Maswali na majibu kutoka https://ichthys.com by Dr. Robert Dean Luginbill.
Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Somo la Kanuni ya Kudura ya Mungu kama inavyofundishwa katika Biblia
Doctrine of Foreknowledge and Foreordination / Predestination as it is taught in the Bible

Kutakuwa na sehemu mbalimbali zinazonyumbulisha taswira tofauti za somo hili. Sehemu hii ya mwanzo kutoka: mail-Plan-of-God.rtf

Yeremia 1:5
5 Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.

Ufunuo 1:8
1.8  Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.

NOTE: Ndugu msomaji, majibu ya swali hili la kwanza yanaweza kuwa “mazito” au magumu kidogo; hili ni somo gumu kwa wengi wetu. Kupunguza ukali wa suala hili, nimeweka addendum kama tano hivi hapa chini zinazonyumbulisha taswira mbalimbali zinazohusiana na fundisho hili. Hivyo nashauri usikate tamaa pindi utakapoona kuwa fundisho linakuwa zito kidogo; endelea tu mpaka mwisho; nakuhakikishia kwamba ukiwa na Roho Mtakatifu, na ukajituma kwa bidii, kuna mwanga wa kutosha mwisho wa safari hii. Nakaribisha maswali pia. Ubarikiwe sana - Respicius Luciani Kilambo.

Swali #1: Habari yako Dr. Luginbill. Una maoni gani kuhusu suala la mafundisho ya Biblia la kudura ya Mungu (predestination)? Mimi naamini kwamba dhana na mafundisho ya Kalvini kuhusu suala hili siyo sahihi.

Jibu #1: Nimefurahi kufahamiana na wewe. Mimi hupendelea kutofanya maamuzi au hukumu juu ya “mafundisho” ya Kalvini kutokana na yale niliyoyaona katika siku zilizopita ambapo kuna tofauti fulani kati ya yale ambayo yanaweza kuthibitishwa kuwa yalifundishwa naye, na yale ambayo baadhi ya watu katika vizazi vilivyofuata walifundisha katika jina lake. Nitaanza kwa kusema kwamba mimi ninaamini ya kuwa misimamo ya wale wanaoitwa hyper-Calvinists inarahisisha kupita kiasi mafundisho ya Kalvini mwenyewe, na pia naweza kusema kwamba misimamo hiyo haiko sahihi. Kwa mfano, kanuni ya “ustahamilivu / uvumilivu wa watakatifu” inapochukuliwa kumaanisha “ukishaokolewa basi umeokolewa daima” (OSAS – Once Saved, Always Saved), hapo inakuwa ni kanuni / fundisho lisilo sahihi kabisa kabisa (iwe au isiwe kwamba Kalvini mwenyewe aliufikiria “usalama wa muumini” katika namna / maana hiyo).

Kuhusiana na kanuni ya “kudura” au “predestination/foreordination” (fundisho / kanuni ya Biblia kwamba maisha ya wanadamu yalipangwa na Mungu kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu), kwa kuwa hili ndilo suala uliloliulizia mahususi, kwa hakika mimi mwenyewe siamini kwamba kanuni hii ya kudura kama inavyofundishwa kiuhalisia katika Biblia ina mgongano wowote na uhalisia wa utashi-huru (free-will) wa mwanadamu kama vile baadhi ya wanazuoni wa Kikristo wanaofundisha misimamo ya mrengo wa kushoto au kulia mwa mafundisho ya Kalvini mwenyewe wanavyodokeza, kwa mfano hyper-Calvinists waliotajwa hapo juu, (hapa tena, tukiweka kando kile ambacho Kalvini mwenyewe alikifikiria na kufundisha kuhusiana na suala hili). Kama ambavyo mimi nimesema mara kadhaa, kwa kuwa Kalvini na wenzake wengine walikuwa wakipambana katika ‘vita’ au mgongano wa kufa na kupona dhidi ya taasisi ya kidini (kanisa Katoliki – enzi hizo waasi wa kanisa hili waliuawa) ambayo ilikuwa ikifundisha – na inafundisha mpaka sasa – “wokovu kwa matendo”, kimantiki basi ni wazi kwamba Kalvini na wenzake (the Reformers) wangetilia mkazo katika majibu yao dhidi ya mafundisho haya ya “wokovu kwa matendo” ile neema ya Mungu na mapenzi ya Mungu kuwa ni yenye kuchukua nafasi ya juu na ya kipekee kabisa na kamwe havitegemei matendo ya wanadamu kwa namna yoyote ile, na hilo ni fundisho zuri tu kwa kiasi chake. Tatizo linatokea, kwa mawazo yangu, pale inapodhaniwa kwamba kuna mgongano kati ya mapenzi ya Mungu na mapenzi ya wanadamu (au pale wanazuoni wanapojaribu kutoa maelezo ya kiteolojia mara wanapoona – kimakosa – kwamba kuna mgongano huo).

Acha mimi nilielezee suala hili katika namna rahisi inavyowezekana: Mungu amepanga historia yote ya wanadamu, tangu mwanzo wake mpaka mwisho wake. Mpango huu ni mkamilifu, na umechukua na kuhusisha kila tendo, neno na wazo la kila mwanadamu na uliamriwa kabla ya kuumbwa ulimwengu. Mpango huu umehusisha kila kitu katika historia, kutoka kuumbwa kwa ulimwengu na malaika, mpaka majaribu ya malaika na uasi wa baadhi yao, mpaka kuumbwa na kuanguka kwa wanadamu, mpaka mwisho wa mileniamu ambao ndio mwisho wa historia, na hayo yote yakiunganishwa na kuundwa na kusimikwa juu ya msalaba wa Bwana Yesu Kristo. Mungu aliyajua yote yatakayotokea kabla ya kuumbwa ulimwengu, na licha ya kujua kwamba italazimu dhabihu ya Mwanaye mpendwa, Alifanya hivyo bila ya kusita. Hili lilikuwa jambo la baraka na neema kwetu sisi viumbe wake. Kwani, kwa uhakika, hakuna kinachoumbwa na hakuna kinachofanyika nje ya mapenzi Yake. Mapenzi ya Mungu yanahusika katika mambo yote, kutoka mambo yote yenye mwonekano wa kutokea kwa bahati nasibu, mpaka mambo yote yenye mwonekano wa kutokuwa na umuhimu wowote, mpaka – kuhusiana na swali lako – matendo yote ya kila kiumbe mwenye utashi-huru.

Sasa, suala la kudura au predestination/foreordination linahusiana na mambo yote ambayo wale wote wenye uwezo wa kupambanua kati ya jema na baya wanaamua kuyafanya hapa duniani, na katika fikra za kibinadamu kuna taswira mbili za suala hili ambazo wanateolojia wamegonganisha vichwa vyao dhidi yake kwa sababu ya mwonekano wake wa kutokuwa na mantiki, au kuwa na mwonekano wa mgogoro kati ya taswira hizo, ambazo ni: ikiwa Mungu alijua na alipanga yote yaliyotokea, yanayotokea na yatakayotokea, je, ni sahihi kusema kwamba viumbe wake, kama wanadamu na malaika, wana utashi-huru? Na ikiwa sisi wanadamu (na malaika) tunaamua kutenda maovu, je, Mungu ndiye atakayehusika na uovu huo kwa sababu uovu huo umo katika mpango wake? Majibu ya hayo maswali mawili ni, bila shaka yoyote, “NDIYO!” (tunao utashi-huru halisi) na “HAPANA!” (Mungu si mwanzilishi na hahusiki kwa namna yoyote na uovu). Ukweli kwambu Mungu ameamuru yote yanayotokea haumaanishi kwamba sisi hatuna fursa inayotokana na utashi-huru tulio nao ya kumwamini na kuwa wafuasi Wake, na ukweli kwamba baadhi yetu wameshindwa kuamua kufanya hivyo au wameamua kutenda dhambi au kutenda uovu fulani haumaanishi kwamba Yeye anashiriki katika matendo yetu. Mungu aliazimia kuumba ulimwengu na akafanya hivyo. Na katika kufanya hivyo alifikiria na kuhusisha kila kitu ambacho kila kiumbe mwenye utashi-huru atakiwaza, atakisema na atakitenda. Zaidi ya hayo [na haswa / mahususi], alitoa fursa katika neema Yake kuu kwa wanadamu wote kuweza kuutumia utashi-huru wao katika imani Kwake kwa kumwamini Mwana Wake (au, kabla ya ujio wa kwanza wa Mwana, ahadi ya msamaha katika Yeye ambaye alikuwa anakuja). Hivyo, utashi-huru tulio nao unaweza ukapewa jina bora zaidi la “imani inayowezeshwa na utashi-huru”, au “free-will faith” katika kimombo, kwa sababu kimsingi unatokana na fursa tunazopewa za kuitikia wito Wake na kweli Yake – Neno Lake.

Nafikiri hili ni moja kati ya yale mambo ambayo yanajengewa hoja zilizokuzwa / zilizonyumbulishwa kupita kiasi na wana-teolojia wakati hoja za msingi zinazolijenga jambo lenyewe siyo sahihi. Istilahi hii ya predestination (kudura katika Kiswahili, ingawa katika tafsiri ya Swahili Union Version, SNT na ile ya SRUV neno “kudura” halitumiwi) inaonekana katika aya chache za Agano Jipya (katika tafsiri za Kiingereza) ambamo kitenzi prohorizo kilitumika katika lugha asilia ya Kiyunani ya Agano hilo. Neno hili prohorizo linaonekana hasa katika aya zifuatazo (nitanukuu aya hizi katika lugha mbili za Kiswahili na Kiingereza ili msomaji uone mahala mahususi neno predestination / prohorizo linapoonekana – bold italics):

Warumi 8:29-30 SUV:
8.29  Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.
8.30  Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.

