Mchawi/Mpiga-ramli wa Endori

 

Msomaji wangu, Bwana Yesu asifiwe sana!

 

Leo nitazungumzia tukio linalomhusu mfalme Sauli, moja kati ya matukio ya siku za mwisho kabisa za maisha yake mfalme huyu ambaye masimulizi ya maisha yake yanasikitisha sana. Kwa hakika kuna mafundisho muhimu katika masimulizi ya maisha yake kwetu sisi Wakristo. Na tukio mojawapo, yaani uamuzi wa mfalme Sauli wa kwenda kuulizia hatma ya vita kati ya taifa alilokuwa akilitawala la Israeli na taifa la Wafilisti iliyopiganwa kesho yake kwa mpiga-ramli au mchawi, badala ya kuulizia kwa Mungu mwenyewe kama ilivyokuwa desturi hapo awali lina umuhimu/fundisho kubwa kwetu sisi Wakristo tunaoishi hapa duniani siku hizi. Tukio hili linasimuliwa katika kitabu cha 1Samweli 28. Nasisitiza tena, tukio hili lina mafundisho mengi na makuu kwetu sisi Wakristo wa leo, kwani wametokea “wachungaji” ambao moja kati ya shughuli zao ni kupiga ramli kwa wazi kabisa, ingawa wao wenyewe na waumini wao [ambao tusisahau wanajiita Wakristo] wanadai matendo hayo (ya kupiga ramli) kuwa ni sehemu ya ibada ya kawaida ya kusanyiko la Wakristo, ati ni unabii! Basi tuanze kwa kusoma aya kadhaa zinazoonyesha jinsi Mungu alivyokataza kabisa matendo haya na mengine ya aina hiyo.

 

10Asionekane mtu yeyote miongoni mwenu ampitishaye mwanawe au binti yake katika moto, atakayefanya uaguzi, ulozi, anayetabiri nyakati, anayejishughulisha na uchawi, 11wala arogaye kwa kupiga mafundo, wala mwaguzi au anayeabudu mizimu, wala awaombaye wafu. 12Mtu yeyote afanyaye mambo haya ni chukizo kwa Bwana, tena ni kwa sababu ya matendo haya ya kuchukiza wayafanyayo ndiyo maana Bwana Mungu wenu atayafukuza mataifa hayo mbele yenu.

Kumb. 18:10-12 NEN Biblia

 

10Asionekane mtu yeyote miongoni mwenu ampitishaye mwanawe au binti yake katika moto, atakayefanya uaguzi, ulozi, anayetabiri nyakati, anayejishughulisha na uchawi, 11wala arogaye kwa kupiga mafundo, wala mwaguzi au anayeabudu mizimu, wala awaombaye wafu. 12Mtu yeyote afanyaye mambo haya ni chukizo kwa Bwana, tena ni kwa sababu ya matendo haya ya kuchukiza wayafanyayo ndiyo maana Bwana Mungu wenu atayafukuza mataifa hayo mbele yenu.

1Samweli 15:23 NEN Biblia

 

17Wakawatoa kafara wana wao na mabinti zao katika moto. Wakafanya uaguzi na uchawi, nao wakajiuza wenyewe katika kutenda uovu machoni pa Bwana, wakamghadhibisha.

1Wafalme NEN Biblia

 

14Ndipo Bwana akaniambia, “Manabii wanatabiri uongo kwa jina langu. Sikuwatuma, wala sikuwaweka, wala sikusema nao. Wanawatabiria maono ya uongo, maaguzi, maono ya sanamu zisizofaa kitu, na madanganyo ya mawazo yao wenyewe.

Yer. 14:14 NEN Biblia

 

 

16.16 Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua.

16.17 Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu.

16.18 Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.

16.19 Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila, wakawakokota mpaka sokoni mbele ya wakuu wa mji;

16.20 wakawachukua kwa makadhi, wakasema, Watu hawa wanachafua sana mji wetu, nao ni Wayahudi;

16.21 tena wanatangaza habari ya desturi zisizokuwa halali kwetu kuzipokea wala kuzifuata, kwa kuwa sisi tu Warumi.

16.22 Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora.

16.23 Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana.

16.24 Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale.

Matendo 16:16 SUV

 

5Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa.

Yakobo 1:5 NEN Biblia

 

6 [Mfalme Manase] Akawatoa wanawe kuwa kafara kwa kuwapitisha katika moto katika Bonde la Ben-Hinomu, akafanya ulozi, uaguzi na uchawi, akataka ushauri kwa wenye pepo wa utambuzi na wenye kuwasiliana na mizimu. Akafanya maovu mengi machoni pa Bwana, akaichochea hasira yake.

Nyakati 33:6 NEN Biblia

 

5.19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu [mwenendo wa aibu], ufisadi,

5.20 ibada ya sanamu [madawa ya kulevya – pharmakeia, kutegemea watu, malaika], uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

5.21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.

Waga. 5:19-21

 

5“Basi nitakuja karibu nanyi ili kuhukumu. Nami nitakuwa mwepesi kushuhudia dhidi ya wachawi, wazinzi, waapao kwa uongo, wanaopunja vibarua malipo yao, wanaowaonea wajane na yatima, na wanaowanyima wageni haki, lakini hawaniogopi mimi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

Malaki 3:5 NEN Biblia

 

23 Mwanga wa taa

hautaangaza ndani yako tena.

Sauti ya bwana arusi na bibi arusi

kamwe haitasikika ndani yako tena.

Wafanyabiashara wako walikuwa watu maarufu wa dunia.

Mataifa yote yalipotoshwa kwa uchawi (pharmakeia – kuwatafuta pepo kwa makusudi) wako.

Ufunuo 18:23 NEN Biblia

 

4.4 Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.

1Yoh. 4:4 SUV

 

17Lakini hekima itokayo mbinguni kwanza ni safi, kisha inapenda amani, tena ni ya upole, iliyo tayari kusikiliza wengine kwa unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, tena isiyokuwa na unafiki.

Yakobo 3:17 NEN Biblia

 

31 Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.

Walawi 19:31 SUV

 

6“ ‘Mimi nitauelekeza uso wangu dhidi ya mtu anayeenda kwa waaguzi na wenye pepo, na hivyo kujifanyia ukahaba kwa kuwafuata, nami nitamkatilia mbali na watu wake.

Walawi 20:6 NEN Biblia

 

Malaika ni viumbe. Sisi wanadamu ni viumbe pia. Malaika walioanguka, yani pepo, hawakunyang’anywa nguvu na uwezo wao na Mungu baada ya kuanguka kwao. Bado wanaendelea kuwa na uwezo na nguvu zao kama hapo kabla. Ebu tutizame sifa, uwezo, nguvu walizo nazo kama Biblia inavyofundisha, ingawa taarifa za malaika (wateule na walioanguka) ndani ya Biblia ni finyu, na hili linaonekana kuwa ni jambo lililofanywa makusudi na Mungu kwa sababu zake Mwenyewe.

 

  • Malaika ni roho na wameumbwa kwa moto (Zab. 104:4; Waebr. 1:7, 14)

  • Malaika wanaweza kushika moto bila wao kuteketea (Ezekiel 10:2-7; Mwanzo 3:24)

  • Malaika hawaonekani na wanadamu mpaka Mungu aruhusu jambo hilo (Hesabu 22:31; 2Wafalme 6:17)

  • Malaika wana nguvu na uwezo mkubwa – kwa sasa - kuliko wanadamu (Zab. 103:20; 2Pet. 2:11; Matt. 28:2)

  • Pepo wana uwezo wa kuingia katika miili ya wanadamu [wasioamini] na wanyama na kuimiliki kwa kiasi fulani, wakisababisha madhara makubwa (Luka 8:2; Luka 13:11; Marko 5:1-13; Matt. 9:32-33;

  • Pepo wanaweza kuishambulia miili ya waumini na kuwasababishia magonjwa ya ngozini (Ayubu 2:6-8)

  • Malaika hawawezi kuwa kila mahala kwa wakati mmoja, wanasafiri kutoka mahala hadi mahala, kama sisi (Dan. 10:12-14), ingawa wao husafiri kwa haraka sana

  • Malaika hawana uwezo wa kujua yatakayotokea siku za usoni (Mark 13:32)

 

  • Malaika hawafi (hawafikiwi na umauti wa mwili) kama sisi ingawa hata kwetu sisi kifo [cha mwili] ni hali ya mpito tu – roho akishaumbwa basi hafi tena

 

