Mateso Katika Maisha ya Mkristo
Kumekuwako na umati wa “wachungaji” wanaoahidi wafuasi wao maisha yenye afya njema, utajiri, maisha bila dhiki yoyote, hapa duniani. “Wachungaji” hao, wanaojipa vyeo mbalimbali kama “nabii/prophet”, “mtume”, n.k. wanalitumia Jina takatifu la Bwana wetu Yesu Kristo, na Biblia, katika kuwahakikishia wafuasi wao hao (ambao wanajiita Wakristo ingawa nina shaka kama wanaisoma na kujifunza Biblia, achilia mbali kuiamini) kwamba Mkristo hapa duniani ameahidiwa na Mungu maisha ya usitawi na kufaudu. “Wachungaji” hawa hutoa sharti la kuchangiwa mali, pesa, n.k., ambayo wanaiita “sadaka” ili waumini wao hao waweze kufaudu afya njema, utajiri, maisha bila dhiki, n.k. wakingali hapa duniani. Lakini je, Biblia yenyewe inasemaje kuhusu maisha ya Mkristo hapa duniani? Hapa nitanukuu aya kadhaa zinazoonyesha maisha halisi ya Mkristo halisi yanavyokuwa, yakielezwa na kufundishwa na Biblia yenyewe.
16 Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.
17 Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako;
18 michongoma na miiba [ardhi hiyo] itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni;
19 kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi (kifo), ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.
Mwanzo 3:16-19 SUV
Adamu na Eva (wazazi wetu sote) walihukumiwa kuishi kwa dhiki mara baada ya kitendo chao cha uasi dhidi ya Mungu pale bustanini. Bustani ile ilikuwa na kila aina ya starehe, bila suluba yoyote; na sasa walilazimika kuiacha na kuingia katika maisha ya taabu.
19 Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.
Zab. 34:19 SUV
71 Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa, Nipate kujifunza amri zako.
Zab. 119:71 SUV
Aya hizi mbili kutoka Zaburi zinadhihirisha kwamba muumini atapitia mateso, ingawa kwa upande mmoja Mungu atampatia ahueni, na kwa upande mwingine, mateso hayo yanampa mafunzo na kumuimarisha katika imani muumini wa Mungu hapa duniani.
5.10 Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
5.11 Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu.
5.12 Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.
Matt. 5:10-12 SUV
14.27 Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu (kunifuata), hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
Luka 14:27 SUV
16.33 Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo (mtapitia) dhiki ; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu!
Yoh. 16:33
5.40 Wakakubali maneno yake; nao (baraza) walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao.
5.41 Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo.
Matendo 5:40-41 SUV
Aya hizi hapo juu zinasimulia waliyofundishwa wanafunzi/wafuasi wake Bwana Yesu na yaliyowatokea baada ya kuondoka Kwake. Waliteseka kwa ajili ya Ukristo wao. Shetani alitaka kuuangamiza Ukristo kabla haujaenea duniani, hivyo aliwatesa Wakristo ili awakatishe tamaa. Tuendelee.
5.3 Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi;
5.4 na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini [la thawabu ya milele];
5.5 na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi;
War. 5:3-5 SUV
8.18 Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama (yakilinganishwa na) utukufu ule utakaofunuliwa kwetu [katika Ujio wa Pili].
War. 8:18 SUV
8.35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au kukosa mahitaji, au adha, au njaa, au ufukara, au hatari, au upanga?
War. 8:35 SUV
1.3 Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote;
1.4 atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu.
2Wakor. 1:3-4 SUV
4.8 Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa;
4.9 twaudhiwa, bali hatuachwi (hatutelekezwi); twapigwa na kutupwa chini, bali hatuangamizwi;
4.10 siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu.
2Wakor. 4:8-10
6.2 Mchukuliane mizigo na [kwa namna hii] mtaitimiza sheria ya Kristo.
Waga. 6:2
3.10 ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso Yake, nikifananishwa na kufa kwake; Wafi. 3:10 SUV
3.12 Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa (watapitia dhiki). NOTE: Tafsiri ya NEN Biblia-Kiswahili inatumia neno “watateswa” badala ya “wataudhiwa”.
2Tim. 3:12
Naam, hapo Paulo anaeleza bayana kwamba Mkristo anayemtafuta Kristo na kutaka kuijua nia Yake halisi atateseka katika hii dunia. Shetani na majeshi yake, wanadamu na pepo, watampinga na kumwekea vikwazo Mkristo katika kila hatua atakayopiga Mkristo huyu katika safari yake hapa duniani; hata hivyo siku na wakati wote Bwana wetu yuko bega kwa bega, mkono kwa mkono nasi, akituvusha salama katika kila mitihani, magumu, mateso tutakayoyapitia. Hii ni ahadi madhubuti tuliyo nayo kutoka Kwake, ikiwa tu tutamtegemea Yeye.
2.10 Kwa kuwa ilimpasa Yeye (Mungu), ambaye kwa ajili Yake na kwa njia Yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha Kiongozi Mkuu wa wokovu wao (Bwana Yesu) kwa njia ya mateso.