Warumi 8:29-30 ikiwa na misamiati ya ziada:
8.29 Maana wale Aliowajua [uamuzi wao wa kumwamini Yeye] tangu asili (kabla ya kuumbwa ulimwengu), [hao] aliwachagua tangu asili [ili] wafananishwe na mfano wa Mwana Wake (i.e., wawe na mwili wa ufufuo kama wa Mwana Wake), ili [Mwana] awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.
8.30 Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita (ili waokolewe), na hao aliowaita, akawahesabu kuwa ni waongofu [kwa njia ya imani yao katika Kristo], na hao aliowafanya waongofu, hao akawatukuza (i.e., ufufuo wetu na uzima wetu wa milele uko imara katika mpango wa Mungu tangu kabla ya kuumbwa ulimwengu).

Romans 8:29-30 Dr. Luginbill’s translation:
(29) For those whom He foreknew, He also foreordained to share the likeness of His Son (i.e., to have identical resurrection bodies), so that He might be the Firstborn over many brothers [and sisters].  (30) And those whom He foreordained, these He also called [to salvation], and those whom He called, He also made righteous [through faith in Christ], and those whom He made righteous, these He also glorified (i.e., our resurrection and eternal life has been set fast in the plan of God since before the world was made).

Romans 8:29-30 NIV (1984):
29For those God foreknew he also predestined to be conformed to the likeness of his Son, that he might be the firstborn among many brothers.
30And those he predestined, he also called; those he called, he also justified; those he justified, he also glorified.

1Wakorintho 2:7 SUV (2006):
7 Sisi tunanena hekima ya Mungu ambayo ni siri, tena iliyofichika kwa wanadamu, ambayo Mungu aliikusudia ( kabla ulimwengu kuwepo), kwa ajili ya utukufu wetu.

1Wakorintho 2:7 SUV (1958) yenye misamiati ya ziada:
2.7  bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu / aliiamuru tangu milele [iliyopita], kwa [ajili ya] utukufu wetu;

1Corinthians 2:7 NIV (1984):
7No, we speak of God's secret wisdom, a wisdom that has been hidden and that
God destined for our glory before time began.

1Corinthians 2:7 HCSB:
On the contrary, we speak God’s hidden wisdom in a mystery, a wisdom God predestined before the ages for our glory.

Waefeso 1:5 SUV (1958):
1.5  Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.

Waefeso 1:5 Tafsiri yangu (R. Kilambo, kutoka expanded translation ya Dr. Luginbill):
1.5 Kwa kuwa alituteua / alituchagua kabla [ya kuumbwa ulimwengu] katika upendo Wake kwa nia ya kututwaa tukae Kwake kwa njia ya Yesu Kristo kulingana na furaha ya mapenzi Yake,

Ephesians 1:5 Tafsiri ya Dr. Luginbill:
(5) Having foreordained us in [His] love for adoption to Himself through Jesus Christ according to the good pleasure of His will,

Ephesians 1:5 NIV (1984):
he predestined us to be adopted as his sons through Jesus Christ, in accordance with his pleasure and will--

Waefeso 1:11 SUV (1958):
1.11  na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake.

Waefeso 1:11 Tafsiri yangu, kutoka tafsiri ya Dr. Lugibill:
1.11 na katika Yeye (Mungu Mwana) sisi tunao urithi, kwa kuwa tulichaguliwa [kabla ya kuumbwa ulimwengu] kutokana na mpango wake Yeye – Mungu Baba – ambaye anafanya kila kitu kulingana na nia ya mapenzi Yake,

Ephesians 1:11 Tafsiri ya Dr. Luginbill:
(11) In whom we also have an inheritance, having been ordained according to the design of Him who is working everything out according to the desire of His will,

Ephesians 1:11 NIV (1984):
11 In him we were also chosen, having been predestined according to the plan of him who works out everything in conformity with the purpose of his will,

Katika Kiyunani, horos ni mpaka na kitenzi chake cha msingi horizo kinamaanisha kuweka mpaka au kuweka ukingo (neno hili ndilo chanzo cha neno la Kiingereza “horizon”, ambalo tafsiri yake sisisi ni “kile kinachotumika kama mpaka au ukingo”). Neno “predestination”, kwa Kiswahili “kudura”, na maneno mengine yaliyo na asili na maana moja, linatoka katika Kilatini, na maneno hayo yote yanatoka katika kitenzi cha msingi destino, destinare, ambacho maana yake ni “amua, panga, chagua, teua”, na kiambishi-awali pre kinamaanisha kufanya hivyo kabla. Kwa mfano, maana mojawapo ya neno pre-destination itakuwa: ‘teua kabla’ au ‘chagua kabla’ au ‘pangia kabla’, n.k. Neno hili katika Kiingereza limeazimwa moja kwa moja kutoka katika tafsiri ya Biblia ya Jerome inayoitwa “Latin Vulgate” (ambamo kitenzi cha Kilatini cha neno hili katika Warumi 8:29-30, kwa mfano, ni predestinavit [hapa neno hili limeundwa kwa kuunganisha maneno matatu: pre, destino, -are]). Kwa wazi kabisa, neno hili la Kilatini lina tofauti kidogo na lile la Kiyunani, ijapokuwa maneno haya ni visawe (synonyms).

Kitenzi hiki cha Kiyunani pamoja na tafsiri yake katika Kilatini / Kiingereza vinawakilisha dhana ile ile ya kwamba Mungu aliamuru yote yatakayotokea, lakini tatizo lililoko katika mfumo wa maneno ya Kilatini / Kiingereza yanayohusiana na dhana hii ni kwamba maneno hayo yamefungamana na kuchanganywa na hadithi za kipagani za kubuni za mithiolojia na dhana ya “majaliwa” au “fate” (jambo lililotamkwa na miungu: Kilatini fatum) na “takdiri” au “destiny” (kinachopangwa na miungu: Kilatini destinatio). Lugha ya Kiswahili nayo imeambukizwa dhana hizi, kupitia lugha za Kiarabu, Kihindi, Kireno, Urdu, Bantu, n.k. kama tunavyoona katika matumizi yetu ya maneno yaliyotajwa hapo: majaliwa na takdiri ambayo yanapelekea kwenye dhana kama bahati, kismet/kismati, nasibu, n.k. Tofauti kati ya maana ya fundisho la Kibiblia na ile ya fundisho la kipagani ni ndogo sana, lakini wakati makundi yote mawili ya maneno katika lugha zote mbili (Kiyunani na Kiingreza / Kilatini) yanawakilisha dhana ya tendo la Mungu, neno predestination (kudura katika Kiswahili) linachanganya [pia] kidokezo kwamba tendo hilo limetalikiwa / limeachana kabisa na mwenendo, matendo na mapenzi au nia za wanadamu. Na, wakati ni kweli kabisa kwamba Mungu hadaiwi kitu chochote na wanadamu, kutoa wazo / kudokeza kwamba hakutilia maanani na hakuhusisha katika mpango Wake yale yote ambayo tutayafikiria au tutayasema au tutayatenda ni kutoyaelewa maandiko ya Biblia kabisa katika ujumla wake na pia kutozielewa zile aya ambamo maneno haya yameandikwa. Mithiolojia za kipagani zinatuletea dhana kuwa Mungu anafanya yote anayoyafanya bila kuchukua na kuhusisha katika mpango na matendo Yake mambo yote ikiwa ni pamoja na kama mwanadamu ni mwema au la, ataitikia wito Wake au la. Lakini sisi Wakristo tunajua kwa uhakika kwamba tunayoyawaza, tunayoyasema na tunayoyatenda ni yenye umuhimu mkubwa kabisa kabisa. Biblia inatufundisha hili kwa dhahiri kabisa na bila kusita katika kila ukurasa wake. Haiwezekani kwamba Mungu, katika Neno Lake, anajali wema wa mwenendo wetu kwa kiasi hiki kama mwenendo wetu huo hauna maana yoyote Kwake. Hata wale wanaoitwa au wanaojiita hyper-Calvinists watalazimika kukubaliana na hili. Uchunguzi wa makini wa ile aya muhimu katika Warumi sura ya 8 unatufunulia wazi kabisa nini maana ya “aliowachagua tangu asili” - SUV. Hapa chini nitanukuu tena tafsiri kadhaa, za Kiingereza na Kiswahili, kutoka Warumi 8:29-30 ili kudhihirisha maana halisi ya [ma]neno yafuatayo:

kudura / “aliowachagua tangu asili”
foreordained / predestined / “marked out ahead of time”

Warumi 8:29-30 SUV:
8.29  Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.
8.30  Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.

Warumi 8:29-30 ikiwa na misamiati ya ziada:
8.29 Maana wale Aliowajua [uamuzi wao wa kumwamini Yeye] tangu asili (kabla ya kuumbwa ulimwengu), [hao] aliwachagua tangu asili [ili] wafananishwe na mfano wa Mwana Wake (i.e., wawe na mwili wa ufufuo kama wa Mwana Wake), ili [Mwana] awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.
8.30 Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita (ili waokolewe), na hao aliowaita, akawahesabu kuwa ni waongofu [kwa njia ya imani yao katika Kristo], na hao aliowafanya waongofu, hao akawatukuza (i.e., ufufuo wetu na uzima wetu wa milele uko imara katika mpango wa Mungu tangu kabla ya kuumbwa ulimwengu).