Katika aya zilizotajwa hapa juu tunaweza kuona kwamba malaika wana uwezo mkubwa sana ukiwalinganisha na sisi wanadamu. Ebu tuichunguze dondoo ya mwisho hapo juu – malaika hawafikiwi na umauti kama tunavyokufa sisi wanadamu. Malaika wamekuwako hapa duniani kabla yetu, wameumbwa kabla yetu - soma Ayubu 38, na haswa msitari/aya ya 7 ambapo inasimuliwa jinsi malaika [wateule] walivyofurahishwa na uumbaji wa dunia uliokuwa ukifanywa mbele yao na Mungu. Soma pia jinsi Shetani alivyoanza kuzungumza na Eva (baada ya kumpagawisha nyoka na kumtawala) na kufanikiwa kumrubuni Eva pale bustanini. Ni wazi Shetani alikuwa akiwatizama viumbe hawa wapya wa kibinadamu kwa muda mrefu tu akipanga mkakati wake wa udanganyifu – jambo linaoonyesha kwamba alikuwako kabla yao na alichukizwa na uumbaji wa viumbe hawa wapya kwani wakati huo Shetani alikwishafanya uovu mbele ya Mungu na kuanguka (Isa. 14:12-20; Eze. 28:13-19). Pepo wamekuwa wakituchunguza sisi wanadamu katika maisha yetu yote – na kumbuka kwamba hatuwezi kuwaona bali wao wanatuona; wameishuhudia historia yote ya wanadamu. Bila ya shaka kwa uwezo wao huu wana kumbukumbu muhimu kuhusiana na tabia ya kila mmoja wetu, katika kila familia na mahusiano yake, ingawa hawana uwezo kwa kujua kilicho ndani ya moyo wa mwanadamu – ni Mungu pekee mwenye uwezo huu (1Sam. 16:7). Hii inawawezesha kuonekana kama vile wana uwezo wa kubashiri juu ya maisha ya wanadamu; wanaweza ‘kuwaambia’ baadhi ya wanadamu kupitia mpagawisho (possession) kuhusu mambo yanayoendelea katika maisha ya wenzao na waliyoyafanya na kuyapanga – hili ndilo linalotokea katika kupiga ramli au bao (soma Matendo 16: 16-21 hapa chini kuhakiki hili).

 

16.16 Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua.

16.17 Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu.

16.18 Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.

16.19 Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila, wakawakokota mpaka sokoni mbele ya wakuu wa mji;

16.20 wakawachukua kwa makadhi, wakasema, Watu hawa wanachafua sana mji wetu, nao ni Wayahudi;

16.21 tena wanatangaza habari ya desturi zisizokuwa halali kwetu kuzipokea wala kuzifuata, kwa kuwa sisi tu Warumi.

Matendo 16:16-21

 

Kwa maneno mengine, malaika wanaifahamu historia ya matukio ya kila mwanadamu kwa undani kabisa, na kwa njia hii pepo wanawarubuni watu kwa kujifanya kwamba wao wana uwezo ambao ni Mungu pekee ndiye anao, wa kuijua kudura/hatma ya uumbaji wote. Hivyo, ndugu yangu Mkristo, hata kama mtu anayejiita “mchungaji” akivunja amri za wazi za Mungu zinazokataza kuagua, kubashiri, kutabiri, kupiga ramli, kupiga bao kwa kisingizio cha unabii, basi kaa mbali na “mchungaji” huyo; huyo ni nabii wa uwongo, si mchungaji. Kuwa makini na hili. Kwa mantiki hii, wachawi, wapiga ramli, wafanya mazingaombwe, waaguzi, nk wanashirikiana na pepo na katika ushirikiano wao huu ndipo wanapata “uwezo” wanaouonyesha.

 

Sasa tuzungumzie madai ya uwezo ambao watu fulani ati wanao wa “kuwanga”, yaani kwamba watu hao, wachawi hao, wana uwezo wa kuja nyumbani na kuingia ndani kwako wakati wewe umekwishafunga milango ya nyumba yako na umelala. Inadaiwa kwamba watu hao, wanga hao, wataingia ndani kwako, bila kufungua milango, na kukufanyia kila aina ya uovu na wewe mwenyewe usiweze kuamka. Biblia iko kimya kabisa kuhusiana na jambo hili, madai haya. Hivyo tunapaswa kuona kwamba huu ni udanganyifu mwingine wa Shetani. Kwa nini? Mwanadamu ni mwili na roho (Mwanzo 2:7); hawezi kupaa; hawezi kupenya ukuta na kufika upande wa pili wa ukuta huo. Ikitokea mwili na roho vikatengana basi mwanadamu huyu atakuwa mfu papo hapo (Yakobo 2:26). Biblia iko wazi kwamba wanadamu tutakuwa na uwezo huu baada ya ufufuo kwani tutakuwa kama Bwana wetu Yesu Kristo katika ufufuo (Luka 24:36; Yoh. 20:26; 1Yoh. 3:2; Wafi. 3:21; 1Wakor. 15:43-44). Soma rejea hizo uone jinsi Bwana wetu, baada ya ufufuo Wake, alivyofanya mambo mapya ya ajabu mbele za wanafunzi Wake. Sasa, malaika wana uwezo huu pia – wanaweza kupenya kuta, kupaa, kwani wao ni roho. Hivyo pepo anampagawisha (demon possession) mwanadamu na kumwaminisha kwamba ameondoka kitandani mwake akiwa usingizini, “akapaa” hadi nyumba ya jirani yake na kumfanyia uovu; na wakati huo huo pepo huyu akamshambulia jirani huyo ambaye naye anaamini kwamba amewangiwa akiwa usingizini; hivyo udanganyifu huu unakamilika na watu wanakuwa watumwa wa ushirikina na wokovu unakuwa mgumu sana kwao. Ndiyo maana mwanadamu aliyeokolewa au aliyezaliwa upya / aliyezaliwa kutoka juu kwa njia ya imani katika Yesu Kristo, akapata ubatizo wa Roho Mtakatifu (Yohana 3:16; 1Yohana 5:13), kamwe hawezi kupagawishwa (demon possessed) na pepo; anaweza kushambuliwa katika sehemu za nje za mwili wake (Ayubu 2:6-8), lakini moyoni mwake hili halifanyiki kamwe, kwani yeye sasa ni hekalu la Mungu. Hivyo mwanga ni mtu aliyepagawishwa (possessed) na pepo tu. Asikutishe, usimwogope!

 

Sasa na tuzungumzie suala la “roho wa mizimu – ancestral spirits”. Kuna “wachungaji” wanaowafundisha waumini wao kwamba wanasumbuliwa na “roho wa mizimu” wao katika maisha yao; hudai kwamba wana uwezo wa kuwatoa (exorcise) roho hao na baada ya hapo wasiwasumbue tena waumini wao hao. Ndugu Mkristo, hakuna kitu kama “roho wa mizimu”, hili ni “fundisho la mashetani” (1Tim. 4:1). Kila mwanadamu anayefariki hutokewa na moja kati ya mambo haya mawili:

 

1. Kama alikuwa Mkristo katika maisha yake, yaani alimwamini na kumpokea Bwana Yesu Kristo (Yoh. 3:16-18; 1Yoh. 5:13, etc), basi ataenda mbinguni, au mbingu ya tatu, kwa Mungu – Ufunuo 6:9 (kabla ya kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo, wafu katika imani walienda Paradiso, katika eneo linaloitwa Abraham’s Bosom (Luka 16:21-31).

2. Kama hakuwa Mkristo, yaani hakuokolewa, basi ataenda katika mateso atakakongojea hukumu ya mwisho kabla ya kutupwa katika ziwa la moto (rejea Luka 16:21-31).

 

Hivyo hakuna roho wa mtu yeyote aliyekufa anayebaki akizurura baada ya kifo cha mwanadamu – haya ni “mafundisho ya mashetani” (1Tim. 4:1) katika juhudi zao za kuwapoteza wanadamu, wakisaidiwa na “wachungaji” waongo wanaotafuta pesa tu. Wapo pia “wachungaji” watakaokwambia kwamba wao wana taarifa na kinachoendelea katika “ulimwengu wa roho”. Huu ni uwongo mwingine. Kwa taarifa zaidi kuhusu uwongo huu, soma jarida langu linaloitwa “Karama za Kiroho” linalopatikana bure katika tovuti yangu – https://sayuni.co.tz

 

Sasa, hapa chini tutasoma maswali na majibu kutoka katika tovuti ya https://ichthys.com ambapo wasomaji wa tovuti hiyo walimwuliza mwendeshaji wa tovuti hiyo yenye jukumu la kufundisha Biblia, Profesa Robert D. Luginbill. Maswali na majibu hayo yalihusiana mahususi na 1Samweli 28 – ziara ya mfalme Sauli kwa Mchawi wa Endori kwa lengo la kupiga ramli.

