuata maagizo na mafundisho ya wanadamu?
2.23  Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili.
Wakolosai 2:20-23

Mtume Paulo anatufundisha katika aya hizi hapo juu kwamba hata katika mwenendo wetu wa Kikristo, Neno la Mungu linapochanganyika na imani na uongozi wa Bwana wetu na ualimu wa Roho Mtakatifu moyoni mwa muumini, linakuwa na nguvu na uwezo mkuu. Hii ni tofauti kabisa na pale tunapojilazimisha kwa uwezo wetu wenyewe kuwa na mwenendo mwema, bila ya uongozi na uweza wa Mungu.

5.27 Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza,
5.28 akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili [la Kristo]? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu.
5.29 Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.
5.30 Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti.
5.31 Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi.
5.32 Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio.
5.33 Wao waliposikia wakachomwa mioyo yao; wakafanya shauri kuwaua.
Matendo 5:27-33

Hapa juu tunaona sasa nguvu, ujasiri, ushujaa, uthubutu mkuu ambao Mitume waliuonyesha kutokana na Roho Mtakatifu kuwajaza Mitume wale mara baada ya Pentekoste. Mitume, wakiongozwa na Petro, walithubutu kupambana uso kwa uso na Mafarisayo na watawala wa Israeli ambao walimwua Kristo kitambo kidogo tu kilichopita. Mitume wale walikuwa wakijificha kwa woga hapo kabla, lakini mara baada ya kujazwa na Roho Mtakatifu, waligeuzwa na kuwa mashujaa wakuu wa Mungu! Kwa hakika mafundisho na kutiwa moyo tu kwa kibinadamu kusingeweza kuwapa watu ushujaa na uthubutu wa namna hiyo. Huu ni mfano mwingine wa uweza wa kweli ya Mungu inapotumiwa kikamilifu katika kumwabudu Yeye Aliyetuumba.

Hivyo, tahadhari:

4.1  Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;
1Tim. 4:1

Tunamaliza makala hii fupi kwa tahadhari, ilani kutoka kwa Mtume Petro, akituonya tuwe macho katika nyakati hizi za mwisho; kwani kutatokea walimu wa uwongo, ambao kwa kuwa wanasikiliza pepo, watafundisha uwongo, na kwa kweli tumekuwa tukiliona hili likifanyika. Watu wengi, Wakristo na wale wasio Wakristo, wamedanganyika na mafundisho ya kupata utajiri mkubwa, uwezo dhidi ya wenzao, madaraka, n.k. ati kwa kutumia Neno la Mungu!! Wengine wanafundisha ati kutafsiri ndoto zako Kibiblia ili uweze kufanikiwa / kutajirika! Matangazo ya mikutano mikubwa “ya Injili” inaambatanishwa na ahadi za kuona miujiza ikitendwa na wanadamu; hili ni jambo la kushangaza. Kwani mwujiza mkuu kabisa katika enzi hii ya Kanisa ni kushuhudia mwanadamu akizaliwa upya, akiweka matumaini yake yote katika Bwana Yesu Kristo, akiokolewa. Huo ndio mwujiza, na si uponyaji, utoaji wa pepo wa maigizo tunaouona ukifanyika kwenye majukwaa mbali mbali siku hizi. Neno la Mungu, likieleweka, likiaminiwa huzaa nguvu na uwezo mkuu ndani ya moyo wa mwanadamu, na kulijenga Kanisa la Kristo, na huo ndio mwujiza halisi. Mitume wa Bwana wetu, walioliamini Neno la Mungu kwa asilimia 100, walikabili mateso, shida, dhiki, vipigo, mahabusu, jela, njaa, jua, mvua, baridi na kila aina ya taabu na wakashinda hayo yote, kwani majina yao yataandikwa katika ile misingi 12 ya Yerusalemu mpya. Mkristo, hilo ndilo linapaswa kuwa lengo lako, kusudi lako na si kupata mali za muda za hapa duniani, ambazo punde zitakuwa mavumbi. Tumaini letu haliko katika ulimwengu huu wa mavumbi

Yohana 21:15c:
[Bwana] Yesu Akamwambia [Petro] , Lisha wana-kondoo wangu.

Mwamini Bwana Yesu Kristo upate uzima wa milele, upate kuurithi ufalme wa Mungu!

2.8  Kwa maana mmeokolewa kwa neema [ya Mungu], kwa njia ya imani [yenu kwa Kristo]; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa [cha bure] cha Mungu;
2.9  [na] wala si kwa matendo [yenu], mtu awaye yote asije akajisifu.
Waefe. 2:8-9

Imeandikwa na Respicius L. Kilambo

https://sayuni.co.tz