Romans 8:29-30 Dr. Luginbill’s translation:
(29) For those whom He foreknew, He also foreordained to share the likeness of His Son (i.e., to have identical resurrection bodies), so that He might be the Firstborn over many brothers [and sisters].  (30) And those whom He foreordained, these He also called [to salvation], and those whom He called, He also made righteous [through faith in Christ], and those whom He made righteous, these He also glorified (i.e., our resurrection and eternal life has been set fast in the plan of God since before the world was made).

Romans 8:29-30 NIV (1984):
29For those God foreknew he also predestined to be conformed to the likeness of his Son, that he might be the firstborn among many brothers.
30And those he predestined, he also called; those he called, he also justified; those he justified, he also glorified.

Kama ambavyo aya hizi mbili zilizonukuliwa hapo juu zinavyoweka wazi kabisa, kitu muhimu sana katika kulielewa fundisho la kimaandiko / Kibiblia la “kuchaguliwa tangu asili” ni kwanza kuelewa maana ya “aliowajua tangu asili” au “kabla ya kuumbwa ulimwengu”. Kwani katika aya ya 29 hapo juu, “aliowajua tangu asili” inatangulia “aliowachagua tangu asili”, yaani uchaguzi ni matokeo ya ufahamu; aliwachagua kabla ya kuumbwa ulimwengu kwa sababu aliwajua kabla. Kwa kuwa ni waumini pekee watakaofufuliwa na kuingia katika uzima wa milele, basi ni sahihi kuhitimisha kwamba ufufuo huo unatokana na uamuzi wetu wa kuamini wakati tukiwa katika utashi-huru halisi hapa duniani, kwamba uamuzi huu wa kuamini ndio lengo au shabaha ya ufahamu ule wa Mungu kabla ya kuumbwa ulimwengu – hili ndilo jambo muhimu alilolifahamu Mungu wakati ule (kabla ya uumbaji) alipotufahamu (yaani sisi ndio “wale” katika aya ya 29 na ile ya 30). Uamuzi wetu katika maisha yetu hapa duniani, unaotokana na utashi-huru tuliopewa, ndio Mungu “aliujua tangu asili”, kama ambavyo aya ya 29 inaweka wazi kabisa, kwamba kudura ni matokeo ya moja kwa moja ya ufahamu wa Mungu kwa wale watakaoamini, ambao maisha yao Mungu anadhihirisha wazi hapa kwamba aliyapanga katika kila kipengele chake.

Suala jingine hapa ni kwamba si sahihi kufikiri kuwa kwa sababu Mungu anajua kwamba jambo fulani litatokea basi Yeye ndiye mhusika au mwanzilishi / mwasisi wa jambo hilo. Ufahamu wa Mungu kabla ya majira / historia kuanza wa kwamba punde atakapotoa fursa kwako na kwangu basi tutaichukua fursa hiyo na kumwamini Kristo kama Mwokozi wetu haina maana kwamba hatukuwa na uwezo wa kukataa katika suala hilo. Vivyo hivyo, utambuzi Wake kabla ya majira / historia kuanza wa dhambi na uovu utakaotendwa na watu mara baada ya kuanguka kwa Adamu na Eva hauna maana ya kwamba Yeye ndiye anayehusika na uovu na dhambi hiyo. Kwani bila ya shaka yoyote, ulimwengu umejaa dhambi na uovu, na kwa hakika Mungu hahusiki na dhambi na uovu huo kwa namna yoyote ile. Hivyo basi, tunapaswa kuelewa kwamba Mungu aliporuhusu (na kuamuru) mchakato wa historia ambamo baadhi ya viumbe wake watamchagua Yeye lakini wengi wa viumbe hao watamkataa katika mambo yote, makubwa na madogo, haina maana ya kwamba Yeye alipanga namna viumbe wake hao watakakavyofanya maamuzi yao katika historia / maisha yao, bali tu ni kwamba Yeye aliidhinisha maamuzi yetu hayo (hata kama yalikuwa au hayakuwa “mapenzi Yake” kwa ajili yetu). Kwani kitabu cha Warumi kinatupatia utaratibu sahihi: Mungu alijua uamuzi wetu utakuwa upi, halafu akaamuru [historia], yaani kwanza aliangalia na kuzingatia yote ambayo alijua tutayafikiria, tutayasema na tutayatenda kabla ya kuamuru historia kuanza, halafu ndiyo akaamuru historia yote ianze. Na tusisahau ukweli kwamba katika ufahamu Wake wa yote yatakayotokea, hakuwa na ulazima wa kuamuru, lakini katika kuamuru Akajiwajibisha kumtoa Mwanaye wa pekee kufa kwa ajili ya dhambi zetu, dhambi ambazo zisingetokea bila ya Yeye kuamuru historia, lakini ambazo haziepukiki katika ulimwengu ambamo viumbe (watu na malaika) wangeishi.

Hivyo basi, katika aya zote zilizoorodheshwa hapo juu (ambamo tunaweza kuona kitenzi-neno horizo [katika Kiyunani, lugha asilia ya Agano Jipya] kinachoonekana [pia] katika Luka 22:22; Matendo 2:3; 10:42; 17:26; 17:31; Warumi 1:4; Waebrania 4:7), tunaona kwamba Mungu hakupuuza maamuzi huru ya wanadamu, bali aliyaidhinisha, aliyathibitisha. Hivyo basi, kudura (foreordination / predestination) ya Mungu haiharibu utashi-huru unaoiwezesha imani bali inauwezesha utashi-huru huo. Hii ni baraka kuu kwa waumini, kwani, kama ambavyo Mtume Paulo anadhihirisha katika sehemu zote anamotumia kitenzi-neno prohorizo, anamaanisha kwamba hadhi yetu [sisi tunaoamini] ya uzima wa milele, ufufuo na thawabu imekwishaamuriwa na Mungu mwenyewe na hivyo haina shaka hata kidogo, na wala haiwezi kubadilika (ikiwa tutaendelea na imani yetu katika Bwana Yesu Kristo). Kwa hakika, hii ndiyo sababu Paulo anatufundisha hapa kanuni ya kudura (foreordination / predestination), si kupendekeza kwamba sisi ni viumbe tusio na utashi ulio huru (yaani sisi ni maroboti – automatons), bali ni kinyume chake kabisa, na kudhihirisha kwamba uamuzi wetu huru wa kuamini na maamuzi yetu huru yanayofuata katika kustahamili katika imani hiyo yana matokeo makuu yaliyo mema kabisa. Aya hii na mtiririko wake wa hoja unatolewa hapa (na Paulo) kama maelezo ya jinsi “katika mambo yote Mungu hufanyia kazi wale wampendaye katika kuwapatia mema” (ambayo ndiyo aya iliyotangulia, War. 8:28), yaani kwa kuuandika mpango Wake usiobadilika katika historia, wokovu alioutoa kwa neema Yake na ambao sisi tumeupokea, na utukufu tunaoungojea, na kwa ajili ya utukufu huo tunastahamili yote.

Unaweza pia kutazama link hizi:

Against Universalism I: Free Will and the Image of God.

Does God’s Choice Eliminate Our Free Will?

Katika neema isiyo na mfano na busara zisizo na kina zake Yeye aliyetupenda sana, kiasi cha kumtoa Mwana wake Mpendwa afe kwa ajili yetu,

Bob Luginbill.
https://ichthys.com

Msomaji, sina shaka kwamba sehemu hii ya kwanza ya fundisho la predestination / kudura ina ugumu wa kiasi fulani katika kuielewa. Hii ni kwa sababu fundisho hili kwa kweli ni gumu kidogo. Hata hivyo, ni wajibu wetu kama Wakristo kujitahidi kiasi tunachoweza, tukiongozwa na kufundishwa na Roho Mtakatifu, kulielewa fundisho hili. Kwani fundisho hili ni muhimu sana. Kwa sababu hii, kumekuwa na maswali mengi ambayo mwalimu wangu wa Biblia, Dr. Robert D. Luginbill, ameyapokea kuhusiana na kanuni hii. Hapa chini ninaweka tafsiri zangu za maswali hayo pamoja na majibu yake katika addendum kadhaa ili kulinyumbulisha fundisho hili kufikia mahala ambapo fundisho lenyewe linakuwa rahisi zaidi. Tafadhali soma mpaka mwisho ili upate ufahamu wa somo hili. Ushauri wangu ni usome mara kadhaa ili uweze kufikia uelewa utakaokusaidia kwa kiasi kikubwa katika kukua kwako kiroho. Nakaribisha maswali pia. Karibu sana.