 

1. Kutoka: mail-old-testament-interpretation6.rtf

 

Swali #8:

 

Hello Dr. Luginbill,

 

Ningependa kukuuliza swali jingine. Swali hili linahusiana na sura/ibara isiyo ya kawaida katika Biblia. Dada yangu na mimi tumekuwa katika mazungumzo mara kadhaa … kuhusiana na nini haswa kilitokea katika 1Samweli 28. Katika sura hii tunasoma kwamba roho wa Samweli alimtokea Sauli. Sasa, yawezekana nimekosea hapa, lakini ninavyokumbuka ni kwamba hata wewe Dr. Luginbill unaamini kwamba kwa hakika roho wa Samweli ndiye aliyeonekana hapa na si roho/pepo wa kichawi.

 

Mazungumzo yangu na dada yangu yalihusiana na suala hili. Mimi naamini kwamba roho aliyeonekana pale kwa kweli ni wa Samweli na kwamba Mungu aliamuru tukio hili litokee kwa sababu Biblia yenyewe kwa wazi kabisa inamtambulisha roho huyu kuwa ni Samweli lakini dada yangu naye alikuwa na dondoo nzuri dhidi ya hoja zangu. Dada yangu anahoji kwa nini Mungu aamuri jambo kama hili lipitie katika mikono ya mchawi? [Mungu] angeweza kutumia njia nyingine yoyote kwa kusudi la kumwonya Sauli. Kwa kumtumia mchawi Mungu anakwenda kinyume na viwango vya mwenendo Wake Mwenyewe; hivyo kwa nini [Mungu] Aliruhusu hili litokee? Haya ni maoni ya watu wengi kanisani kwetu pia.

 

Mimi nafahamu kwamba wewe umefundisha kwamba roho yule alikuwa Samweli mwenyewe na kwamba hata yule mchawi mwenyewe wa Endori alishituka sana, lakini je, haiwezekani kwamba yule mchawi alishitushwa na kuogopa kwa sababu aligundua kwamba mtu aliyekuwa mbele yake alikuwa mfalme Sauli na si kwamba ni kwa sababu aliona mzuka?

 

Tafadhali nipatie ushahidi zaidi wa msimamo wangu huu (ambao ni msimamo wako pia).

 

Natanguliza shukrani!

 

Wako katika Kristo,

 

Jibu #8:

 

Karibu sana. Kuhusiana na swali lako, hapa inapasa nianze kwa kutoa maoni yangu kwamba mara nyingi watu wanaona wana uhalali wa kulazimisha dhana zao juu ya yale ambayo Biblia inaweza na haiwezi kusimulia, na juu ya yale ambayo Mungu anaweza na hawezi kuyafanya – bila kujali yale ambayo Biblia inayasimulia kuihalisia, na bila kujali yale ambayo Mungu anaweza kuyafanya na mara nyingi Anasimuliwa [na Biblia] kwamba anayafanya (mfano mzuri wa hili ni pale Mungu anapoonyesha uweza na mamlaka Yake kamili juu ya historia pale Anapowatumia pepo kufanya kazi Yake; tazama linki hiyo).

 

Katika 1Sam. 28:12 Biblia inasimulia kwamba “yule mwanamke alimwona Samweli

 

Katika 1Sam. 28:14 Biblia inasimulia kwamba “Sauli mwenyewe akatambua kwamba ndiye Samweli

 

Katika 1Sam. 28:15 Biblia inasimulia kwamba “Samweli akamwambia Sauli ...”

 

Katika 1Sam. 28:16 Biblia inasimulia kwamba “Samweli akasema ...”

 

Katika 1Sam. 28:20 Biblia inasimulia kwamba “Sauli akaingiwa na hofu kuu kwa sababu ya maneno hayo ya Samweli

 

Kuna viashiria vingine katika aya hii kwamba kwa hakika huyu ni Samweli (nitakupa linki hapa chini ambamo hili suala linajadiliwa), lakini mjadala mnyofu na wa kweli wa aya hii unapaswa kuanza na makubaliano kwamba Biblia kwa uwazi kabisa inamsimulia roho huyu kwamba ni Samweli katika sehemu kadhaa na bila ubishi kiasi kwamba mtu itabidi aitangaze Biblia yenyewe kuwa “imekosea” ili kuuepuka ukweli huu.

 

Kwa nini Mungu alifanya mambo haya kwa namna hii ni suala jingine kabisa; kuanza na ‘mantiki’ inayosema “mimi nafikiri Mungu hakupaswa kufanya mambo haya kwa namna hii, hivyo mambo hayo hayakutokeo hivyo” ni kuchukua barabara inayoelekea kwenye uharibifu. Wakristo wenye shauku ya kutaka kuujua ukweli wa maandiko wanapaswa kuanza na msimamo kwamba Biblia/maandiko ni KWELI, nukta. Namna/jinsi ya kuunyambua ukweli kutoka katika maandiko pale ukweli huo unapokuwa katika namna ya fumbo ni shughuli ya walimu wanyenyekevu, wenye ujuzi, teolojia pamoja na ufafanuzi wa kimungu, ambao Mungu Mwenyewe amewatayarisha baada ya kuwapa kipaji hicho pale walipookolewa na akawaweka katika Kanisa Lake kwa ajili ya kazi hiyo – na kila Mkristo ana haki na wajibu wa kumtafuta mwalimu anayemfaa, na pia kuugundua utumishi aliopangiwa na Bwana (kwa msaada na uongozi wa Roho Mtakatifu) ili naye alitumikie Kanisa. Lakini hakuna Mkristo yeyote atakayeweza kufanya maendeleo yoyote ya kiroho kwa kufanya dhana na mawazo yake mwenyewe [anayoyatoa nje ya Biblia] kuwa ni mbadala wa kweli halisi ya Biblia. Kama tuna nia ya kweli ya kujifunza na kutenda matakwa ya Bwana wetu katika maisha yetu, tutakutana na mambo ambayo yatatushangaza, yatatupa changamoto, na ambayo yatatuletea magumu, mioyoni mwetu na katika mazingira tunamoishi pia – na kwa namna hii tutapitia mitihani mingi. Jambo la muhimu sana ni kufahamu kwamba ni kwa njia ya kweli halisi ambayo imeaminiwa na kuwekwa moyoni ndiyo tutaweza kufaulu mitihani yetu itakayotuwezesha tuingie katika hali ya upevu wa kiroho (na kabla ya hapo kupitia mchakato wa kuelekea katika upevu huo), ili tujiweke katika nafasi ya kuweza kutumiwa na Bwana wetu katika kulitumikia Kanisa Lake. Hapa chini tafadhali tizama zile linki:

Was Saul saved? Samuel and the Witch of Endor

The Witch of Endor and the Spirit of Samuel

Spiritual Warfare II (the witch of Endor)

Eternal Security and Perseverance (the case of Saul)

Katika Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo ambaye ndiye kweli, Neno hai la Mungu,

Bob L.

 

Kutoka: mail-Spiritual-Warfare II.rtf

 

Swali #1:

 

Nataka tu kusema asante sana kwa majibu yako yanayotia faraja, na mimi nafahamu kwamba Bwana atakutumia wewe katika kuwasaidia kwa kuwatia faraja wale wanaokua na kuendelea kupevuka katika Roho Mtakatifu. Swali langu linahusiana na 1Samweli 28. Nimesoma ufafanuzi/fasiri kadhaa zilizoandikwa na wanateolojia kadhaa maarufu wa zamani na pia walimu wa siku hizi wa Biblia na wote wanatofautiana katika tafsiri/uelewa wao. Biblia ninayoisoma inaeleza kwamba ni Mungu, na siyo yule mpiga ramli wa Endori, ndiye aliyeendesha kikamilifu mazingira ya tukio lile, naye Mungu ndiye aliyelitumia tukio lile kutoa tamko la kifo cha Sauli (pamoja na watoto wake) katika mikono ya Wafilisti (tizama aya ya 19). Hata hivyo, moja kati ya fasiri/fafanuzi zangu za Biblia inaeleza tukio hili kama ifuatavyo, nanukuu:

 

1Sam. 28:15 – ‘Na Samweli akamwambia Sauli, Mbona umenitaabisha mimi, hata kunipandisha juu?’ … Hii inaonyesha wazi kwamba huyu hakuwa Samweli kiuhalisia; roho wake (Samweli) alikuwa akipumzika katika [sehemu inayojulikana kama Kifuani mwa Abrahamu – Abraham’s Bosom], akiwa katika [hali ya] upeo wa furaha mbinguni, na akiwa mahala pale hakuna mwanadamu wala pepo mwenye uwezo wa kumtaabisha; wala naye (Samweli) asingeuliza kwa nini amepandishwa juu, bali angeuliza kwa nini ameshushwa chini, kama kweli angekuwa yeye (Samweli); na wala asingetamka kwamba ameshushwa chini kwa uwezo wa mpiga ramli, na kwa msaada wa Shetani”.