Waebr. 2:10
Hapa tunaambiwa kwamba Bwana Yesu mwenyewe aliteseka katika mwendo Wake hapa duniani, na kwa njia hii alikamilishwa (bila ya shaka ikijumlishwa na kukua Kwake kiroho kwa kutumia masomo ya Biblia pia) – Matt. 4:3-4; Luka 4:16-17.
1.2 Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali;
1.3 mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.
1.4 [Basi acheni] Saburi [ifanye] kazi [yake kwa] ukamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kuonekana wenye mapungufu.
Yakobo 1:2-4
1.12 Heri mtu (Mkristo) astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao.
Yakobo 1:12 SUV
1.6 Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu na mitihani ya namna mbalimbali;
1.7 ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo (haidumu, huisha), ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika [ile siku ya] kufunuliwa kwake Yesu Kristo.
1Pet. 1:6-7
2.19 Kwa maana ni jambo la sifa [mbele ya Mungu] kama mtu akivumilia [ili awe na dhamiri safi] anapoteswa kwa uonevu kwa ajili ya Mungu].
2.20 Kwa maana mna sifa gani kustahimili adhabu kwa sababu ya kutenda dhambi? Lakini kustahimili [mateso] mtendapo mema, huu ndio wema hasa mbele za Mungu.
2.21 Ninyi mliitwa kwa makusudi haya, kwa sababu Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akiwaachia kielelezo, ili mfuate nyayo zake.
1Pet. 2:19-21
3.14 Lakini mjapoteswa kwa sababu ya haki, mna heri. “Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike” (Isa. 8:12).
1Pet. 3:14
4.1 Basi kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, sisi nasi tujivike silaha ya nia ile ile (yaani mtazamo wa aina hiyo hiyo); kwa maana yeye aliyeteswa katika mwili wake (kama Bwana Yesu alivyoteseka) ameachana na dhambi.
1Peter 4:1
4.12 Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba (siyo kifo) ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.
4.13 Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.
1Pet. 4:12-13
5.10 Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu.
1Pet. 5:10 SUV
1 Kama ayala (mbawala) aioneavyo shauku mito ya maji. Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu.
2 Nafsi yangu inamwonea kiu MUNGU, Mungu aliye hai, Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu?
3 Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako.
4 Nayakumbuka hayo nikiweka wazi nafsi yangu ndani yangu, Jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano, Na kuwaongoza nyumbani kwa Mungu, Kwa sauti ya furaha na kusifu, mkutano wa sikukuu.
5 Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.
6 Nafsi yangu imeinama ndani yangu, kwa hiyo nitakukumbuka, Toka nchi ya Yordani, na Mahermoni, na toka kilima cha Mizari.
7 Kilindi chapigia kelele kilindi kwa sauti ya maboromoko ya maji yako, Gharika zako zote na mawimbi yako yote yamepita juu yangu.
8 Mchana Bwana ataagiza fadhili zake, na usiku wimbo wake utakuwa nami, Naam, maombi kwa Mungu aliye uhai wangu.
9 Nitamwambia Mungu, mwamba wangu, Kwa nini umenisahau? Kwa nini ninakwenda nikihuzunika, adui wakinionea?
10 Watesi wangu hunitukana mithili ya kuniponda mifupa yangu, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako?
11 Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.
Zaburi 42 SUV
1 Ee Bwana, unihukumu, unitetee kwa taifa lisilo haki, Uniokoe na mtu wa hila asiye haki.
2 Kwa kuwa Wewe ndiwe Mungu uliye nguvu zangu; kwa nini umenitupa? Kwa nini ninakwenda nikihuzunika, adui wakinionea?
3 Niletewe nuru yako na kweli yako ziniongoze, Zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu na hata maskani yako.
4 Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa Mungu, kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu; Nitakusifu kwa kinubi, Ee MUNGU, Mungu wangu.
5 Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.