ADDENDUM #1:

From Q & A #3 of the same Mail

Jibu la Swali #3: Kama inavyoonekana mara nyingi katika Biblia, kanuni / kauli / mafundisho mawili ambayo mbele za macho ya dunia yanaweza kuonekana kuwa yana mgongano na / au yanalazimisha misimamo miwili tofauti, mara zote katika uweza na busara kuu ya Mungu kiuhalisia hayako hivyo kabisa. Nafikiri ni jambo la wazi kabisa kwamba Biblia inafundisha kanuni zote mbili, yaani kwamba Mungu aliwachagua wale aliojua watamwamini, kabla ya historia kuanza, kabla ya kuumba ulimwengu, ili wawe sehemu ya mwili wa Kristo, na pia wanachaguliwa kwa sababu ya uamuzi wao huru kabisa wanaoufanya katika maisha yao ya sasa, katika historia, wa kumwamini Yesu Kristo, uamuzi wanaoushika imara mpaka mwisho wa uhai wao wa hapa duniani. Wana-teolojia wengi wanaona mtazamo huu kuwa umerahisishwa kupita kiasi, na wako tayari kujizamisha katika maelfu ya kurasa yaliyo na hoja kutoka nje ya Biblia ili waendelee na mjadala huu. Lakini, kwa nini wasiisome na kujenga hoja zao kutoka ndani ya Biblia!? Kwani kwa hakika Yohana 3:16 iko wazi na inaeleweka kwa urahisi, vivyo hivyo kwa Warumi 8:28-39.

Yohana 3:16 SUV:
3.16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

Warumi 8:28-39:
8.28  Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu huwafanyia kazi wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.
8.29 Maana wale Aliowajua [uamuzi wao wa kumwamini Yeye] tangu asili (kabla ya kuumbwa ulimwengu), [hao] aliwachagua tangu asili [ili] wafananishwe na mfano wa Mwana Wake (i.e., wawe na mwili wa ufufuo kama wa Mwana Wake), ili [Mwana] awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.
8.30 Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita (ili waokolewe), na hao aliowaita, akawahesabu kuwa ni waongofu [kwa njia ya imani yao katika Kristo], na hao aliowafanya waongofu, hao akawatukuza (i.e., ufufuo wetu na uzima wetu wa milele uko imara katika mpango wa Mungu tangu kabla ya kuumbwa ulimwengu).
8.31  Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani atakayekuwa dhidi yetu?
8.32  Yeye asiyemwachilia (ambaye hakumhurumia - SRUV) Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?
8.33  Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki.
8.34  Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.
8.35  Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?
8.36  Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa.
8.37  Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.
8.38  Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,
8.39  wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Kwa nini wana-teolojia hawa wasiutumie muda wao kufanya utafiti na kujifunza jinsi ambavyo kanuni zinazofundishwa na nukuu hizo mbili hapo juu kwa yakini hazina mgongano wowote? Lakini kwa hakika teolojia ya leo (pale inapojadili mambo ambayo yanahusiana na Mungu) haina tofauti sana na siasa, na mahala ambapo motisha ya mjadala wowote ni siasa, basi utafiti wa ile KWELI unapotea njia na nafasi yake inachukuliwa na mabishano ya maneno matupu. Mimi sijihusishi na siasa za aina yoyote. Ninataka tu kujua maandiko ya Biblia yanasema nini. Kwa mjadala zaidi, unaweza kufungua link zifuatazo:

The meaning of the word “chosen” in the Bible.

Predestination and the Plan of God.

Election in (Peter #8). NB: Peter #8 iko katika Kiswahili pia.

Katika Bwana wetu mpendwa Yesu Kristo aliyeutoa uhai Wake ili sisi tuweze kuishi milele.

Bob L.
https://ichthys.com

ADDENDUM #2:

Swali liliulizwa:

Ikiwa Mungu ana mpango Wake ambao aliukusudia tangu hata hajauumba ulimwengu, kuna haja gani basi ya sisi wanadamu kufanya sala na maombi Kwake tukiwa hapa duniani?

Jibu:

Kuhusiana na suala la kusali au sala na maombi naweza kusema kwamba Mungu angeweza kuamua kuiondoa “historia” ya wanadamu kabisa, ambayo kama tulivyoona hapo juu ina lengo la kuwatenganisha watakaokataa kumtumaini Yeye na watakaokubali kufanya hivyo, na badala yake kuwaweka duniani wale – malaika na wanadamu – ambao alikwishajua watamtumaini Yeye, moja kwa moja katika uzima wa milele. Katika dhana hii, basi Bwana wetu Yesu Kristo asingelazimika kufa kile kifo cha mateso kwa ajili ya dhambi zote za ulimwengu. Hata hivyo, kwa kuwa uelewa wetu wa uhalisia wa msalaba ni mdogo kwa wakati huu tukingali bado ndani ya “historia” hiyo, na kwa kuwa Mungu angeweza kuepusha tukio hilo la msalaba dhidi ya Mwanaye mpendwa (cf. Matt. 26:39-42), basi kwa wazi kabisa msalaba ni tukio lililolazimu kutokea … na hivyo hivyo “historia” ililazimu kutokea ili ule mpango timilifu wa Mungu – ambao ni MMOJA TU na usio na mbadala wowote mwingine unaoweza kufikirika wenye tofauti hata kidogo tu – uweze kufanyika.

7 Basi ikawa, baada ya Bwana kumwambia Ayubu maneno hayo, Bwana akamwambia huyo Elifazi Mtemani, Hasira zangu zinawaka juu yako, na juu ya hao rafiki zako wawili; kwa kuwa ninyi hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.
8 Basi sasa, jitwalieni ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba, mkamwendee mtumishi wangu Ayubu, mjisongezee sadaka ya kuteketezwa; na huyo mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi; kwa kuwa nitamridhia yeye, nisiwatende sawasawa na upumbavu wenu; kwani ninyi hamkunena maneno yaliyonyoka katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.
9 Basi Elifazi, Mtemani, na Bildadi, Mshuhi, na Sofari, Mnaamathi, wakaenda, wakafanya kama vile Bwana alivyowaamuru; naye Bwana akamridhia Ayubu.
10 Kisha Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; Bwana naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza.
Ayubu 42:7-10 SUV

Kama tunavyoweza kuona katika nukuu hapo juu, ilikuwa muhimu na lazima kwa Ayubu kusali na kuwaombea kwa Mungu wale rafiki zake, kwanza ili waweze kuepuka hatua za kinidhamu / adibisho kutoka kwa Mungu, na pili ili Ayubu mwenyewe aweze kurejeshewa mali na familia pamoja na afya yake. Ama kwa hakika, Mungu mwenyewe aliamrisha kwamba sala na maombi hayo yafanyike. Hii ni kwa nini? Kwa sababu Mungu mwenyewe ameamuru / ameagiza uwepo wa historia na sala pamoja na maombi vikiwa ni sehemu muhimu ya historia hiyo katika kuhakikisha yale aliyoyaamuru yaweze kufanyika. Sala na maombi ni sehemu muhimu sana katika mpango wa Mungu ambamo amefungamanisha utashi wetu huru katika mpango huo timilifu. Kuna kanuni za msingi katika mpango wa Mungu, na sala pamoja na maombi ni namna mojawapo ambayo Mungu amekusudia ifanywe nasi ili impe Yeye fursa ya kuwabariki wale tunaowaombea kwa kufuata kanuni hizo za msingi. Utondoti (details) na undani wa kanuni hizo za msingi tunaweza tu kuuona katika mifano kama huo wa Ayubu hapo juu; hata hivyo, tuna mifano ya kutosha kutuwezesha kujua na kuelewa kwamba sala pamoja na maombi vina umuhimu mkubwa sana – ingawa hatujui kwa ukamili ni vipi na kwa namna gani. Tutajua kikamilifu undani wa jambo hili pale tutakapoingia katika ufufuo. Lakini kabla ya hapo, inatupasa kumtumainia Yeye na kuendelea kumpelekea sala pamoja na maombi yetu.
Hivyo, ingawa Mungu anaweza kufanya jambo lolote analoamua bila ya kwanza kusikia sala na maombi kutoka kwetu, hata hivyo ni dhahiri kutokana na yote ambayo Biblia inatusimulia kuhusiana na sala na maombi, kwamba ni jambo muhimu kwa sisi kulifanya, kutumia utashi [huru] tuliopewa kwa niaba ya ndugu zetu katika Kristo (kama ambavyo tunawatia moyo na kuwasaidia kwa njia nyingi nyingine za kimwili na kiroho). Je, Mungu wetu anaweza kutusaidia na kutupatia baraka zake bila ya sisi kusali na kuomba? Ndiyo! Lakini bila ya shaka yoyote ni jambo jema kwa sisi kuomba baraka hizo kutoka Kwake – na ni jambo jema zaidi kwa ndugu zetu katika Kristo kusali na kuomba kwa niaba yetu. Hii ni namna mojawapo muhimu sana ambayo inatuwezesha sisi tushiriki katika vita hii ya kiroho inayoendelea kwa wakati huu. Suala la sisi kusali na kuomba linashabihiana na mpiganaji katika vita anapomwomba sajenti wa platuni ahakikishe kwamba mpiganaji mwenzake hapewi “ugali na maharage” mara nyingi kwani “menu” hiyo huwa inamvuruga tumbo na kupunguza ufanisi wake na hivyo inamfanya asiwe askari mzuri na matokeo yake si mazuri vitani.

Kwa hivyo, Mkristo mwenzangu, mimi nasali kwa ajili yako – na pia ninakushukuru sana kwa sala na maombi yako kwa niaba yangu. Sote tunahitaji sala – na kwa wakati huu, tukingali hapa duniani, haijawekwa bayana [kwamba] tunahitaji sala kwa kiasi gani. Lakini tutakapofika katika makao yetu ya milele suala hili litawekwa wazi kwa ajili yetu. Mpaka wakati huo, tunafuata kanuni zote zinazotufanya tuwe askari wenye mafanikio katika vita hii hapa duniani ambamo Mpango wa Mungu unaendelea kufunuliwa Naye, na hili linajumuisha “kuomba bila kukoma” (1Wathess. 5:17).