 

Note: Hii si tafsiri rasmi ya fasiri hii ambayo mwuliza swali hataji jina lake wala jina la mwandishi wake – R. Kilambo

 

Kwa nini huyu awe roho halisi wa nabii Samweli ikiwa 1Sam. 28:15 inatamka wazi kwamba Mungu na manabii wote walikataa kumjibu Sauli alipoomba msaada? Halafu shauku yangu inatekenywa pale ninaposoma aya ya 13 na kumwona yule mpiga ramli wa Endori akiogopa mara baada ya kuiona taswira ile, au vinginevyo ilikuwa ni Ibilisi (na siyo Samweli) kama fasiri hii inavyosimulia? Lakini kama huyu alikuwa ni pepo, basi ni vipi pepo anaweza kuyajua matukio ya baadaye au kutoa unabii [wa kweli]? Mimi natambua ya kwamba ni Mungu pekee anayeweza kutamka unabii wa kweli kwa njia ya manabii Wake, hivyo kilichotokea hapa kitakuwa si kitu cha kawaida ikiwa huyu hakuwa roho halisi wa Samweli. Je, huyu alikuwa roho halisi wa Samweli au huu ulikuwa ni ujanja-ujanja tu?

 

Jibu #1:

 

Huyu alikuwa [roho halisi wa] Samweli. Ibilisi hakujua lolote kuhusu lililomkuta Sauli kesho yake kama ambavyo Samweli alitabiri kwa usahihi, na wala [Ibilisi] hana uwezo wa kutengeneza aina hii ya taswira ya ajabu kama ambavyo maandiko yanasimulia. Hakuna mtu yeyote katika tukio lile aliyetilia shaka kwamba huyu alikuwa Samweli, na hata wewe unayeonyesha shaka hii bado unapaswa kukubali kwamba tukio hili liliendeshwa na Mungu kwa malengo Yake mwenyewe. Kipingamizi chako hiki, msingi wake unaonekana kutoka katika dhana kwamba Samweli alipaswa kutoka “juu” na siyo kutoka “chini”, lakini kwa hakika kipindi hiki cha historia ambacho tukio hili lilifanyika, yaani kabla Kristo hajapaa [kuelekea] mbingu ya tatu “akiteka mateka” (Waefe. 4:8; linganisha na Zab. 68:18; tizama pia linki hii: BB 4A: "The Transfer of Believers from the Subterranean Paradise to the Third Heaven at the Ascension") "chini" ndiko haswa mahala ambako waumini wa Bwana wetu walioondoka walikohifadhiwa. Kabla ya msalaba, waumini wa Agano la Kale walioaga dunia walikaa katika paradiso ya muda chini ya dunia (mahala palipoitwa Kifua cha Abrahamu – Abraham's Bosom": Luka 16:19-31), kwa sababu kabla ya [sadaka ya Kristo] iliyolipia dhambi zetu zote hawakuweza kuingia katika uwepo mtakatifu wa Mungu (War. 3:25). Hii ndiyo sababu hata Bwana wetu Yesu Kristo "aliteremka na kuingia 'kuzimu' – sheol" katika zile siku tatu za kifo chake cha kimwili, yaani aliteremka na kuingia katika paradiso iliyoko chini [ya dunia], na siyo juu (Luka 23:43); ling. na 1Pet. 3:19-20); kuingia Kwake mbele ya Baba kulifuatia ufufuo wa Bwana wetu ambao ulikuwa udhihirisho wa uweza wa Mungu katika kuweka uzima palipo na mauti kutokana na msingi wa sadaka ya Mwana Wake, Bwana wetu Yesu Kristo, na ni baada ya ufanisi wa kuoshwa kwa dhambi zetu ndio sasa waumini wanapelekwa mbingu ya tatu baada ya kifo hapa duniani, wakihalalishwa kiuhalisia [hapo] kwa njia ya imani kutokana na kile kilichofanywa na Bwana wetu kwa ajili yetu sote.

 

Hivyo basi, ni kweli, Mungu aliendesha kila kitu katika tukio lile, na akamruhusu Samweli kuonekana/kutokea pale (jambo ambalo halina mfano wake mahala pengine katika maandiko!), hivyo basi hii haikuwa séance (kikao cha kuwasiliana na pepo – ramli) iliyokuwa ikitarajiwa na yule mama mchawi, ambapo Shetani anaendesha matukio na pepo fulani anageza kama mtu aliyekufa zamani – hili lilikuwa ni tukio halisi. Ziada na linki nilizokupa hapo juu, tafadhali tizama linki hizi hapa kwa taarifa zaidi:

 

Did the witch of Endor really conjure up the spirit of Samuel?

Demon Influences

Demon Possession (in SR #4)

The Demon Possessed Girl in Acts 16:16.

Necromancy

Exorcism

Witchcraft, Sorcery and Magic in the Bible.

Drugs and Witchcraft

Katika mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo,

Bob L.

Swali #2:

Habari, Dr. Luginbill!

Nilikuwa natizama kipindi cha Kikristo katika luninga ambamo mwendesha kipindi alitamka kwamba yule roho aliyeonekana katika 1Samweli 28 hakuwa Samweli mwenyewe na akadai ana uhakika na hilo. Kwanza alidai kwamba Mungu hawezi kujipinga mwenyewe katika kauli Zake na kwamba Mungu Mwenyewe aliamuru kwamba kuanzisha mawasiliano na roho za watu waliokufa (necromancy) ni chukizo Kwake na amekataza kitendo hicho (Kumb. 18:9-14). Sababu ya pili ambayo mwendesha kipindi aliitaja ni kwamba Sauli alimsujudia "Samweli" (1Sam. 28:14) na kwamba kama roho yule alikuwa Samweli kikwelikweli ... basi Samweli angemwambia Sauli kuacha kufanya vile na kusimama, kama ilivyo katika kitabu cha Ufunuo ambamo Yohana anamsujudia malaika. Mimi niliposikia maneno haya ya yule mwendesha kipindi sikukubaliana nayo. Mimi naamini kwamba Sauli alisujudu katika kuonyesha heshima au kustahi na siyo katika maana ya kuabudu. Pia niliona kuwa ni jambo la kushangaza kwamba kama roho yule hakuwa Samweli, basi aliwezaje kufanya unabii uliokuwa sahihi namna ile wa kifo cha Sauli? Je, pepo wanaweza kutabiri kwa usahihi kwa kiwango kile? Pia nimewahi kuisikia hoja kwamba haiwezekani kwa roho yule kuwa Samweli kwa sababu Mungu alikwishakataa kumjibu Sauli na pia hakuna nabii yeyote aliyejibu maombi yake. Je, inawezekana kufahamu kutokana na fasili/ufafanuzi (exegetics) wa aya za maandiko yale ya sura ya 28 kama huyu alikuwa Samweli au la? Nakubaliana kwamba amri [ya Mungu] imesema kwamba kujaribu kufanya mawasiliano na pepo imekatazwa kabisa, lakini je, inawezekana huyu alikuwa roho wa Samweli? Asante!

Na Mungu akubariki.

Jibu #2:

Nemefurahi kupata e-mail yako. Katika utafiti wangu wa ibara hii, huyu alikuwa Samweli kikwelikweli. Tunaambiwa mara mbili katika maandiko, katika aya ya 15 na ya 16, "Samweli akasema". Maandiko hayakusema "taswira ile ilisema" au "mzuka ule ukasema", bali "Samweli akasema". Pia tunaambiwa katika aya ya 20 kwamba "Sauli akaingiwa na hofu kuu kwa sababu ya maneno hayo ya Samweli". Nimeona mara nyingi kwamba ibara hii inawasumbua sana watu (na kwa kweli ibara hii inawasumbua watu wengi kwa sababu mbalimbali), sioni namna yoyote ingine ya kuelewa kinachoelezwa na maandiko kwa dhahiri kabisa. Sioni kwamba ni sahihi maelezo ya huyu mwendesha kipindi wa luninga kwamba hapa "Mungu anapingana na maneno Yake Mwenyewe". Alichofanya Sauli, yaani kwenda kwa mganguzi, mpiga ramli, ni machukizo makubwa kwa Mungu. Mungu hakumpeleka Sauli kwa mpiga ramli yule; Sauli alienda mwenyewe. Si jambo jipya kwamba Mungu huwaacha watu wafanye maamuzi na matendo Aliyoyakataza. Kwa mantiki anayoitumia huyu mwendesha kipindi wa luninga, Eva asingeweza kula tunda la mti wa ujuzi wa mema na mabaya, kwa sababu [tendo] hili lilikuwa kinyume na mapenzi ya Mungu. Lakini sisi wanadamu tumekuwa tukienda dhidi ya mapenzi ya Mungu tangu Eva afanye uasi ule – na tumedhurika sana kwa hilo. Sauli angejitendea mwenyewe fadhila kuu kama angeutumia usiku ule kwa kutubu katika kujutia uasi wake dhidi ya Bwana – akijipaka majivu na kuvaa magunia - badala ya kufanya machukizo mapya yaliyoongeza orodha yake ya makosa dhidi ya Mungu (ling. na 2Sam. 12:16).