Zaburi 43 SUV
Nina matumaini kwamba kama umenifuatilia kwa makini katika nukuu za aya hizi hapa juu, utakuwa umeona kwamba kiuhalisia maisha ya Mkristo si ya starehe na afya njema na utajiri kama sehemu kubwa ya “wachungaji” wanavyosimulia na kufundisha, bali ni maisha ya kupingwa na Shetani katika kila hatua tunayopiga katika kusonga mbele. Tizama kilio cha Daudi katika hizo Zaburi mbili nilizonukuu hapo juu; Daudi anateseka, anapingwa, anakejeliwa, anahuzunishwa; lakini wakati wote anapeleka kilio chake kwa Mungu, aliye tumaini lake. Kwa hakika tunapaswa kufurahia mateso haya, kwani hii ndiyo ishara kwamba kwa hakika tumechaguliwa na Mungu, kwamba tunashiriki katika mateso ya Kristo. Hii haina maana kwamba Mkristo hawezi kuwa na pesa, au utajiri mkubwa, la hasha. Wala hii haina maana ya kwamba Mkristo hawezi kuwa na afya njema na imara, la hasha. Shetani hutafuta namna anayoweza kututesa na kutujaribu ili tujikwae na kuanguka – na hivyo yeye apate fursa ya kutushitaki kwa Mungu (Zakaria 3:1-2; 2Wakor. 2:11; Ufu. 12:10). Tumeamriwa na Kristo kuwa na amani hata tunapokuwa katikati ya dhiki (Yoh. 16:33). Soma kwa makini kitabu cha Ayubu; mtumishi huyu mkuu wa Bwana alikuwa tajiri, lakini Shetani aliomba ruksa ya Mungu ili amtese kwa kumfanya mgonjwa na masikini wa kutupwa, na aliruhusiwa kufanya hivyo! Shetani alifikiri kwamba Ayubu akipoteza mali na afya yake atamwasi Mungu. Licha ya hayo yote, Ayubu alifaulu mtihani ule – Shetani alishindwa. Tunapingwa na Shetani na jeshi lake la pepo, ambao hatuwaoni; tunapingwa pia na vikaragosi wao ambao ni wanadamu wenzetu, tunaowaona. Sasa kwa nini Mkristo wa leo unaamini kwamba mali na afya njema ni ishara ya kwamba wewe ni Mkristo mzuri?! Mantiki ya haya yote ninayoyasema ni kwamba Ukristo una gharama; Mkristo anapaswa kuhesabu gharama ya kuwa mfuasi wa Bwana Yesu kabla hajaanza kujitangaza ya kwamba yeye amezaliwa upya:
14.26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
14.27 Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
14.28 Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?
14.29 Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,
14.30 wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.
14.31 Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule [mfalme] anayekuja juu yake na watu elfu ishirini?
14.32 Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, [wakati mfalme] yule [mwingine akiwa bado] akali mbali.
14.33 Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiye [kuwa tayari ku] acha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
14.34 Chumvi ni kitu chema; lakini chumvi ikiwa imeharibika, itiwe nini ikolee?
14.35 Haiifai nchi wala jaa; watu huitupa nje. Mwenye masikio ya kusikilia, na asikie.
Luka 14:26-35
Hayo ni maneno ya Bwana Yesu Mwenyewe, akikuasa wewe Mkristo kwamba unapaswa kuhesabu gharama ya ufuasi wako. Hakuna ahadi za “kula kuku” hapo! Hata hivyo, Kristo anatuahidi yafuatayo:
6.31 Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini?
6.32 Kwa maana hayo yote Mataifa (wasioamini) huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.
6.33 Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.
6.34 Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake [siku hiyo].
Matt. 6:31-33
Soma pia Zaburi 23. Tunapewa faraja kwamba tukingali katikati ya mateso hapa duniani, Bwana atakidhi mahitaji yetu, na atatupa faraja tele. Hatuahidiwi utajiri, afya njema, maisha yasiyo na dhiki wala vipingamizi, bali mateso na wakati huohuo mahitaji yetu – chakula, makazi, nguo, nyenzo za kutendea utumishi wetu - yatatimizwa na Mungu kwani Yeye anajua tuna mahitaji katika maisha yetu. Kwa mfano, mimi katika utumishi wangu sijawahi kukosa kompyuta mpakato, simu wala intaneti, n.k. tangu nimpokee Kristo, kwani nyenzo hizi ni muhimu sana kwa mwalimu wa leo wa Biblia.
8.28 Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hu[wa]fany[i]a kazi wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.
War. 8:28
3Vumilia taabu pamoja nasi kama askari mwema wa Kristo Yesu. 4Hakuna askari yeyote ambaye akiwa vitani hujishughulisha na mambo ya kawaida ya maisha haya kwa sababu nia yake ni kumpendeza yule aliyemwandika awe askari (Kristo). 5Vivyo hivyo, yeye ashindanaye katika michezo hawezi kupewa tuzo ya ushindi asiposhindana kulingana na kanuni za mashindano.
2Tim. 2:3-5 NEN Biblia
Ndugu yangu Mkristo, tumo katika vita, na wewe ni askari wa Kristo katika vita hii; cha muhimu sana hapa ni wewe kutambua kwamba kuna kanuni za kupigana katika vita hii. Vita si starehe, si raha, si lelemama. Vita yetu hii tutaipigana mpaka siku ile tutakapomfuata Bwana wetu mawinguni. Tuwe makini, hivyo tujihadhari na hawa jamaa:
3.1 Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.
3.2 Maana watu [walimu wa uongo] watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi (wasioheshimu utakatifu),
3.3 wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali (wakatili), wasiopenda mema,
3.4 wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;
3.5 wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.
2Tim. 3:1-5
Na juu ya yote tunayo ile ahadi kuu kuliko zote, ambayo kwayo sisi tumechaguliwa:
21.4 Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.
Ufunuo 21:4 SUV
Mkristo, elekeza macho yako kwa ahadi hii kuu (Ufu, 21:4).
Respicius Kilambo Luciani
+255 737 05 0950