Mimi rafiki yako katika Yesu Kristo Bwana wetu.

Bob L.

ADDENDUM #3:

(Kutoka E-Mail posting: Confronting False Groups and False Teaching V)

Swali # 18:

Mpendwa Pastor Robert,

Nakushukuru sana kwa majibu ya swali langu lililopita. Nina swali moja la ziada kwa wakati huu. 1. Wapo wahubiri wa Kikristo wanaosema / wanaofundisha kwamba Mungu amepanga kila kitu kinachotokea hapa ulimwenguni, ikiwa ni pamoja na kila uovu unaotokea. Je, jambo hili ni kweli kwa mtazamo na mafundisho ya Biblia, na kama ni hivyo, yawezekanaje akatupatia amri ya kujitenga na dhambi ikiwa Yeye Mwenyewe ameipanga dhambi hiyo itokee / ifanyike?

Kama kawaida, umaizi wako wa mafundisho ya Biblia utanisaidia hapa.

Natanguliza shukrani zangu.

Jibu #18:

Kila kitu kinachotokea au kinachofanyika katika ulimwengu, katika majira yake, historia yake, ni kudura ya Mungu, kinatokana na “decree” (amri) Yake. Mungu aliumba majira (time) na maada (space + matter), na hakuna kitu chochote kinachoweza kuwapo bila Yeye, bila amri Yake (Zab. 8:3; Isa. 42:5; Wakolosai 1:16-17; etc). Hili halina maana ya kwamba Mungu anapuuzia [uwepo wa] uovu – wazo hili lipite mbali kabisa! Mungu angeweza, kwa urahisi kabisa, akaumba ulimwengu na kuweka ndani yake viumbe ambao hawana uwezo wa kuamua kutenda uovu. Lakini viumbe wa aina hiyo wasingekuwa “sisi”, wasingekuwa kama tulivyo sisi. Ili sisi tuwe “sisi”, Mungu alituumba tukiwa na sura Yake, uwezo halisi wa kuitikia wito Wake kwa utashi wetu wenyewe … au la. Malaika wameumbwa na uwezo huo huo. Hivyo basi, majira yaliumbwa ili kutupatia sisi fursa ya kufanya uchaguzi, kufanya uamuzi. Kwanza, malaika waliumbwa kabla yetu ili wafanye maamuzi yao kuhusu kumtii Mungu au la, na tukio hili limekwishafanyika (Isa. 14:12-17: Eze. 28:11-19; Ufu. 12:3-4a); halafu sisi wanadamu tumepewa majira yetu (Mwa. 1:27; Ayubu 38:6-7) ili nasi tufanye uamuzi / uchaguzi wetu – jambo ambalo linaendelea kwa kila mmoja wetu anayefikia akili timamu (Mwa. 3:1-7; Yoh. 3:16 - 18; Waefe. 2:8-9), japo majira hayo (historia ya wanadamu - na malaika) yanakaribia mwisho wake. Amri / agizo la Mungu linauwezesha au linaufanya uamuzu au uchaguzi wetu katika ulimwengu huu uwezekane (na siyo kwamba unauzuia uamuzi / uchaguzi huo kama ambavyo baadhi ya watu ambao hawajalichambua suala hili kwa undani wanavyofikiria) – kwa sababu sisi hatuwezi kuwepo wala kuwa na sura au taswira ya Mungu bila ya amri au agizo (decree) hilo. Kila jambo tunalolichagua / tunalolifanyia maamuzi lina umuhimu. Kila jambo tunalolifanyia maamuzi limekwisha-amriwa au limekwisha-agizwa (decreed) – na katika hili (yaani maamuzi yetu) hatulazimishwi na Mungu, tunaamua katika utashi huru kabisa tulioumbwa nao; ni sisi tunaochagua katika kila jambo tunalolifanyia maamuzi. Mungu ni mwenye uweza mkubwa na ni mwenye hekima tosha iliyomwezesha kujua kila kitu kabla hakijafanyika na aliweka katika mpango wake wa uumbaji kila jambo tunalolifanyia maamuzi hapa duniani, yaani katika historia, katika majira / wakati wetu hapa duniani. Huu ndio ukweli wa uumbaji wa Mungu, ingawa kuna watu wanaotaka kuanzisha mabishano juu ya mpango wa Mungu. Hivyo alichokifanya Mungu ni [ki]timilifu: mpango huu pekee (hakuna mpango mwingine mbadala / wa kufikirika na wanadamu), ulio mtimilifu, uliojumuisha kila kitu, ulikuwa ni mpango pekee na ndiyo njia pekee iliyowezesha na inayowezesha viumbe wenye utashi kuishi [katika] milele, pamoja Naye, tukishiriki katika kila jambo na katika kila Alicho nacho, sisi ambao tuliamua, tulichagua kuwa Naye. Mpango ule timilifu ulilazimu uwepo wa viumbe wenye utashi ambao wataupinga na kuukataa, yaani malaika – Shetani na wenzake – na pia wanadamu walio wengi. Lakini haya ni maamuzi yao.

Bwana apewe sifa kwa ule uzima wa milele tulio nao kwa njia ya imani katika Mwana Wake Yesu Kristo, kwani kwa njia Yake pekee sisi tunaokolewa kutokana na imani yetu katika nafsi Yake timilifu, Mungu na mtu, na katika yote Aliyoyafanya katika kulipia gharama yote ya dhambi zetu pale msalabani!

Katika Yesu Kristo Bwana na Mwokozi wetu,

Bob L.

Mwendelezo wa ADDENDUM #3:

Swali #35:

Nimeandika barua (e-mail) ndefu kwa baba yangu mzazi, nikizungumzia “uhakika” wa uwepo (existence) wa Mungu kifalsafa. (Taarifa nyingine za faragha zimeondolewa).

Jibu #35:

Mimi nafikiri “utashi huru” ni dhana ya kutisha sana, lakini hii ndiyo sababu tuko hapa duniani; yaani tuko hapa kwa ajili ya kufanya maamuzi. Hata hivyo, kwa neema ya Mungu sisi kama waumini (na kwa wale ambao watamtumainia Mungu katika siku za usoni) utashi wetu huru unahusisha kumtumainia Yeye katika kila kitu. Hivyo hatuna kitu wala jambo la kuogopa wala kututia wasiwasi au shaka. Bwana Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu zote. Kwa sisi ambao tumefanya azimio mioyoni mwetu la kuweka imani na tumaini letu la kuwa na uzima wa milele Kwake, mambo yote tunayokabiliana nayo baada ya kufanya azimio hilo kuu yanahusiana na mitihani ya jinsi tunavyoitikia wito Wake, tukidhihirisha kwamba tunampenda Yeye zaidi ya kitu chochote katika ulimwengu huu wa mpito.

Tunapaswa kuweka wazi mioyoni mwetu kwamba tunampenda Bwana Yesu Kristo, na siyo kwa upendo vuguvugu tu. Tunapaswa kumpenda Bwan Yesu kwa upendo ulio “red hot” - kama moto wa tanuri (furnace). Na kwa wale wanaoufahamu upendo huu, hili ni jambo jema na la kufurahisha tunapoliona hapa duniani. Ni muhimu sana kutoacha migogoro (upheavals) ya hisia zetu yatupe mfadhaiko wa moyo au kutupoteza njia; pia ni muhimu kutoyafikiria mateso yetu hapa duniani kupita kiasi [hata] tupate mfadhaiko wa moyo au kutupoteza njia. Kiuhalisia, mchakato wetu wa Kikristo ni rahisi sana. Sali na kuomba kila unapopata wasaa, soma Biblia yako kila siku, endelea kukua kiroho kwa njia ya kufundishwa Biblia, amini unayoyasoma na kufundishwa, endelea kulitumikia Kanisa la Bwana wetu – yaani Wakristo wenzetu – kutokana au kulingana na karama za kiroho alizotupatia Mungu. Hili la kuhudumia Kanisa linahitaji tafakuri na kupima kwa uangalifu sana kile Roho Mtakatifu anachotuambia mioyoni mwetu na uelekeo Anaotupeleka. Tunalihudumia Kanisa kwa jinsi tunavyoishi maisha yetu Kikristo na kwa namna nyingine mbalimbali za utumishi na misaada.