Kwa mtazamo wangu, kuna uwezekano mkubwa kwamba hili ni tukio pekee katika historia ya wanadamu ambapo ramli ya aina hii imemfikia yule mtu aliyekusudiwa. Ni kweli pia kwamba hili lisingefanikiwa kama Mungu asingeruhusu litokee. Katika masimulizi ya ibara ile yule mwanamke mpiga ramli aliingiwa na hofu ya wazi mara alipomwona Samweli, na mimi nafikiri kwamba chochote alichokuwa "akikiona" katika matukio ya ramli zilizopita kilitokana na udanganyifu wa pepo, yaani kilikuwa ni matukio bandia yaliyofanywa na pepo – au tuseme yalikuwa mazingaombwe tu. Lakini hapa, Mungu alimruhusu Samweli aongee na Sauli ... ili kumwonya kwa mwenendo wake mbovu na kuweka wazi kabisa sababu ya kushindwa kwake katika vita iliyopiganwa kesho yake, pamoja na kifo chake kesho hiyo hiyo (na pia kwa faida yake na yetu: War. 15:4).

Uchambuzi wako wa tukio hili ni mzuri. Mimi nakubaliana na wewe katika hoja zako dhidi ya "kusujudu" anakozungumzia jamaa yule, na pia katika kufahamu kwa usahihi matukio ya siku za usoni ambayo ni Mungu pekee anayeweza kuyajua na kutusimulia. Huo ni uelewa mzuri sana wa maandiko, na kwangu mimi hii inatuhakikishia bila utata kwamba huyu alikuwa Samweli mwenyewe. Mungu alijibu wito wa Sauli kwa mara hii ya mwisho, lakini kwa kutabiri kifo chake tu. Ili upate kusoma zaidi juu ya suala hili, tafadhali tizama linki hii:

Did the witch of Endor really conjure up the spirit of Samuel?

Katika Yesu Kristo Bwana wetu mpendwa,

Bob L.

 

 

Swali #3:

 

Mambo Dr. Luginbill!

 

Mimi nilimpelekea yule mwendesha kipindi wa luninga majibu yako (swali & jibu #2 hapo juu) na mshauri wake wa kichungaji akanijibu. Mshauri huyo aliandika yafuatayo:

 

Ninakualika uyatafakari yafuatayo:

 

Mtume Paulo aliandika (2Wakor. 11:13,14) kwamba ni jambo linalowezekana kabisa kwa Shetani kugeza na kujibadilisha ili aonekana kama malaika wa nuru.

 

Ebu pia jiulize swali hili: Maandiko ya Mungu yanatufundisha nini kuhusu wafu? Je wafu wanarejea hapa duniani katika maumbile ya aina yoyote? Ayubu 7:9 - “Kama vile wingu likomaavyo na kutoweka, Ni vivyo hivyo ashukaye kuzimuni hatazuka tena kabisa” SUV. Sasa, fuata maelezo yangu kwa uangalifu. Tumaini kuu ambalo maandiko yanatupatia sisi wanadamu ni kwamba katika asubuhi ya ile siku ya ufufuo – siyo siku ya kifo – wapendwa wetu waliotutoka watajumuika nasi tena. Kwa hakika, mfumo mzima wa Ukristo umejengwa juu ya ufufuo wa Bwana Yesu Kristo kutoka kwa wafu na ufufuo wa mwisho wa wafuasi Wake pale atakaporudi mara ya pili. Katika siku ile, na siyo kabla, kifo kitasalimu amri mbele ya uzima wa milele.

 

Biblia inaendelea kutufundisha kwamba katika mauti uweza wa mwanadamu wa kufikiri unakoma, Zaburi 146:3,4. Pia katika Mhubiri 9:5,6 tunaambiwa: 5. Kwa sababu walio hai wanajua kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lolote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa. 6. Mapenzi yao na machukio yao, na husuda yao imepotea yote pamoja; wala hawana sehemu tena katika jambo lolote lililofanyika chini ya jua SUV.

 

Umeona basi? Wafu hawajui lolote. Hawakumbuki kitu chochote. Hawawezi kupenda, wala kuchukia, wala kuona wivu. Wanabaki kaburini mpaka siku ya ufufuo wa uzima au ufufuo wa hukumu/hatia. Tizama pia maneno ya Bwana Yesu mwenyewe katika Yohana 5:28,29.

 

Tukiwa na ukweli huu akilini mwetu, sasa tugeukie ile simulizi ya Sauli alipomtembelea yule mama mpiga ramli wa Endori – jambo ambalo Mungu alilikataza kwa wazi kabisa. Tunaona hapo kwamba yule hakuwa Samweli aliyeitwa na mpiga ramli, bali ni pepo.

 

Ingawa maandiko yanasema kwamba mpiga ramli yule alimwona “Samweli” na kwamba Samweli aliongea, hii haimaanishi kwamba Samweli alikuwako pale kiuhalisia, iwe katika mwili wa ufufuo au kiroho. Mwandishi anatuambia tu kutoka kwa mtazamo wa yule mpiga ramli na mtazamo wa mfalme Sauli aliyedanganywa kile walichofikiri wamekiona na kusikia.

 

Kwa kifupi, Ibilisi alimdanganya yule mwanamke mwovu, halafu akamdanganya Sauli. Ilikuwa tu ramli iliyosimamiwa na Ibilisi.

 

Mungu akubariki katika masomo ya Neno Lake!

 

Sasa Dr. Luginbill, wewe una maoni gani kuhusu uchambuzi huu? Mimi nina uhakika kwamba tafsiri yake ya Zaburi 146:3,4 haimaanishi kwamba wafu hawana ufahamu mpaka siku ya ufufuo, lakini mimi nilitaka kujua pia mtazamo wako hapa. Asante sana!

 

Mungu akubariki,

 

Jibu #3:

 

Nina tumaini kwamba mambo yanendelea vyema hapo kwako na katika ushuhuda wako wa Injili ya Bwana Yesu Kristo.

 

Hata kama kungekuwa na kiasi fulani cha ukweli katika mapingamizi unayotaarifu hapa, maoni uliyoyatoa kwangu katika barua pepe iliyopita (swali #2) pamoja na dondoo nilizoongezea mimi, kwa mtazamo wangu zinamaliza ubishi katika suala hili – na hakuna hata moja kati ya hoja zako na zangu inayojibiwa kwa umahiri wa kutosha katika barua pepe hii yake. Zaidi ya hapo, kwa hakika kuna ukweli kidogo sana katika mapingamizi yaliyoorodheshwa na huyu mshauri wake wa kichungaji.

 

para1: Kitendo cha pepo kuwageza malaika wateule hakifanani kabisa na kitendo cha pepo hao hao cha kuwageza wanadamu; katika maandiko hakuna tukio la pepo kuwageza wanadamu, na inaweza kuwa ni kwa sababu hawana uwezo huo au wanakatazwa na Mungu kufanya hivyo.

 

para 2-4: Eliya na Musa watarejea hapa duniani kutoka kwa wafu (tizama linki: CT 3A "The Two Witnesses"); baada ya kusulubiwa Bwana wetu watakatifu wengi waliolala waliinuliwa (Matt. 27:52 SUV) na kuishi tena; Lazaro na mtoto wa mjane wa Naini waliinuliwa kutoka mauti na Bwana Yesu; na kuna ushahidi tosha katika maandiko unaoonyesha kwamba baada ya kuondoka hapa duniani hatulali usingizi wala hatupotezi fahamu (ling. na Luka 16:19-31; 2Wakor. 5:3 [katika Kiyunani]; Ufu. 6:9-11; 7:9-17). Bwana yesu anamwambia Martha katika Yohana 11:26, "naye kila aishiye na kuniamini hatokufa hata milele" (SUV); namna pekee hili laweza kuwa kweli ni ikiwa baada ya "kifo" kiuhalisia "hatufi" bali tu hai mbele ya Bwana (kama ambavyo kila Mkristo/muumini ni "mwenye uzima katika Yeye": Luka 20:38). Kama unavyoweza kuona mwenyewe, fundisho la uwongo la "soul sleep" ('kulala kwa roho' au 'usingizi wa roho' linalofundishwa na JW's na SDA's) ni uzushi wa hatari sana. Tafadhali tizama linki hizi:

The False Doctrine of "Soul Sleep"

Sleep as a Euphemism for Death.