Siku zote mimi husema kwamba katika kuishi maisha yetu ya Kikristo, yaani katika kuitumia kweli ya Biblia katika maisha yetu, ni jambo muhimu sana kuhakikisha tunajizuia kuwa na misimamo mikali yenye mrengo wa kulia au kushoto mwa njia yetu hii ya imani tunamopita (extremism). Kwa mfano, kwa Mkristo anayetafuta kazi, kuutumia muda wake wote katika kutafuta ajira si jambo jema; na pia [kwa Mkristo huyu huyu] kutofanya juhudi yoyote katika kutafuta ajira na badala yake kungojea ajira imwangukie kutoka mbinguni si jambo jema. Mfano mwingine: kama lengo lako ni kumtangazia Injili mtu asiyeamini (uinjilisti) na mbinu yako katika jukumu hili jema ni kuielezea Injili katika utondoti (detail) mkubwa kupita kiasi (badala ya kumpa ujumbe rahisi wa Neno) unaohusiana na hali yetu ya dhambi na kazi aliyoifanya Bwana wetu kwa ajili ya wokovu wetu, unaweza kujikuta ukipoteza malengo yako; na pia kutomweleza mtu huyu [asiyeamini] kiasi cha kutosha cha ujumbe wa Injili na kutarajia Mungu akupe thawabu kwa juhudi zako hizo [finyu] si jambo jema. Katika maisha ya Kikristo, ambapo Mkristo anatakiwa kuishi kwa kulitumia Neno la Mungu, wale waumini wapya – na wale waumini ambao siyo “wapya” bali ni wa siku nyingi ila tu sasa ndiyo wameanza kujifunza Neno la Mungu kwa juhudi stahiki na wanaanza kutafuta kusudi la Mungu kwa maisha yao hapa duniani – mara nyingi wanaenda kama kijana anayeanza kujifunza kuendesha gari, pale anaposhika usukani kwa mara ya kwanza. Pale mtu anapoanza kujifunza kuendesha gari, ni jambo la kawaida kumwona dereva huyu mpya akiyumba mara kulia na mara kushoto bila tahadhari wala simile. Lakini mara dereva huyu anapopata uzoefu wa kutosha, hufanya marekebisho ya usukani, tena bila hata kufikiria – anafanya “automatically” tu – na anahakikisha gari linakaa katikati ya upande – au “sight” - wake. Vivyo hivyo jinsi tunavyojifunza kweli ya Biblia zaidi na zaidi, na jinsi tunavyozidi kupata uzoefu katika kulitumia Neno katika maisha yetu kama Wakristo, tunaongeza usikivu wetu kwa ile sauti ya Roho Mtakatifu na tunafanya marekebisho katika mwenendo wetu wa Kikristo bila hata “kufikiria sana”.

Mwendelezo wa ADDENDUM #3 (E-mail ile ile):

Swali #45:

Habari yako Dkt. Luginbill,

Naomba Mungu mambo yako yaende sawa na salama katika familia yako na katika huduma yako kwa Kanisa la Bwana wetu Yesu Kristo.

Dkt., wakati fulani uliandika kuhusu watu wasioamini (watu wasio Wakristo) kwamba hawamtaki Mungu, na mwisho wa yote hili ndilo wanalovuna, yaani wanapelekwa Jehanamu ambako kuna maisha bila Mungu.

Je, unaweza kunieleza kwa upana zaidi jinsi ulivyofikia hitimisho hili la Kibiblia (Matt. 7:14) na kwa nini wasioamini hawataki kuweka imani yao katika muumba wao? Kwa nini walio wengi kati ya wanadamu wameitumia zawadi tuliyopewa bure na Mungu wetu ya utashi huru kumkataa Mungu aliyewaumba? Kwa nini wateule ni wachache kiasi hiki? Mtu asiyeamini ana matumaini gani akiwa nje ya maisha na Mungu?

Natanguliza shukrani kwako.

Jibu #45:

Habari yako rafiki yangu, nimefurahi kuupata ujumbe wako na swali lako.

Kuhusiana na swali lako; ebu [kwanza] tuanze kwa kukubaliana kwamba Mungu ni mtimilifu. Kwa hivyo, mpango Wake ni mtimilifu pia. Na hii ina maana kwamba kila jambo linalotukia ndilo jambo timilifu lililostahili kutukia. Hii ni kwa sababu kama kungekuwa na njia nzuri [na njema] zaidi kwa matukio hayo kufanyika, basi mpango huu wa Mungu ambao kila mmoja wetu anaushuhudia ukifanyika mbele ya macho yake usingekuwa mtimilifu, kwa sababu hapo sasa usingekuwa “mzuri” [na mwema] kama ule mpango mwingine wa kufikirika. Hivyo kwa kweli hakuna uwezekano wa uwepo wa mipango mingine ya kufikirika ya Mungu zaidi ya ule mpango mmoja mtimilifu, na hivyo Mungu wetu ameamuru kufanyika kwa mpango huu mmoja, mpango ulio mtimilifu, aliouunda kutoka milele iliyopita – kwa hakika kabla hata hajauumba ulimwengu. Ama kweli kazi ya Mungu haina makosa. Hivyo basi wokovu wako na wokovu wangu hauwezi kutokea, nje ya mpango huu mmoja mtimilifu. Na hivyo ikiwa watu wengine hawaokolewi, kwa hakika hii si kwa sababu Mungu wetu hakutaka waokolewe kwani Yeye anataka watu wote waokolewe (soma 1Tim. 2:4).

3.16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
3.17 Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.
3.18 Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa*; kwa sababu hakuliamini jina [yaani Nafsi] la Mwana pekee wa Mungu.
Yohana 3:16-18 SUV
*Utashi huru!

Mungu anasikitishwa sana na ukweli kwamba watu wengine hawataki kuokolewa, hawataki kuamini, zaidi ya tunavyosikitishwa mimi na wewe, kwa kuwa Yeye ni mtimilifu. Lakini kama mpango wa Mungu usungekuwa unaendelea kufanyika katika namna timilifu , mpango huu ambao ndio pekee mtimilifu na hakuna mwingine, basi wewe na mimi tusingeokolewa.

Pili, Mungu ni mwongofu na mwenye haki kabisa kabisa. Haiwezekani kwa Mungu kuwa mwonevu, vinginevyo Yeye asingekuwa Mungu (somo hili linapatikana katika BB1: Theology, tovuti ya https://ichthys.com). Kwa kuwa Yeye ni mwenye haki kwa kiwango timilifu, hakuna Analolifanya kwa watu wasiomwamini ambalo ni uonevu, kuanzia jinsi anavyowashughulikia na kuwajali katika maisha yao hapa duniani mpaka atakavyowahukumu [siku ya mwisho] kwa kukataa kwao kuja kwa Bwana Yesu Kristo (nukuu ya Yoh. 3:16-18 hapo juu). Je, Mungu amefanya kila kitu ili kuhakikisha hata wasioamini waokolewe? Kwa hakika Amefanya hivyo, kwani Bwana Yesu amekufa kwa ajili ya kila dhambi ya kila mwanadamu, [ikiwa ni pamoja] na kila dhambi ya wale wasioamwamini Yeye (tazama somo hili katika Unlimited Atonement, tovuti ya https://ichthys.com). Kwanza, Mungu amempa uhai kila mtu asiyeamini. Pili, Mungu amempa utashi huru kabisa kila mtu anayekataa kumwamini. Na tatu, Mungu amempa kila mtu asiyemwamini uwezo wa kuepuka lile ziwa la kutisha la moto kwa kuipokea [tu] ile zawadi ya Mwanaye Yesu Kristo. Hata hivyo, watu wengi wanaikataa zawadi hii kuu ya neema. Na hili si kosa la Mungu, kwani kila mtu ana utashi [huru kabisa] unaomwezesha kukubali au kukataa (Mwanzo 1:26a). Je, kuna jambo lingine ambalo angeweza kulifanya zaidi ya kumtoa Mwana Wake wa pekee ili abebe mzigo mzima wa adhabu za dhambi zetu zote ambao watu hawa wasioamini (pamoja na dhambi za sisi tunaoamini) walistahili? Kwa kiasi kikubwa sana hii ni zaidi ya kile ambacho tunastahili kama adhabu ya dhambi zetu. Lakini hata hivyo Mungu wetu aliyafanya yote hayo [kwa ajili yetu], kutokana na upendo wake mkuu kwetu. Naye ni upendo. Na pia aliyafanya haya kutokana na haki yake kuu – vinginevyo hakuna hata mmoja wetu angeweza kuokolewa, hii ikiwa ni pamoja na mimi na wewe.

Hakuna kabisa matumaini kwa wasioamini – na hata kwa sisi tunaoamini – bila ya Mungu. Wanaoikataa neema [ya bure] ya Mungu ya uzima wa milele wakati mbadala wake ni hukumu ya milele [katika ziwa la moto] wanaonekana wendawazimu, sivyo? Kwa hakika ndivyo. Lakini huo ndio uamuzi wa wengi kati ya wanadamu (Matt. 7:13-14). Hii ni kwa nini? Ni kwa sababu ya kiburi, majivuno. Watu wasioamini hawataki kuweka utashi wao chini ya matakwa ya Mungu ili maisha yao yaongozwe na Mungu. Je, unamkumbuka yule kiumbe maarufu mwenye tabia hii? Unapaswa kumkumbuka! Huyu ni Shetani, na malaika waliomfuata wana tabia hiyo hiyo. Kama kuna kiumbe ambaye alipaswa kujua kwamba Mungu hawezi kushindwa, na kwamba kumkataa Mungu na uzima wa milele pamoja Naye ulikuwa ni uamuzi mbaya kuliko maamuzi yote mabaya yanayowezekana kufanywa na kiumbe yeyote, basi kiumbe huyu ni Shetani – kwa sababu Shetani alikuwa mbele za uso wa Mungu kwa dahari (aeons) tele, siyo tu akifaudu uwepo wa Mungu na neema zote zinazoambatana na uwepo huo, bali pia akiutazama na kuutafakari uweza Wake mkuu na silika (character) Yake timilifu.

12Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni,
Ewe nyota ya asubuhi, mwana wa
mapambazuko!
Umetupwa chini duniani,
wewe uliyepata kuangusha mataifa!
13Ulisema moyoni mwako,
“Nitapanda juu hadi mbinguni,
nitakiinua kiti changu cha enzi
juu ya nyota za Mungu,
nitaketi nimetawazwa juu ya mlima wa
kusanyiko,
kwenye vimo vya juu sana vya mlima
Mtakatifu.
14Nitapaa juu kupita mawingu,
nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.”
15Lakini umeshushwa chini kaburini,
hadi kwenye vina vya shimo.
16Wale wanaokuona wanakukazia macho,
wanatafakari hatima yako:
“Je, huyu ndiye yule aliyetikisa dunia
na kufanya falme zitetemeke,
17yule aliyeifanya dunia kuwa jangwa,
aliyeipindua miji yake na ambaye
hakuwaachia
mateka wake waende nyumbani?”
Isa. 14:12-17

11Neno la BWANA likanijia kusema:
12“Mwanadamu, mfanyie maombolezo mfalme
wa Tiro nawe umwambie: ‘Hili ndilo BWANA
Mwenyezi asemalo:
“ ‘Ulikuwa kipeo cha ukamilifu,
ukiwa umejaa hekima na mkamilifu
katika uzuri.
13Ulikuwa ndani ya Edeni,
bustani ya Mungu,
kila jiwe la thamani lilikupamba,
akiki nyekundu, yakuti manjano,
zumaridi, krisolitho, shohamu na yaspi,
yakuti samawi, almasi na zabarajadi.
Kuwekwa kwa hayo mapambo na
kushikizwa kwake kulifanywa kwa
dhahabu.
Siku ile ulipoumbwa yaliandaliwa tayari.
14Ulitiwa mafuta kuwa kerubi mlinzi,
kwa kuwa hivyo ndivyo nilivyokusimika.
Ulikuwa kwenye mlima mtakatifu wa Mungu,
ulitembea katikati ya mawe ya moto.
15Ulikuwa mnyofu katika njia zako
tangu siku ile ya kuumbwa kwako,
hadi uovu ulipoonekana ndani yako.
16Kutokana na biashara yako iliyoenea,
ulijazwa na dhuluma nawe ukatenda
dhambi.
Hivyo nilikuondoa kwa aibu kutoka katika
mlima wa Mungu,
nami nikakufukuza, Ee kerubi mlinzi,
kutoka katikati ya mawe ya moto.
17Moyo wako ukawa na kiburi
kwa ajili ya uzuri wako,
nawe ukaiharibu hekima yako
kwa sababu ya fahari yako.
Kwa hiyo nikakutupa chini,
nimekufanya [kioja] mbele ya wafalme.
18Kwa dhambi zako nyingi na biashara yako ya
dhuluma,
umenajisi mahali pako patakatifu.
Kwa hiyo nilifanya moto utoke ndani yako,
nao ukakuteketeza,
nami nikakufanya majivu juu ya nchi,
machoni pa wote waliokuwa
wakitazama.
19Mataifa yote yaliyokujua yanakusta[a]jabia,
umefikia mwisho wa kutisha na hutakuwepo
tena milele.’’
Ezekieli 28:11-19

Lakini kiburi kiliharibu fikra za Shetani naye akajiaminisha kwamba angeweza kupata njia ya kumshinda Mungu na kisha yeye mwenyewe ndiyo awe Mungu.

Kwa hiyo hili si suala la kukosa / kutokuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu Mungu na hulka Yake. Hakuna kiumbe ambaye alikuwa na ufahamu juu ya Mungu zaidi ya Shetani. Hili ni suala la utashi [huru]. Vivyo hivyo watu wasioamini wanaifanya mioyo yao kuwa migumu dhidi ya kweli ya Biblia inayowakumbusha kwamba siku moja watakufa, kwamba wao ni wenye dhambi, kwamba Mungu yuko na ni mwenye uongofu timilifu ambao unamlazimu [Mungu huyu huyu] kuwahukumu wanadamu siku ya mwisho (War. 1:18-32). Kila mwanadamu anaujua ukweli [huu] ndani ya moyo wake (Mhubiri 3:11), pia ukweli huu unaonekana wazi na kwa ung’avu katika uumbaji Wake (pia Zab. 19:1-6; cf. War. 1:19-20). Ni pale kiburi kinapoamua kugeuza sura yake kutoka kwenye ukweli ndipo moyo unakuwa mgumu. Hapo ndipo wasioamini wanabuni kwa ajili yao wenyewe kila aina ya kisingizio ili kuhalalisha uamuzi wao kichaa, wengine wakitamka kwamba hakuna Mungu, au kwamba Mungu yuko lakini hajali yanayoendelea katika ulimwengu na viumbe Wake, au kwamba Yeye ni mwonevu kwani Hajahakikisha kila mtu anaipata Injili na hivyo hana haki ya kuwahukumu – au aina yoyote ya upumbavu utakaowawezesha kujidanganya kwamba maisha hayana mwisho. Wanajua kwamba hii si kweli, kwamba maisha ya mwanadamu yana mwisho wake; lakini wanautia kitanzi ukweli huu ndani ya mioyo yao na kuumaliza, na kisha wanaukumbatia uwongo badala yake.

Uungu (godliness), kwa kiasi kikubwa ni mabadiliko ya mioyo yetu kutokana na ukweli tunaojifunza (War. 12:2) na matokeo yake ni kuyaona mambo yote kama Mungu anavyoyaona, yaani katika uhalisia wake, na siyo kama ulimwengu unavyoyaona, yaani yanavyoonekana kwa nje tu. Na jinsi tunavyozidi kumsogelea Mungu, ndivyo inavyozidi kudhihirika katika mioyo yetu jinsi uamuzi wa wanadamu wenzetu wa kutoamini ulivyo wa ajabu na wa kushangaza.

Katika Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo,

Bob L.

ADDENDUM #4:

(Kutoka “Mutual encouragement in Christ Part X, Q & A ya 2 January 2021)

Swali #3:

Habari yako Profesa,

Una mtazamo gani kuhusiana na fundisho la kudura [ya Mungu juu ya uumbaji Wake], yaani pre-destination?

Natanguliza shukrani.

Jibu #3:

Fundisho la “kudura” au “predestination” ni la Kibiblia – lakini lile kundi linaloitwa “hyper-Calvinists” hawaelewi fundisho hili lina maana gani!

Biblia inaizungumzia na kuifundisha kanuni ya “kudura ya Mungu” na dhana zinazohusiana nayo katika kurasa zake hapa na pale … lakini wakati huo huo inatuamrisha “tufanye A” na “tusifanye B” katika karibu kila ukurasa wake. Kwa maneno mengine, siyo tu kwamba sisi wanadamu tuna utashi ulio huru kabisa, bali “utashi” ndiyo sababu pekee ya kuumbwa kwetu [sisi wanadamu], na ndiyo lengo pekee la kupewa ile taswira au sura ya Mungu (Mwa. 1:26a) ambapo tumepewa utashi huu unaoshabihiana na ule utashi alio nao Mungu mwenyewe, na kusudi lake [utashi huu tuliopewa] ni ili tuamue kuitikia wito Wake (Yoh. 3:16-18; Waefe. 2:8-9). Hivyo basi, vyovyote unavyoichukulia / unavyoielewa kanuni ya “kudura ya Mungu”, haipingani na kweli hizi za msingi kabisa ambazo zinatawala na kuendesha maisha ya kila mtu, anayeamini na asiyeamini.

Kwa kifupi (kwa maelezo / mafundisho ya utondoti zaidi soma BB 4B: Soteriology at https://ichthys.com), Mungu alijua, kabla hajaanza kuumba ulimwengu na vyote vilivyomo, maamuzi ya kila kiumbe Wake mwenye utashi – malaika na watu – kuhusiana na kila jambo. Mungu alipaswa kufahamu, kwani Kristo amekufa kwa ajili ya kila dhambi ya kila mtu (War. 3:23; War. 2:24; Yoh. 3:16; Waebr. 9:22; nk). Dhambi hizi zote zingewezaje kufahamika kama ufahamu [wa Mungu] wa mambo yote kabla hayajatokea haukuwa mtimilifu katika utondoti wake? Kwa kuwa Mungu alijua kitakachoteokea, kitakachoamuliwa / kitakachochaguliwa na kila mtu, basi Mungu aliamuru kitu hicho kitokee, kifanyike; lakini aliamuru yale tu [ambayo] tutakayoyachagua, tutakayoyafanyia maamuzi kutokana na ufahamu Wake wa historia [yetu] yote kabla ya uumbaji Wake wa ulimwengu. Kwa hakika, bila ya Yeye kuamuru uwepo wa majira, maada na historia, sisi viumbe Wake tusingekuwa na fursa wala mahala pa kuishi na kufanya maamuzi yetu! Mambo haya yanaweza kuwa magumu sana kuelewa kwa sisi wanadamu, lakini kwa Mungu wetu ni rahisi kabisa! Jambo ambalo lilikuwa gumu, gumu kweli kweli, lilikuwa ni lile la Bwana Yesu kufa kwa ajili ya dhambi zetu na kwa Mungu Baba kumtoa Yeye sadaka kwa ajili yetu.