The False Doctrine of 'Soul Sleep' II

Our Heavenly, Pre-Resurrection, Interim State.

 

para 5: Kama unavyosema kwa ukweli kabisa, pepo hawawezi kujua yatakayotokea [baadaye]; na kama ninavyosema [mimi], Biblia inamwita yule roho/mtu "Samweli".

para 6: Maandiko yako wazi. Biblia inasema kwamba Sauli anaongea na Samweli na kwamba Samweli (siyo roho fulani) anaongea na Sauli (1Sam. 28:15; 28:16; 28:20); Biblia inaiita ile taswira [ya ajabu] "Samweli" (1Sam. 28:12; 28:14). Hakuna njia ya kuukimbia ukweli huu – kwa wale wanaofuata maandiko kwa ukaribu.

 

para 7: Sauli alikwishageuka na kumfuata Shetani, na kuanguka kwake kuelekea kwenye uasi (apostasy) kunafikia kilele chake katika ziara yake hii kwa huyu mwanamke mpiga ramli mwenye pepo (au aliyepagawishwa au aliyetawaliwa na pepo) soma note hapa chini; hata hivyo, Mungu aliwageuzia kibao wote waliokuwako na akawapa hadhira na Samweli – ili aweze kutoa unabii wa kifo cha Sauli na vifo vya watoto wake siku inayofuata, mambo ambayo hakuna pepo anayeweza kuyajua kabla, kwani pepo hawawezi kuyajua yatakayotokea baadaye – kama kiumbe yeyote mwingine – kando na yale ambayo Mungu Mwenyewe ameamua kuyafunua.

 

Katika Yesu Kristo mpendwa Bwana wetu,

 

Bob L.

 

NOTE: Katika sehemu nyingine ya tovuti yake (miaka kadhaa baada ya mahojiano haya kwa njia ya barua pepe) Dr. Luginbill amebadilisha kufundisha kwamba Sauli alikamilisha uasi (apostasy) wake, na badala yake [Sauli] alipitia mchakato unaoitwa "Sin Unto Death" au "Dhambi Inayopelekea kwenye/katika Mauti" inayofundishwa katika 1Yohana 5:16-17, ambapo muumini anaokolewa na Mungu kabla hajafikia uasi kamili na kufa/kuuawa kwa njia ya kutisha (1Sam. 28:19b - ... kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami - Samweli alikuwa paradiso tayari). Mifano mingine ya kanuni hii ni Ananias & Safira katika Matendo 5:1-10; kijana aliyelala na mke wa baba yake katika 1Wakor. 5:1-5. Huu ni mfano mzuri wa ule msingi wa uanafunzi wetu kwamba katika mchakato wetu wa kukua kiroho hapa duniani, unapokutana na ushahidi katika Biblia unaopinga kanuni fulani unayoiamini, basi unapaswa kuiacha kanuni ile na kuiamini kanuni hii mpya inayohimilishwa na ushahidi mpya na imara wa Biblia. Mfano: watu huacha msimamo wao juu ya kuamini unyakuo wa kabla ya ujio wa pili wa Bwana Yesu Kristo na kuamini kwamba unyakuo huo utatukia baada ya Dhiki Kuu - R. Kilambo.

 

3. Kutoka: mail-Spiritual-Warfare III

 

Swali #5:

 

Habari ya leo?

 

Nina tumaini kwamba barua pepe hii itakukuta salama. Napenda kukushukuru kwa sala zako unazozitoa kwa niaba yangu, na ninamshukuru Mungu kwani nimeokolewa kutoka katika unabii wa uwongo. Ninakuombea wewe na utumishi wako kila siku. Nilikuwa nikisoma majibu yako katika Spiritual Warfare II na nina maswali yafuatayo yanayonisumbua:

 

Nanukuu kutoka para7: "... hata hivyo, Mungu aliwageuzia kibao wote waliokuwako na akawapa hadhira na Samweli – ili aweze kutoa unabii wa kifo cha Sauli na vifo vya watoto wake siku inayofuata, mambo ambayo hakuna pepo anayeweza kuyajua kabla, kwani pepo hawawezi kuyajua yatakayotokea baadaye – kama kiumbe yeyote mwingine – kando na yale ambayo Mungu Mwenyewe ameamua kuyafunua".

 

Kuna manabii wengi wa uwongo ambao wanaweza kusema mambo kama vile Mungu anawaonyesha mambo ya siri, yaliyofichika, ili wawarubuni watu. Ni wapi basi manabii hao [wa uwongo] wanapata mambo hayo ya siri yatakayotokea, kama siyo Ibilisi aliwafunulia?

 

Jibu #5:

 

Tukio linalozungumziwa katika ibara ile ni la kipekee kabisa. Mkristo mzuri hana sababu ya kuogopa kurubuniwa katika tukio kama hilo, kwani Mkristo huyo hatoonekana kamwe akiomba huduma ya mpiga ramli! Ukweli kwamba Mungu aliingilia na kuleta mema Yake katika tukio ambamo kila kitu Sauli alichofanya hakikuwa sahihi, kwangu mimi ni jambo la kutia moyo sana. Hata hivyo, Sauli aling'ang'ana kwa kiburi katika ubishi wake dhidi ya Mungu mpaka mwisho [wake]. Kwetu sisi tunaompenda Mungu, tunahakikishiwa kwamba Yeye "anafanya kila kitu kwa ajili ya mema [yetu]", hata kama ni vigumu kuliona hili wakati wa mitihani yetu. Ni kweli pia kwamba hata matendo ya watu wabaya na waovu na majeshi yote ya Shetani – ambao wote Yeye anawajua fika – Ameyafanyia mahesabu kikamilifu katika mpango Wake timilifu, na, mwisho wa yote, yatafanyiwa kazi kwa ajili ya mema katika kukamilisha mapenzi Yake yaliyo timilifu (Zab. 76:10). Hii ndiyo busara isiyo na kifani na isiyoweza kufahamika [katika kina na mapana yake], ya Mungu.

 

Kuhusiana na utumiaji Wake wa pepo kwa malengo Yake, tafadhali tizama linki: "God's use of Evil Spirits". Uko sahihi kabisa katika kujilinda dhidi ya udanganyifu. Mimi nafikiri ni vigumu kumrubuni Mkristo anayekua na aliyepevuka kiroho kama wewe, lakini wale ambao hawajapevuka na wale ambao hawafanyi maendeleo kama ambavyo Bwana ameagiza wafanye wanajiweka katika hatari ya mauti ya milele (kwani hao ni rahisi kupoteza imani yao wanaposhambuliwa na shinikizo) – na je, wale wasioamini [kwa sasa] wako katika kiasi gani cha hatari hii, haswa tukikumbuka kipindi kilicho karibu sana cha Dhiki Kuu?

 

13.4 Wakamsujudu yule joka kwa sababu alimpa huyo mnyama uwezo wake; nao wakamsujudu yule mnyama, wakisema, Ni nani afananaye na mnyama huyu? Tena ni nani awezaye kufanya vita naye?

Ufu. 13:4 SUV

 

Nashukuru kwa sala zako, rafiki yangu. Wewe na familia yako mko katika sala zangu pia, kila siku ipitayo. Tafadhali jisikie huru kuniandikia kama una swali lolote kuhusiana na haya tuliyoyajadili.

 

Katika Yesu Kristo mpendwa na Mwokozi wetu,

 

Bob L.

Swali #6:

 

Nashukuru sana kwa jibu lako la haraka. Hofu yangu haihusiani na mimi mwenyewe, bali wale ambao si wapevu [kiroho] na ambao hawafanyi maendeleo [ya kiroho] kama ambavyo Bwana Yesu Kristo ameagiza. Kwa sababu siku zote mimi nina shaka na yale ambayo wanayaita “unabii”, “miujiza”, nk, baadhi yao, kwa hakika wengi wao, wanasema mimi si Mkristo halisi. Lakini kinachoendelea huku kwetu [katika makanisa ya Afrika] ni vigumu sana kuamini utakapoambiwa; na watu wanakataa ushuhuda wako wa Kikristo ikiwa huwezi kuwaambia (kutabiri) chakula walichokula jana usiku au huwezi kuitaja rangi ya nguo zao za ndani ili uonyeshe kwamba wewe ni “mtumishi halisi” wa Mungu. Ninachokiona hapa na ninachokiulizia ni, kwa wale “watumishi” wanaofanya “miujiza” hii, wanapata wapi uwezo huu wa kuwarubuni watu kama siyo kutoka kwa Ibilisi? Na je, jambo hili au uwezo huu haumaanishi kwamba Shetani ana uwezo wa kujua yatakayotokea [siku za usoni]? Nitashukuru sana kwa msaada wako hapa.