Tatizo jingine la mawazo ya kimapokeo katika makundi mbalimbali ya Kikristo kuhusiana na fundisho hili ni kwamba wanaifundisha kanuni hii katika mtazamo ambao ni kinyume kabisa na sababu na makusudi yake ya kuwekwa katika Biblia. Katika kitabu cha Warumi, kwa mfano, Paulo, akiandika chini ya ufunuo wa Roho Mtakatifu analielezea suala hili kwa malengo ya kutotuingiza katika ubishi na mkanganyiko wa kiteolojia na badala yake litupatie uhakika: mpango wa Mungu ni kamili na mtimilifu; Mungu habahatishi na katika mpango Wake huu hakuna hata harufu ya kamari; katika mpango Wake huu hakuna mabadiliko mara baada ya majira na historia kuanza; ikiwa tuna nia ya kuokolewa na tunaishika imani yetu katika Kristo mpaka mwisho, hakuna anayeweza kutupokonya kutoka katika mkono wa Mungu (War. 8:28-30).

Wako katika Yesu Kristo Bwana na Mwokozi wetu mpendwa,
Bob L.

ADDENDUM #5:

Kutoka “Eschatology Issues #56; Q & A #5”.

Jibu #5:

[Kuhusiana na suala la “kudura ya Mungu”] nitasema suala linalosababisha tatizo la ‘kutoelewa’ kwa baadhi ya Wakristo na wengine wasioamini, ni suala la ile taswira au sura ya Mungu tuliyopewa – sisi makundi mawili ya viumbe Wake wenye utashi, yaani malaika na wanadamu. Sisi ni “miungu” au “wakuu” au “hodari” katika maana ya wale wenye uwezo wa kuchagua, wenye utashi huru (Zab. 103:20; Zab. 82:6; Yoh. 10:34). Utashi una nguvu kuu kuliko vyote katika ulimwengu … ukiacha Mungu ambaye ndiye aliyetupatia nguvu hii.

Mungu aliumba ulimwengu ulio na viumbe wenye utashi huru kabisa; na alijua kwamba uasi utafanywa dhidi Yake na baadhi ya viumbe Wake hao; alijua pia kwamba upatanishi na viumbe Wake utahitaji au utalazimu Zawadi kuu na yenye gharama kubwa sana Kwake – Zawadi ambayo ni baadhi tu ya viumbe Wake hao wataamua au watachagua kuipokea.

Kimsingi, uchaguzi huu unadhihirisha kwamba tuko tayari kujishusha na kukubali kwamba Mungu ni Mungu [wetu] , licha ya kwamba tunao utashi huru kabisa wa kuukataa ukweli huu. Malaika walikuwa na uelewa mzuri zaidi wa suala hili kuliko Adamu na Eva wakati wanafanya uchaguzi wao (Ufu. 12:3-4a); hata hivyo Adamu na Eva walifanya maamuzi ya wazi kabisa kutokana na utashi wao, Eva akidanganywa na Shetani lakini Adamu akifahamu wazi kabisa moyoni mwake kwamba alikuwa anavunja amri ya Mungu. Adamu na Eva walifahamu fika matokeo ya ukaidi wao, kwani Mungu alikwishawaambia ukweli tupu juu ya yale yatakayowakuta ikiwa watavunja amri Yake (Mwa. 2:16-17); hata hivyo hawakuliweka jambo hili mioyoni mwao kwa uthabiti uliohitajika, Eva akishindwa kujizuia na kishawishi cha “kuwa kama Mungu” au “miungu” (neno la Kiebrania ni moja kwa “Mungu” na “miungu”), Adamu akishindwa kujizuia kuishi bila Eva. Kwa upande wa malaika, Shetani alijiaminisha yeye mwenyewe na baadhi ya wenzi wake (Ufu. 12:4a) kwamba matokeo ya uasi dhidi ya Mungu hayatakuwa mabaya na badala yake watakuwa huru kutokana na utawala wa Mungu. Kwa hiyo uchaguzi na uamuzi kati ya malaika na wanadamu unafanana kabisa, lakini mazingira yao yalikuwa tofauti – malaika walikuwa uso kwa uso na Mungu mwenyewe lakini wanadamu wale wawili walikuwa katika bustani ya Edeni, wakitembelewa na Mungu mara moja moja tu. Malaika walikuwa na ufahamu wa Mungu zaidi ya ule ufahamu wa wale wanadamu wawili, lakini hawakufahamu kila kitu – vinginevyo wasingeasi! Hawakuujua mpango wa Mungu katika ukamilifu na utimilifu wake wote. Vivyo hivyo kwa Adamu na Eva, ingawa Mungu aliwaelezea ukweli ulivyo kwa uwazi kabisa na matokeo ya uasi yatakavyokuwa. Kuna ufahamu wa kinadharia na kuna ufahamu unaotokana na kujifunza matokeo ya matendo yako – ambayo wakati mwingine yanauma, soma 1Wakor. 2:8!

Mpango wa Mungu ni mtimilifu. Kama Mungu akijifunua katika utukufu na uweza Wake wote mkuu mbele za yeyote katika ya viumbe Wake wenye utashi huru – malaika na wanadamu – hakuna hata mmoja wetu atakayeweza wala kuthubutu kumpinga na kuasi; hilo wazo halitaingia kabisa katika mioyo yetu, kwa sababu kiuhalisia ndani ya mioyo yetu tunatambua matokeo ya uasi huo. Lakini utashi huru wa mwanadamu au malaika unapopewa (au unapowekwa katika) mazingira ambamo kuna uhuru halisi (kwa mfano mazingira ambamo utukufu, uweza, nguvu ya Mungu, n.k. vimefichika kwa kiasi kikubwa) – hata kama utashi huu una taarifa kamili kuhusu ukweli ambao kiumbe huyu yuko huru kuukataa / kutouamini na kuupuuza – basi hulka na matakwa halisi ya kiumbe huyu yatadhihirika. Hiki ndicho kilichotokea na ndicho kinachoendelea kutokea – huu ndio mpango wa Mungu ulio mtimilifu. Ulimwengu huu ndipo mahala “pa kupepetea nafaka” palipo timilifu na panapofaa kwa malengo ya mpango wa Mungu, mahala ambapo “ngano” inatenganishwa na “makapi”.

Pepeto lake liko mkononi [mwake], naye atasafisha pa kupepetea nafaka, na ngano yake ataiweka ghalani, lakini makapi atayachoma kwa moto usiozimika.
Matt. 3:12 SNT

Katika Yesu Kristo Bwana wetu,

Bob L.

Kutoka Q & A ya ADDENDUM #5 (E-mail ile ile).

Swali #6:

Mwulizaji aliuliza kwa nini Biblia haielezei kwa undani zaidi kuhusu mpango wa Mungu unavyohusisha utashi huru walio nao malaika na wanadamu na kudura ya Mungu (pre-destination).

Jibu #6:

Sote tungependa kufahamu zaidi kuhusiana na mpango wa Mungu. Hata hivyo tumepewa taarifa za kutosha sana na katika utondoti mkubwa tu. Na pia, ufahamu pekee hautatui matatizo yetu kama hatuufanyii kazi. Kwa hakika, ufahamu wa matokeo ya uamuzi wake haukumzuia Shetani katika azma na nia yake ya kuasi, na wala haukuwazuia Adamu na Eva kuvunja amri ya wazi ya Mungu … wala ufahamu hautuzuii sisi binadamu wa leo kutenda dhambi (na tunatenda kila aina ya makosa ambayo kwa kweli tunapaswa kutoyatenda). Wakati mwingine baadhi yetu tunajifunza kutokana na matokeo ya matendo yetu. Kwa hakika wanyama hujifunza kutokana na matokeo ya makosa yao. Nakumbuka katika jaribio moja la kisayansi, kundi la panya liliwekewa kinywaji kwa njia ya mrija, kinywaji ambacho kilikuwa na kilevi ndani yake: sasa, yule panya dume aliyetawala kundi lote alimiliki ule mrija … akalewa na akapoteza hadhi yake kwa sababu ya kulala usingizi kupita kiasi. Alipoamka hakuusogelea tena mrija ule! Wanadamu wana tabia ya kusahau [kwa makusudi] makosa waliyotenda kama vile makosa hayo – na matokeo yake – hayakutokea. Huo ni utashi huru. Sisi wanadamu tuna uwezo wa kuutelekeza ukweli ndani ya mioyo yetu; lakini kiuhalisia ukweli unaendelea kuwa ukweli – nje ya mioyo yetu. Lakini pia tunao uwezo wa kuupa kisogo ulimwengu – wenye udanganyifu tele – na kuukumbatia ukweli, na tunapofanya hivyo, tunapomkumbuka Yeye ambaye ndiye KWELI, basi, tukiongozwa na Roho Mtakatifu ndani yetu, tunakuwa na uwezo siyo tu wa kujifunza ufahamu wa ile kweli, bali tunaiweka kweli hiyo ndani ya mioyo yetu na kuifanyia kazi ndani ya mioyo yetu na katika maisha yetu kwa utukufu wa Mungu. Na tunayo / tumepewa aina hii ya ukweli kwa kiasi cha kutosha kabisa – katika Biblia – inayotuwezesha tuendelee kutembea katika hii njia nyembamba na ngumu, lakini inayotupeleka kwenye uzima wa milele. Kinachohitajika ni utashi wetu tu uwe tayari kuukumbatia ukweli huu.

Ninaitazamia ile siku ya ufufuo na thawabu na sherehe ya furaha nikiwa na ndugu zangu katika Bwana ambao wanasonga mbele katika kweli.

Nashukuru kwa sala zako!

Katika Yesu Kristo aliye KWELI yenyewe,

Bob L wa https://ichthys.com

=0=

https://sayuni.co.tz