 

Jibu #6:

 

Karibu sana. Kujibu swali lako, hapana, Shetani na watumishi wake, pepo na wanadamu, hawana uwezo wa kinabii au kutabiri yatakayotokea. Tunafahamu mengi yatakayotokea baada ya dhiki kuanza, ingawa si kwa utondoti, kutoka katika maandiko. Kwa upande mwingine, Ibilisi [na wasaidizi wake] “huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze” (1Pet. 5:8), na [mimi] nina uhakika wanatutizama na wanajua jana usiku tulikula nini. Kuhusu tatizo la watu kukataa ushuhuda na mamlaka yako kama mtumishi mpaka uonyeshe “miujiza” fulani, nakuhakikishia kwamba hata huku kwetu USA hali ni hiyo hiyo, tofauti iko katika namna ukosefu wa mapenzi ya kweli ya Neno la Mungu inavyoonyeshwa na waumini tu, basi! Hapa, katika nchi yangu hii ya USA, wengi kati ya Wakristo hawana shauku ya kuujua ukweli wa Biblia. Kwa sababu hiyo ninatarajia kwamba sehemu kubwa ya wale watakaoasi katika Dhiki Kuu watatoka katika nchi hii. Kama mtu hana shauku na kweli, hakuna mengi tunayoweza kufanya ili kubadilisha hali hii [yake]. Kwanza, Bwana wetu Yesu Kristo alitenda miujiza ya kiwango cha juu kuliko yote iliyokwishaonekana na itakayoonekana, lakini watu wa wakati ule waliomwamini ni wachache sana. Mitume Wake walitenda miujiza ya kiwango cha juu pia, lakini ujumbe wao uliaminiwa na watu wachache tu. Ukweli kwamba hata katika siku hizi mambo yako vile vile tu (wanaoamini ni wachache) haumaanishi kwamba mambo yalikuwa “mazuri” wakati wa siku za nyuma. Ukweli halisi ni kwamba maisha haya tunayoishi lengo lake ni sisi kutumia utashi wetu ulio huru kabisa ili kufanya uamuzi wa lumwamini na kumfuata Bwana Yesu Kristo au la. Hata baada ya kuamini, kuzaliwa upya, kuokoka, fursa za kuutumia utashi wetu huu kufanya maamuzi mbalimbali haziishi. Sisi tunaoridhika na ukweli kwamba kwa kuwa tumeamua si tu kuwa wafuasi wa Bwana Yesu Kristo bali kumfuata kwa ukaribu zaidi siku hadi siku tukipita katika milima na mabonde (faraja na dhiki) basi tutathawabiwa kwa sababu hiyo – hatuna uwezo wa kuuwasha moto wa imani yenye nguvu ndani ya mtu mwingine, awe Mkristo au la. Lakini tunaweza kutoa ushuhuda mzuri. Tunaweza kuukumbatia ukweli kwa moyo wote. Tunaweza kuonyesha kwa imani yetu madhubuti kwamba kweli ni ile tunayoiishi … kwani hatujui kama Bwana anaweza kuutumia ushuhuda wetu huu wa Neno la uzima kumwita mtu mwingine aje Kwake. Sisi ni askari wa Kristo. Ametuweka hapa tulipo wakati huu kwa lengo la kutimiza wito Aliotupangia. Sehemu kubwa ya imani ya kweli ni kuukubali wito huu na kuutekeleza kwa moyo wote, hata kama mbele za macho ya ulimwengu tunaweza kuonekana kuwa ni wendawazimu. Lakini sisi tunatembea kwa imani.

 

11.1 Basi imani [katika Neno lililoandikwa na lenye uhai] ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, [imani] ni bayana [proof] ya mambo yasiyoonekana.

11.2 Maana kwa hiyo wazee wetu walishuhudiwa.

Waebr. 11:1-2

 

11.6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza [Mungu]; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.

Waebr. 11:6

 

Katika matarajio ya kufurahi pamoja pale utakapokuwa ukipokea thawabu yako katika ile siku ya siku,

 

Bob L.

 

Swali #7:

 

Habari yako Dr. Luginibill,

 

Nashukuru sana kwa sala zako. Ninatoa shukrani nyingi sana kwa Mwili wa Kristo kwa kunipa nguvu ninazozihitaji sana na zilizoniwezesha kuvumilia mitihani ya maisha yangu. Nina maswali kadhaa yaliyokuja akilini mwangu wakati ninasoma ibara fulani za Biblia zinazohusiana na watu wanaodai wamewasiliana na wafu. Sioni marejeo yoyote katika maandiko juu ya roho wa watu waliokufa na wakarudi hapa duniani isipokuwa katika ibara ile ambapo roho wa Samweli alitoa unabii kuhusu kifo cha Samweli. Je, “mizuka” wote wanaodai kuwa ni roho wa watu waliokufa ni pepo wenye nia ya kurubuni? Nimesikia kuwa pepo hawa wanawafahamu vizuri watu wale waliokufa kiasi kwamba wanaweza kugeza taswira yao na kuwarubini ndugu zao, nk, kwamba wamerudi duniani kutoka katika mauti. Nimesikia pia kwamba pepo hawa wanapenda sana kuishi na watu/binadamu waovu walioyatumia maisha yao katika dhambi, hivyo pepo hao wanawafahamu vizuri waovu hao, na matokeo yake ni kwamba pepo hawa wanaweza kuwageza waovu hao baada ya kifo chao. Je, Biblia inatupatia rejea zozote kuhusu “mizuka” (ghosts) na kama “mizuka” hii inatokana na watu/wanadamu waliokufa? Je, kuna tofauti yoyote kati ya roho waovu, roho wachafu, na pepo? Natanguliza shukrani zangu.

 

Mungu akubariki,

 

Jibu #7:

 

Kuna aina 3 tu za roho walioumbwa: roho wa wanyama, roho wa watu/binadamu, na roho wa malaika. Roho wa wanyama na watu huondoka baada ya kifo cha miili yao na hawana mawasiliano tena na dunia (mpaka siku ya ufufuo). Pepo wana wasifu wa aina kadhaa katika maandiko. Kwa hakika, roho waovu, roho wachafu, na pepo ni viumbe wa aina moja (hawa wote ni malaika) ingawa Mungu hakuumba kiumbe mwovu (maana yake hawa wote walianguka); hizo zote ni wasifu wa malaika walioanguka.

 

Lile tukio la kuonekana kwa Samweli mbele ya Sauli (na kuongea naye) ni la kipekee kabisa katika historia ya wanadamu. Mara baada ya kifo [cha mwanadamu] roho wake anauacha mwili wa mwanadamu huyu na kuelekea sehemu inayomuhusu: sehemu ya mateso (Torments) kwa wasioamini na mbinguni (mbingu ya tatu) kwa waumini wa Bwana Yesu Kristo (na kabla ya msalaba waumini walipelekwa paradiso, chini ya dunia: waumini wote hawa walihamishiwa mbingu ya tatu baada ya ushindi wa Bwana wetu na kupaa Kwake; tizama linki hiyo). Kumbuka mshituko na hofu aliyoonyesha mwanamke yule mpiga ramli; hii ni kwa sababu tukio lenye uhalisia kama ule lilikuwa halijawahi kumtokea kabla. Mwanamke yule alikuwa mchawi, yaani alikuwa akitumiwa na pepo kuwadanganya wanadamu, na ‘taaluma’ yake ilikuwa ni kuwadanganya watu kwamba yeye anawawezesha kuzungumza na ndugu zao waliokufa zamani. Tangu tulipoletewa neema ya Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste ya Kanisa, Roho Mtakatifu amekuwa akiendesha huduma (ministry) mahususi ya kuzuia/kuhini/kuwabana pepo ili wasifanye matendo haya kwa kiasi kikubwa (tizama linki). Wakati wa Dhiki na Dhiki Kuu, huduma hii ya Roho Mtakatifu itasitishwa, na hapo kila aina ya matendo maovu yatafanywa, na mahususi patakuwa na ufunuo wa mpinga-kristo (2Wathess. 2:6-7). Kwa hakika, hapajawahi kuwa na “mizuka” (ghosts) kwa maana ya roho wa watu waliokufa. Pia ikiwa unasimuliwa na unashuhudia matukio ya uovu yenye shabaha ya kurubuni watu, basi hayo ni matokeo ya matendo maovu ya watu wanaoshirikiana (neno ushirikina!) na wanadamu waovu hata kama matukio hayo ‘yanaonekana’ mema kiasi gani! Wakristo wanapata kiasi kikubwa cha ulinzi dhidi ya mambo haya, ila wanapaswa kukaa mbali na matukio au watu wanaofanya mambo haya.

 

Hapa kuna linki zinazojadili suala hili kwa utondoti zaidi:

 

What is the Difference between Demons and Fallen Angels?

Angelic Issues III: Demons, Satan, Elders, Female Angels and Guardians.

The Witch of Endor and the Spirit of Samuel

Saul and Samuel at Endor

Witchcraft, Sorcery and Magic in the Bible

Religion and the Occult

 

Nashukuru pia kwa sala zako, rafiki yangu!

 

Katika Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu,

 

Bob L.

 

4. Kutoka: mail-witch-of-Endor: “Did the witch of Endor really conjure up the spirit of Samuel?”

June 15, 2003

 

Swali:

 

Nimemsikia mtu fulani akisema kwamba yule roho wa Samweli aliyeitwa na yule mchawi wa Endori katika 1Samweli 28:11-19 alitoka kwa Shetani na si Mungu. Wewe unasemaje kuhusu hili?

 

Jibu:

 

Kwa mtazamo wangu, ni kweli kabisa kwamba alichokuwa akifanya mwanamke yule kilikuwa ni kinyume cha sheria [ya nchi] (Sauli alikwishapitisha sheria dhidi ya uovu wa kuwasiliana na pepo), kilikuwa ni uovu mkubwa, kilikuwa ni kitendo cha kishetani. Kuwasiliana na pepo, ikiwa ni pamoja na namna zote za “kuita, kupunga pepo na wafu” ni uovu mkuu dhidi ya Mungu (ling. na Kutoka 22:18; Walawi 19:26). Yawezekana ukadai kwamba “hukujua” kwamba kwa matendo yako ya aina hii ulikuwa unamwabudu mungu mwingine, wakati, kwa mfano, ulipoipa kipaumbele pesa juu ya Mungu (huwezi kumwabudu Mungu na Shetani kwa wakati mmoja, hivyo tamaa zote kiuhalisia ni ibada ya Shetani – idolatry: Wakol. 3:5; ling. na Waefe. 5:5). Lakini kutokana na sababu za kutafuta mwelekeo wa kiroho unakwenda kwa kiumbe mwingine (na ambaye kwa wazi kabisa hana uelekeo wa ki-mungu) badala ya Mungu, huko ni kumfedhehesha Mungu kwa wazi kabisa. Na hakuna fedheha kwa Mungu inayozidi kitendo cha mtu kuwasiliana na kutafuta ushauri wa pepo.

 

Unapotafuta mawasiliano na pepo kupitia mpiga ramli (yaani pale ambapo si mazingaombwe tu), basi hapo unahusisha pepo, na hivyo unamhusisha Shetani. Na kwa kweli ni wazi kwa kutazama muktadha wa 1Samweli 28 kwamba mwanamke huyu (yaani yule mpiga ramli wa Endori) ni: 1. mtumishi wa moja kwa moja wa Ibilisi (kwa njia ya kupagawishwa na pepo – possession – au angalau kutawaliwa fikra na matendo yake), au 2. kwa njia isiyo ya moja kwa moja (kujitafutia kipato kwa kugeza tu kwamba anaweza “kuita watu waliokufa”).

 

Hata hivyo, kuhusiana na swali lako, ukweli ni kwamba hata pepo wanapoendesha maisha ya mtu (kwa njia ya kumpagawisha, nk), hawawezi “kumwita mtu yeyote kutoka katika wafu” na hawawezi kufanya chochote kilichozuiliwa na Mungu. Wanaweza tu kufanya ‘drama’, kugeza, kuigiza, kama vile kitendo fulani kimefanyika, na neno la Kiebrania lililotumika katika sura ya 28 kuielezea ‘drama’ hii ya pepo, obh, אוב, kwa kuwa maana yake nyingine ni chupa ya mvinyo iliyoundwa kwa ngozi, linaweza kuashiria sauti ya “kimzuka-mzuka” hivi ya ‘drama’ hiyo, au kwamba pepo huyo anamtumia mtu huyu kama “chombo” kinachofanana na chupa tupu ya mvinyo. Kwa vyovyote vile, wakati tukio hili linaweza kuwa linatokana na kupagawishwa kiuhalisia na pepo, haiwezekani kabisa kwamba “mtu aliyekufa aliitwa kweli” - hili haliwezi kufanyika bila kuwezeshwa na Mungu.

 

Na kwa hakika yule alikuwa Samweli – pepo hawezi kufurahishwa na taswira ya Samweli inaposema kile ambacho “roho” yule alisema. Zaidi ya hapo, mpiga ramli yule alipomwona Samweli mwenyewe akipanda kutoka chini ya dunia, alishikwa na mshituko na hofu kubwa, papo hapo akitambua kuwa amedanganywa (na akigundua kuwa mteja wake ni mfalme Sauli mwenyewe). Hivyo tukio hili halikuwa la kawaida kwake mchawi yule, bali lilikuwa nje kabisa ya mazoea yake ya kawaida, kwani kwa hakika alikuwa anamwona mtu aliyekufa zamani, kitu ambacho ni nje ya uwezo wake kukifanya na pia ni nje ya uwezo wa pepo wake kukifanya (kwani matukio yote ya siku za nyuma aliyokuwa akiyafanya yalikuwa mchezo wa kuigiza/mazingaombwe tu).

 

Hapana, mimi nafikiri hapa hakuna shaka kwamba Mungu amejibu ombi la Sauli, ingawa ombi hili lilikuwa ovu na lilipitia njia iliyokatazwa Naye – ambalo limedhihirisha kwamba, 1. Sauli alikwishaporomoka kiroho kwa kiasi kikubwa sana, na 2. kuthibitisha kwamba mwisho wake (Sauli) ulikuwa karibu kwa sababu ya uasi (apostasy) wake – tizama NOTE hapa chini - ulioonekana wazi kwa matendo yake, kama kutaka ushauri wa nini cha kufanya kwa kumtumia mpiga ramli ambaye ni wakala wa Shetani, badala ya kumwomba Mungu (ling. na Isaya 8:19). Hivyo mpiga ramli yule ni wakala wa Shetani, pepo wanaompagawisha / wanaomtawala mpiga ramli yule nao ni wakala wa Shetani, Sauli anafuata matakwa ya Shetani badala ya matakwa ya Mungu, lakini roho yule [wa Samweli] anatumwa na Mungu ili kuwatunduwaza (confound) hao wote, ukweli unaoonekana wazi / dhahiri kutokana na ujumbe uliotolewa, ujumbe ambao ulithibitishwa na matukio yaliyofuata (jambo ambalo haliwezi kufanywa na pepo -wala binadamu- ambao hawana uwezo wa kujua yatakayotukia [hapo baadaye] licha ya uweza mkubwa walio nao).

 

Tafadhali tizama linki zifuatazo:

Demon Influences

Demon Possession (in SR #4)

The Demon Possessed Girl in Acts 16:16.

Necromancy

Exorcism

 

NOTE: Katika sehemu nyingine ya tovuti yake (miaka kadhaa baada ya mahojiano haya kwa njia ya barua pepe) Dr. Luginbill amebadilisha kufundisha kwamba Sauli alikamilisha uasi (apostasy) wake, na badala yake [Sauli] alipitia mchakato unaoitwa "Sin Unto Death" au "Dhambi Inayopelekea Kwenye/katika Mauti" inayofundishwa katika 1Yohana 5:16-17, ambapo muumini anaokolewa na Mungu kabla hajafikia uasi kamili na kufa/kuuawa kwa njia ya kutisha (1Sam. 28:19b - ... kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami - Samweli alikuwa paradiso tayari). Mifano mingine ya kanuni hii ni Ananias & Safira katika Matendo 5:1-10; kijana aliyelala na mke wa baba yake katika 1Wakor. 5:1-5. Huu ni mfano mzuri wa ule msingi wa uanafunzi wetu kwamba katika mchakato wetu wa kukua kiroho hapa duniani, unapokutana na ushahidi katika Biblia unaopinga kanuni fulani unayoiamini, basi unapaswa kuiacha kanuni ile na kuiamini kanuni hii mpya inayohimilishwa na ushahidi mpya na imara wa Biblia. Mfano: watu huacha msimamo wao juu ya kuamini unyakuo wa kabla ya ujio wa pili wa Bwana Yesu Kristo na kuamini kwamba unyakuo huo utatukia baada ya Dhiki Kuu - R. Kilambo.

 

Natumaini hii inasaidia,

 

Wako katika Kristo,

 

Bob L.

 

=0=

 

Hapa nitamalizia na aya kutoka katika Biblia ambayo inatoa njia ya jinsi ya kupata mwongozo wa kiroho katika maisha yetu pale tunapojikuta katika hali ya kutojua nini cha kufanya:

 

5 Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa.

Yakobo 1:5 NEN Biblia

 

Ni kwa neema tu!

 

Respicius Kilambo

https://sayuni.co.tz